JK: Vumilieni shida

Mambo Jambo

JF-Expert Member
Jul 11, 2008
1,100
81
Chanzo: TANZANIA DAIMA, 21ST JULY, 2008

na Anna Makange, Tanga

RAIS Jakaya Kikwete, amewataka Watanzania kuwa wavumilivu kutokana na hali ngumu ya maisha inayowakabili kwa sasa, inayosababishwa na kupanda kwa bei ya mafuta duniani.

Rais Kikwete ametoa kauli hiyo katika kipindi ambacho Watanzania wengi, hasa wa kipato cha chini wamekuwa wakilia kutokana na kupanda kwa gharama za maisha.

Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana, wilayani Muheza, wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa wilaya hiyo, ikiwa ni siku ya tisa ya ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo, mkoani Tanga.

Rais Kikwete alisema kupanda kwa bei ya mafuta, kumechangia kwa kiasi kikubwa kulipuka kwa mfumuko wa bei za bidhaa mbalimbali duniani kote.

Alisema hali hiyo pia imechangia kuzorotesha kasi ya ukuaji wa uchumi hasa kwenye nchi zinazoendelea na hivyo watu wenye kipato duni kukabiliwa na hali ngumu ya maisha, hususan katika upatikanaji wa mahitaji muhimu, jambo ambalo aliongeza kuwa hata yeye limekuwa likimuumiza kichwa.

“Ndugu zangu Watanzania wenzangu…naelewa sana jinsi maisha yanavyozidi kuwa magumu siku hadi siku…na hali hii inasababishwa na kupanda kwa bei ya mafuta hapa nchini, hivyo kila bidhaa kwa sasa gharama zake ni za juu sana, kuanzia vyakula hadi vitu vingine ambavyo ni muhimu kwa maisha ya kila siku. Linatuumiza sana hasa wale wananchi ambao ni maskini wa kipato,” alisema Rais Kikwete.

Hata hivyo alisema Watanzania wasikate tamaa kwa kuona kwamba maisha yataendelea kuwa hivyo, na kusisitiza kwamba yeye kama Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) kwa kushirikiana na viongozi mbalimbali duniani wanalishughulikia suala hilo.

Wakati Rais Kikwete akiwataka Watanzania kutokatishwa tamaa na hali hiyo, Chama cha NCCR- Mageuzi, jana kilisema wananchi hawana sababu ya kuilaumu Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) kwa kupandisha bei ya nauli na badala yake lawama hizo zielekezwe kwa serikali ya Rais Kikwete.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Idara ya Oganaizesheni, Kampeni na Uchaguzi, Faustine Sungura, alisema kutokana na matatizo hayo, kuna haja ya kuwepo kwa serikali mbadala, kwa madai kuwa serikali imeshindwa kutatua matatizo yanayowakabili wananchi, hasa ya upandaji wa gharama za bidhaa mbalimbali.

“Watanzania wanapaswa kujifunza kutokana na makosa, kwani muda waliowapa viongozi wa CCM kutawala unatosha na haujaonyesha mafanikio yoyote katika maisha zaidi ya kuzidisha ugumu wa maisha,” alisema.

“Watu wanakosea sana wanapoilaumu Sumatra badala ya kuilaumu serikali ambayo imeshindwa kudhibiti upandaji wa bei kwenye bidhaa mbalimbali yakiwemo mafuta,” alisema Sungura.

Alisema hata ziara anazofanya Rais Jakaya Kikwete na Makamu wake, Ali Mohamed Shein ni dhihaka kwa Watanzania, kwani ahadi zao hazitekelezeki na wameshindwa kuwasaidia wastaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambao wanashinda Ikulu.

“Hivi hawa ni viongozi wa aina gani kama wameshindwa kuwasaidia wazee wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanaoshinda pale Ikulu, wataweza vipi kuwasaidia watu wa huko mikoani?” alihoji Sungura.

Katika hatua nyingine, Rais Kikwete amesema serikali itahakikisha inafanya kila jitihada za kutafuta wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kuwekeza kwenye kiwanda cha usindikaji wa matunda wilayani Muheza, kwa lengo la kuwatafutia wakulima wa machungwa soko la uhakika.

Alisema lengo la kujenga kiwanda hicho licha ya kumtafutia soko mkulima, lakini pia itakuza kipato cha wakulima sambamba na kupunguza kiwango kikubwa cha machungwa yanayoharibika mashambani kwa kukosa wanunuzi hasa nyakati za msimu.

“Serikali inaamini kwa kufanya hivi tutakuwa tumemsaidia mkulima kwa kiasi kikubwa kuwa na soko la uhakika sambamba na kukuza kipato chake ambacho hivi sasa kinapotea kutokana na kiasi kikubwa cha matunda kuharibika…nawaahidi kwamba hili tutalitekeleza haraka iwezekanavyo,” alisisitiza Rais Kikwete.

