Jinsi ya kutumia Falsafa ya Ustoa Kukabiliana na janga la Corona

Makirita Amani

JF-Expert Member
Jun 6, 2012
1,474
2,000
Tangu mwishoni mwa mwaka 2019, dunia imekuwa inapitia janga kubwa la mlipuko wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona. Mlipuko huu ulianzia kwenye mji wa Wuhan nchini China na wengi hawakuupa uzito unaostahili.

Mpaka kufikia mwezi Machi 2020, ugonjwa ulikuwa umesambaa kwenye mabara yote duniani na kuua maelfu ya watu kwa siku. Hapa ndipo watu walianza kupatwa na taharuki na mataifa kuchukua hatua mbalimbali ili kuzuia ugonjwa huu usisambae na kusababisha vifo zaidi.

Ni rahisi kuona hili ni janga jipya na la kipekee, lakini huo siyo ukweli. Dunia imepitia majanga makubwa kuliko hili, hivyo tuna mengi ya kujifunza kutoka kwenye majanga hayo ya nyuma.

Falsafa ya Ustoa, ina mengi ya kutufundisha kuhusu majanga mbalimbali tunayoweza kukutana nayo kwenye maisha, jinsi ya kukabiliana nayo na kuhakikisha maisha yetu yanaendelea kuwa bora.

Karibu kwenye makala hii tujifunze jinsi tunavyoweza kuitumia falsafa ya Ustoa kukabiliana na majanga mbalimbali kwenye maisha.

Marcus Aurelius na janga la tauni.

Marcus Aurelius (121 - 180) alikuwa mtawala wa Roma (161 - 180) na mwanafalsafa wa Ustoa. Anakumbukwa kama mmoja wa watawala watano bora wa Roma kabla haijaanguka.

Katika kipindi cha utawala wake, Roma ilikumbwa na janga kubwa la mlipuko wa ugonjwa wa tauni (Antonine Plague). Ugonjwa huo ulianza mwaka 165 mpaka 180 na kupelekea vifo vya watu kati ya milioni 5 mpaka 10.

Ugonjwa huu pia ulisababisha vifo vya watawala wote wawili wa Roma, Lucius Verus alifariki mwaka 169 na Marcus Aurelius alifariki mwaka 180 kwa ugonjwa huo.

Ugonjwa huu ulisambaa kwa kasi kwa sababu ulikuwa unasambazwa na watu. Mwanzo ulianza na wanajeshi waliotoka vitani, ambao waliupeleka kwenye kambi za jeshi, na baadaye wanajeshi waliotoka kambini na kwenda majumbani kwao walipeleka ugonjwa huo kwenye jamii.

Katika kilele cha ugonjwa huu, vifo vilikuwa vingi na watu walikuwa wanakufa ghafla kwa kudondoka popote. Inakadiriwa kwamba kati ya vifo elfu 2 mpaka elfu 5 vilikuwa vinatokea kila siku kutokana na ugonjwa huu.

Katika kukabiliana na hili, mtawala Marcus Aurelius alitenga baadhi ya majengo kuwa kama makaburi ya pamoja ambapo waliofariki walipelekwa huko. Lakini pia aliondoa gharama za mazishi ambazo zilikuwa juu kipindi hicho ili kuzuia miili ya watu kutapakaa mitaani kwa kushindwa kuzikwa. Hili lilisaidia maiti kutokutapakaa mitaani na kuleta hofu na taharuki zaidi kwa wananchi.


Jinsi Marcus Aurelius alivyotuimia Ustoa kukabiliana na janga la tauni.

Licha ya kuwa mtawala, Marcus Aurelius alikuwa pia ni mwanafalsafa wa shule ya falsafa iliyojulikana kama Ustoa (Stoicism). Falsafa hii ilifundisha watu kuendesha maisha yao kwa misingi ya asili na kutumia fikra badala ya hisia katika kufanya maamuzi.

Falsafa ya Ustoa ndiyo iliyomwezesha Marcus Aurelius kuweza kuwa tulivu katika kipindi ambacho kila mtu alikuwa anataharuki. Pamoja na changamoto zote alizokuwa anapitia, kila siku Marcus aliandika kwenye kitabu chake alichokiita Meditations, ambapo kila siku aliandika tafakari mbalimbali za maisha kulingana na yale aliyokuwa anakutana nayo. Baadaye kitabu hiki kilikuja kupatikana na ni moja ya vitabu ambavyo viongozi wengi kwa sasa wanakisoma hasa nyakati za changamoto mbalimbali.

