JK unautaka urais kwa bilioni 50 kwa faida ya nani? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

JK unautaka urais kwa bilioni 50 kwa faida ya nani?

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Msongoru, Apr 21, 2010.

 1. Msongoru

  Msongoru JF-Expert Member

  #1
  Apr 21, 2010
  Joined: Apr 16, 2008
  Messages: 306
  Likes Received: 4
  Trophy Points: 35
  Paschally Mayega

  RAIS wangu, vitabu vitakatifu vimeandikwa kuwa huwezi kuwatumikia mabwana wawili, Mungu na Mali. Lazima utamchagua mmoja. Wakale walisema chema chajiuza, kibaya chajitembeza. Tumeamua kuitumikia mali badala ya Mungu. Bilioni 50 ni kibovu gani kitashindikana kuuzika?

  Tunakubali biashara ni matangazo, lakini bidhaa inayotangazwa kwa bei mbaya kiasi hiki jua ni mbovu kupindukia na haitoki. Mara ngapi umesoma au kusikia tangazo la chumvi? Swali ni je, baada ya CCM kufanikiwa kuwauzia wananchi kanyaboya nini kitafuata?


  Waliochangia sh bilioni 50 wataanza kurudisha fedha zao na faida kwa kuifisadi nchi. Hali hii itasababisha mfumko mkubwa wa bei. Maisha yatakuwa magumu zaidi kwa wananchi huku kanga, fulana na kapelo walizopewa wakati wa kampeni zikiwa zimechakaa na kuchanika. Pilau walizolishwa zitakuwa zimewatoka katika matumbo yao.


  Nyimbo walizoimbiwa wakati wa kampeni watakuwa wamezisahau, mbaya zaidi, wagombea wao waliowapitisha watakuwa hawawaoni tena. Ndipo watakapoingia mitaani kudai chao.


  Wanaoombea mgomo wa wafanyakazi ufanyike sasa wameona mbali kwa maana wanaombea maafa ahueni kuliko maafa yatakayotokea katika mgomo wa wananchi wote baada ya kushinda uchaguzi. Mgomo huo utakuwa wa wananchi wote wafanyakazi wakiwa ni sehemu ndogo tu.


  Tutakutana na vituko vya wakubwa katika nchi yetu na habari zetu zitaandikwa kwa herufi kubwa kama ile ya Kumarnbek Bakiyev, kiongozi wa Kyrgyzstan aliyeingia mitini kiana.


  Alitimkia nje akiwaacha nyuma kwenye Kijiji cha nyumbani kwao cha Teyit, wale ambao katika kipindi cha siku saba nyuma walisimama bega kwa bega na rais wao huyo. Wanawake wenye vimbelembele ambao walisimama kwenye jukwaa kubwa mjini Jalalabad wakiimba “Bakiyev! Bakiyev!” wakaachwa solemba.


  Nchi itatatuliwa mishono yake yote. Ndipo mtakapotambua kuwa mlikuwa mnajenga nyumba yenu juu ya mchanga. Kuvuliwa urais si lelemama ni zahama kubwa!


  Katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, tunashuhudia jinsi Chama Cha Mapinduzi kinavyotumia mabilioni kunadi wagombea wake ambao waliishapata nafasi ya kuonyesha uwezo wao kwa muda wa miaka mitano mingine zaidi.


  Kama ni bidhaa za CCM zimeishajaribiwa. Ubora wake au uduni wake uko wazi kwa kila mtu. Jitihada zinazofanywa kukusanya mabilioni mengi zaidi ili kuziuza bidhaa hizo ni ushahidi tosha wa udhaifu au uduni wa bidhaa zake.


  Mtu yeyote anayemwabudu Mwenyezi Mungu hawezi kutafuta hila za kuwauzia waja wake bidhaa mbovu. Na bidhaa zenyewe kama zisingetawaliwa na tamaa na uroho wa madaraka zisingekubali kuuzwa huku zikijua kuwa hazifai.