Miongoni mwa ahadi alizotoa rais wilayani Muheza ni pamoja na kupeleka darubini katika zahanati ya Kijiji cha Kicheba, kuchangia sh milioni mbili katika ujenzi wa madarasa ya Shule ya Sekondari ya Mtindiro, sambamba na kutafuta magari ya wagonjwa katika wilaya zilizokosa huduma hiyo mkoani hapa.

HII SASA KALI, KAZI KWENU WADAU
 
Sawa Muungwana tumekusikia, umeshatuletea kisingizio cha Bei za mafuta. Kama sikosei ulitumia kisingizio hiki miezi kadhaa pamoja na kuyumba uchumi wa Marekani kutokana na uanguka kwa soko la nyumba na mikopo yake.

Sasa sijui Tanzania kushindwa kuzalisha mali kujitosheleza ambako ulisema ungekufanyia kazi kunaendelea kuchangiwa na sababu za nje au ukosefu wa mipango na miundombinu kutoka Serikali yako ili tusiumie sana.

Naona umehalalisha U-VDG kwa kusema kuwa kwa nafasi yako kama Mwenyekigoda wa AU, unalishughulikia hili suala!

Nitavumulia na kusubiri ahadi zako mpya Juni ya 2010!
 
Wakati akiwataka Watanzania waendelee kuvumilia shida, Mafisadi wanaendelea na matanuzi yao na pesa za haramu. Yeye mwenyewe anaendelea na matanuzi ya safari zisizokwisha nchi za nje kila kukicha na msururu wa watu ambao wanaigharimu serikali gharama kubwa. Halafu tukisema nchi imemshinda wengine wanakasirika. Aaanze kujibana yeye kwa kufuta safari yake ya US mwezi ujao maana haina maslahi yoyote kwa nchi
 
Huyu jamaa kwali kichekesho kwanza anakimbilia vijijini kwenda kuongea mbona akiwa Dar anajificha tu, kisha vitu vya muhimu kafumba macho na masikio hawezi kosa kitu cha kusingizia huyu.
 
Hiki kisingizio wana JF tulishakijadili. Nilifikiri ataona aibu kukitumia kwa vile yeye mwenyewe hakai ofisini kila saa mguu na njia. Kama kweli anaona gharama za usafiri zimepanda kwa nini kila akitoka safari anaaza nyingine. I wonder kama anapitia document zote anazozi-sign. Actually JK anatakiwa awe muangalifu kuliko Mkapa kwa kuwa yeye hatakuwa na watu wa kumlinda. Kizazi cha enzi za uhuru cha CCM kulindana wengi wao hawatakuwepo 2015 hivyo kizazi kipya cha kina yakhe kilichozaliwa baada ya uhuru kitakuwa kinashika hatamu na kitamuhukumu peke yake.
 
Sio siri hii sababu ya mafuta na dunia tulimpa last week hapa JF, lakini isiwe sababu ya kujaribu kuficha uozo wa serikali yake kwa kisingizio cha bei ya mafuta na dunia,

kwa sababu it has nothing to do na ubovu wa uongozi wa serikali yake, ambacho ndicho hasa chanzo cha matatizo mengi ya maisha ya wananchi wa Tanzania kwa sasa.
 
Only God knows that we have a fool for a president.Tuvumilie shida while the few and selected are growing rich while majority die of hunger and poverty.My heart is bleeding with anger and hatred.
 
HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, AKIFUNGUA RASMI BUNGE JIPYA LA JAMHURI YA
MUUNGANO WA TANZANIA, DODOMA, 30 DESEMBA 2005

Mheshimiwa Spika:

Serikali ya Awamu ya Nne ambayo nimepewa heshima ya kuiongoza, inaanza kazi wakati nchi ikiwa na hali nzuri kiuchumi, kisiasa na kijamii. Mafanikio hayo yametokana na uongozi imara na thabiti wa Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa. Napenda kutumia fursa hii kumpongeza kwa dhati kwa kazi kubwa na nzuri aliyoifanyia nchi yetu. Kwangu binafsi, amekuwa mwalimu na mwelekezi ambaye amenijengea uwezo na dhamira ya kuendeleza kazi aliyoianza. Namtakia afya njema na maisha marefu, yeye, Mama Mkapa, na familia yao.
 
