Mambo Jambo
JF-Expert Member
- Jul 11, 2008
- 1,100
- 82
Chanzo: TANZANIA DAIMA, 21ST JULY, 2008
na Anna Makange, Tanga
HII SASA KALI, KAZI KWENU WADAU
na Anna Makange, Tanga
RAIS Jakaya Kikwete, amewataka Watanzania kuwa wavumilivu kutokana na hali ngumu ya maisha inayowakabili kwa sasa, inayosababishwa na kupanda kwa bei ya mafuta duniani.
Rais Kikwete ametoa kauli hiyo katika kipindi ambacho Watanzania wengi, hasa wa kipato cha chini wamekuwa wakilia kutokana na kupanda kwa gharama za maisha.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana, wilayani Muheza, wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa wilaya hiyo, ikiwa ni siku ya tisa ya ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo, mkoani Tanga.
Rais Kikwete alisema kupanda kwa bei ya mafuta, kumechangia kwa kiasi kikubwa kulipuka kwa mfumuko wa bei za bidhaa mbalimbali duniani kote.
Alisema hali hiyo pia imechangia kuzorotesha kasi ya ukuaji wa uchumi hasa kwenye nchi zinazoendelea na hivyo watu wenye kipato duni kukabiliwa na hali ngumu ya maisha, hususan katika upatikanaji wa mahitaji muhimu, jambo ambalo aliongeza kuwa hata yeye limekuwa likimuumiza kichwa.
Ndugu zangu Watanzania wenzangu naelewa sana jinsi maisha yanavyozidi kuwa magumu siku hadi siku na hali hii inasababishwa na kupanda kwa bei ya mafuta hapa nchini, hivyo kila bidhaa kwa sasa gharama zake ni za juu sana, kuanzia vyakula hadi vitu vingine ambavyo ni muhimu kwa maisha ya kila siku. Linatuumiza sana hasa wale wananchi ambao ni maskini wa kipato, alisema Rais Kikwete.
Hata hivyo alisema Watanzania wasikate tamaa kwa kuona kwamba maisha yataendelea kuwa hivyo, na kusisitiza kwamba yeye kama Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) kwa kushirikiana na viongozi mbalimbali duniani wanalishughulikia suala hilo.
Wakati Rais Kikwete akiwataka Watanzania kutokatishwa tamaa na hali hiyo, Chama cha NCCR- Mageuzi, jana kilisema wananchi hawana sababu ya kuilaumu Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) kwa kupandisha bei ya nauli na badala yake lawama hizo zielekezwe kwa serikali ya Rais Kikwete.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Idara ya Oganaizesheni, Kampeni na Uchaguzi, Faustine Sungura, alisema kutokana na matatizo hayo, kuna haja ya kuwepo kwa serikali mbadala, kwa madai kuwa serikali imeshindwa kutatua matatizo yanayowakabili wananchi, hasa ya upandaji wa gharama za bidhaa mbalimbali.
Watanzania wanapaswa kujifunza kutokana na makosa, kwani muda waliowapa viongozi wa CCM kutawala unatosha na haujaonyesha mafanikio yoyote katika maisha zaidi ya kuzidisha ugumu wa maisha, alisema.
Watu wanakosea sana wanapoilaumu Sumatra badala ya kuilaumu serikali ambayo imeshindwa kudhibiti upandaji wa bei kwenye bidhaa mbalimbali yakiwemo mafuta, alisema Sungura.
Alisema hata ziara anazofanya Rais Jakaya Kikwete na Makamu wake, Ali Mohamed Shein ni dhihaka kwa Watanzania, kwani ahadi zao hazitekelezeki na wameshindwa kuwasaidia wastaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambao wanashinda Ikulu.
Hivi hawa ni viongozi wa aina gani kama wameshindwa kuwasaidia wazee wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanaoshinda pale Ikulu, wataweza vipi kuwasaidia watu wa huko mikoani? alihoji Sungura.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete amesema serikali itahakikisha inafanya kila jitihada za kutafuta wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kuwekeza kwenye kiwanda cha usindikaji wa matunda wilayani Muheza, kwa lengo la kuwatafutia wakulima wa machungwa soko la uhakika.
Alisema lengo la kujenga kiwanda hicho licha ya kumtafutia soko mkulima, lakini pia itakuza kipato cha wakulima sambamba na kupunguza kiwango kikubwa cha machungwa yanayoharibika mashambani kwa kukosa wanunuzi hasa nyakati za msimu.
Serikali inaamini kwa kufanya hivi tutakuwa tumemsaidia mkulima kwa kiasi kikubwa kuwa na soko la uhakika sambamba na kukuza kipato chake ambacho hivi sasa kinapotea kutokana na kiasi kikubwa cha matunda kuharibika nawaahidi kwamba hili tutalitekeleza haraka iwezekanavyo, alisisitiza Rais Kikwete.
Miongoni mwa ahadi alizotoa rais wilayani Muheza ni pamoja na kupeleka darubini katika zahanati ya Kijiji cha Kicheba, kuchangia sh milioni mbili katika ujenzi wa madarasa ya Shule ya Sekondari ya Mtindiro, sambamba na kutafuta magari ya wagonjwa katika wilaya zilizokosa huduma hiyo mkoani hapa.
HII SASA KALI, KAZI KWENU WADAU