  Yatupasa kujiuliza, tunautaka urais wa mabilioni kwa faida ya nani? Mwanamwema Katherine wa Arusha anasema: “ Asante kwa ushauri wako kupitia makala yako. Nakupa hoja yangu. CCM haiwajali wananchi wake. Bil 50 zingewasaidia wananchi katika afya na elimu au CCM haina imani nasi? Atapita tu hata akiweka jiwe badala yake.


  Serikali imechukua fedha za wanachama wa DECI ikidai inatusaidia mpaka leo hakieleweki. Je, hili nalo si kwazo la uchaguzi? Taifa limekuwa kama nyumba isiyo na mwanaume.”


  Yatupasa tujiulize, tumewafanyia nini watu wetu mpaka watutake tena? Kama kusafiri tumesafiri kupindukia, tumewaletea nini Watanzania? Gerald anauliza Watanzania wenzake, “Habari mzee Mayega, heshima yako. Baba yuko USA , sijui safari hii atarudi na jezi ya mchezaji gani!”


  Tumeifanya nchi ionekane kama tiara iliyokata uzi na hivyo kuelea angani bila mwelekeo. Utawala wetu umekuwa ukizalisha watu wengi waliopewa dhamana ya kushika fedha za walipa kodi na kuzitumia kwa manufaa yao. Wananchi wanaambiwa mtu kanunua maua ya shilingi 42 milioni kupamba nyumba yake.


  Huyu mwingine kanunua mapazia ya nyumba yake kwa fedha ya walipa kodi milioni 17. Tunaambiwa majambazi yamevamia nyumba ya Mkurugenzi Mkuu wa NSSF na kuiba kiasi kikubwa cha fedha. Kiasi kikubwa cha fedha huyu ni benki? Fedha halali inatunzwa nyumbani kwa kiasi kikubwa? Wote hawa bado wako na kazi zao halafu tunataka wananchi watuchague tena ili tusimamie nini?


  Wanaotajwa katika wizi wa Kagoda, DeepGreen kuwa waliba fedha wakazitumia katika uchaguzi kukuingiza madarakani hujawashughulikia ingawaje kwa mara ya kwanza rais alichukua jukumu la kushughulikia jinai. Fedha walizoiba ziko wapi? Wanaosema baadhi zitatumika tena katika uchaguzi huu wanakosea wapi?


  Na wanaosema ukiacha wakashitakiwa watasema na wewe ulishirikiana nao maana ulikuwa ndiye bwana harusi tuwasahihishe vipi? Ndugu Rais, kumbuka maneno ya ndugu Augustine Lyatonga Mrema wakati wa kampeni 2005 aliwaambia Watanzania kuwa: ”Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete hafai kuchaguliwa kuwa Rais wa Tanzania kwa sababu hajawahi kukamata hata mwizi wa kuku tu.” Kwa matukio haya wananchi hawawezi kushawishika na kusema ndugu Augustine Lyatonga Mrema alikuwa sahihi?


  Mwanamwema Demfoo kutoka mbuga za wanyama Arusha anaandika, “Shikamoo Mwalimu Mkuu. Ebu waulize wanasheria na marafiki wa mahakama, ni kipengele gani katika katiba ya nchi yetu kinachomtambua mke wa rais? Mbona tumemwona huku Kilimanjaro akiwa na alama ya taifa? Yeye si mke wa mtu tu kama walivyo wake wa watu wengine? Au baba kamkabidhi? Mungu akujalie.”


  Naomba wanasheria wazamivu, Juvenalis Ngowi, Mary Muniwasa, Halima Mdee na marafiki wa mahakama watakaosoma makala hii wamjibu mwana mwema huyu na wenzake wengi walioniandikia wakilalamika kuhusu mama huyu kutumia gari lenye nembo ya Ikulu na ulinzi uliopindukia.


  Mimi si mzamivu katika mambo haya. Mjibuni kupitia ukurasa huu, kwa faida ya wana wa Kilimanjaro na Watanzania wote kwa ujumla. Tunayoyapokea kwa simu za mdomo kuhusu ajali ya mama yetu kule Musoma yanasikitisha na kukatisha tamaa lakini inaonyesha hasira kubwa walionayo wananchi mioyoni mwao kwa ziara za huyu mama. Kumwongezea ulinzi ni kuwaongezea mzigo wananchi lakini ni kuwaongezea hasira. Mioyo yao ni ya nyama itafika siku isiyo na jina itapasuka. Ole! siku hiyo!


  Mwingine akaandika: “Itabidi na kale kabwana ka miaka 11 tukapishe barabarani, ni kajumbe ka Halmashauri Kuu ya Taifa.” Halafu tunataka watuchague tena, mawe!


  Kwa mara ya kwanza nchi inashuhudia Ikulu ikitafutwa na nyumba nzima; baba, mama na watoto. Wananchi wamebebeshwa mzigo mzito. Malalamiko ya wananchi sasa yako kila sehemu nchi nzima. Malalamiko haya ndiyo yanayoonyesha jinsi watafuta Ikulu wanavyolazimisha kuchukiwa na wananchi. Wakifanikiwa kuipata kwa hila, au kwa fedha au kwa ujanja mwingine wowote watakuwa wamejiweka katika hatari kubwa na amani ya nchi itakuwa juu ya ncha ya wembe.


  Rais wangu tunaambiwa kuwa mtandao ulianza na watu watano. Lakini ni mantiki ya kawaida inayotufanya kujua kuwa kila jambo zito huanza na mtu mmoja. Wengine wanapoingia huwa ni kuwezesha au kuboresha wazo. Mwenye wazo mara nyingi ndiye huchukua madaraka baada ya mafanikio. Kilichotokea katika mtandao huu hakikuwa hivyo.


  Kichwa na mwenye mtandao hakuchukua uongozi wa juu wa nchi. Laiti kama angelikuwa amezingatia habari za John Okello wa mapinduzi ya Zanzibar angechukua tahadhari. Mara nyingi tumeona katika historia watu hawa huuawa. Kilichofanyika ndani ya CCM mwaka 2005 yalikuwa ni mapinduzi kama yalivyo mapinduzi mengine yoyote tunayoyafahamu.


  Wote wanaofanikisha mapinduzi na kuitwaa nchi, ili wabaki na amani katika vifua vyao huwaua au kuwapoteza wote walioshirikiana nao. Kama viongozi hawakuwaua washirika wao, basi washirika wao huwaua viongozi wao kama ilivyokuwa kwa Thomas Sankara.


  Kwa sababu kilichofanywa na mtandao ni mapinduzi, basi sheria ya mapinduzi ilikuwa ni lazima ifuatwe. Waliotaka kumpoteza kichwa walifanya kosa kubwa kwa maana hawakumuua. Walijitahidi kumfunika na kumfukia wakidhani amekufa kumbe hakufa. Sasa anapotutumka akiibuka, uongozi uliopo utasimamia wapi? Katika historia tunaona visasi vilivyomwaga damu nyingi sana. Ni kitu gani jamani kinachoendelea katika nchi yetu?


  Rais wangu tunataka kuendelea na urais wetu kivyetu vyetu kwa kutumia chochote kilichopo katika uwezo wetu. Hili ni kosa kubwa. Kilichotungwa kimetungwa na aliyekitunga ana hiari ya kukitungua pale atakapotaka kufanya hivyo.


  Ni upofu tu na ulevi wa madaraka unaoweza kufanya mtu afikirie kuwa inawezekana kuustawisha mti kwa kustawisha matawi yake na kuiondoa mizizi. Kwa sababu sisi si kichwa kampeni zetu ni mufilisi.


  Tunadhani ni kampeni za kutusaidia kumbe ndiyo zinatumaliza. Tunawasikiliza hata wanaume wapayukaji tu au kufuata ushauri wa mama zetu ambao uwezo wao ni wa “kitchen party” au mafundi wa kucheza ngoma za Waswahili. Ushauri wa watu hawa utatusaidia nini tunapohitaji uongozi imara wa nchi?


  Serikali ya Awamu ya Nne ilianza na idadi kubwa sana ya mawaziri. Kasoro kubwa ya kwanza iliyoonyesha lengo na mwelekeo wa wanamtandao wa kufaidi kwa kutawala na kuchuma mali kwa gharama ya nchi na wananchi wake. Na kamwe, si kutumikia wananchi. Haya yamethibitika kama tutakavyoyaeleza huko mbele ya safari.


  Rais wangu, kasoro kubwa iliyofuata ni pale ulipowakusanya viongozi wa nchi nzima na kuwaweka katika hoteli za kitalii kwa gharama kubwa. Ilionekana kama vile wewe haukuwa katika serikali zilizopita na hivyo umekuja na kitu kipya.


  Wananchi kutokuona kipya kilichotokana na semina ghali elekezi wametafsri kuwa ule ulikuwa ni ufujaji mkubwa wa fedha za walipa kodi.


  Kama siku moja wanaokuja watasema ni matumizi mabaya ya ofisi na kuisababishia serikali hasara kubwa sitashangaa kuja kuwaona watu Kisutu wakijibu mashitaka.


  Rais wangu, katika miaka yako miwili ya kwanza serikali yako ilikuwa na ubavu wa kuyafukia haya. Ulipokuwa ukiyapasua mawingu angani waziri mkuu wako alikuwa anapasua barabara za nchi kuwathibitishia watu wako kuwa serikali ingalipo na inatenda kazi.


  Shule za kata zilianza kuota kama uyoga kila mahali na ile ahadi ya zahanati za kata ilikuwa inajaribu kuonyesha wananchi kile ambacho labda kilikuwamo katika ile ahadi kuu ya maisha bora kwa kila mwananchi. Leo kila kitu kimekufa au kusinyaa. Ahadi ya maisha bora kwa kila mtu inaonekana ni ulaghai wa hali ya juu. Mtu laghai nani atamtaka tena?


  Kuna kelele za ombwe! Ombwe! Kutoka kila pembe ya nchi yetu. Mafisadi waliokuwa wamejificha katika vita bandia dhidi ya ufisadi sasa wanajitokeza hadharani. Mwana mwema aliniandikia akisema, “Ikiwa utakuwa na muda, msikilize nyangumi leo saa tatu usiku”.


  Nilipokuwa nikitazama nikaletewa ujumbe na mwana mwema mwingine ukisema, “Hivi Mwalimu na wewe unaona ninachokiona? Watu wazima wanaunda kwaya ya kanisa wakiimba wimbo wa dini unaomtaja Mungu kumwombea na kumsifia mtu fisadi.”


  Naamini fedha za mafisadi zinaweza kununua hata wanakwaya, wachungaji, mapadri, masheikh na wote wengine wanaojiita watumishi wa Mungu lakini hata kama nyumba yetu imekosa mwanamume kama anavyosema dada Katherine, dini zetu lazima ziheshimiwe.


  Rais wangu, nilichokiona kilinipeleka moja kwa moja mpaka Nyamongo, mkoani Mara. Emongo au chimongo, Wakurya wanasema ni wadudu wanaokula mazao yaliyohifadhiwa. Nyamongo ni sehemu maarufu kwa madini ya dhahabu kule wilayani Tarime.


  Leo makampuni yanayotafuna madini yetu na kujineemesha huku yakiacha wananchi hohehahe yanafanananishwa na chimongo. Wachimbaji wa asili wametupwa nje ya ardhi na utajiri wao waliopewa na Mwenyezi Mungu. Wamejengewa uzio unaowatenga na kampuni za uchimbaji madini za waporaji.


  Baba, mwana mwema Marura anakumbuka ziara yako mwaka jana mgodini hapo na anasema, “Alikuja hapa Rais Jakaya Kikwete na kuzungumza na mwekezaji. Baadaye akatuambia atasaidia kuwapo mazungumzo ili tusiuawe na askari wa mgodini; tuletewe maji safi, tupate umeme na fidia ifanyike kisheria.


  “Lakini siku hiyo hiyo alipoondoka rais tu, askari wa mgodini waliua mwananchi mmoja aitwae Mussa Warema Nyahiri. Na hadi leo hakuna maji safi wala umeme, na sumu itokanayo na kemikali za mgodini bado inatiririka kwenye makazi ya mwananchi”.


  Katika hali kama hii anapotokea mtu na kwenda mgodini, naye akishaafikiana na mafisadi wenzake ambao wakati wakutafuta uhuru waliitwa wakoloni; anatoka nje ya mgodi na kuanza kuwatukuza waporaji mbele ya wananchi wanaoteseka, ni kuwafanya wananchi wapumbavu.


  Kuwataka wahanga wa mgodi sumu huu wauite mgodi ule ni wao, ni sawa na kuwaambia hawana akili! Serikali inapomnyamazia mtu kama huyu inaulinda mfumo unaozalisha wezi upande mmoja na wale waliokata tamaa upande wa pili.


  Ndugu Rais, ni kweli nyumba yetu imekosa mwanaume wakumfokea mtu huyu? Kama kila fisadi atatafuta sehemu yake ya kuabudiwa; huyu aende mbuga za wanyama, mwingine kwa wavuvi haramu na wengine katika biashara nyingine haramu nchi itasalimika? Amani ya nchi itapotea! Tumuogope mtu huyu kama ukoma!


  Rais wangu, naamini katika uwezo wa wanawake lakini kama ambavyo si wanaume wote wanaweza wako wanawake pia ambao hawawezi mfano mzuri ni hawa baadhi ya wake zetu wanaochefua badala ya kusafisha.


  Siungi mkono viti vya upendeleo kwa wanawake, wengi wameonyesha kutoweza lakini wachache wao kama dada yetu Halima Mdee, Batilda Burian wameonyesha uwezo mkubwa.


  Hawa ni wanawake jasiri mfano wa dada yetu Ananilea Nkya. Ananilea alipotangazwa kuwa mwanamke jasiri hakuna mguno wowote uliosikika kutoka kokote nchi nzima. Kwakuwa wanaweza wameamua kwenda kupambana majimboni. Mwenyezi Mungu atawaangazia mwanga wake.


  Dada Batilda wewe unatoka Arusha, Mkoa alikotoka kiongozi shujaa kipenzi cha Watanzania Edward Moringe Sokoine; mwongoze basi mdogo wako Namelock, mtoto wa marehemu njia ulizopitia ili wewe ukiwa mbunge jimboni naye awe mbunge bungeni. Uwezo wenu unarandana sana na uwezo aliokuwa nao marehemu.


  Batilda, tunakulilia tunapoililia damu ya hayati Sokoine kwakuwa sasa tumepondekapondeka mioyo yetu naye wakutufariji hatumwoni. Nasi tumekuwa si watu tena bali mzaha wa wanadamu. Ndugu Rais tujaribu basi wanawake jasiri wa kweli huja wakaikwamua nchi hii kutokana na ufisadi.


  CHANZO: Tanzania Daima
   
 2. Gaijin

  Gaijin JF-Expert Member

  #2
  Apr 21, 2010
  Joined: Aug 21, 2007
  Messages: 11,850
  Likes Received: 57
  Trophy Points: 0
  mmtu hufata status ya urais tu .............kama si rais angeonana na barack obama?! angefika holywood?, angevaa suti za Milano?

  hivi ndo anavyofikiria
   
 3. Tumain

  Tumain JF-Expert Member

  #3
  Apr 21, 2010
  Joined: Jun 28, 2009
  Messages: 3,158
  Likes Received: 9
  Trophy Points: 0
  Ili awe rais wa Tanzania kwa faida ya watanzania period!
   
Loading...