JKT kusaka wavuvi haramu

R.B

JF-Expert Member
May 10, 2012
6,296
2,573
JESHI la Kujenga Taifa (JKT) kambi ya Mwalukoma iliyoko katika kijiji cha Bulamba, wilayani Bunda kwa kushirikiana na halmashauri ya Wilaya ya Bunda, wataanza kuwasaka wavuvi haramu, pamoja na vikundi vya watu wanaoendesha vitendo vya uharamia katika ziwa Victoria.

Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Joshua Mirumbe aliyasema hayo juzi wakati akifungua mkutano mkuu wa chama cha kuweka akiba na kukopa cha Bunda SACCOS, ambacho wanachama wake ni wakulima, wavuvi, wafugaji na wafanyabiashara.

Alisema kambi ya JKT Bulamba, pamoja na mambo mengine ya kijeshi, zikiwemo shughuli wanazoendesha za uvuvi, watashirikiana na halmashauri ya Wilaya ya Bunda kukabiliana na wavuvi haramu.

Alisema jeshi hilo, kwa kuwa linaendesha shughuli za uvuvi ndani ya ziwa hilo, litashirikiana na halmashauri hiyo katika kusaka maharamia ambao wanajiita jina la Mungiki, ambao wamekuwa wakivamia na kuteka wavuvi na kuwapora maziwa pamoja na zana zao za uvuvi.

“Tumekubaliana JKT kambi ya Byulama, ikianza shughuli za uvuvi itashirikiana na halmashauri ya wilaya yetu katika kusaka wavuvi haramu, pamoja na wale wavamizi wa wavuvi wanaojiita Mungiki,” alisema.

Alisema uvuvi haramu katika ziwa hilo, upande wa wilayani hapa umeshamiri na kwamba baadhi ya wavuvi, wamekwishakamatwa na kufikishwa mahakamani na wengine tayari wamehukumiwa.

Katika hatua nyingine, Mirumbe aliipongeza Saccos hiyo kwa hatua iliyofikia ya kukuza mtaji wake, ambapo sasa mtaji na madeni kwa wanachama wake ni zaidi ya Sh milioni 693.

Alibainisha njia pekee ya mwananchi kuondokana na umasikini, ni kujiunga kwenye vyama vya ushirika na kwamba ni jukumu la maofisa ushirika wilayani hapa, kuhamasisha wananchi, ili waweze kujiunga kwenye vyama hivyo.

Akitoa taarifa yake Mwenyekiti wa Saccos hiyo, John Kitang’osa, alisema ushirika wao sasa una jumla ya wananchama 4,543.

Alibainisha hadi Novemba, mwaka huu, Saccos hiyo ina hisa milioni 71, akiba ya Sh milioni 427.9.

Meneja wa Saccos hiyo, Thecla Matemu alisema Saccos hiyo inakabiliwa na changamoto kubwa ya baadhi ya wanachama wake kutokurejesha mikopo kwa wakati.
 
Back
Top Bottom