Jiji la Mbeya lageuzwa 'shamba la bibi'

Pdidy

JF-Expert Member
Nov 22, 2007
50,956
22,138
Jiji la Mbeya lageuzwa 'shamba la bibi'


KWA serikali Shilingi milioni 68.2 ni pesa kidogo sana, na kwa mafisadi hiyo sio pesa kabisa kwao kwani inawatosha kununulia whisky tu, lakini kwa wananchi, hiyo ni pesa nyingi sana. Kwao ni mabilioni yenye kuokoa maisha yao!

Ukubwa wa pesa hiyo kwa wananchi unaonekana kwenye matumizi yake. Wao whisky sio kipaumbele, bali kipaumbele chao ni huduma za jamii kama vile elimu, afya, maji safi na barabara. Kwa hiyo, Shilingi milioni 68.2 zinapotumika vizuri kwenye huduma hizo za jamii zinakuwa na thamani kubwa zaidi kuliko shilingi bilioni 133 za kashfa ya EPA.

Katika Jiji la Mbeya Shilingi milioni 68,255,544 zilitolewa kwa ajili ya ujenzi wa chumba cha upasuaji na wodi ya wazazi kwenye Kituo cha Afya cha Igawilo kilichopo pembezoni mwa jiji hilo, lakini kwa bahati mbaya kazi iliyokusudiwa ilikamilika pasipo kukidhi viwango.

Ni matumizi haya ya ujenzi wa chumba cha upasuaji na wodi ya wazazi yanayoifanya pesa hiyo kuwa nyingi, ni sawa na mabilioni kwa wananchi kwani huduma hizo zitaokoa maisha ya wananchi masikini wasio na uwezo wa kwenda kutibiwa nje ya nchi au kulipia gharama kubwa zinazotozwa kwenye hospitali za watu binafsi kama ilivyo kwa waporaji wa kodi zao.

Lakini Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2007/08 ilibaini kasoro katika utekelezaji wa mradi huo, kwamba pamoja na kukamilika kwa ujenzi wa vyumba hivyo, mkandarasi wa mradi huo, Judex Contractors, hakukidhi viwango hivyo jengo kutokabidhiwa kwa Halmashauri ya Jiji la Mbeya.

Hadi Februari 18, mwaka huu wakati wa Mkutano Mkuu wa Baraza la Halmashauri ya jiji hilo, mkandarasi alikuwa hajakabidhi jengo wala kuyafanyia marekebisho kwenye maeneo ambayo hayakukidhi viwango.

Kitendo cha jengo hilo kutokabidhiwa kutokana na kutokidhi viwango hakuonekani kukera uongozi wa jiji hilo, na kwa mtazamo huo ni wazi hiyo pesa inaonekana kuwa kidogo, na kweli kwa serikali na wafujaji wa fedha ya umma hiyo ni pesa kidogo, lakini wanasahau kuwa ni kubwa sana kwa wananchi ambao wanaiangalia katika thamani ya huduma itayotolewa kwenye lile jengo.

Kutokereka kwa uongozi wa jiji kutokana na kitendo cha mkandarasi kutokabidhi jengo hilo kwa zaidi ya miaka miwili sasa kunadhihirika katika hatua iliyochukuliwa, ambayo kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi wa Jiji hilo, Dk. Samwel Lazaro ni kuvunja mkataba na mkandarasi huyo pamoja na kumuondoa katika orodha ya wakandarasi wenye nafasi ya kupewa kazi na jiji hilo, zaidi ya hapo hakuna maumivu zaidi dhidi yake.

Hatua hiyo ya uongozi wa jiji kuhusu mkandarasi huyo ilizua maswali mengi zaidi kuliko majibu wakati wa Mkutano Mkuu wa Baraza la Halmashauri, hususani kutoka kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Beatha Swai.

Katibu Tawala alihoji mambo kadhaa kuhusu mkataba na mkadarasi huyo ikiwemo jiji kukamilisha malipo yake kabla ya kuridhika na kazi yake pamoja na mantiki ya kukatisha mkataba tu pasipo uwajibikaji kwa kurejesha sehemu ya fedha kwa sababu alitenda kinyume cha mkataba.

“Kuvunja mkataba na kumnyima kazi mkandarasi haina nguvu sana, hapa kuna ukiukaji wa taratibu na hasara, mwajiri lazima ajiridhishe kuwa huduma zinazotolewa na wataalamu zinalingana na fedha wanazolipwa (mishahara), value for money lazima ionekane,” anasema Katibu Tawala huyo.

Kwa mujibu wa Katibu Tawala huyo, thamani ya fedha si kwamba ionekane kwenye kazi za wakandarasi tu bali hata kwa waajiriwa serikalini, nao utendaji wao upimwe kwa kuangalia huduma za utalaamu wao uliowapa ajira iwapo zinalingana na thamani ya mishahara wanayolipwa.

Wakati uongozi wa Jiji hilo ukijaribu kujivua lawama katika mradi huo, Mkandarasi mwenyewe, Judex Contractors Ltd ameiambia Raia Mwema kuwa uongozi wa jiji hilo ndio uliotengeneza BOQ ambapo uliweka makadirio ya chini ambayo hayakuzingatia gharama halisi.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo, Bi Judith alitoa makadirio aliyopewa kuwa ni Shilingi milioni 24,941,630 kwa wodi ya wazazi na Shilingi milioni 27,231,990 kwa chumba cha upasuaji tofauti na gharama halisi za wakati huo zilizokadiriwa kuwa zaidi ya Shilingi milioni 90.

Anasema uongozi wa jiji ulimsihi kutekeleza mradi huo kwa kiwango walichokikadiria kwa madai kuwa hawakuwa na fedha lakini wakihitaji kuweka huduma hiyo katika hospitali hiyo kuwapunguzia wananchi, hususani kina mama usumbufu.

Mhandisi Majengo wa Jiji hilo, Bashiganya ndiye aliyehusika na ukaguzi kwa kila hatua na kutoa cheti kwa ajili ya malipo kushindwa kumwelewa anapomtupia mzigo wakati anaelewa wazi kuwa yeye ndiye mhusika mkuu wa kazi hiyo kuwa chini ya kiwango.

Kinachotatiza zaidi kuhusu hatua ya uongozi wa jiji kujivua kuhusika katika sakata la mradi huo ni kuwepo kwa taarifa kuwa kiliwahi fanyika kikao chini ya aliyekuwa Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya wakati huo, Bi Asumpta Ndimbo kilichowajumuisha Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya na mhandisi wake wa majengo, Wakurugenzi wa Halmashauri na Maafisa Elimu toka wilaya zote za mkoa huo na wakurugenzi toka Wizara ya Afya kuhusu mradi huo.

Kwa maelezo ya Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo ya ujenzi, kikao hicho kiliitishwa baada ya viongozi hao kutembelea mradi huo na kuona mapungufu yake na mwisho wa kikao Mkurugenzi wa Jiji aliagizwa kumuongeza mkandarasi Shilingi milioni 30 kwa ajili ya kukamilisha na kufanyia marekebisho jengo hilo, agizo ambalo halikutekelezwa na badala yake mwaka jana mkataba ukasitishwa na kuzuiawa kufanya kazi na jiji hilo.

Mhandisi wa Majengo wa Jiji hilo anaonekana kujiweka mbali na sakata hilo wakati ukweli unabaki pale pale kuhusika kwake kutokana na ukweli kuwa yeye ndiye mtaalamu mwenye dhamana ambaye alikubali kuendesha mradi huo kiujanja ujanja na kumwingiza mkandarasi mtegoni.

Lakini katika hatua ya kushangaza, Meya wa Jiji hilo, Athanas Kapunga alitoa utetezi wake, utetezi ulio tofauti na maelezo ya watendaji akiwemo Kaimu Mkurugenzi waliokiri kufanyika makosa katika suala hilo, kwani Meya aliitupia lawama Serikali Kuu kwamba ndiyo iliyowaelekeza kuwabeba wakandarasi wa ndani ili kuwajengea uwezo.

Mbali ya kuitupia lawama Serikali Kuu, Meya Kapunga alidai kuwa madiwani wanashindwa kukagua miradi ya maendeleo kutokana na Kamati za Ujenzi wa miradi hiyo kuwawekea mizengwe huku wakiwatisha kuwa watahakikisha wanawaangusha kwenye udiwani.

Hata hivyo Katibu Tawala wa Mkoa huo alizikanusha hoja hizo kwa kusema kuwa Serikali Kuu haiagizi halamashauri kutoa kazi kwa wakandarasi wasio kuwa na uwezo, huku ile ya madiwani akiwaeleza kuwa ni heri wakaangushwa kwenye udiwani kwa kusimamia vema miradi ya maendeleo kuliko kutetea udiwani wao kwa kuendekeza uzembe na wizi kwenye miradi ya maendeleo iliyopo kwenye maeneo yao.

Viongozi kutoka mkoani wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo, John Mwakipesile walionyesha kukwazwa zaidi na hatua ya uongozi wa jiji hilo kukamilisha malipo wakati kazi imetekelezwa chini ya kiwango.

Kitendo cha Mhandisi wa Jiji hilo kutoa cheti cha kuthibitisha kukamilika kwa kazi hivyo mkandarasi kukamilishiwa malipo, na baadaye uongozi huo huo tena kutoa maelezo ya kutokabidhiwa jengo kwa sababu ya kutokukidhi viwango, kinazua utata zaidi, lakini wakati huo huo kikidhihirisha jambo moja kwamba tatizo halikuwa kwa mkandarasi bali ni mhandisi mwenye dhamana ya majengo.

Diwani mmoja aliyezungumza na Raia Mwema mara baada ya mkutano ule alifichua siri ya mkanganyiko katika miradi mbali mbali ya maendeleo kwenye jiji hilo kwa kusema,

“Haya ndiyo matokeo ya kukandamiza fikra za watu, tunapohoji kwenye vikao kuhusu ufisadi unaofanyika kwenye miradi tunafokewa, tunaambiwa ni wakorofi kazi yetu ni chokochoko, leo imedhihirika na huu ni mradi mmoja tu katika mingi yenye utata.”

Lakini tatizo jingine linalojitokeza kwenye usimamizi wa miradi katika jiji hilo ni kukosekana kwa ufuatiliaji na ukaguzi wa miradi ya maendeleo kutokana na uhaba wa wakaguzi wa ndani unaolikabili jiji hilo.

Mkaguzi wa Ndani wa Halmashauri ya Jiji hilo, Clementine Robert alithibitisha kutofanya ukaguzi wowote kwenye miradi hiyo hadi siku ya mkutano huo na kubainisha kuwa kwa wakati huu yupo peke yake baada ya wenzie wawili kwenda masomoni.



Jiji la Mbeya limo hatarini
Kilichojibainisha katika mkutano huo ni ukweli kuwa Halmashauri ya Jiji la Mbeya haina utaratibu wa kukagua miradi yake ya maendeleo, si mkaguzi wa ndani wala madiwani wenye kutambua umuhimu wa ukaguzi katika kujiridhisha na thamani halisi ya fedha inayotolewa kwenye utekelezaji wa miradi hiyo.

Swali linalosumbua hapa ni kwamba iwapo hali iko hivyo kwa mradi huo mmoja, hali ya mingine mingi iliyosalia ikoje iwapo haikaguliwi.

Ni wazi kwamba katika mazingira ya aina hii Jiji la Mbeya haliwezi pata maendeleo, litabaki kuwa shamba la bibi ambako wajaja wataendelea kujichotea kodi za wananchi bila ya hofu yoyote, kwani wananchi wanachapa usingizi wakati madiwani wao hawaelewi kilichowapeleka kwenye uongozi wa jiji hilo, hivyo kutoa uhuru usio mipaka kwa wezi kujichukulia watakacho pasipo hofu.
 
Back
Top Bottom