- Source #1
- View Source #1
- Source #2
- View Source #2
Wakuu nimekutana na video inayosambaa kwa kasi sana mtandaoni ambapo wanaonekana John Mrema na John Mnyika, na Mrema akisikika kuwa atatoa maoni juu ya usafiri huo mara baada ya safari kukamilika lakini kinachonipa utata ni sauti inayosikika katika video hiyo baada ya Mrema ikisema viongozi hao wamesifia huduma za usafiri wa treni ya mwendokasi (SGR) na filamu ya royal tour wakati Mnyika na Mrema hawaonekani wakitoa maoni hayo, Je kuna ukweli wowote hapa?
- Tunachokijua
- Kumekuwepo na video inayosambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii ambayo inawaonesha katibu mkuu wa CHADEMA pamoja na mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano na mambo ya nje wa CHADEMA wakiwa ndani ya treni ya mwendokasi (SGR) ambapo inasikika sauti inayosimulia kuwa viongozi hao wametoa maoni wakisifia huduma za usafiri huo pamoja na filamu ya royal tour.
Baadhi ya madai hayo yamehifadhiwa hapa, hapa, hapa na hapa.
John John Mnyika ni Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambaye mbali na nafasi ya ukatibu Mkuu wa CHADEMA pia amewahi kuwa mbunge wa Ubungo, mwaka 2010-2015, na mwaka 2015 - 2020 alikuwa ni mbunge wa jimbo la Kibamba. Kwa upande wa John Mrema huyu ni mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano na mambo ya nje wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA.
Ni upi uhalisia kuhusu jambo hili?
Ufuatiliaji wa kimtandao uliofanywa na JamiiCheck ulibaini kuwa sauti ya video inayosimulia kuwa viongozi wa CHADEMA John Mnyika pamoja na John Mrema kuwa walisifia huduma za usafiri wa treni ya mwendokasi (SGR) na filamu ya royal tour madai ambayo imebainika kuwa si ya kweli kwani maneno hayo hayakuzungumzwa na John Mnyika na John Mrema ambapo mwanzoni mwa video hiyo inamuonesha John Mrema akisema atatoa maoni yake baada ya kufika mwisho wa safari jambo ambalo halikufanyika.
Kadhalika video hiyo haiwaoneshi John Mrema na John mnyika ambao ni viongozi wa CHADEMA wakizunguzia maoni yao juu ya usafiri wa treni ya mwendokasi (SGR) wala filamu ya royal tour wakati wa safari hata baada ya safari ambapo John Mrema aliahidi angetoa maoni yake baada ya safari kukamilika jambo ambalo halikufanyika.
JamiiCheck imemtafuta John Mrema ili kujua undani wa suala hilo ambapo amekiri kupanda treni hiyo lakini akikanusha kile ambacho kinadaiwa wamekisema.
“Tulipanda kweli treni , ila nilisema nitatoa maoni baada ya safari. Hayo mengine ni ya kwao, ndio maana hawana sauti yetu . Wanafanya propaganda tu”
Vilevile JamiiCheck ilimtafuta mkurugenzi wa Shirika la Reli (TRC) Masanja Kadogosa ili kujua undani wa video hiyo, ambaye alisema video hiyo haihusiani na Shirika la reli kwani haijarekodiwa wala kuchapishwa na Shirika hilo.
Aidha ufuatiliaji wa JamiiCheck ulibaini kuwa kituo cha Televisheni cha EATV kilichapisha habari kupitia ukurasa wake wa Mtandao wa Instagram wakibainisha kuwa viongozi hao wa CHADEMA walipongeza utekelezaji wa mradi wa treni ya mwendokasi (SGR) na kutoa maoni juu ya filamu ya filamu ya royal tour na kuwa hatua hiyo ni ya kipekee katika kuhamasisha utalii, habari ambayo baadaye iliondolewa katika mtandao huo.
Picha ikionesha habari ikiwa kwenye Ukurasa wa Mtandao wa Instagram wa East Africa TV