Jitihada Kubwa Bado Inahitajika Kuziba Pengo la Kijinsia katika Ajira

The Sheriff

JF-Expert Member
Oct 10, 2019
617
1,799
AJIRA NA USAWA WA MALIPO KWA WANAWAKE.jpg


Licha ya kuongezeka kwa mijadala inayohusu ukosefu wa usawa ambao wanawake wanakumbana nao katika maeneo ya kazi, bado kuna jitihada kubwa inayohitajika ili kuziba pengo la kijinsia katika ajira.

Ikilinganishwa na wanaume, wanawake wana uwezekano mdogo wa kuajiriwa katika kazi zenye malipo ya juu, na uwezekano mdogo wa kuendelea katika taaluma zao. Matokeo yake ni kuwa pengo la malipo baina ya kijinsia linaendelea na wanawake wanajikuta katika hali ya kuwa na uwezekano mdogo wa kujikwamua katika umasikini.

Kwa mujibu wa makadirio ya Shirika la Kazi Duniani (ILO), kiwango cha sasa cha ushiriki wa wanawake katika ajira ni chini ya 47%. Kwa wanaume, ni 72%. Hiyo ni tofauti ya asilimia 25, huku baadhi ya maeneo yakikabiliwa na pengo la zaidi ya asilimia 50.

Wanawake katika kazi za kulipwa kwa saa wana uwezekano mkubwa wa kufanya kazi kwa saa chache kuliko wanaume, lakini kwa kawaida si kwa hiari. Katika nchi zinazoendelea, viwango vya “ajira duni” (underemployment) zinazohusiana na wakati kwa wanawake inaweza kufikia 46%.

ILO pia inasema kuwa Wanawake wanaotaka kufanya kazi huwa na wakati mgumu kupata kazi kuliko wanaume. Tatizo hili linaonekana hasa katika Afrika Kaskazini na Mataifa ya Kiarabu, ambapo viwango vya ukosefu wa ajira kwa wanawake vinazidi 20%.

Hata hivyo, ingawa ajira katika mazingira magumu imeenea kwa wote – wanawake na wanaume – wanawake wana mwelekeo wa kuwakilishwa kupita kiasi katika aina fulani za kazi zilizo hatarini.

Wanaume wana uwezekano mkubwa wa kufanya kazi zisizohitaji shuruti wakati wanawake wakiwa na uwezekano mkubwa wa kuwa “mama wa nyumbani” au kuwa wasaidizi katika biashara za ndugu zao nk.

Takriban 16% ya wanawake walioajiriwa – ikilinganishwa na 6% ya wanaume walioajiriwa – wanachangia katika shughuli za kifamilia (yaani waliojiajiri au walioajiriwa katika biashara inayomilikiwa au kuendeshwa na jamaa).

Wafanyikazi kama hao wana uwezekano wa kulipwa vipato duni (ikiwa watalipwa) na kuishi katika umaskini, bila mikataba ya ajira na ufikiaji mdogo wa ulinzi wa kijamii. Pengo hili linaonekana zaidi katika nchi zinazoendelea, kwa mujibu wa ILO.

Hii inaelezwa pia kuwa ni sababu ya wanawake kuathiriwa na kutokuwepo kwa usawa katika maeneo mengi kama vile kielimu, kiafya na kijamii. Jambo hili linaathiri kwa kiasi kikubwa maendeleo ya dunia.

PENGO LA KIJINSIA KATIKA USHIRIKI WA KAZI DUNIANI (2).png

Kiwango cha chini cha uajiri wa wanawake katika viwango vya kimataifa husababisha uzembe wa kiuchumi na kijamii katika nyanja nyingi.

Lakini je, nini kinaweza kupatikana kutokana na usawa wa kijinsia katika mifumo ya ajira?

Miongoni mwa mambo makubwa na muhimu zaidi yanayoweza kupatikana kwa kujumuisha jinsia tofauti katika nyadhifa mbalimbali maeneo ya kazi ni kupunguza unyanyapaa. Unyanyapaa kwenye nafasi na mahali pa kazi unaweza kuwafanya wafanyakazi wajihisi kana kwamba hawafai na hivyo kuwakatisha tamaa kufanya kazi kwa bidii au kubaki ndani ya maeneo haya ya kazi ambapo hawastawi.

Maeneo ya kazi ambayo hayahimizi uwepo wa usawa wa kijinsia katika timu na nyadhifa mbalimbali yanakosa fursa ya kutumia vipaji na uwezo mkubwa wa wanawake.

Lakini pia, kuwa na wanawake na wanaume kwa usawa katika timu kunamaanisha kufaidika kutokana na mitazamo na mbinu tofauti zinazotokana na uzoefu tofauti wa maisha. Wingi wa mitazamo unaweza kuibua ubunifu na uvumbuzi, na kusaidia mashirika kutambua na kuchukua fursa mpya. Inaweza pia kuhimiza mashirika kupinga dhana potofu za kijinsia.

Zipo faida nyingi sana za kuajiri watu wa jinsia zote kwa usawa katika taasisi. Lakini, kama inavyoelezwa duniani kote, kumuwezesha mwanamke ni kuiwezesha jamii nzima. Wanawake wanapaswa kuwa sehemu ya maendeleo na ustawi wa dunia na hivyo hawapaswi kuachwa nyuma.

Ukosefu wa wanawake katika nafasi za usimamizi – nyadhifa zinazotoa mishahara ya juu – unachangia kwa kiasi kikubwa katika uwepo pengo la mishahara kati ya wanaume na wanawake. Je, nchi zinaweza kufanya nini ili kubadilisha mwelekeo huu?

Inaelezwa kuwa kuna baadhi ya ishara za kutia moyo kutoka duniani kote. Nchini Iceland kwa mfano, sheria inaeleza kwamba makampuni yenye wafanyakazi ishirini na watano au zaidi yatoe ushahidi kwamba wanaume na wanawake wanapokea malipo sawa kwa kazi sawa.

Hata hivyo udhibiti wa kisheria tu hauwezi kutatua matatizo yote. Kitakachosaidia kuziba pengo la mishahara duniani kote ni wanawake zaidi kupata fursa za kufanya kazi ambazo siku zote zimetawaliwa na wanaume, na kinyume chake. Hii inamaanisha pia kuzingatia nyanja za teknolojia, utafiti n.k.

Tathmini mpya inahitajika kushughulikia mazoea katika michakato ya uajiri, mawasiliano na uendelezaji wa wafanyakazi.

Uhuru wa kufanya kazi kwa hiari, katika hali ya utu, usalama na usawa, ni muhimu kwa ustawi wa binadamu. Kuhakikisha kuwa wanawake wanapata haki hii ni muhimu sana.
 
Kwa kweli mzani huu haubalance kabisa, jambo zuri ni kwamba wanawake wengi kwa sasa wameamka na wamekuwa wathubutu kuziendea fursa mbalimbali.

Naamini miaka michache ijayo takwimu zitabadilika hata kama zisipokuwa sawa moja kwa moja angalau zitakuwa nafuu.
 
Back
Top Bottom