Jinsi biashara ya mtandaoni ilivyoua na Kuhuisha Ndoto Zangu; Kicheko Kisicho na Mwisho

Status
Not open for further replies.

Amani Ne

Member
Dec 15, 2018
10
8
Kustaftahi

Ongezeko la vijana wengi wano maliza elimu ya juu, vyuo vya kati na shule za upili limesababisha upungufu mkubwa wa ajira nchini. Taasisi binafsi na taasisi za serikali ambazo zina nafasi ya kuajiri zimekua zikitumia mwanya wa uwingi wa wahitimu wa vyuo na vyuo vikuu kama fimbo ya kunyonya nguvu kazi kwa kuwalipa maslai haba.

Kuajiri kwa kigezo cha umeletwa na nani au umetoa nini ndio msingi wa ajira kwa sasa, na kwa wanaobahatika kuajiriwa tatizo la ucheleweshaji wa mishahara na stahiki za wafanyakazi imekua kilio cha kila mwajiriwa hususani katika taasisi binafsi. Hali hii huwapelekea vijana wengi kutafuta namna bora ya kuishi maisha yao kwa uhuru kwa kujiajiri wenyewe katika kilimo, ujasiriamali na biashara mbali mbali ikiwemo biashara za mtandaoni.

Nikiwa mwaka wa tatu, 2018 nilipokua namalizia shahada ya awali ya Elimu na Sayansi kutoka chuo kikuu kishiriki cha Elimu Mkwawa, nilikumbwa na msongo wa mawazo juu ya ni nini nitaenda kufanya nikimaliza masomo yangu?.

Nilikua na rafiki yangu ambaye kwa wakati ule hakua na mkopo na liweza kujisomesha kwa kufanya biashara ya FOREX, nilimuomba anifundishe, na akanifundisha kwa muda mrefu lakini sikuwa tayari kwa wakati ule kuanza kufanya hiyo biashara. Nilipomaliza chuo nilirudi nyumbani Sumbawanga na kufungua kituo cha Elimu ya ziada katika kanisa la Pentecoste katandala nilifundisha kwa miezi nne kutokea mwezi wa nane hadi mwezi wa 12 mwaka 2018.

Ninamshukuru Mungu, nilibahatika kuwa mwanafunzi bora mwenye ufaulu wa juu kwa vyuo vyote vya chuo kikuu cha Dar Es salaam kwa GPA ya 4.8/5.0 hapo niliamini maisha yangu yatakua yamebadilika. Kitu kilichonishangaza, baada ya mahafari hakuna kiongozi yeyote wa chuo au chombo chochote cha habari kilichonitafuta hata kwa mahojiano.

Nilikaa Iringa zaidi ya siku saba baada ya mahafari nilipoona kimya nikafuata cheti changu kampasi kuu Mlimani. Baada ya kurudi Sumbawanga niliandika barua na kuambatanisha vyeti vyangu na kutuma kwa barua pepe ya naibu mkuu wa chuo taaluma wa chuo cha Elimu Mkwawa kuomba kujitolea kufanya kazi lakini haikujibiwa. Nikapoteza mawazo ya kufanya kazi chuo nikaweka nguvu kufanya mambo yangu.

Mwaka 2019, nilipata nafasi ya kujitolea kusajili kadi za kielektroniki za chama X, nilifanya kazi miezi mine ambapo makubaliano ni kulipwa 150,000/= kwa mwezi lakini hadi naondoka nilikua nimelipwa 250,000/= kwa miezi minne, hizo zingine sijalipwa hadi leo. Mwezi wa tano mwaka 2019 nilianza kazi ya kufundisha masomo ya Baiolojia na Kemia katika shule ya upili ya Aggrey Chanji yenye mkataba wa mshahara wa 400,000/= kwa mwezi.

Wakati naanza kazi niliweka malengo ya hadi kufikia mwezi wa pili mwaka 2020 niwe nimefikisha akiba ya Tsh 2,500,000/= ili inisaidie kwenye nauli ya kufika Hungary ambako nilipata ufadhiri wa masomo kwa shahada ya umahiri katika Elimu ya viumbe hai. Huwezi amini, hakuna mwezi niliwahi lipwa mshahara kamili, ilikua ni mara tumelipwa elf 50,000/= mara mwezi unaisha hamjalipwa, ikifika likizo ndio hata senti moja hamlipwi, ilikua kama ndoto hadi inafika mwezi wa pili 2020 nilikua nimeweka akiba ya Tsh 800,000 tu, hapo ndio nikaona ni wakati sahihi wa kuanza FOREX ili nipate nauli ya kwenda masomoni.

Siku ya kwanza tu nimenza biashara nilipoteza TSH 500,000, akili ikachanganyikiwa nikajikuta nimepoteza pesa yote ya akiba. Wazo likawa kutafuta namna ya kurudisha pesa ambazo nimepoteza, nikauza kiwanja lakini wapi, nikauza vitu vya geto hadi nikakosa sehemu ya kulala lakini wapi.

Bahati nzuri nilikua nimeomba ufadhiri wa chuo kikuu cha Dar es salaam, Matokeo yalitoka mwezi wa kwanza mwanzoni nikawa nimepata, lakini sikutaka kuifatilia kwakua sikutaka kusoma tena UDSM. Kwa hiyo baada ya kupoteza kila kitu tumaini lililokua limebakia ni mimi kuikubali nafasi ya kusomeshwa na UDSM.

Ilinibidi nifanye taratibu za kukubali hiyo ofa na kuanza masomo mwezi wa tano nyuma semista moja maana ilitakiwa nianze masomo mwezi wa kumi na moja 2019 na kwa kua majibu ya ufadhiri yalichelewa basi nikaanza masomo semista ya pili mwaka 2020. Kati ya mwezi wa tano na mwezi wa tatu nilipokea pesa ya kujikumu ambayo ilitakiwa itolewe mwezi wa 11 mwaka 2019 hadi mmwezi wa tano kama wanafunzi wengine ambao baadhi yao walikua wameshaanza masomo.

Mimi niliamini mtaji mkubwa ungeweza kunisaidia kufanya vizuri sokoni na kurudisha pesa zilizopotea. Niliweka tena Tsh 3,000,000/= sokoni, lakini ndani ya juma moja nikawa sina hata mia mbovu. Hadi chuo kinafungua baada ya kupungua makali ya korona nilikua sina hata nauli ya kunirudisha Iringa. Nilianza kuishi maisha ya kukopa hadi nikarudi chuo. Masomo yangu na maisha yangu hayakua kama ya mwanafunzi anayefadhiliwa na chuo kikuu cha Dar es salaam, niliishi maisha ya kukopa na nikawa na madeni makubwa. Ilipokuja kutoka pesa ya kujikimu kazi ikawa kulipa madeni na kuanza kuweka tena kwene FOREX nikiamini nitafanikiwa. Nilijikuta ni mtu wa kukosa usingizi, hamu ya kuendelea na masomo ikaisha, kila muda nina presha, mapigo ya moyo hayakai sawa nikaamini nitakufa kabla ya kumaliza chuo.

Hadi inafika mwaka 2021, nikawa sina kitu mkononi na muda wa kupewa pesa za kujikimu umeisha na chuo natakiwa kumalizia utafiti wangu. Nikawa nimekopa madeni hadi nimekosa mbinu ya kuwadanganya wanao nidai, vitisho vikawa vingi kila kona, tarehe 22/11/2022 ni siku ambayo niliamua kunywa sumu ili nife nikiamini nitakua nimetatua matatizo mengi yanayo nizunguka. Nilinunua sumu nikapika chakula changu nikaweka kwene chakula basi nikaamua kula.

Kabla sijakula lilinijia wazo la kupitia barua pepe zangu, nilipoingia nikakutana na barua ya kukubali kazi yangu niliyotuma katika jarida moja kwa ajili ya uchapishaji ambayo ilikua na maelezo ya marekebisho. Nikaona nighairi kujiua nishughulike na suala la kazi ili ikichapishwa tu ndio nijiue. Kazi yangu ilichapishwa na kuwekwa mtandaoni tarehe 15/12/2021 nilipokea hongera kila kwa walionifahamu hiyo ikanifanya nihisi kuwa kuna watu wana nipenda na kunijali basi lile wazo la kujiua likapotea kabisa.

Bado shida ikabaki sina pesa ya kujikimu na sina kwa kukopa tena, basi mwezi wa kwanza tarehe 26 mwaka 2020 nikaamua kutoroka chuo ili kurudi mtaani kujipanga, bahati mbaya hadi kufikia mwezi wa tano bado mambo hayakua vile nilivyopanga yawe. Ikafika hatua nikabadili mawasiliano na watu wote wanaonfahamu, nikafunga akaunti zangu za mitandao ya kijamii ili mradi nisipate presha juu ya habari za chuo. Hadi naandika makala hii leo tarehe 18/7/2022 nimeweza kulipa madeni yote na kupata pesa ya kumalizia tafiti zangu.

Mlo

Biashara za Mtandaoni ndio mwelekeo wa duniani katika karne ya 21 na karne zijazo. Kwa bahati mbaya kundi kubwa la watu wasio waaminifu hutumia wigo huu kama fimbo ya kuwatapeli na kuwatia katika umaskini mkubwa vijana husasani vijana wanaomaliza Elimu ya vyo na vyuo vikuu.

Kwanini vijana wanao maliza Elimu ya vyuo na vyuo vikuu na si vijana wasio na Elimu kabisa au walio na Elimu ya darasa la saba?. Vijana walio maliza vyuo na vyuo vikuu hutumia muda mwingi shule kujifunza nadharia ya masomo ambayo haina matumizi ikitokea wamekosa ajira kwa taaluma walizo somea.

Jiulize, je mwalimu anaweza kufanya kazi gani nje ya ualimu kwa kutumia masomo aliyojifunza chuoni?, Daktari , na mwanasheria nao wanaweza? Unakuta majibu ni hapana. Kwa hiyo hawa wakimaliza vyuo wanajikuta hawana ujuzi wowote wa kuwawezesha kuishi katika Jamii. Wengi hujikuta wameangukia mikononi mwa biashara za mitandaoni kama ilivyokua kwangu, ukosefu wa Elimu ya kutosha na tamaa huwaingiza katika wimbi la umaskini mbaya zaidi.

FOREX ni moja ya biashara za mtandaoni ambayo vijana wengi wanaifanya kwa sasa. Hii ni tofauti na michezo ya kubashiri inahitaji taaluma na weredi wa hali ya juu. Wapo vijana baadhi wa kitanzania walio fanikiwa katika hii biashara akiwemo Sirjeff Deniss (Richest forex traders in Tanzania | successful Traders - MYAJIRATODAY). Sababu zilizopelekea nisifanikiwe na nifanikiwe.

Kujifunza mara kwa mara
Vijana wengi hawatumii muda mrefu kujifunza mbinu mbali mbali za FOREX. Adui mkubwa wa mafanikio ni uvivu. Kosa nililolifanya ni kujifunza kwa muda mfupi na nilipoona Napata faida katika akaunti ya majaribio hapo hapo nikaanza kuweka pesa.

Kuwa na mipango kazi
Vijana wengi tunaonza kufanya biashara za mtandaoni huwa hatuna mipango mkakati na mipango kazi, hujukuta unaendeshwa na tama wakati wa faida hadi unajikuta umepoteza.

Saikolojia
Hii ndio changamoto kubwa hususani kwa FOREX trader, wengi hutuchukua muda kuweza kujimudu kihisia

Kutokua na Mshauri (Trading mentor)
Mshauri ni mtu ambae anauzoefu katika biashara na anajua wakati gani ufanye nini na wakati gani usifanye. Kutokua na mtu anae jua na wa kukuongoza ndio sababu haswa ya kufanya vibaya sokoni

Dhifa
Zipo sababu nyingi za kumuwezesha mtu anaefanya biashara mtandaoni kufanikiwa au kutofanikiwa. Jambo la muhimu ni kutokukata tamaa, simamia unachokiamini hata kama itachukua miaka mingi hadi kufanikiwa. Tukubali kujifunza kila wakati, ukifanikiwa kujua na kuelewa biashara za mtandaoni itakua ni kicheko kisicho na mwisho na ikitokea umeingia kichwa kichwa basi itakua ni kilio kisicho na mwisho. Ni muhimu kujua kua hassara ni darasa la kutuimarisha.

Hakuna biashara ambayo inakua na faida siku zote. Mafanikio ni matokeo ya nidhamu katika biashara, kuweka akiba kidogo kidogo, kusimamia malengo n.k. Sijawahi kukata tama kwa sababu niliwahi pata hasara. Hasara niliyopata na maisha niliyoyapitia limekua darasa kwangu juu ya aina ya watu wanaonizunguka, marafiki wa kweli, marafiki wanafiki na kuchagua watu ninao weza kushirikiana nao kwa badae. Hasara imenifundisha kuwa unaweza poteza vyote ukavipata lakini hauwezi kupoteza uhai ukarudi tena.

Kupitia haya, nimefungua taasisi inayosaidia watu wenye ulemavu inayoitwa APeDi (Advocacy for People with Disabilities) lengo kuu ni kuwasaidia watu wenye ulemavu wa akili unaotokana na msongo wa mawazo.
 
Nmekuelewa ndugu,lakin kutokana na ulipo base hata mi pia nmelizwa sana na hzo biashara kwahyo nahs kama naww unatangaza tu biashara kama watu wengine
 
Hongera umeweza kueleza changamoto za vijana wengi wanaomaliza Vyuo vikuu.

Utakuwa mtu mwema sana, mwishoni kutoeleza kuwa na darasa la foreksi
 
Pole Sana Kwa changamoto mkuu, ila kama ungejiua ungefeli big time, kubwa umesimama na kusonga mbele,nakupa heshima yako
 
Fx inatukanwa sana aisee.

Inasikitisha sana.

Ubaya ni kwamba una risk Hela ndefu halafu huna skillz tamaa na uoga vimeku cost.

Tafuta maarifa usikurupikie vitu.

Yaani sijui kama R.M kama ulikuwa unafuata.

Hata kama unazo skillz za kutosha usipofuata R.M ni kazi Bure utaunguza within a week.

Msije P.M sifundishi mtu Mimi.
 
Nmekuelewa ndugu,lakin kutokana na ulipo base hata mi pia nmelizwa sana na hzo biashara kwahyo nahs kama naww unatangaza tu biashara kama watu wengine
Vijana wengi wanaumizwa na kulizwa sana. Nimeandika haya ili wengi wajifunze na wachukue hatua. Kwa kua wapo watu ambao wamefanikiwa na kufanya vizuri na kwakua wapo watu ambao wamefanya vibaya katika hizi biashara ninwazi sasa siwezi shauri watu kuacha au kuwahamasisha kufanya. Ninachowatia moyo vijana wengi ni kutokata tamaa kama wanaweza kuvumilia matokeo au kukata tamaa mapema kabla hasara haijakua kubwa
 
Fx inatukanwa sana aisee.

Inasikitisha sana.

Ubaya ni kwamba una risk Hela ndefu halafu huna skillz tamaa na uoga vimeku cost.

Tafuta maarifa usikurupikie vitu.

Yaani sijui kama R.M kama ulikuwa unafuata.

Hata kama unazo skillz za kutosha usipofuata R.M ni kazi Bure utaunguza within a week.

Msije P.M sifundishi mtu Mimi.
Kitu cha muhimu ni kuwa na jamii inayokubali kujifunza. Wengi tunajifunza vizuri zaidi baada ya kushindwa ni wachache sana wamefanikiwa moja kwa moja pasipo kushindwa. Kwa sababu hiyo nimeyaandika haya ili kuwapa tahadhari vijana ambao wanawaza kuifanya hii biashara na kuwatia moyo wale ambao wameona hii biashara ndio njia pekee ya kujikimu mahitaji yao
 
Pole Sana Kwa changamoto mkuu,Ila kama ungejiua ungefeli big time, kubwa umesimama na kusonga mbele,nakupa heshima yako
Kitu kikubwa nachoamini ni kua hakuna hasara kama hasara ya kuipoteza nafsi yako. Watu wanapoteza mabilion sembuse hizi milioni. Pesa inatafutwa na itapatikana kikubwa ni kuulinda mtaji namba moja ambao ni uhai.
 
Hongera umeweza kueleza changamoto za vijana wengi wanaomaliza Vyuo vikuu.
Utakuwa mtu mwema sana, mwishoni kutoeleza kuwa na darasa la foreksi
Ninacho amini ni kuwa wapo watu wangi sana wanafariki kwa kujiua kwa sababu ya msongo wa mawazo unaotokana na kupata hasara katika biashara. Sio tu biashara za mtandaoni bali pia biashara ambazo zinahusisha kukutana na watu. Mfano, wangapo wamekopa pesa benki wakalima mvua haikunyesha kwa wakati, wangapi wamenunua magari yakapata ajari, ni wangapi wamejenga nyumba zikaungua? Je tunajua ni wangapi wanajiua kila siku kwa sababu mbali mbali. Kwa upande wangu nafikiri shida ni afya ya akili na kudhorota kwa afya ya akili husababisha watu kuchukua sheria mkononi na kujidhuru. Nachokifikiri ni kuwa na mfumo wa matibabu ya afya ya akili kwa wafanya biashara na si kufungua madarasa mbali mbali ya forex
 
Trading facts

Rely on yourself, the world does not give a f*ck
Live the moment, no expectations no disappointments
Every master was once a beginner, mindset is everything

Read twice
 
Status
Not open for further replies.
Back
Top Bottom