Juhudi za Mkurugenzi Kivulini Mwanza zaleta manufaa

Nyanswe Nsame

Senior Member
Jul 9, 2019
158
175
Juhudi za Mkurugenzi Kivulini Mwanza zaleta manufaa.

JUHUDI zinazoendelea kufanywa na Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la kutetea haki za watoto na wanawake mkoa wa Mwanza, Yasin Ally zimeanza kuzaa matunda.

Mkurugenzi huyo, amekuwa mdau mkubwa katika shughuli za maendeleo kwenye Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza hususani ni shule ya sekondari ya Ibinza.

Juhudi hizo za Yasin zimefanikisha kukamilika kwa ujenzi wa chumba kimoja cha darasa katika shule hiyo, hatua iliyochangia kupunguza uhaba wa vyumba vya madarasa shuleni happy.

Yasin Ally, akizungumza leo katika hafla fupi ya kuwapongeza wanafunzi wa kidato cha tatu wa shule ya sekondari ya Ibinza kwa kufanya vizuri kwenye mtihani wa kitaifa wa kidato cha pili, aliwahimiza wazazi kuamka na kuchangia shughuli za maendeleo.

Yasin ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, aliendelea kuwaomba wazazi na walenzi wa wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo kuwa na utamaduni wa kuchangia shughuli za maendeleo kwani itasaidia watoto wao kusoma na kufanya vizuri darasani.

Alisema, yeye kwa muda mrefu amekuwa mdau mkubwa wa maendeleo katika shule hiyo, kwani tayari amefanikisha kukamilisha kwa ujenzi wa chumba kimoja cha darasa.

Alisema kutokana na yeye kufanya kazi kubwa ya kuhakikisha darasa hilo linakamilika, amewaomba wazazi na walenzi ambao wamejitokeza katika hafla hiyo, kumalizia darasa moja lililobaki.

Yasin alisema, kwa hali ya sasa urithi pekee uliobaki kwa mtoto hususani ni mtoto wa kike ni elimu huku akidai wazazi wanapaswa kuwakwamua watoto wa kike kwa elimu bora.

"Mwaka 2017 kipindi mimi nakuja hapa nilikuta ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha pili upo kwa asilimia 94 lakini kwa sasa (2019) ufaulu umeongezeka na kufikia asilimia 97 ni hatua kubwa.

"Kwa sasa shule hii imefanya vizuri kutoka nafasi ya 15 kati ya shule 25 mwaka 2017 hadi nafasi ya tatu kati ya 25 mwaka 2019 kwa shule zote za Wilaya ya Ilemela ni hatua kubwa," alisema Yasin.

Hata hivyo, pamoja na kuzungumzia suala la ufaulu wa wanafunzi na maendeleo ya shule hiyo, pia amezungumzia tabia ya wazazi na walezi kushindwa kuwaangalia vizuri watoto wao.

Alisema kwa sasa wazazi wengi wameshindwa kutoa malezi mazuri kwa watoto wao na kusababisha watoto kujilea (kujihudumia) jambo ambalo alidai linachangia kuendelea kuwepo kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Alisema ubize wa wazazi umekuwa chanzo kikubwa cha watoto wa kike kuendelea kufanyiwa ukatili pamoja na kuongezeka kwa mimba za utotoni.

Yasin alisema kwamba mkoa wa Mwanza ni miongoni mwa mikoa yenye kiwango kikubwa cha ukatili wa kijinsia, ambapo Mwanza ikiwa na asilimia 60 ya ukatili wa kijinsia.

Pia Yasin aliwaomba wazazi kwa kusema kwamba, migogoro yao ya ndoa ya mume na mke, isihamie kwa watoto kutokana migogoro hiyo kuwaathiri na kusababisha watoto kushindwa kufanya vizuri kwenye masomo yao shuleni.

Awali akisoma risala kwa mgeni rasmi, Julieth Samwel, Mwanafunzi wa kidato cha tatu, alisema kwamba shule hiyo inakabiliwa na upungufu wa vyumba vya madarasa.

Alisema kuwa endapo vyumba hivyo vitapatikana, kimoja kitatumika kwa ajili ya wanafunzi kusomea huku kingine akieleza kitatumika kwa ajili ya maktaba ya kujisomea wanafunzi wote.

Afisa elimu kata ya Ibinza, Daud Gabriel aliwataka walimu wa shule hiyo kuongezeka mikakati zaidi ili kuhakikisha shule hiyo inafanya vizuri katika masomo yao ya kidato cha pili na nne.

Katika matokeo ya kidato cha mwaka huu, jumla ya wanafunzi 195 walifaulu mtihani huo ambapo wavulana ni 106 wasichana 89 huku sita wakifeli.

Kwenye ufaulu huo, daraja la kwanza wanafunzi 33, daraja la pili 31, daraja la tatu ni 40 na daraja la nne wakiwa wanafunzi.

Mwisho
 

Attachments

  • IMG20200207115348.jpg
    IMG20200207115348.jpg
    153.5 KB · Views: 2
  • IMG20200207122341.jpg
    IMG20200207122341.jpg
    111.7 KB · Views: 2
  • IMG20200207125412.jpg
    IMG20200207125412.jpg
    148.7 KB · Views: 2
  • IMG20200207115512_01.jpg
    IMG20200207115512_01.jpg
    146.8 KB · Views: 2
  • IMG20200207115450.jpg
    IMG20200207115450.jpg
    193.6 KB · Views: 2
Back
Top Bottom