DOKEZO Jiji la Dodoma kuna changamoto ya mpango mji, Watu wengi wanaishi maeneo hatarishi

Hili ni dokezo maalum toka kwa mwananchi mtumiaji wa JF mwenye nia ya kuusaidia umma kuwa na taarifa 'maalum'

Mzee wa Code

Member
Sep 23, 2024
55
79


Hali ilivyokuwa ya Desemba 2024
Dodoma, mji ambao umekuwa na ongezeko la idadi ya Watu kwa kasi kubwa tangu kuanza kutumika kwa Chuo Kikuu cha Dodoma Mwaka 2007.

Mbali na hapo uamuzi wa Hayati Rais John Magufuli kuhamishia rasmi makao makuu ya Serikali jijini hapo kumeifanya Dodoma iwe ‘busy’.

Hata hivyo, ukuaji huu wa haraka umesababisha changamoto mbalimbali, mojawapo ikiwa ni usalama na afya ya wakazi wanaoishi karibu na mabwawa ya maji taka.

Awali, Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) ambayo ilianzishwa wakati wa uongozi wa Hayati Rais Julius Nyerere, ilikuwa na jukumu la kupanga na kupima Mji wa Dodoma kwa kuzingatia usalama na ustawi wa wakazi wake.

Baada ya mamlaka hiyo kuvunjwa, Jiji la Dodoma lilikosa mpango bora wa matumizi ya ardhi, na viwanja vingi vya makazi na biashara vilitolewa kiholela, hata katika maeneo hatarishi kama yale yanayozunguka mabwawa ya Maji Taka ya Swaswa.

Eneo la Swaswa, ambalo lilianzishwa kama Kijiji cha Kilimo Mwaka 1974, limekuwa maarufu kwa kilimo cha mbogamboga.

Mabwawa ya maji taka yaliyopo eneo hilo yalianzishwa ili kuhudumia mfumo wa maji taka, lakini kutokana na uhaba wa ardhi ya kilimo na mahitaji ya mboga, wakazi wa eneo hili wamekuwa wakitumia maji ya mabwawa hayo kwa kumwagilia mboga zinazouzwa katika masoko kama Sabasaba.

Changamoto za Kiafya na Kijamii
Wakazi wa Swaswa wameanza kushuhudia athari za mabwawa haya katika maisha yao. Wanaeleza wasiwasi juu ya usalama wa afya zao kutokana na matumizi ya maji taka kwa kilimo, huku Wakulima wakiambiwa kuwa maji hayo yamewekewa dawa, hivyo ni salama kwa kilimo.

Hata hivyo, Wakulima hawa hawana kinga yoyote wanaposhughulikia maji hayo, baadhi yao hutumia maji hayo kwa kuoga, hali inayoongeza hatari za kiafya.

Mbali na changamoto za kiafya, Watoto wamekuwa wakihatarisha maisha yao wanapocheza karibu na mabwawa hayo na baadhi yao kuripotiwa kuzama.

Eneo hilo la mabwawa pia lipo Mita 700 kutoka makazi ya Waziri Mkuu, ikionyesha kwamba athari hizi ziko karibu na maeneo muhimu ya mji.

Ushahidi wa Hatari
Uchunguzi unaonyesha kuwa maji katika mabwawa ya Swaswa hayavutii hata wadudu wa kawaida kama nzi, hali inayotoa ishara kwamba maji haya yana kemikali hatari.

Mfugaji mmoja alieleza kuwa mifugo, hasa ng’ombe, hawanywi maji hayo hata wakilazimishwa, ikithibitisha hofu kuhusu usalama wa maji hayo kwa viumbe hai.

Mvua ikinyesha hali huwa mbaya, ni kama ilivyokea wiki iliyopita Desemba 6, 2024 ambapo hali ilikuwa mbaya kwa kuwa miundombinu mingi ya kupitisha maji haikuwa

Wakati wa Mvua ndipo hasa Mji unapoonekana kuwa haujapangiliwa vizuri, maji yanasambaa mitaani na kuwa tishio, miundombinu iliyopo nayo haikidhi mahitaji ya kucontrol maji ya mvua.

Wito kwa Mamlaka za Jiji la Dodoma
Kwa kuzingatia athari hizi, ni muhimu kwa Mamlaka za Jiji la Dodoma na Serikali kuchukua hatua za haraka ili kuhakikisha usalama wa Wakazi wa Swaswa na wakulima wanaotumia maji hayo, wanakuwa salama.

Mabwawa hayo yanaweza kuhamishwa au kuwekewa mfumo wa kusafisha maji taka kwa usahihi ili kuhakikisha kwamba hayaleti madhara kwa jamii.

Hatua hizi zitasaidia kulinda afya na ustawi wa wakazi wa Dodoma, ambao wanastahili mazingira salama ya kuishi na kufanya kazi.
 
Back
Top Bottom