JK tumia nguvu ya Katiba kuvunja uongozi CCM | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

JK tumia nguvu ya Katiba kuvunja uongozi CCM

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by nngu007, May 8, 2011.

 1. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #1
  May 8, 2011
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 56
  Trophy Points: 145
  Na John Kibasso
  [​IMG]

  JUHUDI za Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete za kutaka kukinusuru chama baada ya kubaini kwamba kimepoteza mvuto na haiba mbele ya jamii kwa kutumia falsafa mpya ya kujivua gamba hapana budi kikatazamwa upya kwa nia njema ya kuinusuru nchi kutojitumbukiza kwenye malumbano yasiyokuwa na tija kwa taifa.
  Uamuzi wa chama tawala kupitia kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (CC) hatimaye kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya kuwapa baadhi ya wajumbe wake nafasi ya kujiuzulu nafasi zao za uongozi ndani ya siku 90, binafsi nadhani chama hakijawatendea haki kwa mujibu wa Katiba ya CCM Ibara ya 14 (4). Katibu Mwenezi na Itikadi wa CCM, Nape Nnauye ndiye kinara wa mbiu hiyo.
  Kwa faida ya wasomaji, haki za mwanachama kimewekwa wazi katika Katiba ya CCM Ibara ya 14 (4) kisemacho ‘Haki ya kujitetea au kutoa maelezo yake mbele ya kikao cha CCM kinachohusika katika mashtaka yeyote yaliyotolewa juu yake, pamoja na haki ya kukata rufani ya kwenda katika kikao cha juu zaidi cha CCM kama kipo endapo, hakuridhika na hukumu iliyotolewa.’
  Kwa tafsiri ya Ibara hiyo nashawishika kuamini kuwa, kikao cha (NEC) Taifa hakikuwapa nafasi watuhumiwa hao kujitetea au kutoa maelezo yao mbele ya kikao ingawa wote walikuwa ni wajumbe halali wa kikao hicho cha NEC.
  Awali ya yote ningependa kuweka wazi kuwa hakuna mtu yeyote miongoni mwa hao watuhumiwa watatu walioniomba niwatetee ila mimi nikiwa mzalendo wa nchi hii nimehisi kuwapo kwa dhuluma ambazo zinagusa haki na uhuru wa mtu kikatiba.
  Wazee wetu walikuwa na msemo kuwa, mto ukifurika kwa sababu ya kunyesha kwa mvua kubwa, mafuriko hayo ya mto yatazoa takataka zote na kupeleka ziwani au baharini.
  Kwa maana nyingine mvundo na uozo ndani ya CCM haziwezi kuwalenga wajumbe watatu tu bali dhana hii ya kujivua gamba ingeanzia ngazi ya Taifa hadi chini ili kubaini viongozi wote mafisadi ndani ya chama.
  Jamii wamesikika wakimlaumu Mwenyekiti wa CCM kuwa ameshindwa kuwachukulia hatua za kisheria mafisadi wanaomzunguka hususan ndani ya chama (CCM).
  Binafsi, naamini kwamba mafisadi ndani ya CCM au ndani ya vyama vingine siyo hawa watatu wanaotajwa bali wako wengi kuanzia ngazi ya taifa, mkoa, wilaya hadi kata.
  Uchaguzi Mkuu uliopita jamii walishuhudia wagombea wakizidiana kete katika nafasi walizoomba kwa kutumia nguvu za uchumi.
  Uchafu, uozo, uvundo na mikakati ya kimafia zilioenekana kutumika hadharani na wala hazikutendwa na hawa watuhumiwa watatu. Ufisadi uligusa watu wengi nchi nzima.
  Nionavyo mimi, nadhani Mwenyekiti wa CCM Taifa, Jakaya Kikwete pamoja na nia yake nzuri ya kuamua CCM kujivua gamba angekubali kupiga hatua kubwa zaidi ya kuagiza harakati hizi za mabadiliko ndani ya chama zianzie ngazi ya taifa hadi vijiji.
  Kwa kuwa chama kimepoteza mvuto na haiba mbele ya jamii na kwa kuwa chama kinahusishwa na mafisadi basi yafaa mwenyekiti akubali kutumia Katiba ya chama kuwavua nyadhifa zao viongozi wote ndani ya chama kuanzia ngazi ya Taifa hadi vijijini ili uchaguzi uitishwe upya.
  Mwenyekiti wangu Jakaya Kikwete kwa heshima hebu rejea Katiba ya chama Ibara ya 75 vifungu viwili vya (3) na (4) kuhusu kazi za mkutano mkuu wa CCM Taifa visemavyo (3) kuthibitisha, kubadili, kukataa au kuvunja uamuzi wowote uliotolewa na kikao chochote cha chini yake au na mkuu yeyote wa CCM. (4) kubadili sehemu yeyote ya Katiba ya CCM kwa uamuzi wa theluthi mbili za wajumbe walio na haki ya kupiga kura kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili kutoka Tanzania Zanzibar.
  Kwa kuwa uamuzi wa chama cha kujivua gamba ni kitendo kinachogusa watanzania wote kwa hisia chanya na hasi, na kwa kutambua kuwa haki za msingi zinahesabika pale mtu akishafikishwa mbele za sheria na kuthibitishwa tuhuma zinazomkabili, na kwa kuwa kitendo hiki ni cha kihistoria ndani ya chama, nadiriki kutamka kwamba ili haki itendeke bila kuwepo na hisia za uonevu basi Mwenyekiti Kikwete anapaswa kutumia kifungu hiki cha Katiba Ibara ya 75 ama kifungu kidogo cha (3) au cha (4).
  Binafsi ningefarijika endapo Mwenyekiti angetumia kifungu cha (4) kinachoruhusu wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM- Taifa kubadili sehemu yoyote ya Katiba ilihali nguvu za sheria zipatikane kumruhusu kuvunja uongozi mzima wa CCM kuanzia ngazi ya taifa hadi vijijini.
  Uamuzi huu wa kijasiri utatoa uwigo mpana wa demokrasia na kitathibitisha uzoefu na umakini wa CCM katika kuamua mambo mazito bila kuingiliwa wala kualazimishwa kwa sababu zozote zile za kisiasa au kijamii.
  Tukubali tusikubali, mafisadi wanaosemwa nao ni sehemu ya Watanzania. Kama tunakubali kuweka mambo wazi hatutakuwa tunawatendea haki hawa watatu peke yao kwa sababu wanachama wa vyama vyote wawe CHADEMA, CCM, UDP, NCCR – Mageuzi, TLP na vyama vingine vilivyosajiliwa karibu wagombea wao wote walitumia ufisadi wa kisiasa hadi kufanikiwa kushindwa nafasi zao.
  Hakika ningependa kuwatahadharisha wana CCM kuwa, wajumbe hawa watatu wakienguliwa ndani ya chama, wasitarajie CCM kubaki salama. Wala CCM wasitarajie kuwa chama kitakuwa kimesafishika mbele ya jamii eti kwasababu mafisadi watakuwa wamekwisha la hasha.
  Ikumbukwe kwamba Dk. Willbrod Slaa katika Uwanja wa Mwembe Yanga aliwataja watuhumiwa 11 na hivi majuzi amewataja watuhumiwa (mafisadi) wengine wapya sita. Je, wote hawa wataenguliwa? Hata kama nao pia watakuwa wameenguliwa je huo ndio utakuwa mwisho wa mafisadi? Mbona wengi wametajwa kuwa wapo serikalini na wengine ndani ya CCM katika ngazi tofauti tofauti?
  Ieleweke wazi kuwa viongozi wa CHADEMA ni watu makini sana, natamka wazi wazi kuwa hawa mafisadi (watuhumiwa) wakienguliwa ndani ya chama, hakika watapokewa na CHADEMA tena kwa vifijo, nderemo na vigelegele na hakika wataonekana lulu huku wakitumiwa kuiangamiza CCM.
  Njia pekee ya kumaliza utata huu wa kujivua gamba ni kwa Mwenyekiti Jakaya Kikwete kukubali kuitisha mkutano mkuu wa CCM Taifa kabla ya muda kikatiba ili waridhie kifungu kidogo cha (4) Ibara ya 75 ambacho kitamruhusu Mwenyekiti kutamka kuvunjwa rasmi kwa uongozi mzima wa CCM kuanzia ngazi ya Taifa hadi vijijini ili uchaguzi uitishwe upya.
  Kwa kufanya hivyo, uongozi mpya utakaoingia madarakani watakuwa ni wale watakaopitishwa na wananchi badala ya uongozi wa juu wa chama. Isitoshe viongozi hawa wapya watachujwa kulingana na taratibu, kanuni na miiko ya uongozi.
  Binafsi nashawishika kuamini kwamba kama Mwenyekiti ataamua kuvunja uongozi mzima wa CCM nchini, hapo ndipo falsafa ya kuvua gamba itakapokubalika na jamii nzima ya watanzania.
  Ni imani yangu kuwa, hatua hii ya kuvunja uongozi wa CCM Nchi nzima, kitaijengea CCM heshima kitaifa na kimataifa. Isitoshe hatua hii itamwongezea heshima kubwa Mwenyekiti Kikwete na kubwa zaidi kitaepusha malumbano ya viongozi kuchafuana hadharani mbele ya jamii.
  Hatua hii ingawa itakuwa ya gharama kubwa lakini itaondoa lawama ya kuonekana kuwa baadhi ya watu wametoswa eti ndio mafisadi wakati, nchi hii kuna mafisadi wakubwa (Papa) ambao wanawazidi hata hao maradufu.
  Nadhani tujenge tabia ya kuheshimiana, hakuna mtu aliye msafi duniani. Akithibitika mtu kuwa ni fisadi ni vema akafikishwa mbele ya vyombo vya sheria ili aweze kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria, kama walivyo wahalifu wengine nchini.
  Vinginevyo tukianza kuwanyooshea vidole watuhumiwa watatu tu kati ya watanzania milioni 40 hatutakuwa tunawatendea haki. Ufagio wa chuma pamoja na kujivua gamba ndani ya chama yapaswa utumike kumulika viongozi wa ngazi zote kuanzia taifa, mkoa, wilaya hadi vijijini.
  Mafisadi hawapo kwenye vyama tu, bali hata kwenye taasisi binafsi (NGO’s) serikalini, makanisani na misikitini.
  Mwenyekiti Kikwete, njia pekee ya kumaliza malumbano haya ni kwa yeye kuamua kuteua kamati maalumu ya muda itakayoongoza chama baada ya kuvunja uongozi wote uliokuwepo kuanzia ngazi ya taifa hadi mashina.
  Bila kumumunya maneno, Mwenyekiti Kikwete atakuwa amekata kilimi cha wanafiki, wababaishaji, waropokaji, wafitini, wachochezi na wale wote wenye kidomo domo ndani ya chama. Hakika atakuwa ameepusha kuongeza maadui katika kipindi hiki kilichobaki cha kumaliza muda wake.
  Kama jamii wanahitaji imani mpya haiba mpya na Tanzania mpya inayokwenda na wakati, hapana budi waiunge mkono hoja yangu hii ili watakaokuwa wagombea wapya wa chama wachujwe na jamii. Waridhishwe na jina la mtu wanayemtaka.
  Kwa njia hii majina yote yanayotajwa kuwa ni mafisadi yatachujwa kabla ya kupigiwa kura. Namalizia makala haya kwa kumshauri Mwenyekiti Kikwete atumie falsafa yake ya kuvua gamba kwa kuivulia mbali uongozi mzima wa CCM kuanzia ngazi ya Taifa kwenye mashina. Kwa kufanya hivyo dhana nzima ya kujivua gamba itakuwa imeleta heshima bila malumbano.
  Mwandishi wa makala haya ni mwanamageuzi. Anapatikana kwa simu: 0713 399 044 au 0767 399 004.
   
 2. M

  Malila JF-Expert Member

  #2
  May 8, 2011
  Joined: Dec 22, 2007
  Messages: 4,410
  Likes Received: 734
  Trophy Points: 280
  Hivi siku tisini zinaisha lini vile? Nasubiri kuiona siku ambayo watuhumiwa watatimuliwa ktk chama chao.
   
Loading...