Jina la Ulimboka na nembo ya tiba nchini(Tanzania daima 8/7/2012). | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Jina la Ulimboka na nembo ya tiba nchini(Tanzania daima 8/7/2012).

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by asakuta same, Jul 9, 2012.

 1. a

  asakuta same JF-Expert Member

  #1
  Jul 9, 2012
  Joined: Mar 1, 2011
  Messages: 15,065
  Likes Received: 81
  Trophy Points: 0
  Prudence Karugendo

  UKOSEFU wa udadisi huwafanya baadhi ya watu wayaangalie mambo na kubaki kuyafurahia tu kama mapambo au kuyashangaa bila kuelewa sababu zilizoyafanya mambo hayo kuwa kama yalivyo.

  Mfano kwenye nembo za tiba mara nyingi huwekwa picha ya nyoka, nina imani watu walio wengi wamezizoea nembo hizo za tiba wakiziangalia na kuziacha zilivyo bila kujiuliza ilikuwaje mdudu huyo hatari kwa afya ya mwanadamu akawa kwenye nembo inayoashiria usalama wa afya ya mwanadamu.

  Ni kwa nini nyoka akawekwa kwenye nembo ya tiba hilo ni suala jingine, kwa sasa tuiangalie alama nyingine inayoelekea nayo kujiingiza kwenye nembo hiyo ya tiba hapa nchini kwetu na pengine duniani kote, pale alama hiyo itakapokuwa imeeleweka kwa watu wote ambao akili zao timamu zinawatuma kuijali tiba. Na alama hiyo si nyingine bali jina la Dk. Steven Ulimboka.

  Dk. Steven Ulimboka ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini. Msimamo wa rais huyo ulikuwa ni wa kuiondoa taaluma ya tiba kwenye porojo za kisiasa na kuifanya isimame pekee kama taaluma nyeti inayozigusa moja kwa moja roho za wanadamu, taaluma ambayo ikifanyiwa uzembe kidogo tu roho inapotea na ikishapotea haipatikani tena.

  Ni kweli kwamba zipo taaluma nyingine nyeti katika maisha ya mwanadamu lakini sidhani kama kuna taaluma nyingine ambayo ikifanyiwa uzembe kidogo tu roho inapotea kama ilivyo taaluma ya tiba.

  Tuuchukulie ualimu kwa mfano, nayo ni taaluma nyeti, sababu bila walimu hata taaluma ya tiba ni lazima iyumbe. Lakini hata hivyo taaluma ya ualimu bado haijaufikia unyeti wa kupoteza roho ya mtu papo kwa hapo unapotokea uzembe kwenye taaluma hiyo.

  Uzembe wowote kwenye taaluma ya ualimu utasababisha tu ujinga lakini roho za watu zikibaki salama. Heri kubaki mjinga ukihifadhi roho yako na uhai ukiyalinda maisha.

  Hapo naonyesha unyeti wa taaluma unavyozidiana nguvu. Taaluma zote mbili, ualimu na utabibu, ni nyeti lakini unyeti unaocheza na akili za watu hauwezi kuufikia unyeti unaocheza na roho za watu.

  Mtu anaweza kupoteza maarifa, akawa mjinga, baadaye ujinga wake ukapatiwa tiba na kumrudisha kwenye uerevu. Lakini mtu akipoteza roho hakuna jinsi nyingine ya kuitafutia tiba hali anayokuwa ameiingia, mauti, sababu anakuwa amepoteza maisha, amekufa.

  Kwa miaka ya hivi karibuni hapa nchini utawala wa nchi yetu umetokea kuishusha hadhi taaluma na sekta ya tiba kwa ujumla hapa nchini kiasi cha kuifanya ionekane ni taaluma ya kawaida tu inayozidiwa na taaluma nyingine.

  Imetokea hata uhasibu umeonekana ni taaluma nyeti kuliko utabibu!

  Kijana anayemaliza chuo, mhasibu, na kupata kazi mfano kwenye Mamlaka ya Mapato (TRA), kwa kipindi cha miezi sita tu anakuwa ameishakuwa na uwezo wa kujenga nyumba na kununua gari, kama si magari, vyenye thamani ya mamilionii!

  Ukiuliza inakuwaje mtu anapata uwezo huo kwa muda mfupi kiasi hicho utaambiwa ni mhasibu huyo yuko TRA, kazi nyeti!

  Hali ni tofauti kabisa kwa vijana wanaohitimu masomo yao kwenye fani ya tiba. Hawa wanalishwa viapo vya kuwabana waamini kwamba kazi yao ni ya wito, wafanye kazi ya wito bila tamaa ya kumiliki nyumba wala gari.

  Kazi yao ibaki kuyanusuru maisha ya watu kwa vile ni kazi ya wito!

  Sekta ya tiba nchini imeshushwa hadhi kwa kiwango cha kutisha kutokana na ushahidi unaojionyesha. Isingekuwa hivyo watawala wetu wakatumia pesa ya kodi zetu kwenda nje ya nchi kutibiwa hata kwa magonjwa madogo madogo kama vile mafua na maumivu ya kichwa.

  Wanakwenda nje ya nchi kutibiwa kwa vile wanaamini kwamba huko sekta ya tiba bado inathaminiwa na kuheshimiwa pamoja na watabibu wao, kitu ambacho watawala wetu wamepuuzia kukizingatia na kukitekeleza hapa kwetu.

  Nchi yetu kwa sasa imegeuka kitalu cha kuzalisha soko kwa ajili ya hospitali za nje hasa ya nchini India . Pesa ya kodi zetu inaishia kuwaneemesha watabibu wa India wakati wa hapa nyumbani wakihimizwa kufanya kazi kwa uvumilivu wakiwa wamekitilia maanani kiapo chao cha wito wa kazi!

  Ni kitu gani kinatufanya tushindwe kuiboresha sekta ya tiba hapa nyumbani kwetu na badala yake tunachangia uwezo wetu wote kuzidi kuiboresha sekta hiyo katika nchi za wenzetu?

  Hili ni swali ambalo pengine watawala wetu ndio walio katika nafasi nzuri ya kulitolea ufafanuzi.

  Najua katika kulijibu swali hilo vitatajwa vitu kama zana (vifaa vya tiba) ambazo sisi hatuna katika mahospitali yetu pamoja na kwamba zana hizo zimo ndani ya uwezo wetu.

  Akili za kawaida zinaweza kumfanya mtu ajiulize kwamba kama rais wetu anaweza kuwa na ndege ya bei mbaya kuliko ya Waziri Mkuu wa India , maana tunaona kwamba Waziri Mkuu wa India mara nyingi anatembelea ndege za abiria wa kawaida, inawezekanaje hospitali zetu zikose vifaa vya tiba ambavyo vimejaa tele kwenye hospitali za India kwa kisingizio cha kukosa uwezo?

  Tujiulize kwa nini waziri wa Tanzania awe na hadhi sawa au hata iliyoizidi ya waziri wa India lakini hospitali za Tanzania zishindwe kuwa na hadhi sawa na hospitali za nchi hiyo?

  Tofauti hiyo lazima inaletwa na mpangilio wa vipaumbele, wala sidhani kama ina uhusiano wowote na uwezo wa nchi kiuchumi.

  Uchumi wetu hauwezi kutufanya tuwe na uwezo wa kumiliki ndege ya kifahari kwa ajili ya mtu mmoja tu, rais, lakini ukashindwa kutuwezesha kuzihudumia hospitali zetu na watabibu wetu kwa kiasi kinachofaa kwa usalama wa afya za wananchi wote.

  Kwa nini hatusemi kwamba nchi yetu ina uwezo mdogo hawezi kununua ndege ya kifahari kwa ajili ya mtu mmoja, rais, kwahiyo rais wetu akadandie lifti kwenye ndege za viongozi wa nchi nyingine, kama India na nyinginezo, anapotaka kusafiri nje ya nchi?

  Nakumbuka iliwahi kusemwa kwamba ndege ya rais ni lazima inunuliwe hata kama wananchi wanakula majani. Kinachoshindikana ni upatikanaji wa vifaa vya kuyanusuru maisha ya wananchi kwa upande wa tiba na si starehe za watawala. Hapo ndipo tunapoona kuwa hatuna pesa, pesa kidogo iliyopo ikawatibie wateule wachache nchini India na kwingineko ulimwenguni.

  Nimeyaangalia hayo kufuatia kudorora kwa sekta ya afya hapa nchi sanjari na migomo ya madaktari inayojirudiarudia na kuleta adha kubwa nchini huku maisha ya wananchi walio wengi wa kipato cha chini yakiwa yamewekwa rehani.

  Madai ya madaktari yanaeleweka hata kwa mlipa kodi wa kiwango cha chini kabisa kiuelewa lakini yanashindikana kueleweka kwa watawala wetu wanaoonekana kuwa na uelewa wa juu.

  Badala yake watawala wetu wanatumia kauli za ubabe na vitisho kuwanyamazisha madaktari wakijiamini kuwa wao wameshika mpini wakisahau kuwa madaktari wameshikilia bomu.

  Ndani ya vitisho hivyo dhidi ya madaktari kulimojitokeza kisa cha kutekwa nyara Rais wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka, na baadaye kupatikana kesho yake akiwa ametelekezwa katika pori la Pande, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, akiwa nusu mfu.

  Mazingira ya kutekwa kwa Dk. Ulimboka mpaka sasa ni utata mtupu. Jinsi yalivyo kumhisi mtu kuwa ndiye kahusika ni kujichumia dhambi za bure.

  Ninachoweza kusema ni kwamba waliotenda unyamaume huo bilashaka walilenga kuzizima harakati za daktari huyo kijana za kuhakikisha sekta ya tiba na afya kwa ujumla inaimarika nchini.

  Walidhani pengine wakimpoteza kinara huyo kila kitu kingesahaulika. Madaktari wangesahau kudai mazingira bora ya kutolea tiba, vifaa bora kwa ajili ya kutolea tiba pamoja na mafao yao.

  Nikumbushe kidogo, Makaburu wa Afrika Kusini walipoinyofoa roho ya kijana mzalendo wa nchi hiyo, Steven Bantu Biko, mwaka 1977, walidhani wamepunguza kwa kiasi kikubwa harakati za kuupinga utawala wao dhalimu.

  Walikosea kwani walikuwa wameuchochea moto. Baada ya kuinyofoa roho ya Biko makaburu wakawa wamezalisha kina Biko wasiohesabika. Biko mwenyewe akabaki kutumika tu kama alama ya ukombozi.

  Kwahiyo waliodhani kwamba wamemuua Biko wakawa wamemtengenezea maisha yasiyokatika.

  Biko anaishi hata leo na anaendelea kuenziwa wakati waliodhani wameshiriki kifo chake wengi wao wakiwa wamekufa na mizoga yao kuzikwa pamoja na majina yao, hatuwakumbuki tena. Hakuna anayekumbukwa hata mmoja.

  Kwahiyo hata waliohusika na unyama dhidi ya Dk. Ulimboka wanapaswa kuelewa kwamba walichokifanya, hata kama hakikufanikiwa kama walivyokusudia, kisingekuwa na matokeo waliyoyatarajia.

  Katika mazingira kama hayo ni vigumu kumpoteza Ulimboka akatoweka na kusahaulika. Kinyume chake jina la Ulimboka litachapwa kwa mhuri wa moto kwenye roho za Watanzania wote wanaopenda kuona mabadiliko kwenye sekta ya afya, hususan tiba, nchini mwao.

  Watanzania wote wanaopenda kuona huduma ya tiba ikiimarika hapa nchini kiasi cha kuwafanya hata viongozi (watawala?) wawe na imani ya kutibiwa nchini mwao badala ya mtu mmoja mmoja kubeba pesa ambayo ingeweza kuwatibu hata watu 1,000 kwenda kutibiwa peke yake nchini India, Marekani na kwingineko, hawawezi kulisahau jina la Dk. Ulimboka.

  Kwa vyovyote vile jina la Ulimboka litabaki kwenye nembo ya tiba na huduma bora za afya hapa nchini pale itakapokuwa imepatikana. Watakufa wao lakini Ulimboka atadumu kwa karne nyingi zijazo.

  prudencekarugendo@yahoo.com 0784 989 512
   
 2. Tume ya Katiba

  Tume ya Katiba JF-Expert Member

  #2
  Jul 9, 2012
  Joined: Apr 6, 2012
  Messages: 4,892
  Likes Received: 730
  Trophy Points: 280
  Old story
   
 3. Joyum

  Joyum Senior Member

  #3
  Jul 9, 2012
  Joined: Oct 30, 2007
  Messages: 153
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Old is gold and valuable. however for narrow minded person(NMP), is nothing. so watch out NMP
   
Loading...