Na kweli wananchi tuvumilie tu shida labda mpaka 2010 kama atatokea mkombozi mwingine, maana JK wakati anaingia tuliambiwa yeye ni mesiah yaani mkombozi wa dhiki na matatizo yote ya Watanzania. Lakini kwa kauli yake hii anamaanisha kukiri kushindwa kutupa nchi imimikayo maziwa na asali, yenye neema kwa kila mtanzania na maisha bora kwa kila mtanzania. Nakumbuka wakati JK amepitishwa na CCM kuwa mgombea wa kiti cha urais nilipita mtaa wa Mosque nikamsikia mlemavu mmoja omba omba akisema kwamba hatimaye shida zao zitakwisha sasa na wao walemavu wataishi maisha bora. Ukweli ni kwamba nilimsikitia na kumuonea huruma kwa kuwa nilijua kwamba hiyo ni ndoto ya mchana.

Ukiacha huyo ambaye "obviously ni illiterate" nilishangazwa sana siku moja nimekwenda kuwatembelea ndugu zangu fulani huko Kiwalana ambao walibahatika kuliona darasa. Wakati tunakunywa bia wakapigiwa simu kutoka US, wakawa wanamwambia yule ndugu yao kwamba wao hapa Bongo mambo yatakuwa tamabarare muda si mrefu kwa kuwa JK anaingia madarakani.

Si ajabu kuona kwamba muungwana alishinda kwa 80% ya kura zote zilizopigwa. Mimi binafsi kwa mara ya kwanza alipa matumaini makubwa sana ya Tanzania yenye neema na yenye maisha bora kwa kila Mtanzania pale alipotoa hotuba yake ya kwanza bungeni. Laiti kama leo hii tungepata nakala ya hotuba ile tuanza ku "tick" kitu kimoja kimoja tutagundua kwamba hata 20% ya aliyoyaongea hajayafanya bado. May be he was he too ambitious?

Ninachojiuliza kwa sasa ni je nafsi yake inamsuta huko aliko kwa kushindwa kuwatimizia ndoto Watanzania hawa masikini? Au ilikuwa lengo ni kufika Ikulu tu kisha mliobaki mtajijua?
 
HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, AKIFUNGUA RASMI BUNGE JIPYA LA JAMHURI YA
MUUNGANO WA TANZANIA, DODOMA, 30 DESEMBA 2005

Mheshimiwa Spika:

Serikali ya Awamu ya Nne ambayo nimepewa heshima ya kuiongoza, inaanza kazi wakati nchi ikiwa na hali nzuri kiuchumi, kisiasa na kijamii. Mafanikio hayo yametokana na uongozi imara na thabiti wa Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa. Napenda kutumia fursa hii kumpongeza kwa dhati kwa kazi kubwa na nzuri aliyoifanyia nchi yetu. Kwangu binafsi, amekuwa mwalimu na mwelekezi ambaye amenijengea uwezo na dhamira ya kuendeleza kazi aliyoianza. Namtakia afya njema na maisha marefu, yeye, Mama Mkapa, na familia yao.

Mzee hebu irushe link ya hii hotuba tafadhali.
 
HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, AKIFUNGUA RASMI BUNGE JIPYA LA JAMHURI YA
MUUNGANO WA TANZANIA, DODOMA, 30 DESEMBA 2005

Mheshimiwa Spika:

Serikali ya Awamu ya Nne ambayo nimepewa heshima ya kuiongoza, inaanza kazi wakati nchi ikiwa na hali nzuri kiuchumi, kisiasa na kijamii. Mafanikio hayo yametokana na uongozi imara na thabiti wa Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa. Napenda kutumia fursa hii kumpongeza kwa dhati kwa kazi kubwa na nzuri aliyoifanyia nchi yetu. Kwangu binafsi, amekuwa mwalimu na mwelekezi ambaye amenijengea uwezo na dhamira ya kuendeleza kazi aliyoianza. Namtakia afya njema na maisha marefu, yeye, Mama Mkapa, na familia yao.

Mkubwa kama hiyo link unayo tafadhari hebu tumwagie janvini, au kama vipi ilete ki thread waungwana wadodose...
 
HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WATANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, AKIFUNGUA RASMI BUNGE JIPYA LA JAMHURI YA
MUUNGANO WA TANZANIA, DODOMA,30 DESEMBA 2005

Mheshimiwa Spika:

Namshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujalia uhai na afya, na akatukutanisha hapa. Ninamshukuru pia kwa Uchaguzi Mkuu wa amani, utulivu na heshima kubwa kwa nchi yetu. Nakishukuru sana Chama changu, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa heshima kubwa kilichonipa kwa kuniteua niwe mgombea wake wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ninawashukuru wananchi kwa kunipa mimi na Chama changu ushindi mkubwa sana. Shukrani zangu kwa Watanzania wenzangu—wana-CCM na wasio wana-CCM—ni ahadi ya kuwatumikia kwa uwezo wangu wote. Nawashukuru wapinzani kwa ujasiri wao mkubwa wa kujitokeza kushindana na Chama Cha Mapinduzi. Uchaguzi sasa umekwisha. Kauli ya wananchi imedhihirika. Tuungane, tuwe kitu kimoja; tujenge na kuendeleza nchi yetu.

Nawashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa kumkubali mteuliwa wa CCM kwa nafasi ya Spika, Mheshimiwa Samuel John Sitta, Mb., na pia kwa kukubali uteuzi wangu wa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Edward Ngoyai Lowassa, Mb. Naomba mumpe Waziri Mkuu, pamoja na Mawaziri na Naibu Mawaziri nitakaowateua hivi karibuni, ushirikiano mkubwa. Wachangamsheni, lakini watendeeni haki na wapeni ushirikiano.
Mheshimiwa Spika:

Nawapongeza Wabunge wote waliochaguliwa. Ninyi, Waheshimiwa Wabunge, ndio macho na masikio ya wananchi. Mmeaminiwa na kuheshimiwa. Naomba kila siku mnapoingia au kutoka katika Bunge hili, mnapozungumza humu ndani au mnaposikiliza wengine wakizungumza, mnapokuwa macho au mnapofumba macho kutafakari kwa kina, kila mara mkumbuke imani na heshima hiyo kubwa mliyopewa na wananchi.

Nakupongeza sana wewe mwenyewe, Mheshimiwa Spika, kwanza kwa kuchaguliwa kuwa Mbunge, na pili kwa kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge hili Tukufu. Umepata kazi ya heshima kubwa sana, yenye wajibu mkubwa sana. Unao uwezo na uzoefu wa kuifanya. Hivyo, sina shaka utaimudu vema kazi hiyo, na utaliongoza Bunge hili kwa hekima na busara, ukiwatendea haki Wabunge wote, na upande wa Serikali pia. Ninakutakia kila la kheri, na ninakuhakikishia ushirikiano kamili katika kazi zako.
 
Mheshimiwa Spika:

Ninampongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Amani Abeid Karume, kwa kuchaguliwa tena kuiongoza Zanzibar. Namhakikishia ushirikiano wangu na wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Mheshimiwa Spika:

Navipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya ya kuhakikisha kuwa nchi yetu inaendelea kuwa kisiwa cha amani na utulivu wakati wote wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu. Wameonyesha uaminifu kwa Taifa na uzalendo wa hali ya juu. Nawapongeza sana.

Mheshimiwa Spika:
Wananchi wengi wameelimika na kufuatilia mchakato wote wa Uchaguzi Mkuu kutokana na kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na vyombo vya habari. Nawashukuru na kuwapongeza.

Mheshimiwa Spika:

Serikali ya Awamu ya Nne ambayo nimepewa heshima ya kuiongoza, inaanza kazi wakati nchi ikiwa na hali nzuri kiuchumi, kisiasa na kijamii. Mafanikio hayo yametokana na uongozi imara na thabiti wa Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa.

Napenda kutumia fursa hii kumpongeza kwa dhati kwa kazi kubwa na nzuri aliyoifanyia nchi yetu. Kwangu binafsi, amekuwa mwalimu na mwelekezi ambaye amenijengea uwezo na dhamira ya kuendeleza kazi aliyoianza. Namtakia afya njema na maisha marefu, yeye, Mama Mkapa, na familia yao.
 
Nazipongeza Tume ya Uchaguzi ya Taifa, na Tume ya Uchaguzi Zanzibar, kwa kazi nzuri sana waliyoifanya katika chaguzi zilizopita. Naomba waendelee kunoa uwezo wao, maana Watanzania-Bara na Zanzibar-wanastahili uchaguzi mzuri. Kadhalika tunao wajibu wa kihistoria wa kuwa mfano bora barani Afrika na hata kwingineko.

Siasa

Mheshimiwa Spika:

Chama Cha Mapinduzi kimerejeshwa madarakani kwa kura halali za wananchi zilizotupa idhini ya kutawala, tena idhini kubwa isiyo na shaka hata kidogo. Hatutaona aibu kuitumia idhini hiyo, kupitia Bunge hili, kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2005.

Kama mwana-CCM nafurahia sana ushindi wetu. Lakini, nikiwa Rais, napenda niwahakikishie wapinzani kuwa hatuna nia au sera ya kuua vyama vya upinzani. Serikali ya Awamu ya Nne itaendeleza, kwa dhati, mfumo wa siasa wa demokrasia ya vyama vingi. Ushauri wangu kwa vyama vya upinzani kwa wapinzani ni kuwa wasiwe wepesi kutafuta mchawi kila wanaposhindwa uchaguzi. Badala yake nawaomba wajiulize kwa nini Watanzania wamewakataa kiasi hicho. Nina uhakika watapata jibu.

Mheshimiwa Spika:

Ni kweli nchi yetu sasa ni ya demokrasia ya vyama vingi. Lakini ni wazi bado utamaduni wa mfumo huu wa siasa ni mchanga na kwa ujumla haujaimarika vya kutosha. Tutajitahidi kujenga utaratibu na misingi ya mahusiano mema zaidi baina ya vyama vya siasa nchini Tanzania.

