Joaquim Chissano wins the the Mo Ibrahim Prize for Achievement in African Leadership

BY MTANZANIA DAIMA

Mkapa apata pigo




na Chacha Nyakega



RAIS mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, jana alijikuta akibwagwa katika kinyang'anyiro cha kwanza cha moja ya tuzo zenye hadhi ya juu ya Mo Ibrahim, ambayo ingemwezesha kuvuna kitita cha dola za Marekani milioni tano (karibu sh bilioni sita).
Aliyembwaga Mkapa, ambaye kipindi cha miaka 10 ya urais wake (1995-2005) alikuwa kipenzi cha mataifa makubwa na taasisi zao za fedha na uchumi, ni Rais mstaafu wa Msumbiji, Joaquim Chissano.

Tuzo ya Mo Ibrahim ambayo matokeo yake yalikuwa yakisubiriwa kwa hamu maeneo mbalimbali duniani kwa kuwa ndiyo yenye thamani kubwa kifedha kuliko nyingine yoyote ya kabla yake, ilikuwa ikigombewa na viongozi wakuu wastaafu 13 wa mataifa mbalimbali ya Afrika, akiwamo Mkapa.

Mbali ya fedha hizo Chissano atapata pia kiasi cha dola za Marekani 200,000 kila mwaka zitakazotolewa katika maisha yake yote.

Aidha kwa kushinda tuzo hiyo, Chissano atakuwa na uwezo wa kupata kiwango cha fedha kinachofikia dola za Marekani 200,000 katika kipindi cha miaka 10 ijayo, fedha ambazo zitaelekezwa katika mradi wowote wa kuimarisha utawala bora atakaouchagua mwenyewe.

Vigezo ambavyo vilitumika kumpata mshindi wa tuzo hiyo vilihusisha rekodi ya kiongozi mhusika katika kuendeleza misingi ya utawala bora, upiganiaji wa haki za binadamu na namna alivyoshiriki katika kuiletea nchi yake na Bara la Afrika maendeleo wakati akiwa madarakani.

Viongozi ambao walikuwa wakichuana kusaka tuzo hiyo iliyotolewa kwa mara ya kwanza jijini London jana na Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, ambaye ni raia wa Ghana, ni pamoja na Mathieu Kerekou (Benin), Azali Assoumani (Comoros), Domitien Ndayizeye (Burundi) na Henrique Rosa (Guinea Bissau).

Wengine ni Maaouya Ould Sid'Ahmed Taya (Mauritania),
Joaquim Chissano (Msumbiji), Sam Nujoma (Namibia)
Benjamin Mkapa (Tanzania), Abass Bonfoh (Togo)
Gnassingbe Eyadema (Togo), Bakili Muluzi (Malawi)
France-Albert Rene (Shelisheli) na Abdiqassim Salad Hassan (Somalia).

Chissano, mtu aliyekuwa akipewa nafasi kubwa ya kuchukua tuzo hiyo alikaa madarakani kwa miaka 19, na katika kipindi hicho akachukua hatua mbalimbali zilizosaidia kumjenga kisiasa kitaifa na kimataifa.

Miongoni mwa masuala yaliyomjengea umaarufu mkubwa ni pamoja na namna alivyoweza kumaliza vita ya wenyewe kwa wenyewe kati ya serikali yake na Chama cha upinzani cha Renamo kinachoongozwa na Alfonso Dhlakama.

Aidha, katika kipindi chake cha urais, Chissano, anatajwa kuwa rais aliyeweza kusimamia vyema rekodi ya kukuza uchumi wa taifa lake, sambamba na kuheshimu haki za binadamu.

Wakati Chissano akiweka rekodi hizo, Mkapa analaumiwa kwa kushindwa kumaliza mgogoro wa kisiasa uliodumu kwa zaidi ya miaka 10 Zanzibar, ingawa amekuwa akisifiwa kwa kukuza uchumi wa Tanzania.

Aidha, katika siku za hivi karibuni, Mkapa amekuwa akituhumiwa kutumia madaraka yake vibaya akiwa Ikulu, kwanza akilaumiwa kwa kufanya biashara na baadaye kuendesha kwa upendeleo mchakato wa kumsaka Rais wa Nne wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 ndani ya CCM.

