Jinsi Safari ya Matumaini Ilivyomuwezesha Jema Kupona Saratani

Boniphace Kichonge

JF-Expert Member
Jul 31, 2017
1,606
1,956
Zaidi ya wagonjwa 5,529 wa saratani za aina mbalimbali wamerekodiwa mwaka 2016 katika hospitali ya Ocean Road (ORCI) ambayo ni taasisi kubwa ya saratani nchini.

Miongoni mwa wagonjwa hao, yumo Jema Baruani ambaye anasimulia safari nzima ya matibabu aliyoyapata hadi kufikia hatua ya kupona maradhi hayo.

Msemo wa, ‘Imani huponya, tiba hufuata….,’ ndiyo sababu inayomfanya Jema Baruani awe imara katika kupambana na aina ya saratani ya damu inayotambulika kwa jina la ‘Hodgkins lymphoma’ iliyokuwa ikimkabili.

Kwa kawaida saratani hiyo huanzia kwenye chembe nyeupe za damu.

Wataalamu wanasema hali hiyo hutokana na mwili kuzalisha kiwango kikubwa cha seli zenye maumbo mabaya zisizo na uwezo wa kufanya kazi zake sawasawa.

Wanasema kazi ya chembe nyeupe za damu ni kulinda mwili dhidi ya vimelea waletao maradhi mbalimbali.

Lakini kwa Jema mwenye miaka 31 na mkazi wa Mbezi Dar es Salaam ambaye ni mtaalamu wa masoko katika Taasisi ya Afya ya AAR, anasimulia hadithi yake yenye kuleta matumaini katika kipindi ambacho Watanzania wengi wanahofu juu ya ugonjwa huo.

Hata hivyo, anasema yeye ameamua kupigana vita na saratani, vita isiyo isha huku adui yake mkubwa akiwa ni mawazo hasi dhidi ya matibabu yake yanayotolewa na jamii.

“Wagonjwa wa saratani wanaweza kupata matibabu yote wanayoyahitaji lakini haitosaidia kama mgonjwa ataendelea kupokea mawazo hasi ya namna ya kutibu ugonjwa huo,” anasema Jane

Jema anasema alianza kuugua Januari mwaka jana. Alihisi ana maumivu makali kifuani, lakini akajua huenda anatatizo la mapafu na hakuwahi kufikiri kama anaweza kuugua maradhi mengine yakiwamo ya saratani.

Kama ilivyokua rahisi kuelezea maumivu aliyokuwa akiyapata kiundani zaidi kwa watu wake wa karibu, Jema anasema hakuwahi pia kufikiri kutafuta tiba zaidi ya maumivu aliyokuwa akiyapata kwenye hospitali kubwa.

“Lakini baada ya wiki kadhaa kupita na hali ikizidi kuwa mbaya, nilianza kufikiri vitu tofauti,” anasema Jema na kuongeza;

“Mara nikaanza kupungua uzito wa mwili kwani kabla ya kuanza kuugua, nilikuwa na kilo 62, nikaporomoka na kufikia kilo 58 katika kipindi kifupi, ilipofika Aprili, nikajikuta nina kilo 52,” anasema Jema.

Anasema kabla ya kuugua, alikuwa akifanya mazoezi na kuzingatia mlo aliokuwa akiutumia kwa lengo la kulinda uzito wake usipande wala kupungua.

“Lakini nilishangaa kuona uzito wangu ukiporomoka kwa kasi kubwa, nikahisi kuna kitu hakiko sawa kwenye mwili wangu, licha ya kuwa nilikuwa naugua kifua,” anasema Jema.

Mwanadada huyo anasema baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya, aliamua kuanza kusaka tiba kwenye hospitali kubwa.
“Kuna muda pia nilidhani labda ni kutokana na hali ya hewa, lakini baadaye niliporejea kwa daktari kwa ajili ya uchunguzi zaidi, aliniambia siumwi vidonda vya tumbo, bali ninasumbuliwa na homa ya mapafu,” anasimulia Jema.Anasema wakati anaendelea kusaka tiba ya kile kilichokuwa kikimsumbua, si yeye wala daktari aliyewahi kuwaza au kufikiri kufanya kipimo cha saratani hata mara moja na wazo hilo halikuwapo.

Mwanadada huyo ambaye ni mwanzilishi wa Taasisi ya Jema foundation, ni miongoni mwa wagonjwa waliopona saratani baada ya kuibaini na kuanza matibabu haraka.

Safari ya matibabu yake ilianzaje?

“Asubuhi moja nilikohoa nikatoa makohozi yaliyochanganyika na damu. Nilishtuka sana, nikasema hali hii si njema inabidi nifanye uchunguzi wa kina, nikaenda Hospitali ya Aga Khan kutibiwa,” anasimulia Jema.

Anasema kabla ya kwenda hospitali, alifikiri huenda kuna kitu kimemkwaruza kwenye koo.

Alipofika kwa daktari na kumuelezea tatizo lake, alimshauri apime kipimo cha X-ray akafanya hivyo, baada ya majibu kutoka, yalionyesha ana uvimbe kwenye mapafu upande wa kushoto, na ndiko alikokuwa akipata maumivu wakati wote.

“Licha ya kubaini nilikuwa na uvimbe, lakini bado madaktari wa Aga Khan hawakuweza kutambua uvimbe ule ulikuwa ni dalili ya saratani, kwa sababu si kila uvimbe ni saratani,” anasema Jema.

Jema anasema madaktari walimfanyia pia uchunguzi wa mfumo mzima wa mwili wake na damu.

Vipimo hivyo vikaja na majibu ana uvimbe karibu na moyo ulioanza kugandamiza mapafu, hali iliyomfanya apumue kwa shida na kupata maumivu muda wote.

Alipokeaje majibu ya vipimo hivyo?

Jema anasema kwanza alipigwa na butwaa, pale alipoambiwa ana uvimbe karibu na moyo.

Anasema alistaajabu na akaanza kuwaza, huenda anaugua saratani, mapigo yake ya moyo yalianza kumuenda kasi huku hofu ikitawala mawazo yake.

“Daktari mmoja alinipa matumaini, akaniambia si kila uvimbe ni saratani, nilitamani iwe hivyo kwa upande wangu,” anasema Jema.

Anasema kwa kujiridhisha madaktari walimwambia wanakata tishu kwenye uvimbe huo ili wakaufanyie uchunguzi zaidi na majibu yalipotoka, aligundulika ana saratani.

Jema anasema baada ya kupatiwa majibu, familia yake ilishtuka, mshtuko wao ulimfanya aanze kumfikiria binti yake ambaye alikuwa bado mdogo, akawaza tena, Je! Mume wake angepambana vipi na hali hiyo.

“Nililia sana, lakini nikawaza tena, kwani nikiendelea kulia, kilio hicho kitanisaidia nini? Niliyaona maisha yangu yameshafikia mwisho. Lakini namshukuru Mungu, mume wangu aliipokea jaribu lile kwa mikono miwili, pamoja na kuwa alishtuka baada ya kupata taarifa, ila alijikaza na kunitia moyo,” anasema Jema.

Anasema aliendelea kuwaza kama madaktari wangeweza kuuondoa ule uvimbe ule kwa njia ya upasuaji labda angekuwa salama.

Lakini isingewezekana kwa sababu licha ya vimbe nyingi kutolewa kwa njia hiyo, lakini uvimbe wake uliota kwenye eneo hatari karibu na moyo, hivyo kwa usalama wake, madakari hawakutaka kuhatarisha maisha yake.

Lakini hawakuchoka, walimtia moyo na walimweleza ipo tiba ya mionzi. Jema anasema alianza kupata matumaini kidogo.

Je aliianzaje safari ya matibabu ya mionzi

Jema anasema alijipa moyo na aliamini tiba aliyoambiwa na madaktari ni tiba sahihi kwake.

“Muda ukafika nikaanza mzunguko wa tiba ya mionzi, hivi ninavyozungumza hapa, nimeshachomwa mizunguko 16. Ilikua ni safari ndefu ambayo bila mtu kuwa na imani na matumaini, inaweza kukuletea shida zaidi na ukajikuta ukiishia njiani.

“Lakini kupitia usimamizi mzuri wa familia yangu, nimeweza kuipita hii misukosuko. Hapo ndipo niligundua kwamba Imani na matumaini huponya pia,” anasema Jema.

Namna ya kuvumilia tiba ya mionzi

Jema anasema tiba hiyo imemfunza mengi ikiwamo uvumilivu.

Anasema tiba hiyo huumiza kwa kuwa inamaumivu makali , lakini baada ya muda mfupi huisha.

“Inahitaji mtu ale chakula chenye virutubisho, vyakula vya asili, matunda na mbogamboga bila kusahau kupumzika kwa muda wa kutosha, na mgonjwa anatakiwa kuepuka mawazo potofu,” anasema na kuongeza:

“Nilijua natakiwa kuivumilia hali ya kutapika mara kwa mara, maumivu ya tumbo, homa na mengineyo… nilifanya hivyo, ndiyo maana hivi sasa maisha yangu yanasonga. Mionzi imeniponya na mwili wangu haujapata madhara. Ni jaribu kubwa ila linamanufaa yake.”

Maradhi hayo yamemfundisha nini?

Anasema baada ya kuishi maisha hayo, anapenda kutoa wito kwa jamii umuhimu wa kupima afya mara kwa mara.

“Binafsi baada ya kuugua saratani, nilijifunza kitu, niliona kuna umuhimu wa kuwaelimisha wengine, ndiyo maana nilikuja na wazo la kuwa na taasisi yangu ya kutoa elimu ya Jema Foundation.

“Nilipofikiria mara ya kwanza, niliona ni wazo zuri, mfuko huu unachangia wagonjwa wa saratani wenye mahitaji mbalimbali pale Ocean Road na katika kitengo cha watoto, Muhimbili”.

Jema anasema watu wengi hawana ufahamu juu ya saratani, kupitia taasisi yake amefanikiwa kufikisha ujumbe wa matumaini kwa wagonjwa wengine wenye saratani.

“Nawasihi wale wote wenye saratani wasikate tamaa, wakiwahi kupata matibabu wanapona kabisa,” anasema Jema.

Anatumia njia gani kutoa elimu zaidi ili iifikie jamii?

Jema anasema anatumia mitandao ya kijamii kuwafikia watu wengi. Kwenye ukurasa wake wa Instagram, ujumbe wake mkubwa aliouweka unahimiza wagonjwa wa saratani kuishi kwa matumaini wakiamini maradhi hayo yanatibika, kwani jamii ikishirikiana inaweza kuleta mabadiliko chanya dhindi ya saratani.

“Watu wengi hawatambui kwamba saratani inatofautiana hatua kwa wale waliopo kwenye hatua ya nne na wale waliopo kwenye hatua ya awali. Mimi niliiwahi isisambae na kufika kwenye hatua mbaya,” anasema Jema.

“Kwenye jamii zingine hawaamini dawa za hospitali, ndiyo maana huishia kwenye mikono ya waganga wa kienyeji, niwahakikishie, dawa za saratani zikitumika kama zinavyotakiwa hamna mtu atakayepoteza maisha yake. Kila mmoja wetu anapaswa kuwa na matumaini hayo.”

Baada ya kuugua saratani, bado anaendelea kufanya kazi aliyoajiriwa?

Jema anasema saratani haijamfanya apoteze kazi yake, baada ya kupona anaendelea kufanya kazi.

Anasema kila siku huamka Saa kumi na moja asubuhi, anasali na baada ya hapo humuandaa mtoto wake kwa ajili ya kwenda shule na yeye huelekea kazini kwake anakofika saa mbili kamili.

“Ila sasa hivi situmii saa nyingi kuwapo ofisini kama awali, lakini namshukuru Mungu wafanyakazi wenzangu na uongozi wako bega kwa bega na mimi tangu nilipoanza safari yangu ya matibabu ya saratani hadi sasa nilipona,” anasema Jema.
Chanzo: MCL
 
Back
Top Bottom