Joka Jeusi ana kwa ana na Mange Kimambi

Jokajeusi

JF-Expert Member
Jun 1, 2018
6,305
10,578
Habarini Wakuu.

Tafadhali naomba Wikiendi iishe kwa Mtindo huu.

Masikini haachi kuota ndoto. huota ndoto nyingi za kila namna. Huota akisukuma Mikoko yenye wadhifa. Huota akiishi katika jumba mithili ya Ikulu ya Gadafi. Kwa vile yeye ndiye muotaji basi si ajabu akawa bosi wa ndoto yake. pengine huelewi, namaanisha yeye ndiye tajiri nambari wani. Katika ndoto yake hiyo huamua kuwatesa maadui zake hasa wale waliomchukulia mademu zake, hawezi kuwasahau wale waliomnyanyasa kipindi akiimba "ipos siku yangu". Sasa siku si ndio hiyo imefika acha wakione kilichompata mtema kuni.

Kama walivyo masikini Wengine, Joka Jeusi nilipitiwa na mstari huo wa umasikini. Nilikuwa kijana mwenye kukatisha tamaa. Chumba changu kimoja ambacho muda wote kilikuwa na giza kutokana na kuwa na dirisha dogo kilielezea kinagaubaga ufukara uliokuwa unanipiga. Pamoja na kuwa chumba kilikuwa kidogo huwezi amini nilishindwa kukijaza vitu vya ndani. Kulikuwepo tu na godoro la kulalia la inchi nne kwa sita ambalo juu yake kulikuwako na shuka chafu.

Uchafu unatoka wapi ikiwa Joka Jeusi ni mmoja wa mabrazameni enzi hizo akimeza desa. Joka jeusi aliyeshinda katika mashindano ya Mr. Udsm. Je si huyu Joka Jeusi aliyekuwa akishobokewa na vidosho wa chuoni. Tena nasikia Joka Jeusi alipoenda JoBeji kwa Zuma kwenye Kongamano la kimataifa la vyuo vya Afrika, warembo wote wakizulu walijing'ata kwake. Wengine walichukua mapicha na kutupa huku na huko kwenye mitandao ya kijamii.Nakwambia mitandao ilichafuka haijapata kutokea. Sasa nini kimempata kijana wawatu. Nauliza ni nini hicho?

Ikiwa ninakosa hela ya kula, vipi nipate hela ya kununulia maji ya kufulia mashuka, nguo na kusafisha nyumba. Ule msemo wa mwili ni bora kuliko mavazi ulitimia kwangu. Kuoga tuu ilinibidi nipange bajeti. Maisha yangu yalikuwa zaidi ya Bunge la kipare kwenye bajeti ya mwaka.

Kunguni tayari walishanizoea, na nadhani walianza kufanya jitihada ya kuacha kuning'ata usiku mara baada ya kugundua damu yangu ilikosa virutubisho kwenye miili yao. Mbu pekee ndio waliendeleza mapambano. Zaidi ya yote mbu wa chumba changu walikuwa na tabia ya kupiga makelele ungedhani ni kelele za vuvuzela za washabiki wa simba.

Kurudi kwetu sikutaka, niliapa nitafia katika jiji la Daudi. Ugumu wa maisha na ukosefu wa ajira ulizidi kuniumiza kichwa. Nilifikiri lakini muda ulivyozidi kwenda ndivyo mambo yalivyozidi kuwa magumu. Rafiki niliokuwa nimebaki nao ni wale nisiowajua na ambao hatujawahi kuonana. Rafiki wa mitandaoni huko Jamii Forum. Huko nilipewa heshima kubwa mno kutokana na madini ya kimakinikia niliyokuwa natoa. Pia nilitumainiwa kwa semina mbalimbali za kijasiriamali nikipewa shukrani kama mtu mwenye heshima. Wengine waliniona kama mmoja wa watu wenye pesa, wengine waliniona na kuhisi mimi ni mmoja wa watu wanaomiliki kampuni. Kumbe ni Mlalahoi anyimwaye usingizi na kunguni wakatili na mbu wasio na huruma.

Mkombozi atoke wapi. Mkombozi ni nani hasa. Je ni Elimu hii niliyokuwa nayo niliyosomea kwa kusota vimbwetani kwa miaka mitatu. Je ni Wanasiasa wanaopiga tambo huko kwenye majukwaa na media kila iitwapo leo. Au ni taasisi za kifedha zinazotoa mikopo yenye riba isiyo rafiki kwa watu dizaini ya kina Joka Jeusi. Nilifikiri kidogo kisha nikatabasamu lakini punde tabasamu lilinyauka nywaa! baada ya kukumbuka habari za yule kijana aliye shinda milioni themanini kwenye Kamari ya BIKO. Looh!! Nchi ya viwanda bhana we acha tuu.

Siku moja niliingia Instagram huko ndiko nilipopata Mtu niliyedhani ni Mkombozi wangu. Mtu ambaye pengine alikuwa akiona maisha ninayoishi, maisha ya dhiki na tabu. Nilisoma baadhi ya posti zake nakuona dhamira yake kwa vijana wavuja jasho kama mimi.

"Mambo ni Moto" ulikuwa ni msemo aliokuwa akipenda kuusema mara aanzapo au amalizapo posti zake. Hata wafuasi wake kwa chini waliitikia hivyo hivyo kwenye komenti zao. "Huenda ndio salamu" Nilijisemea moyoni wakati nikiwa nasoma. "Kweli mambo ni moto si kwa njaa hii, na kunguni hawa" Nilijisemea kwa sauti ndogo huku nikicheka kama mtu aliyeumbuka.

"Maandamano ya kumtoa Jiwe" Ndio ujumbe mkubwa alioubeba mwanadada huyo aitwaye Mange Kimambi ambaye alikuwa kiongozi wa maandamano hayo. Jiwe ni nani sasa. Nilijiuliza.
Nami nilijiunga kwenye maandamano ya kimtandao. Watu kuhamasisha, watu kuhamasishwa. Mwendo mdundo hakuna kulala mpaka jiwe litoke. Hofu ilitanda hasa kwa waliokuwa wakifuatilia lakini wale wenzangu na mie wa visimu vya tochi hawakujua kinachoendelea.

Magari ya vita yalijipanga, watu waliovalia kijeshi na wenye silaha waliranda randa huku huku katika viunga vya majiji makubwa yote. Hii ilishtusha wale waliokuwa hawajui na kutaka kujua nini kinachoendelea. Huko kwenye Media napo matamko kadha wa kadha yalitamkwa.
"Ole wa mtu aandamane, nitamkata muguu"
ilikuwa ni sauti ya moja wa wakuu wa nchi. Pamoja na mikwala na vitisho lakini mwanadada Mange aliendelea kuhamasisha wafuasi wake ambao wengi wao si ajabu hajawahi kukutana nao ana kwa ana.

Miezi ilikata, siku zilikimbia na siku iliyotarajiwa ilifika. Usiku wa kuamkia usiku wa tukia nakumbuka ana kwa ana kupitia sijui teleguram(telegram) niliwasiliana na Mkuu wa maandamano nikiwa nipo katika chumba changu cha giza kama cha mpiga picha. Nilihisi kama maandamano yatafanikiwa na Jiwe tukiliondoa basi nitapata kitengo cha TAMISEMI. Taratibu kichwani nilianza kujiona kama mmoja wa makamishina kama si Wakurugenzi baada ya maandamano kufanikiwa.

Usingizi ulinipitia nikiwa katika ndoto za umangimeza kama nilivyosema hapo awali kuwa ndoto za masikini haziishi. Saa Kumi na mbili nilikuwa macho nikiperuzi kuona kama kuna picha limeanza au CD ndio imewekwa. Bado kulikuwa kimya. Niliingia Telegram sijui instagram lakini kulikuwa kimya tuu. Tayari jua lilikuwa limeshafika mbali angani yapata saa nne lakini sikusikia maandamano yoyote.

Mlango wang uligongwa, Kulikoni. Nani aliyekuwa anagonga wakati tokea nihamia hapa kwa Bibi nyau sikuwahi kutembelewa. Mlango uliendelea kugongwa nikaenda kufungua. Kufika niliwakuta wanaume wa nne ambao sura zao zilikuwa ngeni kwangu kama fomula za kifizikia. Waliangaliana kisha walinisalimia wakiwa wamechangamka.

"Tumekuja kwenda kuandamana, wengine wapo Pale Posta"
Aliongea mwanaume mmoja dizaini sura siielewi elewi. Lakini kutokana amesema kuhusu maandamano na mimi nina ndoto ya kuwa Waziri wa Nishati na madini Ilibidi nilazimishe kuielewa sura yake.

Nilivaa na tukaondoka kwenda Posta. Tulipanda daladala na kudondokea Posta mpya. Nilishangaa naingizwa kwenye Gari moja nyeusi yenye vioo vya tintedi. Nilitaka kuwazuia lakini walinikaba na kuniwekea kitu puani na hapo hapo nikapoteza akili.

Nilishtuka nikiwa nimevaa kipenzi changu cha jinsi ambacho nilikikata kama Boxer kutokana na sikuwa na pesa za kununulia nguo za ndani. Sikujua pale ni wapi. Mbele yangu kulikuwa na meza kubwa na kiti. Ukutani kulikuwa na maandishi yenye maneno yaliyoandikwa "Operesheni Butua Butua" . Hofu ilinong'ona moyoni mwangu, mashaka yakanibusu. Huu ndio Ukamishina. Huu ndio Ujenerali, au huu ndio ukatibu wenezi niliokuwa nauhitaji. Masikini Joka.

Aliingia Mtu mmoja aliyevaa nadhifu akiwa na simu ikionyesha watu fulani wakipige kelele. Alinisogelea kisha akaisogeza karibu na macho yangu ili nione.
"Jiwe Goo! Jiwe Goo!Jiwe gooo!!"
Wale watu kwenye video ya simu walikuwa wakiimba kwa kurudia rudia. Nilimuona Pia Mange Kimambi akiimba tena kwa kuinjoi kana kwamba anafanya shouting ya video ya Bongo fleva.

Yule mtu alinyanyuka, akakausha koo kisha akanambia wenzako wanaimbia Marekani wewe unaimbia kwa Mtogole. Vijana bhana kwa nini mnapenda kudanganyika.
" Ni haki yangu kikatiba kuandamana"
Nilimjibu
"Basi andamana"

Mara paaap!! waliingizwa vijana wengine kama ishirini hivi. Hawa walionekana wamechezea kichapo cha kufa mtu. Kila mmoja alionekana analia. Nilimuona kijana mmoja akiwa hana nguo kabisa bila shaka hajui hata nguo ziliondokaje mwilini mwake.

Ndio hivyo tena.
Mange yupo kwa Tirampu mimi nipo korokoroni.

Jioni Njema
 
You got a talent buddy.
Try to meet with Mr Shigongo and the likes to fuel your writing skills into another level.🙌🙌🙌
 
Back
Top Bottom