Kimsingi, kwa kukosa kwake tuzo hiyo, Mkapa kwa mara ya kwanza anakabiliana na kishindo cha kuangushwa katika medani za kimataifa, baada ya kuwa na rekodi ya ‘Mr. Clean' ambayo wapinzani wake wanasema aliipoteza miaka michache baada ya kuchukua madaraka.

Kwa upande mwingine, Mkapa anaikosa tuzo hiyo ambayo mmoja wa majaji wake alikuwa ni Waziri Mkuu mstaafu wa Tanzania na mwanadiplomasia aliyetukuka, Dk. Salim Ahmed Salim, ambaye aliukosa urais wa Tanzania mwaka 2005, baada ya Mkapa kuchukua uamuzi wa wazi wa ‘kumbeba' Jakaya Kikwete.

Aidha, wakati akipoteza tuzo hiyo jana, Mkapa, yuko katika shinikizo kubwa la kumtaka ajitokeze hadharani kujibu tuhuma za kutumia vibaya madaraka yake zinazomkabili.

Hivi karibuni Mkapa aliwashangaza watu wengi pale alipokwepa kuzungumza nao na badala yake akamuagiza mkurugenzi wa taasisi yake binafsi inayojishughulisha na masuala ya ukimwi ya Mkapa Foundation, Dk. Hellen Senkoro, kuzungumza na waandishi wa habari.

Hata hivyo, licha ya waandishi wa habari kuwa na kiu ya kuona kuwa tuhuma zinazomkabili zinajibiwa, waliishia kujibiwa kuwa, mkutano waliokuwa wamehudhuria haukuwa wa kisiasa, bali ulikuwa ukihusu masuala ya ukimwi.

Tuzo hiyo yenye thamani kubwa kifedha kuliko hata ile ya Nobel ambayo Kofi Annan alipata kuishinda, iliasisiwa na bilionea raia wa Sudan na mwanzilishi wa Kampuni ya simu ya Celtel, Mo Ibrahim.

"Tunahitaji kuondoa rushwa, tunahitaji kuboresha utawala, tunahitaji kuwa na afya na baadaye hatutahitaji misaada," alisema Ibrahim.

Mfanyabiashara huyo alitangaza azima ya kuanzisha tuzo hiyo mwaka jana kwa matarajio ya kuongeza uwezo wa Bara la Afrika kujitegemea na ili siku moja watu wake waishi bila ya kutegemea misaada.

Mafanikio ya Joaquim Chissano yamechangiwa hasa na hatua yake ya kukataa kugombea kipindi cha tatu cha uongozi nchini mwake, jambo ambalo lilionekana kuwa ukomavu wa demokrasia nchini Msumbiji, uamuzi ambao pia ulichukuliwa na Mkapa.

"Siku ambayo hatuhitaji msaada wowote itakuwa siku nzuri na ya ajabu katika maisha yangu," alikaririwa akisema Mo Ibrahim.

Kofi Annan ambaye aliongoza jopo lililotoa tuzo hiyo ya kwanza, alisema ni zawadi kubwa na ya aina yake.

"Hii ni kutokana na mchango wake katika kuiongoza Msumbiji, kutoka katika vita na kuingia katika amani na demokrasia. Kwa kweli Chissano ametoa mchango mkubwa," alisema Annan wakati akitangaza mshindi.

"Maridhiano haya ya kuigwa kati ya pande mbili hasimu yanatoa mfano wenye kung'aa kwa dunia na ushuhuda wa uimara wa tabia na uongozi wake," aliongeza.

Baada ya kupata uhuru kutoka kwa Wareno mwaka 1975 Msumbiji ilijikuta ikiingia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe, ambayo ilidumu hadi mwaka 1992.

Chissano aliingia madarakani mwaka 1986, baada ya kifo cha Rais wa kwanza, Samora Machel, na kuongoza hadi mwaka 2005 alipoamua kustaafu.

Mbali na kuwa rais wa Msumbiji, Chissano alipata pia kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) mwaka 2003 na 2004 , pamoja na kuwa mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa (UN).

