JKCI kupasua mishipa ya damu bila kufungua kifua

esther mashiker

JF-Expert Member
May 29, 2018
616
552
1579153910882.png

TAASISI ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa mwaka wa 2020 imejipanga kufanya upasuaji wa mishipa ya damu na mapafu, upasuaji wa moyo wa kufungua na bila kufungua kifua kwa wagonjwa 2,140. Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo Profesa Mohamed Janabi katika kikao cha kufungua mwaka cha wafanyakazi wa JKCI kilichofanyika jijini Dar es Salaam.

Profesa Janabi alisema idadi ya wagonjwa wanaosubiri kufanyiwa upasuaji mkubwa wa kusimamisha moyo, upasuaji wa bila kufungua kifua pamoja na upasuaji wa mishipa ya damu na mapafu ni kubwa, hivyo taasisi hiyo imejipanga kuhakikisha wagonjwa hao wanapata matibabu kwa wakati. “Kwa mwaka huu wa 2020 tumejipanga kufanya upasuaji mkubwa wa kusimamisha moyo kwa wagonjwa 400, kati ya hawa watu wazima watakuwa 250 na watoto 150.

Pia tutafanya upasuaji wa mishipa ya damu na mapafu kwa wagonjwa 240,”alisema na kuongeza: “Kwa upande wa upasuaji wa bila kufungua kifua kupitia tundu dogo linalotobolewa kwenye paja kwa kutumia mtambo wa Cathlab (Catheterization laboratory) tumejipanga kufanya upasuaji kwa wagonjwa 1,500 kati ya hawa watoto ni 96 na watu wazima 1,404”, amesema.

Mkurugenzi huyo Mtendaji ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisisitiza kuwa idadi hiyo ya wagonjwa inaweza kamilika kama watafanya kazi kwa kujituma, ushirikiano na kufuata maadili ya kazi.

Aidha Profesa Janabi aliwasihi wafanyakazi wa taasisi hiyo kuwaelimisha wagonjwa pamoja na ndugu zao ili waweze kujiunga na mifuko ya bima za afya, kwa kufanya hivyo wataweza kuepukana na gharama za matibabu kwani wagonjwa wengi wanaotibiwa katika taasisi hiyo wanatoka katika familia maskini, hivyo kushindwa kulipia gharama za matibabu.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Afya na Serikali kuu (TUGHE) tawi la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete, Godfrey Tamba aliushukuru uongozi wa taasisi hiyo kwa kusimamia maslahi ya wafanyakazi na kuahidi wataendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuendeleza huduma zinazotolewa na taasisi hiyo.
 
Back
Top Bottom