Jijengee Uwezo wa Kuwa na Nidhamu Binafsi Katika Maeneo Haya Yafuatayo

willtarimo

Member
Mar 20, 2014
21
10
Neno Nidhamu lina maana kubwa sana katika safari yoyote ile ya mtu ya kukimbilia katika maisha ya mafanikio makubwa anayoyataka hapa duniani. Kama unahitaji kuwa bora na mwenye mafanikio mazuri katika kazi, biashara, masomo, ubunifu, vipaji na karama ulizonazo, nakadhalika; basi ujue itakubidi kujijengea nidhamu mbali mbali zinazoweza kukusaidia kufikia katika hatua ya Mafanikio makubwa hasa katika maeneo unayohitaji kufanikiwa.

Nidhamu ni nini basi? Katika maana nzuri ya nidhamu ninayoweza kukupa ili ikusaidie kuelewa ujumbe wa makala hii kwa uzuri zaidi ni kwamba; Nidhamu ni hali ya kujijengea tabia njema ndani yako zitakazokusaidia katika kufanikiwa na kufikia mafanikio makubwa unayoyahitaji juu ya eneo fulani. Nidhamu ni kujenga tabia katika uaminifu, uwazi, ukweli, heshima, hekima na busara, nakadhalika.

Kwa maana hiyo kila mtu anayehitaji Kufanikiwa katika jambo lolote lile ni lazima hajihakikishie anajijengea nidhamu binafsi na ya kutosha katika maisha yake, ili kumfanya awe bora na afanye mambo kwa ubora na ufanisi mkubwa pasipo kukata tamaa au kuacha. Hivyo ni kazi kwangu mimi na wewe kujenga nidhamu kubwa na ya kutosha katika kutusaidia kufanikisha mambo yetu yote tunayohitaji tufanikiwe.

Kama nidhamu ni uaminifu, uwazi, ukweli na heshima. Maana yake tunatakiwa kujenga uaminifu, uwazi, ukweli na heshima binafsi katika maeneo mbali mbali ya maisha yetu binafsi ili tuweze kufanikiwa katika ndoto na maono yetu tuliyonayo hapa duniani. Katika makala hii ya leo nimejaribu kukuandikia maeneo 10 unayohitaji kujenga nidhamu binafsi (Self-Discipline) ili uweze kufanikiwa na kuwa bora zaidi katika kujiletea mafanikio makubwa zaidi katika maeneo unayohitaji kufanikiwa.

Maeneo unayohitaji kujenga Nidhamu binafsi katika maisha yako ni kama ifuatavyo; jenga nidhamu hizi baada ya kusoma hapa ili uweze kufanikiwa zaidi katika Maisha yako.

1: Nidhamu ya Muda:

Hakuna eneo muhimu linaloweza kukuletea mafanikio makubwa au kupoteza mafanikio kabisa, kama eneo lako binafsi la kuwa mwangalifu katika kuheshimu muda. Muda ni chombo muhimu sana na nganzi kuu ya kukupelekea kufikia katika Mafanikio yoyote yale unayoyahitaji hapa duniani. Kama husipokuwa mwangalifu nakujijengea nidhamu ya kutunza na kuheshimu muda wako uwe na uhakika ni ngumu sana kufikia katika hatua za kufanikisha malengo na mipango yako ya kila siku, mwenzi, mwaka, nakadhalika.

Kila mtu anahitaji rasilimali ya muda kama sehemu ya kumsaidia katika safari yake ya kupata mafanikio anayoyahitaji. Jambo mojawapo ambalo Mwenyezi Mungu aliwapa wanadamu wote sawa pasipo upendeleo ni suala la muda; kumbuka watu wote kwenye jamii wawe matajiri au masikini, wafupi au warefu, wembamba au wanene, wasomi au wasiosoma; katika wote hao wamepewa masaa 24 ya siku ili waweze kuyatumia vyema kwa ajili ya kulitumikia kusudi la kuwepo kwao hapa duniani.

Maanake ukitumia vyema masaa 24 uliyopewa nina uhakika hautokuwa mtu wa kulalamika juu ya mafanikio ya watu wengine bali nawe utachukua hatua; kubwa zaidi ni lazima ufahamu ndoto na maono ya maisha yako ni nini? Kisha ni vyema uchukue hatua ya kubadilika kwa ajili ya kuhakikisha unakuwa mwangalifu katika muda ili uweze kujiletea mafanikio makubwa unayoyahitaji.