Annan alisifu pia mchango wa Chissano alioutoa kwa nchi yake pamoja na Bara la Afrika kwa ujumla.

"Hatua yake ya kukataa kuwania muhula wa tatu wa uongozi iliimarisha ukomavu wa demokrasia nchini Msumbiji na kudhihirisha kuwa nchi na harakati za kidemokrasia vilikuwa muhimu zaidi kuliko haiba," alisema.

"Alikuwa sauti yenye nguvu barani Afrika, katika jukwaa la kimataifa na alionyesha juhudi kubwa katika kulifanya suala la nchi maskini kusamehewa madeni kuwa moja ya ajenda muhimu za kimataifa."

Mwandishi wa BBC aliyeko kusini mwa Afrika, Peter Biles, alisema Chissano ni kiongozi adimu Afrika, aliyetoka madarakani akiwa na heshima.

Jopo la majaji ambalo lilichagua mshindi lilijumuisha marais wa zamani wa Ireland , Mary Robinson, na wa Finland Martti Ahtisaari, pamoja na Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), Dk. Salim Ahmed Salim .

Jopo hilo lilipitia sifa za kila kiongozi kwa majina yote 13 ya viongozi ambao wametoka madarakani katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Katika orodha hiyo wapo viongozi sita ambao waliingia madarakani kwa njia ya mapinduzi.

BY MWANANCHI
Chisano wa Msumbiji aibuka Rais Bora Afrika
Na Ramadhan Semtawa

RAIS mstaafu wa Msumbiji, Joaqium Chissano, amewabwaga Marais wengine 12 akiwemo Benjamin Mkapa wa Tanzania, katika kinyang'anyiro cha Tuzo ya Rais bora wa Afrika.


Ushindi wa Chissano umetangazwa London, Uingereza jana na Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa (UN), Kofi Annan.


Tuzo hiyo ambayo imetolewa na Taasisi ya Mohamed Ibrahim, bilionea mzaliwa wa Sudan. Tuzo hiyo ina zingatia mambo makubwa matatu ambayo ni kukuza demokrasi, utawala bora na maendeleo katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.


Kutokana na ushindi huo, Chissano amenyakua jumla ya dola za Kimarekani 5 milioni (Sh6 bilioni) na pia atakuwa akipata dola 200,000 (Sh 250 milioni) kila mwaka katika siku zote za maisha yake.


Jopo hilo lililoongozwa na Annan, limeeleza kwamba ushindi wa Chissano, ulitokana na juhudi zake za kuimarisha demokrasi, kuleta maendeleo na amani kwa kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Msumbiji.


Msumbiji mara baada ya kupata uhuru kutoka kwa Ureno, ilijikuta katika vita ya madaraka ya miaka 16 ambayo ilikuwa kati ya Chama cha Frelimo na kundi la Renamo, ambavyo vilimazika Oktoba 1992.


Katika uongozi wake Chissano ambaye alikaa madarakani kwa miaka 19, aliweza kuendesha mazungumzo na Renamo pamoja na kuitisha uchaguzi wa kidemokrasi chini ya vyama vingi mwaka 1994 na kushinda, kisha akachaguliwa tena katika uchaguzi wa kidemokrasi mwaka 1999.


Rais huyo mstaafu wa Msumbiji ambaye alizaliwa Oktoba 22, 1939 katika kijiji cha Melehice, pia anaelezwa kuacha uchumi wa nchi hiyo ukiwa katika ustawi na ukuaji wa asilimia zaidi ya 10 kiwango ambacho ni kikubwa duniani.


Mkapa alikuwa ni miongoni mwa marais 13 wa Afrika waliondoka madarakani katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita waliotajwa katika kinyang'anyiro cha tuzo hiyo.


Sifa ambazo zilikuwa zikimfanya Mkapa atajwe kuweza kutwaa tuzo hiyo ni pamoja na juhudi zake za kuihusisha Tanzania katika kuleta amani katika eneo la Maziwa Makuu hasa Burundi baada ya kifo cha Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1999, ambaye alikuwa msuluhishi mkuu wa kwanza.


Mkapa pia alikuwa akipewa nafasi kutokana na juhudi zake za kukuza uchumi wa kitaifa (macro economy), kwa kuvutia wawekezaji, kujenga miundombinu kama barabara na kuacha uchumi ukiwa umekuwa kwa asilimia 7 kwa mwaka.


