JOKATE: Utajiri na Utalii wa Kihistoria Uliopo Kisarawe

Mathayo Fungo

JF-Expert Member
Nov 13, 2018
319
510
Imeandaliwa Na:

Jokate Urban Mwegelo
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe

Kennedy Muhoza
Afisa Utalii Kisarawe

Wa ukae, Jumamosi ya tarehe 28/07/2018 majira ya saa kumi alasiri, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliniteua kuwa Mkuu wa wilaya ya Kisarawe. Hakika ilikuwa siku ya kihistoria kwangu, hasa kwenye safari yangu ya kisiasa na uongozi nchini. Uteuzi huu umenipa nafasi ya kutumia na kuonesha vipaji vyangu vya kiuongozi. Sikuwahi kudhania kuwa ipo siku nitakuwa mkuu wa wilaya, ilikuwa ni siku njema. Ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa mapenzi yake kwangu na pia ninaendelea kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuniamini. Mengine mengi juu ya siku hii adhimu nitaongelea siku nyingine, nikiwiwa.

Nikiri wazi, sikuwahi kufika Kisarawe kabla ya uteuzi wangu. Hivyo basi, kabla ya kula kiapo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo wilayani Kibaha tarehe 03/08/2018, nilijaribu kufanya utafiti kidogo kwa kushirikiana na timu yangu ya kipindi kile katika kujaribu kutengeneza vipaumbele ambavyo ningeanza navyo mara baada ya kuanza kazi rasmi. Wajumbe kadhaa walifika mpaka Kisarawe na kuhoji wananchi mbalimbali sambamba na kujionea mazingira kwa ujumla. Moja kati ya vitu tulivyoweza kuibuka navyo ni utajiri wa historia na vivutio vya kiutalii vilivyopo ndani ya wilaya ya Kisarawe.

Nilianza kazi rasmi tarehe 06/08/2018, kwa bahati na kwa mapenzi ya Mungu, siku hiyo kazi niliianzia msituni hivyo nilipata nafasi ya kuanza kuiona Kisarawe na utajiri wake. Tuliingia hifadhi ya msitu wa Ruvu Kusini, hii ni hifadhi ya msitu ambayo ni kubwa zaidi kwenye ukanda huu wa pwani ikiwa na ukubwa wa hekta 30,633. Mbali na hifadhi ya msitu wa Ruvu Kusini, Kisarawe pia imebarikiwa kuwa na hifadhi zingine tatu za misitu; hifadhi hizi ni Pugu, Kazimzumbwi na Masanganya. Tukumbuke kuwa hifadhi hizi za misitu na hasa hifadhi za msitu wa Pugu na Kazimzumbwi ndizo zinazosaidia kuchuja hewa ukaa iliyopo katika jiji la Dar es Salaam ambalo lipo karibu sana na wilaya ya Kisarawe, hivyo utajiri wa Kisarawe una maana kubwa kwa nchi yetu. Siku hii ilikuwa ni nafasi muhimu kwangu ya kujithibitishia utajiri uliopo katika wilaya ya Kisarawe na jinsi gani tunaweza kuibua fursa mbalimbali za maendeleo na hasa kwenye sekta ya utalii ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa katika pato la taifa na kuingiza fedha za kigeni.

Ijumaa ya tarehe 29/05/2020, ikiwa imepita mwaka moja na miezi kumi tangu nilipoteuliwa na Mhe. Rais, nikiwa na timu ya chama cha waongoza utalii kusini tuliamua kufanya ukaguzi wa barabara kuelekea hifadhi mpya ya taifa ya Mwalimu Nyerere na pia kujaribu kuibua fursa za kiutalii njiani. Katika hili naomba kupigia chepuo kidogo barabara hii; barabara hii ndio njia fupi zaidi takribani kilometa 155 kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimaitaifa wa Julius Nyerere kwenda kwenye geti la Mtemere Mloka, Rufiji kuingia kwenye mradi wa kufua umeme wa bwawa la Nyerere na kwenye Hifadhi mpya ya Taifa ya Mwalimu Nyerere. Hivyo, kama viongozi wa wilaya kwa kushirikana na wenzetu kutoka TANROADS tumekuwa tukifanya jitihadi mbalimbali za kuboresha viwango vya barabara hiyo ikiwa ni pamoja na kuifungua tena rasmi hii barabara kuanzia November 2018 ili iweze kuanza kutumika. Haya turudi kwenye safari yetu, moja ya sehemu tulizosimama ilikuwa ni Boga; Boga ni kata mpya iliyozaliwa kutoka katika kata kongwe ya Maneromango. Katika kata hii ya Boga kuna sehemu wenyeji wanachonga vinyago kwa kutumia miti ya mpingo inayopatikana mbele kidogo kwenye eneo moja linaloitwa Boga Sangamzelu. Pamoja na kuchonga vinyago, kuna huduma ya chakula cha asili ambacho ni kivutio kizuri kwa watalii wanaopita hii njia kuelekea kwenye hifadhi ya taifa ya Mwalimu Nyerere.

Katika ziara hii, sehemu iliyonisisimua zaidi ni eneo la Mtunani ambapo kuna mlima na bonde kubwa sana. Ukiwa sehemu ya juu kabisa ya mlima ukitazama upande wa Kusini Magharibi unaiona wilaya ya Rufiji na bonde lake, upande wa machweo (magharibi) na upande wa Kaskazini Magharibi ni bonde la Selous na Mkoa wa Morogoro unaona mpaka milima ya Uluguru. Hakika inavutia mno! Sasa leo naomba nielezee kidogo historia nzuri sana niliyoikuta kwenye huu mlima ambao ni chimbuko la maeneo maarufu kama Shule ya Kibasila Dar es Salaam, Kikosi cha Jeshi Kibasila Kisarawe na eneo la Kamata jijini Dar es Salaam.

Historia inaeleza kuwa kijiji cha Kisangire kilikuwa na tawala ya kimila iliyokuwa chini ya kabila la Kizaramo. Kisangire kabla ya kuja Mjerumani mtawala alikuwa Chifu Kibasila, kipindi cha vita ya Majimaji iliposhika kasi wajerumani walikimbilia Rufiji na huko walitembea pori kwa pori na kufika kijiji cha Kisangire hapo ndipo walikutana na Chifu Kibasila ambaye alikuwa na utawala wake katika kijiji hicho. Historia inaeleza kuwa Chifu Kibasila alikuwa mkarimu mno hivyo alimkaribisha Mjerumani katika himaya yake. Chifu Kibasila kwenye eneo lake alipanda miti ya aina mbalimbali ikiwemo miembe, minazi, mikungu na miti mingine ya matunda, pia shughuli za kilimo ziliendelea kwenye mashamba ya Chifu huyo yaliyokuwepo katika himaya yake.

Historia inaonesha kuwa kilichomfanya Mjerumani kufika Kisangire akitokea Utete Rufiji wakati Vita vya Majimaji imepamba moto ni kutokana kuwa eneo la Kisangire lilikuwa mlimani hivyo kwa Wajerumani Kisangire lilikuwa eneo muhimu kwao kwa mikakati ya kivita. Tukumbuke kuwa vita vya Majimaji iliongozwa na viongozi wa kimila kama Kinjeketile Ngwale na wengineo. Mjerumani alipofika kijiji cha Kisangire aliomba hifadhi kwa Chifu Kibasila naye alimkubalia, baada ya kukaa muda mrefu Mjerumani alianza kuita Wajerumani wenzake waje eneo la Kisangire. Hapo ndipo mvutano kati ya Chifu Kibasila na Wajerumani ulipoanza na hatimaye Chifu Kibasila kushindwa na hivyo akaamua kuikimbia himaya yake kutokana na kuzidiwa mbinu za kivita na Wajerumani.

Mjerumani akaanza kutawala kwa nguvu kwa kutoza kodi ya kichwa kwa wananchi, na kama mwananchi alishindwa kulipa kodi ya kichwa alikamatwa na kulazimishwa kufanya kazi ngumu au kuchapwa viboko 25 kwa kutumia kiboko kilichotengenezwa kwa ngozi ya kiboko. Kiboko hicho kiliitwa “Henzerani” ambapo historia inaeleza kuwa kiboko hicho kikifika kwenye mwili wa mtu kilikuwa kinatoa na nyama katika mwili wa mtu huyo. Kitendo cha watu wa Kisangire kuchapwa viboko kuliongeza mgogoro kati ya Mjerumani na Chifu Kibasila.

Japo Chifu Kibasila alijiimarisha na alionesha upinzani mkubwa, Mjerumani alifanikiwa kutawala eneo hilo la Kisangire na kujenga ngome yake iliyokuwa na mahandaki ya kujificha yeye na askari wake wakati wa vita. Inaelezwa kuwa baadhi ya mahandaki yalichimbwa na kutokea Utete, Rufiji. Mjerumani alijiimarisha akajenga makazi yake vizuri akawa na mahabusu, sehemu ya kuabudia, na mti wa mwembe uliotumika kunyongea wale waliopinga utawala wake. Mwembe huo ulikuwa maarufu kama mwembe kinyonga ambapo wale waliondelea kukaidi amri alizotoa Gavana wa Kijerumani wakati huo walikatwa vichwa mbele za watu na wengine walinyongwa.

Ili kujiimarisha zaidi, Mjerumani akamua kujenga daraja kwa kuunganisha milima miwili kwa mawe na vifusi. Wananchi walilazimishwa kujenga daraja hilo lililounga milima miwili kwa mateso makali sana.

Wananchi waliamua kuliita daraja hilo “Daraja la Mungu” kwa sababu ya mateso makali waliyoyapata. Walipokuwa wakifanya kazi, jioni baada ya kumaliza kazi za siku hiyo walilipwa ujira wa pesa rupia mbili, pesa hizo zote zilitumika kulipa kodi ya kichwa kwa Mjerumani huyo huyo.

Historia ya Chifu Kibasila haikuishia hapo, bado aliendelea kupambana kwa muda hadi pale watawala wenzake walipomgeuka. Maliwali walionunuliwa na Mjerumani wakamgeuka Chifu Kibasila na hivyo kumpelekea taarifa za uongo Chifu Kibasila kuwa -Mjerumani anataka tukae chini tukubaliane ili tuache vita- kumbe hawa maliwali ambao majina yao yalikuwa Kiwambwa na Chaurembo walikuwa wamenunuliwa na yeye pasina kujua alikubali ombi hilo la kukutana na Mjerumani. Hivyo ndivyo Chifu Kibasila alivyokamatwa na kupelekwa Dar es salaam eneo la KAMATA ili anyongwe. Jina hilo la KAMATA limetokana na kukamatwa kwa Chifu KIBASILA na kunyongwa Dar es Salaam katika eneo hilo. Kwa heshima ya Chifu Kibasila palianzishwa Shule ya Sekondari Kibasila katika jiji la Dar es salaam, na kambi ya Jeshi ya JWTZ ya Kibasila Kisarawe ambavyo vyote bado vipo hadi leo.

Utawala wa Mjerumani uliimarika sana pale Kisangire hadi Vita ya Kwanza ya Dunia kati ya mwaka 1914 hadi 1918. Kwa wilaya ya Kisarawe kambi kubwa ya Mjerumani ilikuwa Kisangire. Wakati wa vita hiyo ya Kwanza Mwingereza alipambana vikali na Mjerumani lakini ngome ya Kisangire ilikuwa haingiliki kutokana na eneo ilipojengwa ngome hiyo sambamba na uhodari wa askari wa Mjerumani. Mwingereza aliomba msaada kutoka maeneo mengi lakini hakuweza kushinda vita katika eneo hilo ndipo kamanda wa Waingereza bwana Hugh Charles Clifford (Alifariki 15.11.1916 kamanda huyu) alipoungana na Wazaramo wa Mtunani kuishambulia ngome ya Mjerumani Kisangire. Wananchi hao walimsaidia kamanda huyo wa Kiingereza kujua njia za maficho zinazoweza kumfikisha kwenye ngome ya Mjerumani. Lakini kabla hawajafika kwenye ngome ya Kisangire walimuonesha kamanda huyo eneo ambalo anaweza akaipiga ngome hiyo akiwa mbali kabla ya kuivamia na kupandisha bendera ya Mwingereza.

Hugh Charles Clifford alitumia guruneti akaliweka kwenye pacha ya mti wa mbuyu uliopo Mtunani na kuishambulia ngome hiyo. Baada ya kujihakikishia kuwa amepiga ngome akaamua kwenda kwa uongozi wa wananchi wa Mtunani kutoa shukrani. Kamanda wa Waingereza alifikiri Mjerumani amekimbia kwenye ngome yake baada ya mashambulizi kadhaa hivyo, kwa bahati mbaya ile anaingia ndani tu kumbe askari wa kijerumani alikuwa amejificha ndipo walipokutana uso kwa uso wakashambuliana na wote wakafa hapo hapo. Waingereza waliona umuhimu kwa askari wao kuzikwa Mtunani kutokana na msaada waliopata kutoka kwa Wazaramo, hivyo walimpasua kamanda Hugh Charles Clifford tumbo wakachukua vitu vya ndani wakazika pale kijijini na mwili waliutia chumvi na kuusafirisha mpaka Uingereza kwa mazishi. Wenyeji baada ya kuona Waingereza wamewapa heshima hiyo waliamua kuunda kitongoji cha Pangala la Mwingereza, neno hili ni la Kizaramo ambalo maana yake ni Kaburi la Mwingereza. Kwa lugha ya Kizaramo Pangala ni ‘Kaburi’, lakini. kutokana na muingiliano wa jamii neno hili limebadilika badala ya kuwa “Pangala la Mwingereza” panaitwa “Panga la Mwingereza.” Kaburi hilo la kamanda Hugh Charles Clifford lipo hadi leo.

Siku ukifika Kisarawe utafurahi kuona mandhari mazuri na historia tamu ya Kisarawe kama hii niliyosimulia leo. Karibu ujionee.

Ila pia kuna la kujifunza kutokana na historia fupi ya Chifu Kibasila.

1. Unaweza kumtendea mtu wema, ukamkarimu lakini wakatumia ule ukarimu kukuumiza.

2. Huu ni msemo wa siku nyingi na hata Mr. Nice aliwahi kuimba- kikulacho ki nguoni mwako, Chifu Kibasila alisalitiwa na wenzake.

3. Waafrika tulikosa mshikamano Chief Kibasila alimkaribisha Mjerumani licha ya vuguvugu la kumkataa huko kusini- ila mwisho wa siku nayeye akashughulikiwa hakukuwa na mshikamano kati ya viongozi wa kimila. Hata leo tunaona jinsi watu wenye nguvu ni rahisi kupenyeza ajenda zao kwasababu ya tamaa ya baadhi ya watu na kukosekana kwa mshikamano na uzalendo. Waafrika hatuwezi kuendelea pasi na mshikamano wa kweli. Tunachosahau ni kwamba kwa kutojitambua kwetu ndio maadui wanapenya na kutumaliza zaidi.

View attachment 1477074View attachment 1477069View attachment 1477070View attachment 1477071View attachment 1477073View attachment 1477075View attachment 1477076View attachment 1477077
1_sUAjZnDUYrsciVMza1wyEw%402x.jpg
1_LVv0TMc495cYgFFTgxJwcg%402x.jpg
1_h6uP0Ltve0pNclaudTApCA%402x.jpg
1_496bNJueLDrjw7akNo-ScQ%402x.jpg
 
Hayo magofu yaliyofunikwa na vichaka ndio historia ya kisarawe....mbona kama pametelekezwa muda..
Ni bora Mh DC akazanie kipaumbele chake cha elimu kwani ameanza nacho vizuri
 
Hayo magofu yaliyofunikwa na vichaka ndio historia ya kisarawe....mbona kama pametelekezwa muda..
Ni bora Mh DC akazanie kipaumbele chake cha elimu kwani ameanza nacho vizuri
Mi nadhani tusijudge kwa picha. . . .ukifika na kujionea kwa macho ndio unaweza ukatoa tathmini nzuri zaidi. Lakini kwa sasa wacha apewe pongezi zake
 
N
Hayo magofu yaliyofunikwa na vichaka ndio historia ya kisarawe....mbona kama pametelekezwa muda..
Ni bora Mh DC akazanie kipaumbele chake cha elimu kwani ameanza nacho vizuri
Najipanga nikatembelee niyaone. Nikaone na kaburi la muingereza. Utalii wa ndani.
 
Back
Top Bottom