Kwenye moja ya tafakari zake Marcus aliandika, “Kila unapoamka asubuhi jiambie; leo naenda kukutana na watu waovu, wasio na shukrani, waongo, wenye wivu na wasiojali. Yote hayo yamewafika watu hao kwa sababu hawajui mazuri na mabaya. Kwa sababu mimi ninajua asili ya uzuri na sahihi, siwezi kudhurika na watu hao, hakuna mtu anayeweza kunihusisha kwenye ubaya, na siwezi kumkasirikia au kumchukia yeyote, kwa sababu tumekuja hapa duniani kushirikiana.”

Hii ni kauli ya kifalsafa inayoweza kumpa mtu nguvu kubwa katika nyakati ngumu kama ambazo Marcus alikuwa anapitia kama kiongozi.

Wakati Marcus anafariki dunia, alitamka, "Msinililie mimi, fikirieni kuhusu ugonjwa uliopo na vifo vya wengi vitakavyofuatia." Kauli hii inatuonesha jinsi ambavyo Marcus alikuwa akipambana siyo kwa manufaa yake, bali kwa ajili ya manufaa ya wengine wengi.

Hatua tatu za kuchukua ili kukabiliana na Corona Kistoa.

Katika kutumia falsafa ya Ustoa kukabiliana na janga la Corona tunalopitia sasa, hapa kuna hatua tatu za kuchukua.

Moja; tafakari siku yako na andika mahali.

Wakati Roma ikiendelea kukumbwa na janga la tauni, kila siku Marcus Aurelius alijipa muda wa kuitafakari siku yake, kuangalia yale aliyofanya, matokeo aliyopata na yale aliyojifunza. Kisha aliandika mambo hayo kwenye kijitabu chake, ambapo baadaye kimekuja kuwa kitabu kinachoitwa Meditations.

Kuitafakari siku yako kunakupa nafasi kubwa ya kuona wapi unafanya vizuri na wapi unakosea. Unajifunza mengi kwa kujitathmini mwenyewe kila siku. Kuandika chini yale unayotafakari ni njia ya kupakua mawazo yaliyo kwenye akili yako na kuyahifadhi. Kunapunguza msongamano wa mawazo kwenye akili yako na kukuwezesha kufikiri kwa usahihi.

Kwa janga la Corona tunalopitia sasa, kila siku tenga muda wa kutafakari na kutathmini siku yako. Angalia kila ulichofanya kwenye siku yako na matokeo uliyopata, ona wapi unafanya vizuri na wapi hufanyi vizuri. Kisha andika tafakari na tathmini yako kwenye kijitabu chako. Unaweza kufanya kijitabu hicho kuwa siri yako, ili upate nafasi ya kuandika kwa uhuru na kutokujali anayekuja kusoma atakufikiriaje.

Zoezi la kuandika yale unayofikiria au kutafakari limethbitishwa kuwa na manufaa makubwa kwa watu, hasa pale mtu unapokuwa na msongo. Janga tunalopitia sasa linampa kila mtu msongo, kupata nafasi ya kuandika yale tunayofikiria na kutafakari, inatupa utulivu mkubwa.

Mbili; jua yaliyo ndani ya uwezo wako na nje ya uwezo wako.

Kwenye falsafa ya Ustoa kuna kitu kinaitwa upacha wa udhibiti (dichotomy of control). Dhana hii ni kwamba mambo yote yanayotokea yamegawanyika kwenye makundi mawili, kundi la kwanza ni yale yaliyo ndani ya uwezo wako na unaweza kuyaathiri au kuyabadili na kundi la pili ni yale yaliyo nje ya uwezo wako na huna namna ya kuyabadili.

Watu wengi wanapata msongo kwenye maisha yao kwa sababu wanahangaika na mambo yaliyo nje ya uwezo wao, na kujaribu kuyabadili.

Kwenye janga hili la Corona tunalopitia sasa, jua nini kipo ndani ya uwezo wako na fanya yale unayoweza kuhusu hili. Mfano yaliyo ndani ya uwezo wako ni mawazo yako, mtazamo wako, tabia zako na hatua unazochukua. Kazana kufanya kile ambacho ni sahihi kufanya.

Yaliyo nje ya uwezo wako yapokee kama yalivyo na usijisumbue kuyabadili, huwezi. Kwenye janga tunalopitia sasa, mambo mengi yako nje ya uwezo wako mfano, mawazo na tabia za wengine, iwapo ugonjwa utakupata, kama utakufa au kupona na jinsi watu mbalimbali wanavyouchukulia ugonjwa huu.

Wewe kazana na yale yaliyo ndani ya uwezo wako, jikinge usipate maambukizi na ukiyapata jikinge usisambaze kwa wengine. Mara zote hakikisha unafanya kilicho sahihi. Usiruhusu hofu au msongo vikutawale, havina msaada wowote kwako katika janga linaloendelea.

Tatu; tegemea mambo kuwa mabaya zaidi.

Kwa janga linaloendelea sasa, tunawasikia wataalamu mbalimbali wakitupa utabiri wao kulingana na hali inavyokwenda. Wengi tunategemea baada ya miezi michache janga hili litakuwa limepita na maisha yatarudi kama kawaida.

Lakini falsafa ya Ustoa inatutahadharisha juu ya hiyo, inatutaka tusiwe watu wa kujipa matumaini hewa, kwa kuweka mategemeo yetu kwenye vitu ambavyo hatuna uhakika navyo.

Kwenye Ustoa kuna zoezi linaitwa kujenga taswira hasi (negative visualization), ambapo unayaona mambo kwa hali ambayo ni mbaya kuliko unavyotegemea. Lengo la zoezi hili siyo kukukatisha tamaa, bali kukupa maandalizi sahihi iwapo mambo hayataenda kama ulivyotegemea.

Taswira hasi za kujijengea kwenye janga la Corona linaloendelea;

Kama wewe ni mfanyakazi na janga hili limepelekea upewe likizo au kukosa mshahara, basi chukulia huna tena kazi hiyo na huwezi kuipata tena, hivyo fikiria maisha yako yataendaje baada ya hapa.

Kama wewe ni mfanyabiashara na biashara yako imeyumba kabisa katika kipindi hiki, chukulia kwamba biashara hiyo imekufa kabisa na haiwezi kurudi tena, kisha angalia ni biashara gani utakayoweza kuifanya ambayo haitaathiriwa na janga kama hili.

Kama wewe ni mwanafunzi na ulitegemea kuhitimu mwaka huu, chukulia kwamba mwaka huu wa masomo umefutwa kabisa, hivyo jipe mwaka mwigine kufikiria kuhitimu na mambo mengine kuendelea.

Kama wataalamu wanakuambia janga hili litakuwa limeisha ndani ya miezi sita, wewe jipe muda wa mwaka kwa janga hili kuendelea kuwepo, hivyo jipange kwa usahihi katika kipindi hicho kirefu.

Kama wataalamu wanakuambia uwezekano wako wa kufa kwa janga hili ni mdogo, wewe chukulia uwezekano ni mkubwa, kisha chukua hatua sahihi na zilizo ndani ya uwezo wako kuhakikisha unaepusha kifo chako kwenye janga hili.

kwa kujipa taswira hasi kwenye janga hili, unaacha kujidanganya, unaepuka kuumia pale mambo yanapokwenda tofauti na ulivyotegemea, na kama mambo yatakwenda vizuri tofauti na taswira yako hasi, basi utafurahia zaidi.

Hivi ndivyo falsafa inayoweza kutusaidia kukabiliana na magumu, kwa kuwa na utaratibu wa kutafakari kila siku yetu na kuandika, kujua yaliyo ndani na nje ya uwezo wetu na kujipa taswira hasi ya mambo kuwa mabaya kuliko tunavyotegemea, kisha kuchukua hatua sahihi.

Unahitaji kuwa na falsafa utakayoisimamia na kuiishi kwenye maisha yako, ambayo itakusaidia kuvuka nyakati ngumu utakazokutana nazo kwenye maisha yako. Siyo lazima iwe falsafa ya Ustoa, unaweza kutumia hata misingi ya imani yako ya kidini kuyaendesha maisha yako. Muhimu ni uwe na kitu kinachokuongoza, kinachokusaidia kufikiri na kufanya maamuzi sahihi katika kila hali unayopitia.

Karibu tuendelee kujifunza na kuishi misingi ya falsafa ya Ustoa kupitia mtandao wetu wa Falsafa Ya Ustoa Tanzania, tembelea www.ustoa.or.tz

Makala hii imeandikwa na Dr Makirita Amani, ambaye ni daktari wa binadamu, kocha wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali.

makirita@ustoa.or.tz / 0717396253
 

ZAK ZAK

Senior Member
Mar 2, 2018
144
225
Wewe ni Mgiriki mweusi. Your are Afrikan-greece. Asante kwa maoni yako. Uzi hauna wachangiaji wengi watu wengi wanaependa kuchangia vitu visivyo na maana wakiacha elimu zuri kama hii
 

Makirita Amani

JF-Expert Member
Jun 6, 2012
1,474
2,000
Wewe ni Mgiriki mweusi. Your are Afrikan-greece. Asante kwa maoni yako. Uzi hauna wachangiaji wengi watu wengi wanaependa kuchangia vitu visivyo na maana wakiacha elimu zuri kama hii
Asante mkuu.
Tuendelee kujifunza kwa tulio tayari.
 

Team JPM

JF-Expert Member
Nov 11, 2018
880
1,000
Big up Doctor, you have presented nicely your message, commendable article
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom