Jitihada za kupambana na ufisadi zianzie kwenye familia

diranqhe

JF-Expert Member
Mar 29, 2012
1,212
2,000
JITIHADA ZA KUPAMBANA NA UFISADI ZIANZIE KWENYE FAMILIA

Hivi majuzi kumegundulika ufisadi wa fedha za umma huko Wizara ya fedha ambapo mamilioni yametumika ovyo. Tayari waziri mkuu kashaelekeza hatua za kuchukuliwa kwa wahusika ikiwamo kusimamishwa kazi kupisha uchunguzi. Nampongeza Waziri Mkuu kufanya jambo sahihi kwa wakati sahihi na kwa manufaa ya taifa. Mara baada ya taarifa kusambaa mitandaoni kukatokea maoni tofauti ila wengi wamedai hatua kali zichukuliwe dhidi ya waliohusika. Mapovu yalikuwa mengi sana mitandaoni. Binafsi niliwaza tofauti baada ya kuona wengi hasira zimekuwa kali kwa kutokuwepo kwenye huo upigaji.

Kwanini ninasema kwamba wengi wetu tunawaonea wivu mafisadi na sio kwamba tuna uzalendo? Yaani tumejaa unafiki. Wengi hatuna nia ya dhati kutokomeza ufisadi ila badala yake tuna nia ya dhati kuwepo kwenye hiyo stream ya upigaji. Sababu kuu ya kusema hivi ni kukosekana maadili kuanzia ngazi ya familia. Familia karibu zote zinamejikita kwenye mazoea ya kudhani ukosefu wa maadili ni kwenye uvutaji bangi, ulevi, uzinzi na matusi peke yake. Familia hazifundishi watoto umuhimu kwamba matumizi mabaya ya mali za umma ni ukosefu wa maadili. Katika ukuaji wao hawaambiwi upigaji wa fedha za umma ni jambo baya.

Badala yake karibu watanzania wote tumekuzwa tukiaminishwa tusome kwa bidii tuje tupate kazi sehemu zenye mishahara minono kama TRA, TPA, na kwenye taasisi za fedha. Pia karibu kila familia inawakuza watoto wao na kuwasisitiza kuwa wapigaji kwa kauli kwamba pale kuna "Marupurupu".... na ikitokea kijana akapata kazi maeneo yanayotajwa kuwa na malisho manono basi kunakuwa na nguvu nyuma yake toka kwa familia na watu wa karibu ya kumtaka awe mpigaji... familia zingine huona kama kijana wao anachelewa na kuenda mbali kwa kumfananisha na kijana mwingine wa rika lake anayeonekana kuwa na ukwasi bila kujua vyema vyanzo vyake vya pesa. Matokeo yake kijana anaanza kuwa fisadi na mwishowe kujikuta mikononi mwa TAKUKURU.

Je nini kifanyike? Wazazi tubadilishe mfumo wa malezi kwa watoto.. tuwakuze wakijua wana wajibu wa kuliletea taifa maendeleo kwa kufanya kazi halali na kulipa kodi. Tuwaambie ukweli kuhusu maisha na hali halisi ya ajira nchini kwa kuzingatia uchumi. Tuende mbali kwa kuwafundisha kujitegemea na ujasiriamali. Vijana wengi wako magerezani kwa kufuata malezi mabovu ya wazazi waliowaaminisha kwenye marupurupu na upigaji. MUNGU AWABARIKI
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom