SoC01 Jinsi kesi ya Mbowe na wenzake inavyoripotiwa ni kielelezo cha mapinduzi makubwa ya upashanaji wa habari

Stories of Change - 2021 Competition

JS Farms

Member
Oct 17, 2011
71
131
Siku moja ya mwaka 2005 sikumbuki tarehe wala mwezi mwalimu wetu mmoja aliingia darasani na gazeti lililokuwa na hotuba ya Bilionea Rupert Murdoch Mmarekani mwenye asili ya Australia na mmiliki wa vyombo vingi vya habari.Hotuba hiyo ilikuwa na mada isemayo 'nafasi ya magazeti katika wakati wa kidigitali ' aliitoa wakati anahutubia jumuiya ya Wahariri wa vyombo vya habari vya Marekani jijini Washington DC .Kwenye hotuba hiyo alitabiri miaka michache (kuanzia 2005) watu wataacha kusoma magazeti yaliyochapishwa(ya makaratasi)na badala yake watakuwa wanasoma au kufuatilia habari kupitia intaneti.Murdoch alisema tekinolojia ndiyo itakayoua na itakayozika uchapishaji wa magazeti .Murdoch aliwataka Wahariri hao na wataalam wa mambo ya habari waumize vichwa vyao kwa kufikiria jinsi gani vyombo rasmi vya habari ambavyo ni magazeti, vituo vya redio na televisheni vitakavyoweza kwenda sambamba na ukuaji huo mkubwa wa tekinolojia.

Wakati Murdoch anaongea hayo hakuna aliyemuelewa na walimshangaa inawezekana vipi Bilionea mmiliki wa magazeti anaweza kutabiri kifo cha magazeti ambayo ili apate faida ni lazima yachapwe.

Mwalimu alitutaka tuijadili hotuba ya Murdoch na kwenye mjadala wetu darasani na sisi tulimshangaa na kumpinga kwa sababu sehemu kubwa ya Tanzana kipindi kile kulikuwa hakuna umeme,umeme ulikuwa umesambaa kwa asilimia 10 tu nchi yote na huduma za intaneti kefu hazikuwa nyingi ,wilaya nyingi hazikua na huduma ya intaneti kefu kwahiyo isingekuwa rahisi kwa Mtanzania kusoma gazeti au kufuatilia habari kupitia intaneti.

Wakati Murdoch anatabiri hayo hakukuwa na twitter ambayo ilianzishwa 2006,hakukuwa na whatsapp mbayo ilianzishwa 2009,hakukuwa na instagram ambayo imeanzishwa 2010,hakukuwa na telegram ambayo imeanzishwa 2013 mtandao wa kijamii uliokuwepo ni facebook ambao ulikuwa haujasambaa kwani ulikuwa mpya ulioanzishwa 2004.

Tangu 2005 mpaka leo Dunia imeshuhudia mapinduzi makubwa ya upashanaji wa habari ambayo hata Murdoch hakuyategemea.Siku hizi kila mtu anaweza kukusanya ,kutuma na kusambaza habari ili mradi awe na simu janja,habari ambazo hazihitaji kizuizi cha mhariri wala uthibisho wa kamanda wa polisi wa mkoa.Ukuaji huu wa tekinolojia umesababisha habari zipatikane kwa urahisi,kwa haraka na zisizochujwa.Mfano habari ya tukio la polisi wa Tanzania waliovuka mpaka na kukamatwa Malawi habari ile haikuhitaji kamanda wa polisi aithibitishe wala kizuizi cha mhariri ambaye kama zingekuwa enzi zile angeweza kuificha au kuipaka paka rangi.

Urahisi huu wa kupashana habari umesababisha wasomaji wa magazeti kupungua, watu wanaofuatilia habari kupitia vituo vya redio na televisheni nao kupungua.

Mabadiliko haya pia yamesababisha Viongozi wa Afrika waichukie mitandao ya kijamii na kutamani kuidhibiti kama wanavyofanya kwenye magazeti,vituo vya radio na televisheni,ni rahisi kukamata mwandishi wa habari, kutumia sheria kudhibiti vyombo vya habari na kufungia vyombo vya habari na vilevile serikali inaweza kuweka kanuni mbalimbali ili kudhibiti habari ambazo hawazipendi lakini kwenye mitandao ya kijamii kuna ugumu kidogo wa kuidhibiti.

Viongozi wa Afrika wanapenda habari za kuwasifia sifia,kupongeza na zile za kuwatukuza watawala ila kwenye mitandao ya kijamii zinapatikana habari zote za kupongeza zipo,za kusifia zipo,za kushauri zipo na za kukosoa zipo na hali hii inasababisha watawala washindwe kuelewa tofauti ya kutukana na kukosoa.Habari au makala za kukosoa zinazoandikwa kwenye mitandao ya kijamii hukimbilia kusema ni matusi.

Watawala wamekuwa hawaiongelei vizuri mitandao ya kijamii wanaiangalia kwa jicho baya ni adui yao mpya disemba 9,2020 wakati alipokuwa akiwaapisha mawaziri aliowateua baada ya kuingia madarakani kwa kipindi cha pili Rais wa awamu ya tano wa Tanzania hayati John Magufuli alitoa maagizo kwa wizara mpya ya mawasiliano na tekinolojia ya habari kwa kusema "nataka wizara ikafanye kazi kwa sababu wizara hii ndiyo usalama wa nchi pia,watu wanacheza tu wanavyotaka " kwa maneno haya inathibitisha hayati Magufuli alianzisha wizara hii kwa lengo la kutaka kudhibiti mitandao ya kijamii.

September 7,2021 waziri wa mambo ya ndani ya nchi George Simbachawene naye alisema serikali inapanga kudhibiti mijadala ya mtandaoni husasani Twitter "Serikali inakusudia kuweka mfumo wa kudhibiti mijadala inayoendelea kwenye mitandao ya kijamii hususani Twitter ambako imekuwa ikikusanya watu wengi kwa pamoja na ikiachwa iendelee bila utaratibu inaweza kuleta uvunjifu wa amani kwani hutumika kukashifu viongozi " alisema Simbachawene.

Kuanzia 2015 hadi sasa nchi 66 Duniani zimeweza kuzima au kufungia mitandao ya kijamii baadhi ya nchi hizo ni Tanzania,Misri,Uganda,Chad na Senegal kwa nje ya Afrika ni Mynamar, Bangladesh na Russia sababu za kufungia ni siasa kwa maana ya uchaguzi na maandamano.

Ni wakati sasa wa viongozi kuiangalia mitandao ya kijamii kama njia muhimu ya kusaidia maendeleo ya wananchi kwani ina faida nyingi baadhi ni;

Inarahisisha upatikanaji wa habari

Tangu enzi za kale mpaka sasa binadamu ana kiu ya kupata habari,habari ni jambo muhimu,hata zikizuiwa atahangaika kuzitafuta na ni haki yake.

Mfano mzuri wa urahisi wa upatikanaji wa habari ni kwenye kesi ya ugaidi inayoendelea kwenye mahakama ya mafisadi na uhujumu uchumi jijini Dar es salam inayomhusu Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na wenzake watatu.


Wanaoripoti kesi hii wanastahili sifa kwani ni kielelezo kikubwa cha kukua kwa upashanaji wa habari kwani kuna mambo ambayo vyombo vya habari vya kawaida haviwezi kuandika wala kutangaza.Mambo kama jinsi watuhumiwa walivyoteswa,watuhumiwa kunyang'anywa fedha zao na mahabusu wa ugaidi kukaa kwenye kituo cha polisi Tazara kwa miezi nane bila kupelekwa mahakamani ni habari za kusikitisha ambazo huwezi kuzipata kwenye magazetj,radio na televisheni.

IMG-20210928-WA0001.jpg

Picha kutoka mtandaoni ikionyesha watu wanaofuatilia kesi ya Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na wenzake watatu.

Ajira

Sasa hivi mitandao ya kijamii si tu inawapa watu ajira hali pia inaweza kuwapa watu utajiri watu wengi wamejiajiri kupitia mitandao ya kijamii na wengine wanapata vipato vya ziada kupitia mitandao ya kijamii. John Plant raia wa Australia mmiliki wa chaneli ya You tube ya Primitive technology ana utajiri wa dola za Marekani milioni 54.5 ambazo amezipata kupitia chaneli yake inayotazamwa na mamilioni ya watu Duniani.

Kinachotakiwa kwa serikali iwasaidie vijana wa Kitanzania wanaorusha vipindi vyao kupitia mitandao ya kijamii kwa kuwapa mafunzo ya upigaji picha,mafunzo ya uhariri wa vipindi vyao na mafunzo ya kuwafundisha jinsi ya kuigiza vizuri au kuchekesha vizuri kwani vijana wengi wa Kitanzania wanatengeneza vipindi vingi kwenye mitandao ya kijamii ambavyo havina ubora kwa sababu hawana elimu ya kazi wanavyoifanya.

Mapato ya serikali

Kama kuna sehemu serikali inakosa mapato ni kwenye mitandao ya kijamii kwa sababu ya kuiangalia kwa jicho baya wameshindwa kugundua kuna kodi inapotea.Biashara nyingi zinafanyika mitandaoni,kuna maduka ya mtandaoni na kwa miaka michache ijayo biashara za mtandaoni zitaongezeka maradufu kwani ni rahisi kufanyika hazihitaji fremu ya duka,mlinzi wa kulinda duka na pia hazihitaji wafanyakazi wengi.Kwahiyo serikali iangalie namna gani inaweza kukusanya kodi kupitia biashara zinazofanyika mtandaoni.

Pia kodi inapotea kwenye matangazo ya biashara kuna matangazo mengi ya biashara yanafanyika kupitia akaunti za mitandao ya kijamii na wenye akaunti wanalipwa ni wakati sasa serikali iangalie namna ya kukusanya kodi kupitia matangazo ya biashara ya mtandaoni.

Inarahisisha upelelezi wa makosa ya jinai

Tukio la ugaidi la Augusti 25,2021 ambalo Hamza Mohamed alifanya mauaji ya polisi watatu na mlinzi mmoja wa kampuni binafsi ya ulinzi jijini Dar es salam mitandao ya kijamii ilifanya kazi nzuri kusaidia jeshi la polisi Tanzania kufanya upelelezi kwani ilifanikiwa kupata ndugu wa Hamza Mohamed, kupata taarifa za Hamza Mohamed kupitia mitandao ya kijamii ambayo ilitoa taarifa nzuri na kuelekeza hadi makazi ya Hamza yalipo ingawa mwanzoni Kamishna wa operesheni na mafunzo wa jeshi la polisi Liberatus Sabas alipoelezwa kwamba mtandaoni kuna taarifa zinazoweza kusaidia upelelezi alijibu kuwa hawafanyi kazi kupitia mitandao ya kijamii.

Kauli kama hizo zimepitwa na wakati ni wakati sasa wa vyombo vya ulinzi na usalama kuiona mitandao ya kijamii kama njia muhimu ya kupata taarifa nyeti kwa ajili ya ulinzi na usalama wa nchi yetu.

Kuna faida kubwa kwenye ukuaji wa tekinolojia hasa mitandao ya kijamii Viongozi wa serikali wanatakiwa waende sambamba na mapinduzi haya hakuna sababu ya kuihofia au kuichukia kwani ina faida kubwa kuliko hasara.Watu wachache wakitumia vibaya isiwe kigezo cha kuifungia au kutaka kuidhibiti.






Waungwana naomba kura zenu.
 
Wewe hupaswi kupata hata kura moja kwa bandiko lako hili kwa sababu umedanganya uma.

Kuna TV channel yoyote ambayo imethubutu kurusha case ya Mbowe live kama ambavyo huwa wanafanya Kenya au south Afrika?
 
Wewe hupaswi kupata hata kura moja kwa bandiko lako hili kwa sababu umedanganya uma.

Kuna TV channel yoyote ambayo imethubutu kurusha case ya Mbowe live kama ambavyo huwa wanafanya Kenya au south Afrika?
Mbona mwandishi kaandika mtandao wa kijamii ndiyo inayoripoti Kama Facebook, Twitter na Jamiiforum sijaona sehemu alipoandika Kuna Tv inaripoti.
 
Mbona mwandishi kaandika mtandao wa kijamii ndiyo inayoripoti Kama Facebook, Twitter na Jamiiforum sijaona sehemu alipoandika Kuna Tv inaripoti.
Sasa kama TV,radio na magazeti hayaripoti kesi hiyo hayo mapinduzi makubwa ya upashaji wa habari ni yapi sasa?Ndiyo maana nikasema kuwa hapaswi kupata hata kura moja kwa sababu taarifa yake inapotosha.Huwezi kusema kuwa nchi ina mapinduzi makubwa ya upashaji wa habari wakati TV,radio na magazeti vimefungwa mdomo.
 
Back
Top Bottom