Julius K. Nyerere: Naililia Tanzania! - Nov 1993

Manyerere Jackton

JF-Expert Member
Dec 11, 2012
2,436
4,429
Wapendwa, katika fukuafukua zetu tumekipata kitabu cha utenzi kilichoandikwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, mnamo Novemba 16, 1993; miaka miwili kabla ya kuchapishwa kitabu chake cha "Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania". Kitabu hiki kinaitwa "Tanzania! Tanzania!" Kutokana na vionjo vilivyomo, na kwa kuzingatia kuwa tupo kwenye kusaka Katiba Mpya, nimeona ni vema tushiriki kujua kile alichkiwaza Mwalimu juu ya hatima ya Muungano wa Tanzania. Kitabu hiki tulikichapisha chote kwenye Gazeti Jamhuri, la jana Machi 4, 2014. Karibuni sana.

TANZANIA! TANZANIA!
(1) Niliuliza mwanzoni:
Sera hii ni ya nani?
Serikali kuwa tatu
Hapa Tanzania kwetu?

(2) Ni ya Serikali yetu,
Au ya Wabunge wetu,
Au ni SISIEMU?
Tungependa tufahamu.

(3) Ikiwa ni Serikali
Inopenda jambo hili
La kuvunja Tanzania,
Yafaa kutuambia.

(4) Kama ni Wabunge wetu
Wanotaka nchi yetu
Imeguke ziwe mbili,
Watuambie ukweli.

(5) Au ikiwa ni Chama
Chataka kugawa Umma,
Tuwe sehemu sehemu,
Kitwambie tufahamu

(6) Ye yote mweye akili
Asiyekuwa jahili,
Sera hii anajua
Itavunja Tanzania.

(7) Wanajua wanavunja,
Na kusema kwa ujanja
Tanganyika kujitenga
Si kuvunja, ni kujenga.

(8) Ati "ndani ya Muungano",
Tudhanie ni maneno
Ya uwezo wa hirizi
Kukinga maangamizi.

(9) Misingi mkishavunja,
Msidhani kwa ujanja
Nyumba mtashikilia,
Ikose kuwafukia.
(10) Kwanza fikiri gharama
Zitobebwa na kauma:
Hizi Serikali mbili
Sasa twaona thakili,
Sembuse zikiwa tatu?
Wataweza watu wetu?

(11) Kuwasomesha watoto
Imekuwa adha nzito,
Mambo mengi hatuwezi,
Tumeachia wazazi.

(12) Vitabu na madawati
Hupata wenye bahati,
Wasopata wadhamini
Huchora, huketi nchini.

(13) Waumwao ni taabu
Kupatiwa matibabu,
Sasa wengi hawajali,
Hawendi hosipitali.

(14) Kupunguza matumizi
Twakata wafanyakazi,
Na wale wanobakia
Kuwalipa ni udhia.

(15) Balozi za ugenini
Zinaishi kwa madeni,
Imekuwa ni taabu,
Acha soni na aibu.

(16) Viwanda tunatangaza
Kutafuta kuviuza,
Tukikoswa wananunuzi
Kuvyendesha hatuwezi.

(17) Wakulima twawakopa,
Tunashindwa kuwalipa,
Pembejeo hatuwapi,
Hatujui tupatepi.

(18) Na kadhaka, na kadhaka,
Yote mashaka mashaka:
Ila Serikali tatu
Twaona kuwa si kitu!
(19) Haya ni mambo ya njozi,
Na ndoto za viongozi,
Japo Nchi ingabaki,
Gharama hazibebeki.

(20) Gharama zikiwa mno,
Zitavunja Muungano,
Maana Bwana Borisi
Hatalipa, ataasi.

(21) Pili, hawa washabiki
Walicho nacho ni chuki,
Hoja wazitumiazo
Nguvu ziwasukumazo,
Ni chuki ilokithiri
Kwa ndugu Wazanzibari.

(22) Chuki ni kitu balaa,
Chuki huvunja jamaa,
Sera zikiwa za chuki,
Jamii itahiliki.

(23) Ndiyo ma'na tukataka
Tufahamu kwa hakika,
Sera hii ni ya nani,
Ya chuki Tanzania.

(24) Yafaa wajifichue
Nasi sote tuwajue,
Wanaounga mkono
Uvunji wa Muungano.

(25) Sasa tumesha baini
Sera hii ni ya nani,
Tena inahuzunisha,
Na ni jambo la kutisha.

(26) Kumbe Viongozi wetu
Wa Dola na Chama chetu,
Ndiyo wenye sera hino
Ya kuvunja Muungano;

(27) Ndio wanaowania
Kuivunja Tanzania,
Na watu kutukasimu
Tuwe sehemu sehemu.
(28) Kumbe hawa Viongozi,
Ndio wenye njama hizi,
Za kujenga uhasama
Na kukasimu kauma;

(29) Ndio wanopapatika
Kuitenga Tanganyika,
Ndio wanaotaka Chama
Nacho kikubali njama.

(30) Majuzi huko Dodoma
SISIEMU imesema,
Sera yake Serikali
Zibakie kuwa mbili.

(31) Tena hii ni baada
Ya kufanywa jitihada,
Na juhudi na bidii
Kubadili sera hii.

(32) Na juhudi zote hizi
Walifanya Viongozi,
Chama kibadili sera
Hii inayowakera.

(33) Wala katu msidhani
Ni Wabunge wa Tanzania
Wanotaka kutuwanya,
Au kutuparanganya,
Watu tuwe mbali mbali,
Nchi moja tuwe mbili.

(34) Kwani hoja ya mwanzoni
Ya Wabunge wa Tanzania
Wenyewe walibadili;
Wakataka Serikali
Ifanye referendumu
Ya maoni ya kaumu.

(35) Serikali yetu ndiyo
Ilopinga hoja hiyo,
Ati kuuliza watu,
"Serikali ziwe tatu?"
Ni swali gumu ajabu,
Watashindwa kulijibu!


(36) Tena ati wanasema
Walihofia gharama,
Ila Serikali tatu
Gharama zake si kitu!

(37) Awali walijificha,
Hawakutoa makucha,
Kazi ya kuleta hoja
Ya kubomoa Umoja
Waliachia Wabunge,
Wao kwa siri waunge.

(38) Wabunge wa Tanzania
Kama nilivyowambia,
Hoja yao ya awali
Wao wakaibadili,
Kutaka referendumu
Ya maoni ya kaumu!

(39) Ndipo Viongozi wetu,
Mithili mbwa wa mwitu
Kwenye ngozi ya kondoo,
Walipostuka, loo!

(40) Tukibakia pembeni
Tusishike usukani,
Mambo yataharibika,
Hatupati Tanganyika!

(41) Ndipo pilika pilika,
Mikutano kufanyika,
Kutafuta "muafaka"
Wa kutenga Tanganyika!

(42) Viongozi wano wano
Wa Chama na Muungano,
Ndio walopuuzia
Zanzibari kuingia
Katika lile Shirika,
Watu wakakasirika.

(43) Viongozi wano wano
Wa Chama na Muungano,
Ndio walioniita
Na Bungeni kunileta,
Niwanasihi Wabunge,
Hoja yao wasipange.
(44) Viongozi wano wano
Wa Chama na Muungano,
Ndio sasa wameshika
Kuitenga Tanganyika!
****************************
(45) Nakiri Wazanzibari
Katiba waliathiri,
Nilidhani kazi yetu
Ni kuwabana wenzetu,
Viongozi wa Zanziba,
Waiheshimu Katiba.

(46) Lakini ni Serikali
Ambayo haikujali,
Na kitendo kama hicho
Ikakifumbia jicho,
Na kuanza kufokea
Wale waloikemea.

(47) Wala kuvunja katiba
Kuvunja Nchi si tiba.

(48) Hivi wakifanikiwa
Na Nchi wakaigawa,
Kumbe hawataandika
Katiba ya Tanganyika?

(49) Wataacha utawala
Uwe shaghalabagala?
Na kama ikiandikwa,
Katu haitakiukwa?

(50) Endapo ikatukia
Nayo ikavunjwa pia,
Tanganyika itengane,
Wapate Nchi nyingine?

(51) Wanaovunja sharia
Na Katiba Tanzania,
Dawa ni kuwashitaki
Waadhibiwe kwa haki:
Nchi yetu kuigawa
Ni uhaini, si dawa.


(52) Na Wabunge wapinzani
Walikuwa hamsini,
Na watano wote pia,
Ndivyo tunavyosikia.

(53) Japo wasingebadili
Hoja yao ya awali,
Ingeweza ikapingwa
Kwa hoja zilizopangwa.

(54) Kwani ni mwaka jana tu
Hawa Viongozi wetu
Waliipinga Bungeni,
Tena kwa hoja makini.

(55) Jambo hili, walisema,
Halidaiwi na Umma,
Tume ya Jaji Nyalali
Yakiri hivyo ni kweli.

(56) Pendekezo ni lake tu,
Halitokani na watu;
Na wenzao, watu tisa,
Walilipinga kabisa.

(57) "Japo kweli", walinena,
"Tumesha kubaliana,
Siyo kila rai yetu
Iwe ni dai la watu;

(58) Pendekezo kama lino,
Linohusu Muungano,
Haliwezi liwe letu,
Bila madai ya watu."

(59) Kwa Viongozi wa Umma,
Wenye dhati na hekima,
Hiyo ni hoja makini.
IMEBADILIKA LINI?

(60) Viongozi wa Nchini
Wakihojiwa kwa nini
Hoja hii wasipinge;
Wanalaumu Wabunge,
(Kwa vijembe nami pia,
Kama ukiwasikia!).
(61) Ati wapinzani hao,
Nikisha kusema nao,
Walikuwa kama mbogo
Kwa Viongozi vigogo!

(62) Kama walikuwa mbogo,
Sidhani hata kidogo
Ati walikusudia
Kuigawa Tanzania.

(63) Akilini sina shaka,
Jambo walilolitaka,
Ni Wakuu Tanzania
Kuongoza kwa sharia.

(64) Nami tulipojulusi
Ndivyo nilivyowausi,
"Viongozi wa kaumu
Msisite kuwahimu,
Wawaongoze raia
Kwa mujibu wa sharia.

(65) Hoja mliyoandika,
Ya kutaka Tanganyika
Ipatiwe Serikali,
Iachilieni mbali.
Ni hoja mlokutubu
Kutokana na ghadhabu."

(66) Ni Viongozi wa Dola
Walopinga mjadala,
Ati mambo siku hizi
Yote ni ya wazi wazi.

(67) Kujadili jambo lino
Linohusu Muungano,
Kungegawa Bunge letu,
Na Chama na Nchi yetu!

(68) Ati huu "muafaka"
Wa kutenga Tanganyika,
Ndiyo njia walopata
Ya kuepusha matata!


(69) Ujinga wa kuzidia
Sijapata kusikia,
Kutoka kwa Viongozi
Wa Chama cha Mapinduzi!

(70) Ni demokrasi gani
Ya mambo kichini-chini,
Tuogope mijadala,
Tupende njia za hila?

(71) Haya wanawambia
Mazuzu wa Tanzania?
Wapumbavu na wajinga,
Au watoto wachanga?

(72) Hivi kweli Watanzania
Mwawafanya punguani,
Watashindwa kuelewa
Kuwa wanaghilibiwa?

(73) Hoja hizi, hila hizi,
Ni mbinu za Viongozi,
Wabunge kuwachanganya,
Ni hila za kudanganya;

(74) Ili na Wabunge nao
Tuseme ni wenzi wao,
Kama hivyo nakosea,
Wao watajisemea.

(75) Nasema naradidia:
Wabunge wa Tanzania
Hoja yao ya awali
Waliachilia mbali.

(76) Wakaandika nyingini
Ya kutafuta maoni
Ya Umma wa Tanzania
Kwa njia nilowambia.

(77) Serikali ikapinga
Kwa sababu za kijinga,
Ikaleta "muafaka"
Wa kutenga Tanganyika.

***********
(78) Tanzania yetu ina
Watu aina aina:
Inao hao Wapemba
Watochomewa majumba,
Sera hii ikipita
Bila ya kupigwa vita.

(79) Lakini ina Wahaya,
Na Wasumbwa na Wakwaya,
Ina Waha na Wamwera,
Na Wakwavi na Wakara.

(80) Ina Anna ina Juma,
Ina Asha ina Toma,
Kadhaka ina Pateli,
Na wengine mbali mbali.

(81) Uhasama ukipamba
Mkafukuza Wapemba,
Anojua ni Manani
Mbele kuna mwisho gani.

(82) Hivi mnavyofikiri,
Wenzetu Wazanzibari
Walitokea mwezini
kuja hapo Visiwani?

(83) Visiwani humo wamo
Wamakonde, Wazaramo,
Wanyamwezi na Wamwera;
Na mbari nyingi za Bara.

(84) Walotoka Arabuni
Waliondoka zamani,
Walobaki ni wenzetu,
Raia wa Nchi yetu.

(85) Mzaramo wa Unguja
Akizuiliwa kuja
Kuishi Darisalama,
Nambieni Msukuma
Mgogo au Mngoni
Aruhusiwe kwa nini.


(86) Na Mchagga watamwacha?
Na Muha na kina Chacha?

(87) Mwajuma wa Zanzibari
Mkimwona ni hatari,
Hivi Juma wa Pangani
Ana uhalali gani?

(88) Na Shabani wa Kigoma?
Na Fatuma wa Musoma?

(89) Na vita vya uhasama
Vitapamba Nchi nzima:
Hawa kufukuza hawa
Kwa udini na uzawa,
Yalo Yugoslavia
Yatufike Tanzania.

(90) Chuki hizi msidhani
Hazina udini ndani,
Maana behewa hili
Lina watu kila hali.

(91) Wamo na maaskofu,
Na mashehe watukufu;
Na wasomi wa sharia,
Na wachumi wetu pia,
Kila mtu ana Iwake,
Anazo sababu zake.

(92) Wamo wale wanosema
Mali yote ya kauma,
Viongozi wa Zanzibar
Wamekithiri kuiba,
Wanataja Loliondo,
Na mengine rundo rundo.

(93) Na tuseme kuna njama
Za kula mali ya Umma:
Hivi kweli tukubali
Watu wanopora mali
Wote ni Wanzanzibari,
Bara hawana dosari?


(94) Wala watu wakiiba,
Kuvunja Nchi si tiba,
Dawa ni kushitakiwa,
Wapate kuadhibiwa.

(95) Na tena Wazanzibaa
Wapata laki sabaa,
Na wengi ni mafukara
Kama wenzao wa Bara:
Hivi kweli tukubali
Wote ni wapora mali?

(96) Jumo humo behewani
Wamo na wenye udini:
Kwa hao Ali Hassani
Si Rais wa Tanzani,
Ila ni Mzanzibari.
Na kama ana dosari,
Ni Ali Muislamu
Ndiye wanaomshutumu.

(97) Wasilimu wa Tanzani
Ni themani milioni,
Na pengine kuzidia,
Maana ni kukisia.

(98) Wasilimu wa Unguja,
Na wa Pemba kwa pamoja,
Jumla yao malaki,
Milioni hawafiki.

(99) Mkivunja Tanzania,
Na udini kuingia,
Waislamu wa Bara
Wao watakuwa bora?

(100) Mumo humo behewani
Wamo wadini wangini:
Kwa hao Ali Hassani,
Rais wa Watanzania,
Kikosa kakoselewa,
Husema kaonelewa,
Ati wanamshutumu
Kwa kuwa ni Mwislamu.

(101) Wamo n'akina Borisi
Yeltisini wa Urusi,
Hawa ndio marubani
Walioshika usukani.

(102) Hizi pilika pilika
Za kutenga Tanganyika,
Ni kutafuta nafasi
Za kupata Uraisi.

(103) Hawa wakifanikiwa,
Walitakao likawa,
Wabunge tahadharini,
Hasa wale wapinzani!

(104) Wamo na watu wajinga,
Wanodhanai wakitenga
Tanganyika iwe pake,
Ina Serikali yake,
Nchi haitavunjika,
Ila itaimarika.

(105) Wangasema hawataki
Kutuletea hilaki,
Bali kwa ujinga wao
Tukaangamizwa nao,
Wao na wanoania
Wote ni wamoja pia,
Na njia ya jahanama
Imejaa nia njema.

(106) Wamo na waso wajinga
Wanokusudia janga,
Ila wao wanadhani
Sisi ndio punguani.

(107) Kwa ulozi wa maneno
Ati "ndani ya Mwungano",
Watulaze usingizi,
Walete maangamizi.

(108) Mumo humo pia wamo
Wasio na msimamo,
Wanofuata mkumbo
Kwa hili na kila jambo.
(109) Upepo uvumiako
Ndiko nao waendako,
Kwao hiki ni kimbunga,
Ni hatari kukipinga!

(110) Hawa ni watu hatari,
Utamboni tahadhari,
Kitali kikizidia
Mara watakukimbia.

(111) Wamo walopungukiwa
Au kuchanganyikiwa,
Waliomo behewani
Bila kujua kwa nini.

(112) Wamo behewani humo
Wenye dhiki na urumo,
Wanodhani watashiba
Tukitana na Zanziba.

(113) Wamo na wengine tena,
Watu aina aina
Kiwauliza sababu,
Hawana la kukujibu.

(114) Wamo na watu wabaya,
Wawi, wana wa hizaya,
Ni watu wanochukia
Umoja wa Tanzania,
Sasa wamepata mwanya
Ili kutuparaganya.

(115) WOTE, na wasowania,
Watavunja Tanzania,
WOTE, na watoumia,
Wamo wanashangilia.

(116) Wanabomoa misingi,
Na sisi hatuwapingi,
Tubaki ni kunyamaa
Na kushikilia paa,
Jumba litapoomoka,
Nani atasalimika?

****************

(117) Sasa wana hoja nyemi
Ya kutaka kujihami,
Ni hoja ya kudanganya
Na kutaka kujiponya.

(118) Wanasema Viongozi,
Ati Chama Hakiwezi
Kukataa sera hino
Ya kuvunja Muungano.

(119) Ati Serikali mbili
Sasa ni sera batili:
Maana Bunge la watu
Limetaka ziwe tatu.

(120) Chama kisipobadili
Hiyono sera batili,
Kitapinga Bunge lake
Pia Serikali yake.

(121) Na hilo, wanatwambia,
Ni kinyume cha sharia,
Siyo halali kwa Chama
Kupinga Bunge la Umma!

(122) Kale twali tukiimba
Wimbo huu wa kasumba:
Furaha kuu, furaha kuu!
Mikono chini, miguu juu!
Twaenda machi, twaenda machi!
Twaenda machi, furaha kuu!

(123) Hizi hoja za Wakuu,
Za miguu kuwa juu,
Na vichwa vikawa chini,
Wabunge tahadharini.

(124) Siyo zenu hoja hizi,
Ni hoja za Viongozi,
Msizipe uhalali,
Kwani ni hoja batili.

(125) Wabunge wote wa Umma
Asili yao ni Chama:
Wale wa kuchaguliwa,
Na walioteuliwa.


(126) Sera zao za Bungeni
Zatokana na Ilani
Ya uchaguzi wa nyuma
Ulofanywa na kauma,
Na wala si sera zao,
Ni sera za Chama chao.

(127) Na sababu ya Ilani
Ni kutafuta idhini
Ya wananchi wenzenu,
Wakubali sera zenu.

(128) Mkisha pata kibali,
Mtaunda Serikali
Mtekeleze Bungeni
Sera zenu, kwa idhini:
Na wale walowatuma
Ni Chama pamwe na Umma.

(129) Ndiyo ma'na ikasemwa,
Wabunge wakisha tumwa
Wana kauli ya mwisho,
Wasikubali vitisho.

(130) Wamesha tumwa na Chama
Kwa idhini ya kauma,
Atowapinga ni nani,
Ila Chama kipinzani?

(131) Na kwa Chama kipinzani,
Kiloshindwa uwanjani
Kupitisha sera zake,
Kupinga ni haki yake.

(132) Bali kwa ambalo katu
Hamkutumwa na watu,
Wala si la Chama chenu,
Ila ni mawazo yenu,
Hamuwezi mkasema
Kukataliwa na Chama
Si halali, ni haramu,
Na ni kupinga kaumu.



(133) Wanaweza Viongozi,
Baada ya Uchaguzi,
Wakawa wanalo wazo,
Au wana pendekezo,
Wasotumwa na kauma,
Wala si sera ya Chama.

(134) Viongozi bila shaka,
Chama chao watataka,
Kijadili jambo hili
Kipate kulikubali.

(135) Likifanywa sera yao,
Kwa uchaguzi ujao,
Wataandika Ilani
Waliombee idhini.

(136) Endapo wapiga kura
Wataikubali sera,
Ndipo tena Bunge lao
La Umma na Chama chao,
Litakwenda kutimiza
Sera waliyoagiza.

(137) Serikali haiwezi
Kwa hila za Viongozi,
Ikapitisha Bungeni
Sera iso na idhini
Ya Chama wala ya Umma,
Kisha ianze kusema,
Chama kikichamaa,
Sera kikaikataa,
Ati hiyo ni haramu,
Chama chapinga kaumu!

(138) Ni nani alowatuma
Kwa uchaguzi wa nyuma?
Jambo hili ni lao tu,
Hawakutumwa na watu.

(139) Kama wanalo haraka,
Kusubiri wamechoka,
Basi wasiwe ajizi,
Waitishe Uchaguzi,
Ufanywe hata mwakani
Waliombee idhini.

(140) Wanasema linapendwa,
Hawawezi wakashindwa,
Wanachohofu ni nini
Kuliombea idhini?

*****************

(141) Kwa hapa Tanzaniani,
Mwajibikaji ni nani?
Kuajibika halali
Ni Chama kwa Serikali?

(142) Au huko Tanganyika,
Nani atawajibika,
Ni Bunge kwa Chama chao
Na wapiga kura wao?

(143) Au ni Chama na Umma
Kwa Bunge walolituma?
Hiyo ndiyo Demokrasi,
Ya mageuzi halisi?

(144) Nilidhania halali
Ni Bunge na Serikali,
Kuwajibika kwa Umma
Na Chama kilowatuma.

(145) Hii sera ya Wakuu,
Ya miguu kuwa juu
Na vichwa vikawa chini,
Ni ya nani, na ya nini?

(146) Nchi isiwe na Vyama
Vinotetea kauma,
Tubaki na utawala
Na uongozi wa hila;

(147) Na Vyama viwe mihuri
Ya watu wenye kiburi,
Na Viongozi wa hewa,
Wasopenda kukemewa.

(148) Wala msidhani ati
"Kwenda kwenda na wakati"
Kila mara ni halali,
Hata kwa mambo batili.


(149) Hivi Chama SISIEMU
Hakina jambo haramu?
Kila wapendalo watu
Ni kuntu kwa Chama chetu?

(150) Na tuseme, mathalani,
Ya kwamba hapa Tanzania,
Serikali kuwa tatu
Ndiyo matakwa ya watu.

(151) Mtayumba na wakati,
Bila dira bila dhati?
Mkondo uvutiako,
Nanyi mkokotwe kuko?

(152) Sera mpya kila mara,
Kufuata mazingira,
Kama vitenge na kanga,
Au rangi za kinyonga?

(153) Sera zingawa za chuki,
Watu washike mikuki,
Zikisha pendwa na wengi,
Chama hiki hakipingi?

(154) Zingawa za uhasama,
Za sumu katika Umma,
Zikisha pendwa na watu,
Chama hakipingi katu.

(155) Zingazua mapigano,
Zingaleta mauano,
Wengi wakisha zipenda,
Chama hakitazikinda?

(156) Hakisimami imara
Kupinga zenye madhara,
Wengi wakisha zitaka
Na Chama kitazidaka?

(157) Mawi hayawi matamu
Kwa kupendwa na kaumu,
Wala sumu kuwa uki
Kwa kupendwa na malaki.

(158) Hata yaletayo janga,
Hatuwezi kuyapinga?
Yangatukusa balaa
Ni mwiko kuyakataa?

(159) Hata yanobwaga zani?
Yangatwingiza vitani?
Yakisha pendwa na watu,
Kupinga hatuthubutu?

(160) Wengi wakichachamaa,
Watakalo watatwaa,
Ila si kweli kusema
Daima hutaka mema.

(161) Wengi wakisha amua
Mama yako kumuua,
Kwa kuwa wao ni wengi,
Utashiriki, hupingi?

(162) Pindi zianzapo nyimbo
Za kugawana majimbo,
Chama hiki yumbayumba
Kitaanza kuziimba?

(163) Huo ndio uongozi
Wa Chama cha Mapinduzi?
Chama cha wapenda vyeo,
Wasio na mwelekeo?

(164) Sharia yao matumboni,
Kwa hili na kila jambo?
La msimamo hawana,
Huuza hata wanina?


***************

(165) Yako mambo ya msingi,
Yasotegemea wingi,
Yanotoka msimamo,
Wengi wangawa hawamo.

(166) Ungabaki peke yako,
Kupinga ni wajibiko,
Ungafa uwe mhanga,
Huna budi kuyapinga.

(167) Na moja ni kama lino
La kuvunja Muungano,
La kujenga uhasama
Katika jamii nzima.

(168) La kuiga Wasomali
Kama watu majuhali,
La kufanya Tanzania
Iwe Yugoslavia.

(169) La kufuata Warusi
Hata katika maasi,
La kuvunja vunja Dola,
Turudie makabila.

(170) LINGAPENDWA NA KAUMU
BADO NI JAMBO HARAMU.

(171) Chama cho chote makini
Kitalipinga kwa kani,
Huo ndio uongozi
Wa Chama kisicho bozi.

(172) Nimewambia wenzangu:
Ningabaki peke yangu,
Nitapinga' Nitapinga
Tanganyika kujitenga!

*****************
(173) Ila narudia tena
Niliyokwisha kunena:
Sera hii, nilisema,
Si ya Umma, Si ya Chama.

(174) Ni Sera ya Viongozi
Wa Chama cha Mapinduzi,
Na waungao mkono
Uvunji wa Muungano.

(175) Chama hiki Mapinduzi
Kimeleta mageuzi:
Si Chama pekee tena,
Viko aina aina.

(176) Na Chama cha Mapinduzi,
Watambue Viongozi,
Ni Chama cha Muungano,
Si Chama cha Utengano.

(177) Kama mwanachama wake
Hazipendi sera zake,
Atoke, asichelewe,
Aanze chake mwenyewe.

(178) Kama Viongozi wetu
Hawapendi sera zetu,
Watoke waende zao,
Waanzishe vyama vyao.

(179) Viko vyama bozibozi
Vyatafuta viongozi,
Waende waviongoze,
Na hiki tukipongeze!

(180) WASITEKE CHAMA NYARA
WAKILAZIMISHE SERA
AMBAZO KATU SI ZAKE,
NI ZA WAPINZANI WAKE.

(181) HASA SERA KAMA ZINO
ZA KUVUNJA MUUNGANO
*************

(182) Hoja ile ya mwanzoni
Ya Wabunge wa Tanzani,
Ilikuwa na sababu:
Na kubwa yali ghadhabu.

(183) Na Dola ilipokiri
Ya kuwa iliathiri
Katiba ya Tanzania,
Wabunge walitulia.

(184) Ndiposa wakabadili
Hoja yao ya awali,
Kutaka referendumu
Ya maoni ya kaumu.

(185) Serikali ikapinga
Kwa sababu za kijinga:
Ikaleta "muafaka"
Wa kutenga Tanganyika.