Mimi naamini wakati umefika, kama alivyowahi kusema Rais Mkapa, kuwa tuwe na maadili yatakayotawala shughuli za kisiasa, ambayo hayategemei hiari ya viongozi wa kisiasa waliopo madarakani. Yanakuwa ni maadili na miiko ya lazima, yanayobana kila chama cha siasa, wanachama na viongozi wake, ikiwemo wale wa Chama Tawala.

Tusipofanya hivyo-na dalili zimeanza kuonekana-wanaweza kujitokeza watu wakavuruga nchi yetu kwa kisingizio cha uhuru wa kisiasa. Uhuru bila mipaka ni fujo, na siwezi kukubali nchi mliyonikabidhi kuiongoza itawaliwe na fujo.

Mheshimiwa Spika:

Yameanza kujitokeza mawazo kuwa uongozi unaweza kununuliwa kwa fedha. Kama ni kweli, tusipokuwa waangalifu, nchi yetu inaweza kuwekwa rehani kwa watu wenye fedha za kununua uongozi au wanaoweza kupata fedha za kufanya hivyo.

Ni kweli kwamba fedha ni nyenzo mojawapo muhimu katika kufanikisha uchaguzi. Lakini, fedha kutumika kununua ushindi si halali. Ni vema sasa tuanzishe mjadala wa kitaifa na hatimaye kuelewana kuhusu utaratibu halali, ulio wazi, wa chama au mgombea kutafuta fedha za uchaguzi; na utaratibu halali, ulio wazi, wa chama au mgombea kutumia fedha hizo. Na utaratibu tutakaokubaliana uwe ni sehemu ya maadili ya uchaguzi katika uchaguzi wa kiserikali na ndani ya vyama vya siasa. Katika mjadala huo suala la takrima nalo tuliangalie.
 
Majukumu ya Msingi ya Serikali ya Awamu ya Nne

Mheshimiwa Spika:

Tangu tupate Uhuru, kila awamu ya uongozi wa taifa imekuwa na majukumu yake ya msingi. Awamu ya Kwanza iliunda na kujenga taifa. Wakoloni hawakujenga hisia za utaifa, maana mkakati wao wa kututawala ulikuwa kutudhoofisha kwa kutugawa ili tutawalike kwa urahisi. Mwalimu Nyerere hakurithishwa taifa na wakoloni. Alirithishwa mkusanyiko wa makabila mbalimbali, na watu wa dini na rangi mbalimbali. Akatambua kuwa hata uchumi wa Tanzania ungekua kwa kasi kubwa kiasi gani, iwapo hakuna misingi imara na hisia za dhati za utaifa, baada ya muda tutasambaratika na uchumi huo utakuwa hauna maana. Kwa kushirikiana na hayati Mzee Karume wakatujengea Taifa la Tanzania lenye umoja, pamoja na watu wake kuwa wa makabila 120, rangi na dini mbalimbali.

Mwalimu aliongoza vita dhidi ya ujinga, umaskini na maradhi. Mtandao mkubwa wa huduma za jamii tunaojivunia leo ulianza na falsafa ya maendeleo ya Baba wa Taifa. Wengi wetu tuliomo humu ndani, wa makamo yangu, tusingesoma na kufika hapa tulipo kama si kuona mbali na sera nzuri za Baba wa Taifa. Tutamshukuru yeye na Mzee Karume daima.

Awamu ya Pili chini ya Mzee wetu, Ali Hassan Mwinyi, ilifungua milango na kupanua uwanja wa ushiriki wa wananchi kwenye uchumi na siasa. Mzee Mwinyi ni muasisi wa mageuzi ya kiuchumi na kisiasa Tanzania. Alimaliza uhaba wa bidhaa na baadhi ya huduma muhimu uliodhalilisha wananchi. Alipanua sana mipaka ya uhuru wa raia katika maisha yao ya kiuchumi na kisiasa.

Nakumbuka siku moja Mzee Mwinyi alielezea awamu yake kama wakati ambapo mtu anafungua madirisha ya nyumba ili hewa safi iingie ndani. Lakini, akasema, ukifungua madirisha ujue nzi, mbu na wadudu wengine nao wataingia. Hapo ndipo Awamu ya Tatu ya Rais aliyenitangulia, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, ilipoanzia. Ilibidi kushughulikia mbu, nzi na wadudu hao. Rais Mkapa alifanya kazi kubwa kurejesha nidhamu kwenye ukusanyaji wa mapato na matumizi ya Serikali. Alipiga vita rushwa kwa nguvu zake zote. Alirejesha mahusiano mazuri na wahisani wetu na washirika wetu kwenye maendeleo.

