JK atoboa siri:Asema maadui walitambika mchana na usiku kuiua CCM, Walitaka kiwe Vipande Vipande

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797

IJUMAA, NOVEMBA 16, 2012 09:39 NA DEBORA SANJA, DODOMA


*Asema maadui walitambika mchana na usiku kuiua CCM
*Adai walijipanga kuona chama kinagawanyika vipande vipande
*Asisitiza kuanzia makada wote kupitia chuo cha Ihemi


MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, amesema watu waliokuwa wanaombea chama hicho kigawanyike vipande vipande baada ya mkutano mkuu wa nane wameumbuka. Alisema kuna watu walikuwa wanatambika mchana na usiku, kuombea anguko la CCM, baada ya kumalizika kwa mkutano wao wameshindwa.


Rais Kikwete, alitoa kauli hiyo mjini Dodoma jana, wakati akizungumza katika hafla fupi iliyoandaliwa na CCM Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya kumpongeza yeye, makamu wenyeviti na sekretarieti mpya.


"Nawashukuru wananchi wa Dodoma kwa kutupokea vizuri na kutuandalia mkutano ambao umeanza na kumalizika salama, hakuna tukio baya lolote lililotokea.


"Mimi pamoja na makamu wenyeviti Bara na Visiwani na Sekretarieti, tunarudisha pongezi kwa wajumbe wa mkutano mkuu kwa kura za kishindo walizotupigia.


"Natambua uamuzi huu wa kutupa kura za kishindo, umekuwa wa majonzi kwa baadhi ya watu wasioitakia mema CCM, wao walikuwa wanataka iharibike, walikuwa wamekaa pembeni wakisali, wakitambika usiku na mchana, wakiomba CCM itoke katika mkutano ikiwa vipande vipande.


"Sasa haijatokea hivyo, CCM imemaliza ikiwa imara zaidi na imetoka na umoja, japo najua bado hawajachoka wataendelea, lakini hawa wanaoiombea mabaya nadhani hawakijui chama chetu.


"CCM inao viongozi makini wanaojua jema na baya kwa chama chao…kubwa zaidi wanajua lipi lina maslahi kwa chama na lipi halina maslahi.


"Wajumbe waliowategemea wafanye ubaya hawajafanya hivyo, ningeshangaa kama ingetokea kama vile walivyotaka baadhi ya maadui zetu, ndio maana mimi sikuwa na wasiwasi niliposikia maneno huku na kule, lakini nikawaambia hayo hayawezi kutokea kwa kuwa mimi nakijua chama kilivyo, hizo ni hadithi za mchana.


"Wametumia nguvu kubwa kupoteza wakati kwa kuomba mabaya, mipango hiyo haikuwepo japo watu walikuwa wanatamani itokee.


"Mimi kabla ya kuanza mkutano ule nilijua ulikuwa ni mkutano wa kufa na kupona, ilikuwa lazima tutoke na nguvu mpya tena ya juu, nilijua tungetoka na nguvu ya chini tu, hatuibuki katika uchaguzi wa 2015.


"Na kama tukitoka na nguvu ya juu, ni jinsi gani tumeilinda nguvu hii hadi mwaka 2015, sasa tumetoka kwenye mkutano na nguvu ya juu, kazi iliyobaki ni kwenda na kasi, ari na nguvu hadi tushinde mwaka 2014 kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa na mwaka 2015 katika uchaguzi mkuu…inawezekana kwa CCM, timiza wajibu wako," alisema Rais Kikwete.


Akizungumzia viongozi wapya, wakiwemo wajumbe wa NEC, alisema safari hii ameamua kubadilisha utaratibu wa kuwapata wajumbe wa Kamati Kuu (CC) ili kupata safu imara kwa kuchagua watu wa aina mbalimbali.


"Nataka safari hii kupata wajumbe wa Kamati Kuu wenye ujuzi katika maeneo mbalimbali, ambao watakisaidia chama kutekeleza ilani ya uchaguzi na nataka muda wote wajishughulishe na shughuli za chama.


"Idara zetu zote, kama vile idara ya Oganaizesheni, mambo ya nje, uchumi zitahusisha pia baadhi ya wajumbe wa NEC, yule ambaye naona atakuwa ‘busy' na biashara zake aendelee na biashara hizo.


"Nataka wajumbe wa NEC wachemke kweli kweli kuanzia sasa, tunapoelekea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2014 na uchaguzi mkuu 2015, hatupaswi kulala," alisema.


Alisema kazi ya kwanza ya Sekretarieti ni kutengeneza mpango kazi wa utekelezaji wa maazimio yote yaliyotolewa katika mkutano mkuu kwa ajili ya kuyawasilisha kwenye kikao cha NEC kijacho ili yaanze kufanyiwa kazi na chama na Serikali.


Alisema katika kuimarisha utendaji kazi ndani ya chama, CCM imepanga kuanzisha programu ya mafunzo kwa viongozi ambapo kwa wajumbe wa NEC mafunzo yataanza mwezi ujao.


"Kuanzia sasa hakuna kupumzika hadi mwaka 2015 ili tuchukue Serikali tena, mafunzo hayo baadaye yatatolewa kwa viongozi wa mikoa, wilaya na katika ngazi za chini.


"Tunajenga chuo chetu cha Ihemi ili kianze kutoa mafunzo hayo kwa viongozi na makada wa chama, chuo ambacho kitasimamiwa na Katibu Mkuu mstaafu, Wilson Mukama," alisema Rais Kikwete.


Awali akimkaribisha Rais Kikwete, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa, aliwapongeza viongozi wote wapya.


Alisema CCM imepata safu thabiti ya uongozi wa juu ambayo itakisaidia chama pamoja na mambo mengine, lakini pia kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa mwaka 2014 na 2015.


Katika halfa hiyo mbali na Rais Kikwete, viongozi wengine waliopongezwa ni Makamu Mwenyekiti Bara, Philip Mangula, Makamu Mwenyekiti Zanzibar Ally Mohamed Shein, Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar
, Vuai Ally Vuai.


Wengine ni Naibu Katibu Mkuu Bara, Mwigulu Nchemba, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, Katibu wa Oganaizesheni, Mohamed Seif Khatibu, Katibu wa Fedha na Uchumi, Zakhia Meghji na Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Dk. Asha- Rose Migiro.
 

Inaonyesha hapa RAIS anaficha kitu; kiko akilini Mwake au Moyoni Mwake... Hajui kukitoa na kukitupa AU Hajui jinsi ya kukileta Karibu na yeye...

Hata WAJUMBE wa CCM-NEC anashindwa kuwateuwa...
 
Ni madui wa nje au wa ndani ya CCM? Kwa nini asiwataje? Au naye hana ushahihidi?
 
Kwani uchaguzi wa Serikali za mitaa (2014) na wa urais/wabunge/Madiwani (2015) utafanywa na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM? Wananchi tunataka kuona ahadi mlizotulaghai tukawapa dhamana ya kuongoza dola, Leo mnatueleza matambiko yenu. Badala ya kupigania maendelo ya nchi,,nyinyi mnapigania kubaki madarakani ili mlinde na kuendeleza ufisadi. Tunnawasubiri kitaa 2015.
 
Kweli CCM wana mwenyekiti, hivi nio lini huyu jamaa atatoa statement ikatambulikana kuwa imetolewa na Mwenyekiti, yaani kila siku statement zake kama za Mpiga Debe bhana Kha, hebu mfundisheni huyu jamaa jamani, anatia aibu
 
wanaandaa viwanda vya uongo kwa ajili ya chaguzi zijazo. Hao aliowateua karibu wote hawana jipya aka mafisadi
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom