Jiulizeni kwanini wananchi wanapiga kelele kuhusu kuporwa kwa rasilimali za nchi?

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,109
Butiku aibana Serikali

2007-10-18
Na Richard Makore


Mwanachama mkongwe wa CCM, Bw. Joseph Butiku, amesema viongozi wanapaswa kujiuliza kwa nini kelele za wananchi zimezidi hasa kuhusu kuporwa kwa rasilimali za nchi.

Wakati Butiku akiyasema hayo, Serikali imekiri imekuwa ikidanganywa na wawekezaji kuhusu kiasi halisi cha madini kinachopatikana kwenye migodi, jambo ambalo linaifanya ishindwe kujua ilipwe kiasi gani cha fedha kama mrahaba.

Akiongea na waandishi wa habari jana katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), kuhusu uongozi na maadili ya viongozi, Bw. Butiku alisema: `Kelele za rushwa, ufisadi na usimamizi mbovu wa rasilimali zetu zimezidi Umaskini hauishi, rasilimali zinazidi kupotea na inaonekana kuna tatizo kubwa.`

Bw. Butiku ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, alisema hali inazidi kuwa mbaya kiasi cha wananchi kusimamisha viongozi barabarani na kuwahoji kwa nini tatizo la umaskini haliishi huku rasilimali zikiporwa.

Alisema viongozi wameapa kuilinda Katiba lakini hawaisimamii ipasavyo na ndiyo sababu ya kutokea mambo yanayozungumzwa na wananchi wengi.

Hata hivyo, Bw. Butiku amewatupia lawama wananchi kuwa nao wamekuwa mstari wa mbele kuchochea vitendo vya rushwa kwa kuwa wamekuwa wakiwaomba fedha wagombea wakati wa uchaguzi.

Aliwafananisha na kinda la ndege ambalo wakati wote linaachama ili liweze kupata chakula kutoka kwa mzazi wake.

`Hilo nalisema na nina ushahidi nalo. Wananchi wamezidi kuwabugudhi wagombea kwa kutaka chochote, mtu ananadi sera zake anaulizwa `mzee huna chochote??` Alisema na kuongeza kuwa hali hiyo imekuwa ikisababisha hata wasiotaka kutoa rushwa watoe.

Katika hatua nyingine, Bw. Butiku alimtaka Rais (mstaafu) wa awamu ya tatu, Bw. Benjamin Mkapa kujitokeza na kujibu tuhuma zinazotolewa dhidi yake kuhusu kufanyabiashara akiwa Ikulu.

Alisema si busara kwa kiongozi huyo kukaa kimya na kwamba hali hiyo inaweza kusababisha watu wengi waamini kuwa tuhuma hizo ni za kweli.

Alisema baada ya kuona CCM inapoteza mwelekeo, aliamua kumwandikia barua aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Bw. Benjamin Mkapa mwaka 2005 kumweleza kuwa chama kinaelekea kwenye kifo chake kutokana na kukumbatia maovu.

Alisema tangu wakati huo, barua hiyo aliifanya kuwa siri yake lakini ameamua kuiweka wazi kwa waandishi wa habari ili umma utambue tahadhari ambayo aliitoa kwa CCM kuhusu ubaguzi, rushwa na kukumbatia maovu mbalimbali.

Kuhusu kudanganywa katika sekta ya madini, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, Bw. Charles Mtalemwa, alisema serikali hivi sasa inatumia taarifa za kubahatisha ambapo wakati mwingine wawekezaji wanaweza kutumia uongo kwa ajili ya kupata faida kubwa na serikali kuambulia mapato madogo.

Bw. Mtalemwa alikuwa anaongea na waandishi wa habari.

Alisema serikali inashindwa kuwadhibiti wawekezaji juu ya mapato, hatua kwa hatua kutokana na kutokuwa na wataalamu wa kutosha wanaojua sekta ya madini.

Alisema uhaba wa wataalam wa madini wazawa ndiyo sababu kubwa inayowapa mwaya wawekezaji kuidanganya serikali wanavyotaka kwa kuwa hakuna mtu anayejua masuala ya madini ili kuweza kuwahoji pale wanapodanganya.

Aliongeza kuwa hiyo ni changamoto kubwa kwa serikali katika kuhakikisha kuwa sekta ya madini inawafaidisha wananchi wote badala ya sasa ambapo wawekezaji wanatumia ujanja ujanja kuidanganya serikali kuhusu faida halisi wanayoipata.

`Hakuna anayejua wawekezaji wanapata kiasi gani ili serikali iweze kudai pale inapopunjwa,` alisema
Aidha, Bw. Mtalemwa alisema, wawekezaji katika sekta ya madini wanatumia teknolojia ya gharama kubwa na wataaaamu wao kwa ajili ya kuwekeza.

Hata hivyo, alisema serikali inafanya jitihada mbalimbali katika kuhakikisha kuwa madini yanawafaidisha wananchi wote pamoja na kuchangia kukuza uchumi wa nchi.

Bw. Mtalemwa alisema, serikali ina dhamira ya dhati katika kupambana na umaskini wa kipato kwa wananchi wake kupitia sekta ya madini.

Alisema kilimo bado ni muhimili mkuu wa uchumi wa nchi hivyo lazima kitiliwe kipaumbele ili kusaidia kuendeleza wananchi.

Aidha, Bw Mtalemwa aliwakumbusha wananchi juu ya umuhimu wa kujiletea maendeleo wao wenyewe.

Jana ilikuwa ni siku ya kupambana na umaskini duniani ambapo Tanzania iliungana na nchi nyingine kupiga vita hali hiyo na kauli ilikuwa ni `wanaoishi katika umasikini ni chachu ya kujiletea maendeleo.`


SOURCE: Nipashe
 
Kuhusu kudanganywa katika sekta ya madini, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, Bw. Charles Mtalemwa, alisema serikali hivi sasa inatumia taarifa za kubahatisha ambapo wakati mwingine wawekezaji wanaweza kutumia uongo kwa ajili ya kupata faida kubwa na serikali kuambulia mapato madogo.

Nadhani kada wa sisiemu Bw Makalla angesoma hii habari angeelewa ni kwa nini sie 'Wadanganyika' tunapiga kelele kuhusu madini yetu. Aliyeamua kuyaacha ardhini tangu uhuru wanadhani alikuwa mwehu sio? Si alijua kuwa hatuna utaalamu wa kutosha? ukizingatia kuwa madini hayaozi.
 
Hakuna anayejua wawekezaji wanapata kiasi gani ili serikali iweze kudai pale inapopunjwa,` alisema



Alex Stewards walikuwa wanavuna 1.8 ya 3% tulokuwa tunapata (1.2%)waliwekwa kufanya nini. Ama Nao ni mali ya fisadi mojawapo.


Mtalemwa, akili imedumaa, kama tumbo limechafuka, tafuta choo kapumzike.
 
"Kuhusu kudanganywa katika sekta ya madini, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, Bw. Charles Mtalemwa, alisema serikali hivi sasa inatumia taarifa za kubahatisha ambapo wakati mwingine wawekezaji wanaweza kutumia uongo kwa ajili ya kupata faida kubwa na serikali kuambulia mapato madogo"


Du, nashindwa hata nicomnent nini, kweli bila ya kuwaondoa watu kama hawa mapema tumekwisha!!
 
"Kuhusu kudanganywa katika sekta ya madini, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, Bw. Charles Mtalemwa, alisema serikali hivi sasa inatumia taarifa za kubahatisha ambapo wakati mwingine wawekezaji wanaweza kutumia uongo kwa ajili ya kupata faida kubwa na serikali kuambulia mapato madogo"


Du, nashindwa hata nicomnent nini, kweli bila ya kuwaondoa watu kama hawa mapema tumekwisha!!
Kwahiyo Na ACCACIA tutegemee kudanganywa
 
Back
Top Bottom