2: Nidhamu ya Matumizi ya Fedha:

Fedha ni rasilimali ya pili baada ya muda ambayo hii si kila mtu amejaliwa kuwa nayo, ila ni sehemu ya zao la mambo mengi mazuri na mabaya kutokana na mtumiaji binafsi anavyoweza kuitumia kwa malengo yake binafsi. Na ndio maana katika makala hii nimejaribu kukuandikia na kukusisitizia kuwa na nidhamu njema na nzuri katika matumizi ya fedha.

Watu wengi sana wameingia katika majuto na malalamiko kutokana na matumizi mabaya ya fedha waliyoyafanya hapo nyuma katika maisha yao. Wapo waliopata fursa ya kupata fedha kupitia katika biashara zao, mshahara, kibarua, marafiki, mikopo, nakadhalika. Lakini walijikuta wakiishia katika matumizi mabaya na yasiyo na umuhimu na ulazima kwa wakati walionao. Leo hii ninavyoongea hivi wamerudia hali zao za shida na umasikini; Je, watakosaje kujuta?

Katika yote haya yanayotokea kwa watu wengi kwa kutumia fedha vibaya hasa kwa matumizi yasiyo ya lazima; hii ni kutokana na sababu kuu ya kukosa nidhamu na heshima na uaminifu wa kutumia fedha vizuri zinazopita mikononi mwao. Ni vyema rafiki ukubali kubadilika katika matumizi yako ya fedha, na kujijengea tangu sasa nidhamu njema ya matumizi ya fedha ili uweze kufanikiwa zaidi katika maisha yako.

3: Nidhamu ya Kusikiliza zaidi ya Kusema:

Kuna msemo usemao, “ni vyema kuwa msikiaji zaidi, kuliko msemaji sana.” Hii ni kweli na hakika kwa kupitia msemo huu tunazibitishiwa kuwa mara nyingi ukiwa msemaji sana unakosa nafasi hata ya kusikiliza wengine wanachotaka kukuambia. Hivyo tabia hii inaweza kukujengea kukosa nafasi ya kupata mawazo ya watu wengine yanayoweza kukujenga na kukuletea fursa nzuri ya kukupa hatua ya kusogea mbele zaidi.

Nakutaka uwe msikiaji zaidi na mtendaji wa mambo mazuri, na zaidi punguza kusema sana kuliko kusikiliza. Jenga nidhamu ya kusikiliza zaidi kutoka kwa wengine kuliko kusema zaidi. Na ni vyema usikilize mawazo chanya na hasi; mawazo hasi yanaua, chanya yanajenga.

4: Nidhamu ya Uvumilivu:

Uvumilivu ni hali ya kukubaliana pamoja na kukabiliana na mambo magumu unayokutana nayo katika maisha yako; na hasa kwa yale yanayokuwa kikwazo kwako cha kufikia katika mafanikio makubwa unayoyahitaji. Kama ukishindwa kujenga nidhamu ya kuvumilia mambo yoyote yanayokukabili mbele yako kama kikwazo cha kukuzuia katika safari yako ya mafanikio, uwe na uhakika ni vigumu sana kupiga hatua kadhaa mbele za kukusaidia kufanikiwa.

Unachotakiwa kufanya ni kuwa mwangalifu katika kutokukata tamaa juu ya maisha yako binafsi. Jijengee tabia na nidhamu ya kujiamini na kuwa mvumilivu katika maisha yako ili uweze kufanikiwa zaidi katika kila jambo unalolihitaji hapa duniani. Ndio maana kuna msemo usemao, aliye mvumilivu hula mbivu. Msemo huu ukiwa na maana kuwa, mtu aliye mvumilivu siku zote ndie anayekula matunda mazuri kutokana na uvumilivu wake aliouonesha.

5: Nidhamu ya Kufanya jambo moja hadi likamilike, au kwa kufikia mwisho pasipo kuamia jambo jingine:

Hakuna mafanikio yanayoweza kuja kwa kujaribu kufanya kila kitu. Kumbuka kuwa kila anayetaka kila kitu mwisho wake hukosa vyote. Na pia mshika mambo mawili huwa moja linamwondoka au yote kiujumla. Na hivi ndivyo watu wengi wamekosea na kujikuta hawapigi hatua yoyote mbele kila mwaka na hasa katika malengo na mipango yao waliyonayo. Hawa ni watu wanaotaka kufanya na kujaribu kila kitu kwa wakati mmoja, na kumbe hapo ndipo wanapoharibu vyote na mwendo kasi wa mafanikio yao unakufa.

Ndugu yangu nakusihi usijaribu kudanganyika kufanya kila kitu kwa wakati mmoja; jaribu kujenga tabia na msimamo wa kinidhamu kufanya jambo moja hadi mwisho, ili uweze kufanikiwa katika hilo moja kikamilifu na kisha baada ya hapo uamie jambo la pili. Katika jambo hili ni vizuri ufahamu kuwa wewe peke yako kufanya kila kitu huwezi, bali jaribu kupangilia mambo yako kwa ufanisi na hasa yale muhimu (priority’s) ili uweze kuanza na hayo kisha uamie mengine.

Katika hili nakusihi kwa wewe unayejua kusoma kwa lugha ya kiingereza, nakuomba tafuta kitabu cha “Eat that Frog” kilichoandikwa na mwandishi maarufu na muhamasishaji aitwae Brian Tracy; utajifunza mengi zaidi hasa namna ya kufanya jambo moja hadi mwisho pasipo kuacha.

6: Nidhamu ya Kukubaliana na Makosa pale yanapotokea:

Kosa lako si kosa bali kurudia kosa ni kosa. Ndio wanavyosema waswahili na watu wamjini. Nami nataka nikuambie ni kweli na wala hawakukosea kusema hayo maneno mazuri. Yawezekana huwa unapokosea unakuwa mtu wa kujilaumu tu kwa muda mrefu hadi unazuia nafasi ya kusogea mbele na kufanya mambo mengine zaidi. Nataka nikuambie hicho si kitu kizuri katika kujifunza juu ya maisha na hasa katika kuyataka maisha ya mafanikio.

Kamwe sahau kuhusu mafanikio kama una tabia ya kutokukubaliana na kosa au makosa yanayojitokeza katika safari ya maisha yako ya kila siku. Nakuomba ujenge nidhamu ya kukubaliana na makosa hasa pale unapofanya jambo na kujikuta umekosea; kwa kufanya hivyo utapanua wigo mkubwa katika kujifunza na kuachia nafasi kubwa zaidi ya kuona fursa nyingi zaidi.

Kutokukubaliana na kosa kunaleta kukata tamaa na kuzuia mwendo kasi (ku-focus) katika kile unachokihitaji katika maisha yako yote hapa duniani. Hivyo ni vyema uache tabia ya kujilaumu juu ya makosa yanayojitokeza katikati yako na cha zaidi sana ni vyema uchukue hatua ya kubadilika na kujenga nidhamu ya kukubali kuwa umekosea kwa kusudi la kujifunza.

7: Nidhamu ya Utendaji na Uwajibikaji:

Hebu jiulize maswali haya. Je, unawajibika vipi sawa sawa katika nafasi yako uliyopewa au uliyonayo kama kiongozi, mwanafunzi, mwalimu, daktari, mfanyabiashara na mjasiriamali, mkurugenzi, nakadhalika? Hayo ni baadhi tu ya maswali ya kujiuliza mimi na wewe kama tunataka kupima kiwango cha uwajibikaji wetu wa kila siku katika nafasi zetu tulizonazo.

Kukosa nidhamu ya kuwajibika sawa sawa katika nafasi yako uliyonayo ni kupoteza hatua kadhaa unazotakiwa kuzipiga ili kufikia katika nganzi ya mafanikio makubwa. Jiulize ni nini ambacho unatakiwa kuwajibika nacho sawa sawa ili kukusaidia kufikia katika mafanikio makubwa unayoyahitaji? Ni vyema sasa uchukue hatua ya kujenga nidhamu ya utendaji na kuwajibika sawa sawa katika nafasi hiyo ili uweze kufanikiwa.

8: Nidhamu katika Matumizi ya Mitandao ya Kijamii:

Mitandao ya kijamii (social network) kwa sasa ina nafasi kubwa katika maisha ya kila mtu anayeitumia kila siku au mara kwa mara. Wapo watu ninaowafahamu wameathirika na mitandao hii ya kijamii kwa kupoteza heshima zao, uaminifu, ukweli na uwazi kwa watu wengine; na hii ni kutokana na suala nzima la kukosa nidhamu katika matumizi ya kila siku ya mitandao hii.

Na hili ni jambo mojawapo kubwa linalochangia kuanguka kwa maadili ya jamii yetu nakadhalika. Kwa sababu watu wengi wamekosa nidhamu ya matumizi ya kila siku ya mitandao hii; hivyo wamekuwa ni watumwa na waarifu wa vyanzo vibaya vya kuporomosha maadili mema ya jamii yetu. Nini ninachotaka nikuambie? Jifunze kuwa na nidhamu njema ya kutumia mitandao ya kijamii kila siku ili ufanikiwe katika kuwajenga wengine.

9: Nidhamu katika Kutunza Afya ya Mwili:

Kama kuna jambo ambalo watu wengi hawajui na wanalotakiwa kulijua katika umuhimu wa kuwaletea mafanikio yao makubwa, ni juu ya suala zima la kulinda na kuhifadhi vyema afya ya miili yao. Kama ukishindwa kuulinda mwili wako na kuuzingatia kwa kila siku dhidi ya vyakula unavyokula, mazoezi, kulala usingizi wa kutosha, nakadhalika. Uwe na uhakika kwa kutokufanya hayo na kukosa nidhamu ya kutekeleza mambo hayo kwa uaminifu na kweli, utapoteza nafasi ya kufanya kazi kwa ufanisi na ubora kwa sababu ya kukosa afya iliyo njema na yenye msaada kwako katika kukusaidia kufanikiwa kwa haraka zaidi.

Usijidanganye rafiki yangu afya ni muhimu sana katika kukupelekea kufikia mafanikio yoyote makubwa unayoyahitaji; unaweza kufanya kazi kwa bidii ukidai unatafuta mali na pesa ila kama usipokuwa mwangalifu na mwenye nidhamu katika kutunza mwili wako kwanza ili uwe na afya njema kwa kuzingatia kanuni za kiafya; uwe na uhakika unaweza kupata hizo mali na pesa lakini mwisho wake ukaishia kutokuzifaidi kutokana na ubovu wa afya yako. Linda afya yako ili afya ikulinde na kukupatia nguvu na uwezo wa kutumikia ndoto yako na maono yako uliyonayo.

10: Nidhamu katika Mahusiano yako na wengine:

Je, unaishi vipi na watu waliokuzunguka? Je, unaonesha nidhamu gani juu ya bosi wako na wafanyakazi wenzako ulio karibu nao kila siku? Je, unahusiana vipi na marafiki na ndugu zako katika maisha yako ya kila siku? Je, unaboresha vipi mahusiano yako na mke au mume au na watoto wako unapokuwa ndani au nje ya nyumba yako binafsi? Hayo ni baadhi ya maswali machache tu kati ya mengi yaliyopo, ambayo yanaweza kuwa somo tosha kwako binafsi la kukusaidia kujua ni namna gani unavyoweza kujenga mahusiano mazuri katika ngazi mbali mbali.

Nataka ufahamu kuwa mahusiano yako mazuri na watu wengine waliokuzunguka, yanaweza kukusaidia kufikia katika mafanikio makubwa sana hasa katika yale unayoyahitaji. Jenga tabia ya nidhamu binafsi katika kuboresha mahusiano yako na wengine kama vile marafiki, ndugu na jamaa, viongozi wako, wanafunzi na wafanyakzi wenzako, nakdhalika. Kwa kufanya itakusaidia kukupeleka katika mafanikio makubwa.

Hayo ndio niliokuandalia kwa leo kama sehemu ya kukusaidia kufahamu ni namna gani unavyoweza kujenga nidhamu mbali mbali katika maisha yako zinazoweza kukusaidia katika kukuletea mafanikio makubwa katika maisha yako hapa duniani; tumikia ndoto na maono yako lakini huwezi kufanya hivyo kama hautojijengea nidhamu binafsi za kukusaidia kufikia katika mafanikio makubwa ya hiyo ndoto yako.

Jenga nidhamu hizo kwa kuchukua hatua leo hii ya kuzitekeleza ili ubadilike na kufikia mafanikio makubwa. Hadi kufikia hapo nakutakia maisha mema yenye mafanikio na yenye kujawa na nidhamu tele siku zote. Wasiliana nasi kupitia mawasiliano yetu yafuatayo:

www.cicbat.com

Simu: +255 767 500994

Barua pepe: cicbanttz@gmail.com
 
Nidhamu hakika ndo kila kitu japo ni mtihani mkubwa kwa walio wengi.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom