KadaMpinzani
JF-Expert Member
- Jan 31, 2007
- 3,716
- 86

:: Akataa nchi kuwa shamba la wajinga
:: Aagiza wababaishaji wageni wasipewe kazi
:: Mkandarasi Sam Nujoma aonjeshwa joto
:: Awageukia TANROADS na bomoabomoa zao
Na Godfrey Dilunga, Singida
RAIS Jakaya Kikwete (pichani) sasa amewageukia wanataaluma na watendaji wa Serikali katika kuhakikisha udhibiti wa fedha za umma unaimarika, akisema nchi haiwezi kuendelea kuwa shamba la wajinga.
Rais alitoa msimamo wake huo kwa kauli kali, mara baada ya kusomewa taarifa ya ujenzi wa barabara mbalimbali nchini, ikiwamo ya Dodoma-Singida, hususan kipande cha Isuna-Manyoni, chenye urefu wa kilomita 55, jana.
Taarifa hiyo ilisomwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu, Omari Chambo, katika eneo la Isuna, barabara kuu ya Dodoma-Singida.
Katika taarifa yake iliyoamsha ari ya Rais kutaka fedha za umma alizoziita fedha za masikini, Chambo alisema baadhi ya makampuni ya ujenzi wa barabara nchini yameshindwa kutimiza wajibu wao kikamilifu.
Alisema hatua ambazo Serikali imechukua dhidi ya kampuni hizo ni pamoja na kuwafukuza baadhi ya makandarasi na wengine kuwakata fedha ya tozo. Aliwataja wakandarasi waliofukuzwa na Serikali kuwa ni pamoja na aliyekuwa akijenga barabara ya Dodoma-Singida, Kigoma-Lusahunga (mkoani Kagera) na kipande cha barabara ya Mbwemkuru-Lindi. Kwa upande wa makandarisi watakaokatwa fedha za tozo ni pamoja na anayejenga barabara ya Sam Nujoma, Dar es Salaam.
Akimzungumzia mkandarasi huyo, Chambo alisema; Si busara kumfukuza kwa wakati huu, bali adhabu anayopewa na Serikali ni kukatwa fedha za tozo.
Baada ya taarifa hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Parseko Korne, alipanda jukwaani na kumkaribisha Rais kuzungumza na wananchi waliokusanyika katika eneo hilo, ambalo pia Rais aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa kipande hicho cha barabara.
Akitumia maneno makali kuonyesha kukerwa na makandarasi na namna fedha za umma zinavyotumika ovyo, Rais alisema: Kinachowaponza ni kutafuta mkandarasi wa gharama nafuu mno isiyolingana hata na tathmini yenu.
Akasema: Bure ina gharama. Kilichotokea ni fundisho. Thamani ya ujenzi wa barabara mnaijua kwa sababu mnatakiwa kwanza mfanye tathmini ya awali, sasa mkandarasi anajitokeza kwa bei nafuu kuliko tathmini yenu mnamkimbilia, mnampa tenda. Baadaye kazi inafika katikati analalamika gharama za ujenzi zimepanda, fedha haitoshi mnaanza makubaliano mapya. Msiwape kazi makandarasi wa namna hii.
Kwanza...hivi hamna namna ya kuwaadhibu. Nadhani sasa wakitokea makandarasi wa namna hii, ambao wengi ni wa kigeni wasipewe tena kazi popote nchini.
Lazima tuonyeshe kuwa wakali. Hawa wananyonya fedha zetu. Sisi ni nchi masikini, wao wanatoka nchi tajiri. Simamieni ukweli na haki kumpata mkandarasi, si kukimbilia tu unafuu msio na uhakika nao.
Lazima watendaji muonekane mna uchungu na fedha za wananchi, alisema Rais na baadaye kwa kauli ya ukali alisema: Tusipofanya hivi siku zote tutakuwa shamba la wajinga.
Aliendelea kutamka; Nasisitiza iwe fundisho, haya yasijiridie, msiwe mbumbumbu, mmesoma mnajua thamani ya barabara, kwa nini mtu awadanganye kujenga kwa gharama yenye unafuu wa kupindukia?
Hata hivyo, katika hatua nyingine, Rais Kikwete aliwageukia watendaji wa Wakala wa Barabara wa Serikali (TANROAD) na Wizara ya Miundombinu, akiwashangaa kuacha watu wakijenga katika hifadhi za barabara na wanapoanza kuishi wanawataka kuhama.
Hivi nyie, mtu anachimba msingi mnamuangalia, tena mnapita hapo, anapandisha ukuta, anapaua anahamia, hatua zote hizo mnamuangalia tu, baadaye akishahamia mnamtaka kuondoka. Sasa hawa wanavunja sheria mnawaangalia kuweni makini, alionya Rais.