(186) Sasa tuko ukingoni,
Twachungilia shimoni,
Shime, naturudi nyuma,
Tusiangamize Umma.

(187) Msiseme: "Tumesema,
Katu haturudi nyuma,
Uzi tutashikilia,
Nchi ingaangamia."

(188) Na wenzetu walisema:
"Katu haturudi nyuma,"
Tukafika ukingoni,
Wakageuza lisani.

(189) Uongozi wa kiburi
Sio uongozi wa heri,
Si aibu kujirudi;
Asokosa ni Wadudi.

(190) Hoja hii "muafaka"
Ya kutaka Tanganyika
Ipatiwe Serikali,
Iachilieni mbali.
Itatukusa hilaki
Na nchi haitabaki.

(191) Mambo ya chuki acheni,
Matukano yazileni;
Mkiita mikutano
Iwe ya mshikamano.

(192) Chuki ni kama kichaa,
Mtu zikimpagaa,
Zikamjaa kichwani,
Hatambui afanyani.

(193) Wakuu wetu wa dini,
Na Viongozi Nchini,
Shindaneni mambo mema,
Ya natija kwa kauma,
Maovu msishindane,
Mwisho watu wauane.

(194) Nchi yetu bado changa,
Acheni kuitabanga,
Mkishindana kwa chuki
Mwisho wetu ni hilaki.


(195) "Wala hakuna hilaki
Kama hilaki ya chuki."
(Maneno hayo si yangu:
Ni ya Kitabu cha Mungu.)

(196) Tanganyika mnadhani
Ina mvutano gani
Wenye nguvu kuzidia
Umoja wa Tanzania?

(197) Wa Pwani na wa Unguja
Mkiona si wamoja,
Mtaona wa Mtwara
Ni wamoja na wa Mara?

(198) Wa Pemba mkiwatenga
Na ndugu zao wa Tanga,
Mtaacha wa Tabora
Wadumu na wa Kagera?

(199) Wafipa wa Sumbawanga,
Na Wasegeju wa Tanga,
Wawatenge Waunguja,
Wao wabaki wamoja?

(200) Hivi Waha wa Kigoma
Na Wakurya wa Musoma
Na Wazaramo wa Pwani
Watabaki majirani?

(201) Msidhani Tanzania
Si sawa na Somalia,
Ati mtaitabanga,
Msihiliki kwa janga.

(202) Mbegu mbaya imepandwa,
Lakini hatujashindwa,
Tunaweza kuing'oa
Na Nchi tukaokoa.

(203) Akipendezwa Jalia,
Itadumu Tanzania,
Amina! Tena Amina!
Amina tena na tena!


HITIMISHO

Kikao mchanganyiko
Cha Dodoma huko huko,
Kimesema wazi wazi
Kuwambia Viongozi:

"Serikali kuwa mbili
Si sera ya Serikali,
Bali ni sera ya Chama
Kile kilichowatuma.

Basi kairudisheni
Kwa wenyewe vikaoni,
Wapate kuijadili,
Kibidi waibadili."

Mimi kwa upande wangu
Nawanasihi wenzangu,
Sera wakiibadili,
Tafadhali, tafadhali:
Chama na kilete hoja
Serikali iwe moja.
Amina tena Amina!
Amina tena na tena!

UTANGANYIKA
"Vijana wa Tanganyika hawana haja ya kumbembeleza ye yote wala chombo cho chote kuhusu utaifa wao; wanalijua Taifa lao. Si jingine ni Tanganyika. Tanzania ife, izikwe, ioze. Hatuitaki."

Mimi nawaheshimu kwa dhati kabisa vijana waliotoa kauli hii. Nawaheshimu kwa sababu wana akili, wana ukweli, na wana ujasiri. Wana akili za kutosha kutambua kuwa ukifufua Tanganyika, Tanzania itakufa; wana ukweli unaowazuia kutumia hila za maneno matupu kama "ndani ya Muungano," kudanganya watu wadhanie kuwa unaweza ukawa na serikali ya Tanganyika, na bado Tanzania ikabaki; na wana ujasiri wa kutosha kutamka wazi wazi kwamba wanachokitaka ni kufa, na kuzikwa, na kuoza kwa Tanzania. Watu wa namna hiyo unaweza kuhitilafiana nao, lakini lazima uwasheshimu, kwa sababu ya akili zao, na ukweli wao, na ujasiri wao.

Najua sababu nyingi na matatizo mengi yaliyowafanya baadhi ya vijana na watu wazima wengene wafikie msimamo huu wa kudai Utanganyik. Lakini Tanganyika haitasaidia chochote. Hizi jitihada za kututoa kwenye haja ya kutazama kwa makini sababu halisi za matatizo ya nchi yetu, ili tuseme kuwa sababu za matatizo yetu ni Tanzania, na dawa yake ni Tanganyika, ni jitihada za kunywesha watu kasumba. Na wako Wazalendo tele wenye akili, na ukweli, na ujasiri, ambao watakataa wazi wazi kunyweshwa kasumba hiyo.
Sababu zile zile zitakazoua Tanzania zitaua Tanganyika. Tanzania haiwezi kwenda na wakati, na Tanganyika isiende na wakati huo huo pia. Vijana wanatambua la kwanza, na hiyo ni hatua kubwa ya kuelewa; kosa lao ni kutotambua la pili pia. Lakini hawa ni vijana. Watu wazima hawana sababu ya kutoona yote mawili; kwamba Tanzania ikifa, na Tanganyika itakufa, kwa sababu zile zile. Kinachoshangaza zaidi ni kwamba hata lile la kwanza, ambalo vijana wanaliona wazi wazi, watu wazima, wakiwamo na viongozi, wao hawalioni; au wanaliona lakini hawana ukweli na ujasiri wa vijana hawa kukiri hivyo.

***********************

SERIKALI YA TANZANIA ni Serikali ya Muungano;
BUNGE LA TANZANIA ni Bunge la Muungano;
CHAMA CHA MAPINDUZI ni Chama cha Muungano.
Vyombo vitatu hivi vikishirikiana kuiua na kuizika Tanzania, adui wa Tanzania atafanya kazi gani? Swali hili nilikuwa nikiliuliza kuhusu viongozi wa Urusi. Watu hawa wanfanya mambo ambayo ni dhahiri kwamba watavunja nchi yao. CIA ya Marekeni wanaiachia kazi gani?

Nasi twaiga Warusi
Hata katika maasi,
Tuivunje vunje Dola,
Turudie makabila?

BUNGE DHIDI YA CHAMA

Ziko jitihada sasa hivi za kugombanisha Wabunge na chama chao kwa kutumia hoja ya hadhi ya Bunge. Ni nani huyu anayefanya kazi hii? Ni haki kabisa ya vyama vya upizani kujaribu kugombanisha Wabunge wa chama kinachotawala na chama chao. Lakini viongozi wa chama kinachotawala pamoja na Serikali yenyewe wanapojaribu kufanya mambo ambayo yatagombanisha Wabunge wa CCM na chama chao, tuna haki ya kuwauliza viongozi hao wanafanya kazi hii kwa niaba ya nani, na chama chao ni chama gani?

Nasema, vyama vya upinzani vinapotumia mbinu kama hii kukiparanganya chama kinachotawala, tunaweza kusema kuwa ni mbinu halali. Ni hiari ya wanachama wa chama kinachotawala kuikataa mbinu hiyo na wakabaki imara, au kuikubali, na wakaparanganyika na kuvipa ushindi na kicheko vyama vya upinzani.
Lakini vyama vya upinzani vikijaribu kutuambia kuwa mbinu hizi wanatetea msingi fulani wa kidemokrasia, na haki na hadhi ya Bunge, hatuna budi tuonye kuwa wanapotea, na wanajaribu kufundisha msingi ambao kwa kweli ni hatari kabisa kwa demokrasia.
Bunge la Tanznaia linaweza kwa njia halali kabisa, likapitisha sheria, kwamba tangu sasa gharama zote za kusomesha watoto zitabebwa na wazazi wao. Sheria hiyo, kama inatokana na ilani ya uchaguzi uliopita, itakuwa ni sheria halali kabisa. Imepitishwa na Bunge la Taifa, kwa kutumwa na wananchi waliopiga kura na kukipa ushindi chama chenye sera hiyo.

Hivi kweli vyama vyetu vya upinzani vinatuambia kuwa sheria hiyo ikisha kupitishwa, vyama vingine vyote vyenye sera tofauti vitalazimika kufuta sera zao? Maana bila kufanya hivyo vitakuwa haviheshimu Bunge la Taifa, na ni kinyume cha demokrasia wanayoijua wao? Mimi nitaogopa kabisa vyama vyenye imani potofu namna hiyo kuitawala nchi yetu.
Kinaweza leo kikazuka chama ambacho kinaona kuwa nchi yetu ingeongozwa vizuri zaidi kama Mkuu wa nchi yetu angekuwa ni Mfalme badala ya kuwa Rais. Bado chama chenye maoni kama hayo kitakuwa ni chama halali kabisa, na maoni yake yatakuwa ni halali kabisa, hata kama Katiba ya nchi yetu, ambayo imepitishwa na Bunge la Nchi yetu, inasema kuwa nchi yetu ni jamhuri. Maana kama ingekua si hivyo, na kama ingekuwa ni kweli kwamba jambo likisha kupitishwa na Bunge haifai kulipinga, maana kufanya hivyo ni kinyume cha demokrasia, basi haya maoni ya serikali tatu yanatoka wapi?
Maana kwa Katiba yetu ya sasa, muundo wa Jamhuri ya Muungano ni wa serikali mbili. Na muundo huo umepitishwa na Bunge la Taifa letu, na kuthibitishwa juzi juzi tu, na Bunge hili hili. Kama ni haramu kuhoji maoni tu ya Wabunge, hata kama wangekuwa ni wote kabisa pamoja na serikali yao, na bila "janja janja" ndani yake, wenye maoni hayo wana uhalali gani kwa kuhoji Katiba, ambayo si maoni bali ndiyo sheria kuu ya nchi yetu?

Mimi nasema kuwa wanayo haki hiyo na uhalali huo. Lakini wanajiuvua haki hiyo kwa kutumia hoja za kijinga. Ati Bunge likisha tamka maoni yake, hata kama maoni hayo hayana uzito wa sheria, vyama vyote, pamoja na chama kinachotawala, lazima viyaheshimu maoni hayo au sheria hiyo, na vifute sera zao, hata kama uamuzi wa Bunge au Wabunge ni kunyume cha sera zao. Na hata kama Wabunge hawakutumwa na wapiga kura kupitisha sheria hiyo. Hivi nyinyi mnafikiri udikteta unaanzaje?

NA WOTE mwashangilia,
Hata mtauoumia!

VYOMBO VYA DOLA

BUNGE Ni Chombo cha Dola: Kazi yake ni kutunga sheria za nchi.