Hata hivyo, wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanaamini kwamba mauaji ya kisiasa ya Januari 26/27,2001, visiwani Zanzibar na tuhuma mbalimbali za ufisadi dhidi ya viongozi katika serikali yake na yeye mwenyewe ni moja ya mambo ambayo yamemtia doa.


Tathimini hiyo ya wachambuzi imezingatia kwamba kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania iliweza kuzalisha wakimbizi ambao walikimbia visiwani Zanzibar kwenda Shimoni Mombasa, Somalia na wachache Uingereza na Denmark.


Mkapa pia anaonekana kushindwa kutokana na kukiuka maadili ya uongozi kwa madai ya kufanya biashara akiwa Ikulu, kukosekana kwa chaguzi huru visiwani Zanzibar na kuongezeka kwa pengo la masikini na matajiri.


Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) sasa AU, ambaye pia ni mmoja wajumbe wa jopo hilo, akizungumza jana na Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), alisema tuzo hiyo ina lengo la kuleta ustawi barani Afrika.


Mbali na Chissano na Mkapa, wengine walioshiriki kinyang'anyiro hicho ni Mathieu Kerekou (Benin), Azali Assoumani (Comoros), Domitien Ndayizeye (Burundi), Henrique Rosa (Guinea Bissau), Maaouya Ould Sid'Ahmed Taya (Mauritania), Sam Nujoma (Namibia), Abass Bonfoh (Togo), Gnassingbe Eyadema (Togo), Bakili Muluzi (Malawi), France-Albert Rene (Seychelles) na Abdiqassim Salad Hassan wa Somalia.


Tuzo hiyo imekuja katika kipindi ambacho nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara zikiwa katika matatizo makubwa ya umasikini unaotokana na ukosefu wa utawala bora na demokrasi.


Tuma maoni kwa Mhariri
MAJIRA NAO KAMAIFUATAVYO
•
Chissano ndiye kiongozi bora Afrika

Habari Zinazoshabihiana
• Viongozi CCM wadaiwa kumsaliti Rais Kikwete 07.09.2006 [Soma]
• Migiro apewa tuzo na marais wastaafu 19.04.2007 [Soma]
• Hatuna maslahi na Shirikisho-Shamsi 02.02.2007 [Soma]

*Awatimulia vumbi marais wastaafu Mkapa, Muluzi, Eyadema, Kerekou
*Kulipwa bil. 6/- kwa miaka 10 kisha m. 200/- kila mwaka mpaka kufa

Na Mwandishi Wetu

RAIS wa zamani wa Msumbiji, Bw. Joaquim Chissano, ameshinda Tuzo ya Uongozi Bora ambayo ni ya kwanza na imetolewa na mfanyabiashara wa simu za mkononi, Bw. Mo Ibrahim.

Tuzo hiyo ambayo imetolewa kwa Mkuu wa Nchi aliyestaafu, ilitolewa jana jijini London, Uingereza, kwa Bw. Chisano kutokana na kurejesha amani nchini Msumbiji.

Mshindi huyo alitangazwa na Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Kofi Annan, ambapo Bw. Chisano kwa tuzo hiyo, atapewa dola milioni 5 za Marekani kwa zaidi ya miaka 10 na baada ya hapo kila mwaka atakuwa akilipwa dola 200,000 kwa maisha yake yote.

Milionea Ibrahim alifadhili mradi huo kwa matumaini, kwamba utasaidia kuboresha utendaji wa Serikali za Afrika.

Viongozi wastaafu 13 ndio walioshiriki na mshindi kupatikana kwa kuchaguliwa na jopo lililoongozwa na Bw. Annan.

Kamati hiyo ilijumuisha Rais mstaafu wa Ayalandi, Bibi Mary Robinson, Rais mstaafu wa Ufini, Bw. Martti Ahtisaari, Waziri wa zamani wa Fedha wa Nijeria Bw. Ngozi Okonjo-Iweala na Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa Afrika, Dkt. Salim Ahmed Salim.

Washiriki katika kinyang'anyiro hicho ni wakuu wa nchi waliostaafu miaka mitatu iliyopita.

Mfanyabiashara huyo wa Sudani, ana matumaini kuwa tuzo hiyo itaongeza hatua ya Afrika kujitegemea na kufanya siku moja watu wa bara hili waachane na maisha ya kutegemea misaada.

"Tunataka kuondokana na rushwa, tunataka kuboresha utawala bora, tunataka kuwa na afya njema, hatimaye tusihitaji misaada tena," alisema Bw. Ibrahim.

"Siku ambayo tutaachana kabisa na misaada, hiyo ndiyo itakuwa siku muhimu katika historia ya maisha yangu," aliongeza.

Wakuu 13 wa mataifa ya Afrika walioondoka madarakani kati ya mwaka juzi na mwaka jana, walikuwa na sifa za kushiriki katika kinyang'anyiro hicho, lakini pia aliyekuwa Rais wa Serikali ya Mpito ya Somalia.

Wengine walioshindanishwa ni Bw. Benjamin Mkapa wa Tanzania na Bw. Mathieu Kerekou wa Benini.

Bw. Kerekou, mathalan alikuwa Mkuu wa Kwanza wa Serikali barani Afrika kuruhusu uchaguzi uliohusisha vyama vingi na kukubali kuondoka aliposhindwa katika uchaguzi huo.

Bw. Chisano alichangia kwa kiasi kikubwa kumalizika kwa mapigano nchini mwake, huku Bw. Mkapa akiendelea kuimarisha utulivu wa kisiasa nchini mwake licha ya kuzungukwa na nchi zenye migogoro.

Licha ya kuwa ameshafariki dunia, lakini kiongozi wa zamani wa kijeshi wa Togo, Bw. Gnassingbe Eyadema, alikuwa katika orodha ya wawaniaji tuzo hiyo.

Naye Rais wa zamani wa Malawi, Bw. Bakili Muluzi alikuwa miongoni walioshindanishwa, ambaye alikaririwa akisema hakuamini kuwa naye alistahili kuingizwa katika orodha, kwani hataki kuitwa 'Rais mstaafu'.

Bw. Muluzi anapanga kuwania nafsi hiyo na hivi sasa anakabiliwa na upinzani mkubwa wa kisiasa na kisheria kuhusiana na azma yake hiyo.

Wakati akitangaza mshindi wa tuzo hiyo, Bw. Annan alisema "Ni kutokana na dhima yake katika kuiongoza Msumbiji kutoka vita hadi amani na demokrasia, Bw. Chissano alitoa mchango mkubwa.

"Mapatano haya kati ya wapinganao yametoa mfano mzuri duniani na ni ushahidi wa uwezo na mwenendo mzuri wa uongozi alionao," alisema.

Baada ya kupata kuhusu kutoka kwa Wakoloni wa kireno mwaka 1975, Msumbiji iliingia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe hadi mwaka 1992.

Bw. Chissano aliingia madarakani kuanzia mwaka 1986 hadi mwaka juzi, pia alikuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika mwaka 2003 na kuwa mjumbe wa Umoja wa Mataifa.

Bw. Annan alimpongeza Bw. Chissano kwa mchango wake mkubwa ndani ya nchi na katika Bara la Afrika kwa ujumla.

"Uamuzi wake wa kukataa kuwania uraia kwa mara ya tatu, ulionesha kukua kwa demokrasia nchini Msumbiji na alionesha kuwa taasisi na mchakato wa ujenzi wa demokrasia ni vitu muhimu zaidi ya mtu binafsi," alisema.

"Alikuwa mwenye sauti kubwa kuhusu Afrika katika majukwaa ya kimataifa na alitoa mchango mkubwa katika misamaha ya madeni kwa nchi changa."

Kati ya viongozi hao 13 walioshindanishwa, takriban sita kati yao waliingia madarakani kwa njia ya mapinduzi ya kijeshi. (BBC)

WATANZANIA TUJITAZAME KWA KILA PANDE ZA SHILINGI YETU.
 
akpew3.jpg


Hata kasungura ka-EL kalisema sizitaki mbichi hizi.

Credit: Mjengwa blog.
 
Back
Top Bottom