Aliweka mazingira bora ya uwekezaji, na ukuaji wa uchumi. Aliimarisha misingi ya uchumi mkuu. Bei za kuruka, na fedha za soksi zikaisha. Ameweka misingi imara ya kuwezesha wananchi kujiendeleza kupitia miradi kama vile TASAF na MKURABITA chini ya mwavuli wa MKUKUTA.
Alikarabati na kupanua sana miundombinu ya elimu, afya, maji na umeme. Barabara na madaraja yamejengwa. Kutokana na juhudi za Rais Mkapa, Serikali ya Awamu ya Nne inaanza bila mzigo wa madeni usiobebeka kama alivyoanza yeye. Tunaanzia mahali pazuri.
 
Mheshimiwa Spika:

Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2005 imetamka bayana majukumu mawili ya msingi ya Serikali ya Awamu ya Nne:.

• Kwanza, kuitoa Tanzania kutoka kwenye dimbwi la uchumi ulio nyuma na tegemezi na kuiingiza katika mkondo wa uchumi wa kisasa wa taifa linalojitegemea.

• Pili, kuwashirikisha wananchi wote kwa njia ya uwezeshaji katika ujenzi wa uchumi na kuutokomeza umaskini.

Mheshimiwa Spika:

Kwa kuzingatia majukumu haya ya msingi, na mbinu na mikakati mbalimbali ya kuyatekeleza, Watanzania watarajie mambo kumi yafuatayo katika miaka mitano ijayo:

• Kwanza, Serikali ya Awamu ya Nne itahakikisha kuwa Amani, Utulivu na Umoja wa nchi yetu na watu wake vinadumishwa;

• Pili, Serikali ya Awamu ya Nne itadumisha na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana tangu Serikali ya Awamu ya Kwanza hadi leo;

• Tatu, Serikali ya Awamu ya Nne itaendeleza vita dhidi ya umaskini, ujinga na maradhi, tena kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya;

• Nne, Serikali ya Awamu ya Nne itatimiza ipasavyo wajibu wake wa utawala na maendeleo, na itaendesha dola kwa misingi ya utawala bora na uwajibikaji; utawala wa sheria unaoheshimu na kulinda haki za binadamu; itaendeleza mapambano dhidi ya rushwa bila ya woga wala kuoneana muhali.

• Tano, Serikali ya Awamu ya Nne itaimarisha uwezo wake wa kulinda maisha na mali za raia wake. Tutapambana na uhalifu wa kila aina, na majambazi hayataachwa yatambe yatakavyo;

• Sita, Serikali ya Awamu ya Nne itahakikisha mipaka ya nchi yetu ipo salama. Hatutamruhusu mtu au nchi yeyote kuchezea mipaka ya nchi yetu na uhuru wetu;

• Saba, Serikali ya Awamu ya Nne itafanya kila iwezalo kuhakikisha Tanzania ina mahusiano mazuri na mataifa yote duniani, pamoja na mashirika ya kimataifa na kikanda;

• Nane, Serikali ya Awamu ya Nne itajali sana maslahi na mahitaji ya makundi maalum katika jamii kama vile wanawake, vijana, watoto, wazee, walemavu na yatima;

• Tisa, Serikali ya Awamu ya Nne itaongoza mapambano mapya ya kuhifadhi mazingira ili vizazi vijavyo virithi nchi nzuri, na msingi imara wa maendeleo endelevu; na

• Kumi, Serikali ya Awamu ya Nne itaendeleza michezo, na shughuli za utamaduni na burudani.
 
Umoja wa Kitaifa Mheshimiwa Spika:

Umoja wa kitaifa wa Tanzania una pande mbili. Upande wa kwanza ni Muungano wetu; umoja wa nchi zetu mbili huru zilizoungana kuunda Jamhuri ya Muungano. Muungano wetu sasa una zaidi ya miaka 41, ni wa pekee barani Afrika. Pamoja na kuwepo matatizo ya hapa na pale Muungano bado ni imara na ni wa kujivunia. Upande wa pili wa umoja wa kitaifa ni umoja wa raia wenyewe, wanaojihisi wote ni Watanzania kwanza, bila kujali tofauti zao za kabila, dini, rangi, jinsia au eneo atokalo mtu Kazi mojawapo ya msingi ya Serikali nitakayoiunda ni kulinda, kudumisha, kuendeleza na kuimarisha Muungano wetu, kwa kufanya yafuatayo:

• Kwanza, kwa jumla tutakuwa makini na wepesi katika kushughulikia matatizo ya Muungano. Tutayazungumza kwa uwazi na kuchukua hatua muafaka kwa wakati muafaka;

• Pili, nitampunguzia Makamu wa Rais majukumu ya kuondoa umaskini ili apate muda wa kutosha wa kushughulikia masuala ya Muungano;

• Tatu, nitaimarisha taratibu zilizoanzishwa na Serikali zilizopita za kujadili, kuainisha na kutatua matatizo ya Muungano; na

• Nne, nitaangalia upya mchango wa Serikali ya Muungano katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Zanzibar, bila kuathiri haki na mamlaka kamili ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mambo ambayo si ya Muungano.

Mheshimiwa Spika:

Kwa upande mwingine, umoja wa Watanzania unahusu umoja miongoni mwa wananchi. Ipo hofu ya kweli miongoni mwa Watanzania kuwa bado wapo miongoni mwetu watu wanaotaka kuturudisha tulikotoka, tuanze tena kuulizana na kubaguana kwa misingi ya kabila zetu, rangi zetu, dini zetu, na maeneo tunayotoka. Nawasihi sana wanaowania uongozi, kuanzia ngazi ya chini kabisa hadi ngazi ya kitaifa—uwe uongozi wa kiserikali, uongozi wa kisiasa au uongozi wa kidini—wasitumie ubaguzi wa aina yeyote ile. Hawatavumiliwa na hawataachwa waigawe nchi.

Mheshimiwa Spika:

Nasononeshwa sana na mpasuko wa kisiasa kati ya Unguja na Pemba. Matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa 2005 yamedhihirisha mpasuko huo ambao naamini chanzo chake ni cha kihistoria. Lakini historia hiyo ni ya wanadamu, na wanadamu hawalazimiki kuwa wafungwa wa historia yao. Iweje Wapemba hawa ambao ni hodari wa kutumia fursa ya Muungano wetu kwa kuishi na kufanya biashara na kuwekeza katika pembe zote za Jamhuri yetu wawe hao hao wanaojitenga kisiasa kwa kiwango tulichoshuhudia kwenye Uchaguzi Mkuu?

Wakati umefika sasa wa kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa mpasuko huo. Nategemea ushirikiano mzuri kutoka kwa wanasiasa wa Tanzania-Zanzibar. Natambua kuwa uamuzi wa mwisho kuhusu hatma ya siasa na utawala Zanzibar ni wa Wazanzibari wenyewe. Lakini, Jamhuri yetu ni moja, na yanayotokea Zanzibar yanatugusa sote. Pengine leo ni zaidi kuliko ilivyokuwa katika historia wakati ulipokuwepo msemo kuwa zumari likipigwa Zanzibar wanacheza mpaka bara. Hivyo, basi, nitakuwa tayari kuanzisha, kuwezesha na kusaidia mjadala mpana juu ya mustakabali wa kisiasa Zanzibar.
 
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge:

Serikali ya Awamu ya Nne inakusudia, miongoni mwa mambo mengine, kuimarisha utaifa wetu kwa kufanya mambo kumi yafuatayo:

• Kwanza, kutumia mfumo wa elimu kujenga na kuimarisha umoja wa kitaifa, ikiwemo kutenga Shule za Sekondari za Kitaifa zitakazochanganya kwa makusudi wanafunzi wenye vipaji mbalimbali kutoka pembe zote za Tanzania;

• Pili, kuandaa mitaala ya somo la uraia itakayopanda mbegu za uzalendo na umoja wa kitaifa katika ngazi zote za elimu;

• Tatu, kuzipa changamoto shule za mashirika ya dini, isipokuwa seminari, kupokea wanafunzi wa dini zote;

• Nne, kuendeleza kazi nzuri iliyoanzishwa na Serikali ya Awamu ya Tatu ya kufufua Jeshi la Kujenga Taifa;

• Tano, kujenga muafaka baina ya vyama na makundi ya jamii juu ya utambuzi wa, na kuheshimu, tunu za kitaifa kama vile haki, usawa, umoja na mshikamano;

• Sita, kutumia michezo, nyimbo na sanaa kuimarisha hisia za utaifa na kujenga uzalendo na kuipenda nchi;

• Saba, kueneza na kuruhusu matumizi ya alama za kitaifa kama mambo ya kila raia kujivuna nayo na kuyaheshimu sana;

• Nane, kujenga na kuimarisha mahusiano kati ya dini, vyama vya siasa na makundi mbalimbali ya jamii;

• Tisa, kuteua Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais atakayeshughulikia mahusiano kati ya vyama vya siasa, dini na makundi mbalimbali ya jamii; na

• Kumi, kuimarisha utaratibu wa mazungumzo ili kutatua mapema migogoro katika jamii.
 
Amani na Utulivu Mheshimiwa Spika:

Zipo sababu kwa nini nchi yetu imekuwa, kwa kiwango kikubwa, kisiwa cha amani na utulivu katika bahari iliyotibuka. Mojawapo ya sababu hizo, kama nilivyosema, ni sera ambazo kwa makusudi zilijenga hisia za umoja, na hazikuwabagua wala kuwanyima haki Watanzania kwa sababu za dini, rangi, kabila, jinsia au eneo wanakotoka. Nitawatarajia watakaokuwa kwenye Serikali nitakayoiunda wasiwabague wananchi kwa sababu yoyote ile, na wawe watetezi thabiti wa haki za binadamu. Ningependa pia tuwe na maadili na miiko ya kitaifa kuhusu jambo hili.

Utawala Bora Mheshimiwa Spika:

Serikali nitakayoiongoza itazingatia na kuendeshwa kwa misingi ya utawala bora, uwazi na uwajibikaji. Tutaheshimu utawala wa sheria, na tutazingatia na kuheshimu mgawanyo wa madaraka kati ya mihimili mikuu ya dola, yaani Utawala, Bunge na Mahakama. Tutaheshimu uhuru wa Mahakama na Bunge; tutatimiza ipasavyo wajibu wetu; na tutawezesha mihimili hiyo kufanya kazi zake ipasavyo. Serikali ya Awamu ya Nne itaimarisha utendaji Serikalini na kupambana na maovu katika jamii bila woga wala kuoneana muhali.

Rushwa

Tutaongeza kasi ya kupambana na rushwa kisayansi kwa kushambulia kiini chake, na kuziba mianya yake. Tutajitahidi kuongeza mishahara na kuboresha maslahi ya watumishi wa umma ili kupunguza vishawishi vya rushwa. Tutaendelea pia kuongeza uwazi katika maamuzi ya Serikali hasa katika manunuzi na mikataba. Tutaimarisha uwezo wa kifedha na kiutendaji wa taasisi zilizo mstari wa mbele kwenye vita dhidi ya rushwa, hususan Taasisi ya Kuzuia Rushwa, Jeshi la Polisi na Mahakama. Lakini yote hayo ni bure iwapo wananchi hawatajitokeza kusaidia vyombo hivyo. Naomba ushirikiano huo kutoka kwa wananchi.
 
Katika harakati za kupambana na rushwa yapo mambo mawili mengine ambayo tutayaangalia kwa karibu. La kwanza ni mikataba. Tutaangalia upya taratibu za mikataba mbalimbali inayoingiwa na Serikali, mashirika ya umma na idara zinazojitegemea kwa nia ya kuongeza uwazi na uwajibikaji. Mikataba ni mwanya mkubwa wa rushwa hasa zile kubwa kubwa za wanaotafuta utajiri.

Kadhalika, hatuna budi kuchukua hatua thabiti za kuzuia watumishi wa umma kutumia nafasi zao kujitajirisha na kujilimbikizia mali. Sisemi kwamba ni haramu mtu kuwa tajiri au kuwa na mali. Ninachosema mimi kuwa ni haramu ni kutumia nafasi yako ya utumishi au uongozi wa umma kujipatia manufaa ya kujitajirisha au kujilimbikizia mali.

Jambo hili ndilo linalokera sana watu kuona mtu ambaye hana chochote lakini miezi michache tu baada ya kupata cheo anakuwa tajiri mkubwa. Ona majumba ya fahari, ona madaladala, teksi bubu, anaishi maisha ya kifahari na kadhalika. Wananchi wanayo haki kuhoji, na wanayo haki kupata majibu. Ndugu zangu, naomba tuwe waadilifu. Tusilaumiane. Nataka Tume ya Maadili ya Viongozi isione haya kutuuliza jinsi tulivyozipata mali tunazosema tunazo. Nitawasaidia kujenga uwezo wa kufanya hivyo kama tatizo lenu ni hilo.

Utendaji Serikalini Mheshimiwa Spika:

Dhana ya utawala bora ni pana sana; ni zaidi ya vita dhidi ya rushwa. Tutahimiza utekelezaji wa majukumu ya Serikali kwa ustadi, kwa haraka na kwa ufanisi. Tunataka watendaji wa Serikali wenye wawe waadilifu, na wanaowajibika; wawe na ari, moyo, na msimamo wa dhati kuhusu utumishi wa umma na huduma bora kwa umma. Tabia ya “Njoo kesho” na nenda rudi tuache. Mwalimu alituasa linalowezekana leo lisingoje kesho. Napenda huo uwe moyo wa utendaji Serikalini.

Natambua tatizo na malalamiko ya watumishi wa umma kuhusu mishahara na maslahi yao. Tutaliangalia. Tutalishughulikia. Nakusudia mapema iwezekanavyo niteue Tume ya Kuboresha Maslahi ya Watumishi wa Umma. Naomba niwatahadharishe kutokana na matumaini ya miujiza. Tutafanya kinachowezekana kadri uwezo wa Serikali unavyojengeka.
 
Back
Top Bottom