SERIKALI Ni chombo cha Dola: Kazi yake ni kuongoza nchi kwa mujibu wa Katiba na sheria nyingine za nchi kama zilivyopitishwa na Bunge.
MAHAKAMA Ni chombo cha Dola: Kazi yake ni kutoa tafsiri ya sheria za nchi, pamoja na Katiba yake kama zilivyopitishwa na Bunge. Kazi hii hufanywa Mahakamani kwa njia ya kawaida ya kuhukumu watu wanaoshutumiwa kuwa wamevunja sheria za nchi.
Ni kanuni moja kubwa demokrasia kwamba vyombo hivi visiingiliane katika kazi zake. Chombo kimoja kisijaribu kufanya kazi ambayo si yake, ni kazi ya chombo kingine.

VYOMBO VYA JAMII

VYAMA VYA SIASA: ni vyombo vya jami, si vyombo vya Dola. Kazi yao ni kuunda na kuelezea sera wanazotaka zikubaliwe na jamii. Ni kanuni moja ya demokrasia kwamba kazi hiyo ifanywe na vyombo hivyo vya jamii; isifanywe na chombo cha Dola au mchanganyiko wo wote wa vyombo vya Dola. Jitihada na hoja zote za kujaribu kuhamisha kazi hii itoke katika vyombo vya jamii, na ifanywe na vyombo vya Dola, ni jitihada na hoja za kujenga udikteta!

Viongozi wa chama kinachotawala wanajaribu kutumia nguvu za Dola kukilazimisha chama chao wenyewe kibadili sera yake wasiyoipenda. Viongozi hao wakifaulu, "walitakalo likawa," mnadhani kuwa sera za vyama vya upinzani ndizo watakazoheshimu? Na la kushangaza ni kwamba:
WOTE, na watoumia,
Wamo wakishangilia!

Mimi nakishukuru sana kikao cha mchanganyiko wa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Wabunge wa Jamhuri ya Muungano, na Wabunge wa Baraza la Wawakilishi, kilichofanyika Dodoma hivi majuzi, kwa kukubaliana kwa kauli moja kulirudisha suala hili la sera ya CCM mahali pake: yaani kwa wanachama na vikao vya Chama cha Mapinduzi.

CHAMA CHA MAPINDUZI ni chama cha Muungano;
SERA YA SRIKALI MBILI ni sera ya Muungano;
MWELEKEO WA CCM ni mwelekeo wa Muungano.

CHAMA CHA MAPINDUZI kitakapobadili sera yake ya Muungano wa serikali mbili, sera yake mpya itakuwa ni sera ya Muungano wa serikali moja. Chama cha Mapinduzi chenye wanachama wenye akili, na ukweli, na ujasiri, hakiwezi katu kukubali sera ya serikali tatu, kikijua wazi wazi kwamba matokeo na shabaha ya sera hiyo ni kuiua, na kuizika, Tanzania. Chama cha Mapinduzi kikiwa na msimamo huo, na wala kisiuonee haya, Tanzania itadumu.

Mbegu mbaya imepandwa,
Lakini hatujashindwa,
Tunaweza kuing'oa,
Na nchi kuikoa.

Akipendezwa Jalia,
Itadumu Tanzania,
Amina! tena Amina!
Amina tena na tena!

16, Nov 1993
 
Yericko Nyerere njoo usikie urithi wa busara za Mwalimu kwa watanzania
 
kwa nini hamuwaagizi zanzibar ambako wawakilishi wa ccm ni wengi waibadili katiba yao iwe kama awali?
 
Katiba ya Zanzibar haijavunja muungano kama ambavyo CHADEMA na CUF wanavyotaka kuua muungano wetu.
 
Nikifikiria Mwalimu Nyerere alivyotulisha sukariguru kwa kukosa sukari huwa hata sina hamu ya kusoma maandiko yake
 
Ingawa sipingani na hii hoja bali nakerwa na mtindo wa Manyerere yaani yeye ni mwepesi sana kuleta jukwaani hoja za gazetini kwake (JAMHURI) na tunajikuta wote tunalisoma bila kujali tunalipenda au hatulipendi, tmelinunua au la. Hii habari imetoka gazetini kwake leo.

Lakini yeye ukimshtua asome habari fulani kama imetoka gazeti jingine anakujibu kwa kifupi "Mimi gazeti langu ni JAMHURI"!!!

Manyerere,
Habari ni habari na si lazima tununue au tusome gazeti lako. Usipopenda ujulishwe kilichotokea kwa magazeti menzako, basi usimamie msimamo wako na wewe usitulazimishe kijanja kusoma lako kutuletea mitandaoni kwa sababu tu tumejiunga kwenye mitandao kama Jamii Forum na mingine.

Cc: Manyerere Jackton
 
Katiba ya Zanzibar haijavunja muungano kama ambavyo CHADEMA na CUF wanavyotaka kuua muungano wetu.

kijiita nchi hawajavunja muungano?mbona ccm hamna mapendekezo ya serikali moja kama nyerere alivyosema?
 
ikishindikana tutafanya hivyo

nyerere alisema ni serikali mbili kwenda moja na sio kwenda tatu maana yake vision ni moja, sasa miaka inaenda mbona mnataka mbili hizo hizo? ambazo mpaka ccm zanzibar wanawasaliti?kwa nini msingeweka msimamo sasa ni moja kuondoa usaliti#?
 
Sera ya CCM ni serikali 2 kuelekea serikali 1 according to Julius Nyerere. Je CCM imekumbwa na nini? Wakati huu tunapotengeneza katiba mpya kwanini hili la SERIKALI MOJA CCM hawalizungumzii kabisa. Je hiyo sera ya SERIKALI MOJA ni KIINI MACHO TU CHA CCM?! Naomba wale ambao mnaweza to put two and two together ndiyo mnijibu. Wengine msioweza nipotezeeni.
 
Back
Top Bottom