Jinsi siasa inavyotumika kuua elimu kwa makusudi

tpaul

JF-Expert Member
Feb 3, 2008
16,248
2,000
Watanzania tujiulize nchi gani iliwahi kuboresha elimu yake kwa kupunguza viwango vya ufaulu?
Hivi karibuni Serikali ilitoa uamuzi wa aina yake na wa kihistoria kwa kupanga upya viwango vya ufaulu.

Kwa watu wengi tatizo siyo upangaji bali ni madaraja ya ufaulu hayo kupunguzwa alama, hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye viwango vidogo vya ufaulu barani Afrika na dunia kwa jumla.

Alama hizo zilizotangazwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome zitakuwa kama ifuatavyo: A=75-100, B+=60-74, B=50-59, C=40-49, D=30-39, E=20-29 na F=0-19,

Malengo ya elimu ya Tanzania
Ukweli ni kuwa uamuzi huo unakinzana na malengo ya elimu ya Taifa hili ambayo ni; Mosi, kujenga na kudumisha stadi za kusikiliza, kuzungumza, kusoma, kuandika, kuhesabu, ubunifu na kuwasiliana kwa ufasaha kwa lugha ya Kiswahili na lugha nyingine za kigeni.

Pili, kukuza na kuendeleza mila, desturi na utamaduni wa jamii ya Watanzania. Tatu, kurithisha, kuendeleza na kutumia maarifa, stadi na mielekeo itokanayo na maandishi anuai, sayansi ya jamii, sayansi ya asili, teknolojia na mafunzo ya kazi kuendeleza jamii anamoishi.

Nne, kukuza na kuendeleza moyo wa kujiamini, kudadisi, kutathmini, kufikiri kiyakinifu na kufanya uamuzi wa busara, kuheshimu utu, haki za binadamu na kuchochea utayari wa kufanya kazi kwa bidii kwa maendeleo binafsi na ya Taifa.

Tano, kujenga uwezo na ari ya kujielimisha na utashi wa kuendelea kutafuta maarifa na stadi za kiutendaji. Sita, kujenga na kuendeleza heshima kwa Katiba ya nchi, kuthamini utawala wa sheria na haki za binadamu.

Saba, kujenga uwezo na misingi ya kutambua, kuheshimu na kupenda kufanya kazi kwa bidii na kwa ufanisi. Nane, kukuza ari ya kuyatambua na kuyahifadhi mazingira. Tisa, kujenga na kudumisha misingi ya kuthamini umoja, amani na ushirikiano wa kitaifa na kimataifa.

Kumi, kujenga misingi na ari ya kutambua na kuthamini mchango wa sayansi na teknolojia katika maendeleo ya taifa.

Malengo haya ambayo yako wazi kwenye sera ya elimu, mihtasari ya shule za msingi na sekondari, kwenye mipango mikubwa ya kitaifa kama MKUKUTA, MMEM, MMES, yametupwa kapuni. Sasa utashi wa watu na ghiliba za kisiasa ndizo zinazoamua hatma ya nchi yetu.

Kwa nini watawala hawataji malengo ya elimu? Kwa nini hatujikiti kwenye malengo ya elimu kwa kuangalia mahitaji ya nchi? Kwa nini hatujifunzi wengine wanafanya nini?

Nchi gani iliwahi kuboresha elimu yake kwa kushusha viwango vya kufaulu na kugawa alama za bwerere kwa wanafunzi? Mtoto aliyesaidiwa ataweza kujitegemea, atajitambua, atakuwa mbunifu?

Dira ya Maendeleo ya Taifa
Upangaji wa viwango hivyo vya ufaulu pia unakwenda kinyume na matamko ya Dira ya Maendeleo ya Taifa inayolenga kuwa na Watanzania wanaoweza kushindana kikanda na kidunia.

Kwa mfano, tamko la dira hiyo linasema: "...ili kufikia maendeleo ya kweli Tanzania inafanya jitihada ya kuwa Taifa lenye watu wenye shauku na mitazamo ya maendeleo pamoja na ari ya kushindana, …sifa hizi zinajengwa na elimu inayokuza maarifa…ubunifu, uvumbuzi …. Tanzania itajitahidi kufanikisha viwango vya juu vya ubora wa elimu ili iweze kuitikia changamoto za kimaendeleo na kuwa na uwezo wa kushindana kikanda au kidunia."

Kushusha viwango vya ufaulu na kuongeza madaraja ndiyo mkakati wa kufanikisha dira ya maendeleo ya kutoa viwango vya juu vya elimu?

Kupanga upya madaraja kutajibu tatizo la wanafunzi kujiunga na elimu ya sekondari pasipo kujua kusoma na kuandika? Kutaongeza ubunifu na ugunduzi ambao sasa unaonekana kutoweka miongoni mwa Watanzania? Kutasaidia kuongeza motisha kwa walimu ya kufanya kazi kwa bidii na kujituma?

Kurahisisha ufaulu wa wanafunzi kutasaidia Watanzania kupata maarifa stahiki ili waweze kujitegemea na kushindana kwenye ulimwengu wa utandawazi?

Kosa kubwa wanalofanya watawala na wasomi wengi ni kudharau maoni ya wengi hasa wananchi na walimu walio darasani. Siku zote tunadhani mtu akiitwa profesa, daktari, waziri au mbunge ndiye mwenye akili kuliko wote, maarifa kuliko wote, ujuzi kuliko wote.

Eti kwamba wasomi na watawala wanaweza kufikiri kwa niaba ya wananchi. Tumewaachia wafanye uamuzi kwa kudhani wanajua wanachokifanya, kumbe wanatupeleka kuzimu.

Pengine inawezekana vigogo wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi hawajui chochote kuhusu nini wananchi wanataka, nini dunia inahitaji na nini utandawazi unahitaji kutoka kwenye elimu.

Wangejua wazazi wanataka nini, soko la ajira linataka nini, maisha ya mafanikio yanataka nini na dunia inataka nini tusingekuwa na uamuzi dhaifu unaoangamiza vipaji vya watoto wetu na kuigeuza Tanzania kuwa nchi ya walinzi, ombaomba, wapagazi, wahuni, wezi na vibarua wa migodini. Wageni ndio wanashika uchumi wa nchi na kuliendesha Taifa.

Wanafurahi kuona watoto wa maskini wanamaliza kidato cha nne hawawezi hata kuandika barua ya kuomba pembejeo za kilimo, wakati watoto wao wanasoma nje ya nchi au shule za kimataifa zenye mazingira mazuri na walimu wazuri wenye motisha.

Source:
Mwananchi
 

Asamwa

JF-Expert Member
Apr 13, 2012
2,982
2,000
Tatizo la viongozi wetu kutokutafuta kiini cha tatizo kabla ya kufanya maamuzi kuhusu njia sahihi ya kulitatua!
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom