Jifunze kuhusu kilimo bora cha mazao. Maswali na ushauri inaruhusiwa

Mack84

Member
Mar 18, 2020
7
6
UTANGULIZI
Mahindi ni zao muhimu la chakula, na ni aina ya nafaka inayotumiwa zaidi kama chakula,uhususani katika matifa ya Afrika, na yamekuwa yakitumika zaidi na nchi zilizopo kusini mwa jangwa la Sahara. Ni chakula cha matumizi ya nyumbani kwa idadi ya watu inayokadiriwa kuwa asilimia 50. Ni chanzo muhimu cha madini na kuongeza nguvu mwilini, protini, madini ya chuma (iron) vitamini na madini mengine asilia.Waafrika

hutumia mahindi kwa njia mbalimbali (uji, ugali na pombe). Na mahindi ya kuchoma.

Kila sehemu ya mmea wa mahindi ina thamani kiuchumi : punje, majani, shina na magunzi huweza kutoa kiasi kikubwa cha bidhaa nyinginezo zilizo chakula na zisizokuwa chakula.

Vile vile mahindi ni chakula muhimu cha mifugo (ng’ombe) na huhifadhiwa kama silage. Pia mabaki ya mimea na nafaka hutumika viwandani kutengeneza wanga na mafuta.

Mahindi ni mimea ambayo hustahimili mabadiliko ya hali ya hewa tofauti tofauti na huweza kumea katika maeneo mengi tofauti hapa nnchini. Kuna aina nyingi za mahindi yanayotofautiana katika muda wa kukomaa, mavuno na ustahimilivu wa hali ya hewa.

HALI YA HEWA NA UDONGO
Mmea huu unahitaji kiwango cha joto cha kila siku cha nyuzi joto 20º ili umee vyema. Joto la juu sana kwa mazao mazuri ni kama nyuzi joto 30º.

Mahindi hustawi katika maeneo mbalimbali hapa nchini kuanzia 0-3000 m kutoka usawa wa bahari kulingana na aina ya mbegu na hali ya hewa ya eneo husika.

Mahindi huwa yanaathirika sana na ukosefu wa unyevu wakati wa kutoa maua na matunda. Pia yanahitaji maji ya kutosha wakati wa kupanda. Katika nchi za joto jingi (tropiki), mahindi hufanya vyema katika mvua ya kiwango cha milimita 600 hadi 900 wakati wa kukua.
Mahindi yanaweza kukuzwa kwenye aina nyingi za udongo lakini hukua vyema zaidi katika udongo wa kichanga au tifutifu usiotuamisha maji mengi, ulio na hewa ya kutosha na ulio na rutuba na madini ya kutosha. Pia h ustawi vizuri katika udongo wenye uchachu wa kiwango cha pH 6-6.5.

Pia ikumbukwe kuwa mahindi ni moja ya zao ambalo huathirika sana na hali ya chumvi katika maji na udongo.

KUTAYARISHA SHAMBA
Shamba la mahindi linahitajika kutayarishwa mapema mapema sana mwanzoni mwa msimu wa mvua au hata kabla mvua kuanza.
Shamba linaweza kuandaliwa kwa aina tofauti tofauti kulinganisha na eneo na aina ya udongo. Shamba linaweza kulimwa kwa trekta au kwa jembe la mkono kwa kina kisichopungua 15 cm ili kuruhusu mizizi kupenya vizuri na udongo kuhifadhi maji kwa wingi. Kama shamba liaasili ya kutuamisha maji matuta yaandaliwe vizuri shambani. Moto usitumike wakati wa kuandaa shamba.
Vilevile kama shamba lina asili ya mmomonyoko wa udongo, basi ni vyema tahathari ichukuliwe katika uhifadhi wa udongo na unyevunyevu ardhini kwa kuweka matandazo.

FAIDA ZA KUTAYARISHA SHAMBA MAPEMA
1. Baada ya kuvuna,udongo bado ni mlaini hivyo hulimika kwa urahisi kwa kutumia jembe lolote.
2. Masalia yatakayofunikwa udongoni huoza mapema.
3. Hupunguza magugu.
4. Hupunguza wadudu waharibifu na kuharibu mazalio yao.
5. Mahindi yanapata mvua ya kutosha hadi kukomaa.
6. Magonjwa kama yale ya ya majani (streak ugonjwa wa milia) hayatatokea au
yatakuwa kidogo.
7. Mbolea uliyoweka itayeyuka pamoja na mahindi na yatastawi vizuri.

WAKATI WA KUPANDA

Wakati wa kupanda hutatanisha kwani mvua haitabiriki,Kama mvua hunyesha nyakati na majira yale yale ya mwaka basi kalenda ifuatayo inaonyesha tahere za kupanda zao la mahindi katika eneo lako.
  • Mbeya na maeneo ya jirani, mwanzoni mwa
    mwezi Novemba hadi Desemba mwishoni.
  • Morogoro,Pwani, DSM, Tanga na Maeneo Jirani Mwezi Januari, February na March Mwanzoni katikati.
  • Iringa na maeneo ya jirani, katikati ya mwezi Novemba hadi Desemba mwishoni.
  • Songea na maeneo ya jirani, katikati ya mwezi Novemba hadi Januari mwanzoni.
Kupanda mahindi mapema ni muhimu kwani uwezekano wa kuvuna mazao mengi ni
mkubwa. Kwa mashamba makubwa sana wakati wa kupanda uwe wiki moja kabla ya mvua
kuanza kunyesha na isizidi wiki mbili kabla ya mvua. Isiwe mapema zaidi kwani mbegu
zitaharibiwa na joto wakati mwingine na wadudu, panya, ndege na wanyama wengineo.

KUCHAGUA MBEGU BORA
Mbegu bora ni zile zilizo zalishwa kitaalamu.
  • Ni safi hazijabunguliwa na wadudu.
  • Huzaa mazao mengi.
  • Hustahimili magonjwa.

AINA ZA MBEGU

  • Mbegu aina ya chotara(hybrid)
  • Aina ya ndugu moja(synthetic)
  • Mbegu aina ya composite
Mbegu za kisasa zikitumiwa vizuri katika misingi ya kilimo zina uwezo wa kuzaa magunia
50-80 au tani 5.5 – 7.5 kwa hekta moja.

MAPENDEKEZO YA MBEGU ZA KUPANDA

Kuna mbegu nyingi za kisasa zilizoko kwenye soko mfano wa UYOLESEEDS, SEEDCO, PANNAR, MERU n.k

KUPANDA

Idadi ya mimea katika eneo ni muhimu kwani ikizidi
  • Kuna uwezekano wa mazao kupungua.
  • Mimea kuwa dhoofu
  • Mimea mingi kutozaa au kuwa na matunda madogomadogo.
  • Kunakuwa na uwezekano mkubwa wa kusambaa kwa magonjwa kiurahisi
Idadi ya mimea nayo ikipungua kwenya eneo husababishwa mavuno kupungua
jambo la kufanya ni kupanda mbegu katika nafasi na kiwango cha mbegu sahihi kilichoshauriwa na mtaalamu hapo chini.

KIASI CHA KUPANDA
Kiasi cha kilo 20-25 za mbegu kinatosha kupanda hekari moja (Hii hutegemea na aina ya mbegu)

NAFASI ZA KUPANDA

Unaweza kupanda mhindi katika nafasi mbalimbali kulingana na mahitaji yako, hali ya hewa na rutuba ya udongo. lakini zifuatazo ni nafasi pendekezwa na hutumika sehemu nyingi hapa nchini kwetu.
  1. 75cm x 30cm mfano:- mstari kwa mstari 75cm na mche kwa mche 30cm hii ni kwa mbegu moja kwa kila shina na kufanya uwe na idadi ya mimea zaidi ya 44000 kwa hekta.
  2. 75cm x 60cm mfano;- mstari kwa mstari 75cm na mche kwa mche 60cm hii ni kwa mbegu mbili kwa kila shina na kufanya uwe na idadi ya mimea 44000 na zaidi kwa hekta.
  3. 75cm x 25cm mfano:- mstari kwa mstari 75cm na mche kwa mche 25cm hii ni kwa mbegu moja kwa kila shina na kufanya uwe na idadi ya mimea zaidi ya 53000 kwa hekta.
  4. 90cm x 50cm Hii ni nzuri kwa sehemu kame na kwa wanaopanda mazao mchanganyiko au kilimo mseto.
Mahindi yanaweza kuchanganywa na mazao mengine ya kutambaa kama kunde, maharage, maboga, karanga nk.

MATUMIZI YA MBOLEA

  • Mahindi hustawi na kuzaa vizuri iwapo yatapatiwa mbolea pamoja na matunzo mengine ya kilimo bora.
  • Angalizo: Ukipanda mbegu bora bila kutumia mbolea ni kazi bure.

KUNA AINA MBILI KUU ZA MBOLEA

  • Mbolea za asili mfano; samadi,mboji na majani mabichi,mbolea hizi hua na virutubisho vya kutosha ambavyo havijulikani vipo kwa kipimo kiasi gani.
  • Mbolea za viwandani, hizi hua na virutubisho vya kutosha na vipimo hujulikana, hii
inasaidia kujua ni kiasi gani kitumike kwa kipindi gani.

KWA MFANO:
Mbolea inayotumiwa na wakulima wadogo mara yingi huwa haitoshi. Mahindi ya kiwango cha juu yaweza tu kufikia kiwango cha juu cha Uzalishaji iwapo yatapewa lishe na madini ya kutosha. Mahindi ya tani 2 kwa hekta na tani 5 kwa hekta hutumia karibu kilo 60 N, kilo 10 za P na kilo 70 K kutoka katika udongo. Mahindi hunyonya Nitrogen pole pole katika miezi ya kwanza baada ya kupanda, lakini huongezeka hadi kiwango cha juu kabisa.

wakati wa kutoa maua na kukuza tunda (Punje). Mahindi huhitaji nitrogen kwa kiwango cha juu na ukosefu huwa ndio kizingiti. Kiwango cha juu cha nitrogen kinahitajika mara tatu; kwanza wakati wa kupanda, pili, wakati ambapo mmea umefikia sentimita 50 za urefu na tatu, wakati matunda ya mahindi yanaanza kutoa zile nyuzi nyuzi nyororo au ndevu (silking). Udongo mwingi huwa na madini ya phosphorous (P) na potassium lakini sio kiwango kinachotosheleza mahitaji haswa ya mbegu za mahindi zinapochipua. Weka Phosphorus (P) karibu na mbegu ili ziote kwa haraka. Potassium (P) hutumika kwa kiwango kikubwa lakini hitaji la mimea hubainika baada ya upimaji wa hali ya udongo kujua kiasi cha mahitaji (soil test). Ndo maana twasisitiza mbolea za viwandani sio lazima iwe ya kemikali.

DALILI ZA UPUNGUFU WA MBOLEA

Ukosefu wa Potassium (K) husababisha ncha za majani kuwa na rangi ya njano na kuunda gunzi (cob)
lisilo na punje hadi juu.

Ukosefu wa Phosphorus (P)hufanya matawi kuwa na rangi ya samawati na mbegu zisizo laini.

Dalili za ukosefu wa nitrogen ni majani ya rangi ya manjano na mimea dhaifu mifupi.

Phosphate haifyonzwi haraka na mahindi na pia udongo mwingi wa nchi za joto hukosa madini hayo ya phosphate. Inashauriwa uwele mbolea ya kiasili kama samadi kabla ya kulima ili uboreshe hali ya udongo na kuongezea madini. Katika Kilimo cha asili (organic farming), Nitrogen (N) hutiwa kwenye udongo kupitia mimea ya jamii ya mikunde (legumes) ambayo hutoa nitrogen katika hewa, Hata hivyo mapendekezo ya kitaalamu yaliyo katika misingi ya uchunguzi wa udongo hutoa nafasi nzuri ya kupata kiasi kizuri cha mbolea bila kuweka kiwango cha chini au juu.

Omba msaada kutoka kwa mafisa ugani wa kilimo walio katika eneo lako. Katika maeneo yanayo tegemea mvua kukuza mahindi, panda mbegu wakati wa mvua ya kwanza. Hii itaruhusu mizizi kunyonya madini yaliyotengenzwa na bakteria katika udongo. Maji yaliyosimama huyeyusha na kuondoa madini ya nitrogen kutoka katika udongo na kusababisha ukosefu wa Nitrogen.

UDHIBITI WA MAGUGU
Udhibiti wa magugu ni muhimu sana. Katika wiki 4 hadi 6 za mbele baada ya kuota, mahindi huathiriwa sana na magugu. Ni lazima mahindi yapandwe mara moja baada ya kutayarisha shamba. Na usiache magugu mpaka yawe makubwa ndipo uanze kupalilia.
Unaweza kulima katikati ya laini za mahindi ili udhibiti magugu.

Nchini Tanzania, kupalilia mara mbili kunahitajika kwa aina nyingi za mahindi, ingawa kupalilia kwa mara ya tatu kutahitajika kwa aina ambazo zinahitaji zaidi ya miezi 5 kukomaa. Njia rahisi za kupalilia kunaweza kufanywa kwa mkono au kwa jembe la mkono ama kwa kutumia viuagugu ambavyo vimethibitishwa.

Angalizo; usitumie viuagugu bila ushauri wa kitaalam kwa sababu kemikali hizi zimegawanyika katika makundi makuu mawili yaani ambazo zinachambua (Selective herbicides) na ambazo hazichambui (Non Selective herbicides). Kwa hiyo basi ni muhimu kuwa makini sana unapofanya maamuzi ya kutumia.

Lakini pia kwa kiwango kikubwa wakulima wengi wanapoandaa shamba huwa hawalimi na kusawazisha vizuri, mara nyingi wanakoma mara moja tuu na kupanda, unashauriwa kupiga kiuagugu aina ya Round Up siku moja au mbili baada ya kupanda. Usipige kuanzia siku ya nne kwani kemikali Hii inaunguza kila kitu chenye kijani kibichi.

UHUSIANO WA NIPE NIKUPE (Push – Pull Technology) KUZUIA BUNGUA
Desmodium (Desmodium uncinatum) nyasi ya Molasses (Melinis minutifolia) zikipandwa kati kati ya laini za mahindi huzuia wadudu kama stalk borers moths. Mimea hii hutoa kemikali ambazo huwafukuza wadudu aina stem borers’ moths. Zaidi ya hayo Desmodium huzuia gugu haribifu aina ya witchweed (Striga hermonthica). Napier grass (Pennisetum purpureum) na Sudan grass (sorghum vulgare sodanese) ni mimea mizuri sana inayonasa wadudu aina ya stem borers. Napier grass ina njia yake madhubuti ya kujikinga dhidi ya wadudu wanaotoboa mmea kwa kutoa utomvu kutoka kwenye shina, ambayo huzuia wadudu kufyoza mmea na kusababisha uharibifu. Nyasi hizi pia huvutia adui wa stem borers kama mchwa, earwigs na buibui. Nyasi aina ya Sudan pia husaidia maadui asilia, kama nyigu (parasitic wasp).

Mahindi huweka kivuli kwenye mimea ya mboga mboga ikipandwa safu moja katikati ya mboga kwenye maeneo yaliyo na jua kali. Hii huongeza mazao ya mboga zilizopandwa hivi, na mimea jamii ya mikunde huongeza nitrogen kwenye udongo ambayo huitajika zaidi katika ukuaji wa mahindi pia hupunguza wadudu aina ya (leafhoppers, leafbeatles, stalk borers na fall army worm), upandaji wa mimea jamii ya mikunde ufanyike mara baada ya palizi ya kwanza.

UVUNAJI NA UHIFADHI
Mahindi huvunwa mara baada ya kukomaa, yanaweza kuvunwa kwa mikono au kwa kutumia mashine maalum ya kuvunia kama shamba ni kubwa. Mahindi yaliyokomaa vizuri huwa na majani ya njano na punje ngumu zilizoshiba. Ili mahindi yawe tayari kuvunwa, huachwa shambani mpaka yakauke vizuri kabisa na majani yote kukauka na kabisa na hali ya unyevunyevu wa punje kufikia asilimia 15-20%. Mahindi yakiachwa sana shambani huaribiwa na wadudu kama mchwa na dumuzi, pia kama mahindi yakivunwa yakiwa bado hayajakauka vizuri au kukomaa vizuri ni rahisi sana kubunguliwa. Hivyo ni vyema kuzingatia muda mzuri wa kuvuna.

Pia uvunaji wa mahindi kipindi cha mvua nyingi hupelekea mahindi kuharibika kama yatahifadhiwa yakiwa yameloweshwa na mvua.
Kuna changamoto nyingi sana hutokea kipindi cha uhifadhi mahindi zikiwemo ukaushaji wa mahindi katika kiwango kinachohitajika (13% grain moisture content), kuzuia wadudu na wanyama waharibifu. Mahindi yakihifadhiwa katika hali ya unyevunyevu na joto kali hupelekea mahindi kuota ukungu ambao huzalisha sumu iitwayo aflatoxin na kufanya mahindi hayo yasifae kabisa kwa chakula cha binadamu.

Ili kuhifadhi mahindi vizuri, kausha mahindi yako katika jua kali mpaka kiwango cha unyevunyevu katika punje kufikia 13%. Njia rahisi ya kujua mahindi yapo katika hali ya 13% ni hivi, baada ya kukausha mahind yako juani chukua punje kadhaa jaribu kuuma punje moja moja. Ukiona punje ni laini na inapasuka kirahisi baada ya kuuma basi endelea kuaniaka mahindi yako tena mpaka yawe magumu kabisa.

Baada ya hapo unaweza ukachanganya dawa za kuulia wadudu katika mahindi yako na kuyajaza katika viroba/mifuko na kuhifadhi gharani. Pia unaweza kuhifadhi mahindi yako katika chombo ambacho hakipitish hewa kama pipa, jaba n.k. Vilevile kuna njia mbadala ya kuhifadhi mahindi katika njia mbadala ya mifuko maalumu ambayo huitaji kuweka sumu ya aina yoyote. Baada ya hapo panga magunia yako gharani vizuri. hakikisha ghara ni safi, kavu na hakuna upenyo wa kuruhusu wadudu na wanyama waharibifu kuingia.

WADUDU NA MAGONJWA YA MAHINDI

WADUDU

Wapo wadudu wengi sana ambao hushambulia mahindi yakiwa shambania na yakiwa yamehifadhiwa gharani, hivyo ni vyema mkulima kuwatambua wadududu wasumbufu shambani na jinsi ya kukabiliana nao.

1. Viwavijeshi / African Amyworm (Spodoptera exempta)
Wadudu hawa ni hatari sana katika mazao ya nafaka na hutokea kwa mlipuko. Wanauwezo wa kuangamiza shamba kubwa kwa muda mfupi sana na kuhamia shamba lililo karibu.

Wadudu hawa unaweza kukabiliana nao kwa kufanya ukaguzi mara kwa mara wa shamba lako na mara tu uonapo dalili za kuwepo unaweza kuwaangamiza kwa sumu ambayo inaweza kuwaangamiza kirahisi kabla ya kuleta tatizo kubwa. Pia ni vyema kuandaa shamba mapema na kuweka shamba katika hali ya usafi ili kuzuia mazalia na kuondosha Mabaki yote shambani.

2. Viwavijeshi vamizi (Fall Armyworm)
Viwavijeshi Vamizi (fall armyworm) ni wadudu hatari kutoka barani Amerika ambao waliingia Afrika mwaka 2016 na kufika Tanzania mwaka 2017. Wadudu hawa wanashambulia mazao zaidi ya 80 lakini chakula chao kikuu ni zao la Mahindi ambayo pia ndio chakula kikuu cha Wanzania.

Wadudu hawa wamesambaa kwa kasi, zaidi ya mikoa 20 mpaka kufikia march 2018 ilikuwa imeathirika na wameleta athari kubwa kwa wakulima wa mahindi na sasa mahindi yanapokauka wanakula Pamba, Mihogo na mazao mengine ya biashara na chakula hali ambayo inawafanya wakulima kupata shaka na wasiwasi wa usalama wa chakula. Wadudu hawa ni wagumu kidogo kuwadhibiti na wakulima wengi wanawachanganya sana. Kwenye somo litakalofuata nitazungumzia kwa undani kuhusu wadudu hawa.

3. Vipekecha shina wa mahindi (Busseola fusca; Chilo and Sesamia species)
Vipekecha shina wa mahindi ni wadudu waharibifu wa mahindi, mtama na mazao mengine katika nchi nyingi za Afrika. Viwavi wa nondo, huchimba na kuingia ndani ya shina la mahindi, wakila tishu za ndani na kusababisha mmea kunyauka na hatimaye kufa.

Wadudu hao wanaweza kudhibitiwa kwa njia mbalimbali kama mbinu za kitamaduni, hasa, kilimo cha mseto na mfumo wa ‘sukuma-vuta’ (‘pushpull’). Pia wanaweza kudhibitiwa na dawa za kuua wadudu, unga wa mwarobaini, lakini katika hatua za mapema, kabla ya mabuu kuchimba na kuingia ndani ya shina.

4. Osama/Dumuzi (Prostephanus truncates)
Dumuzi ‘Osama’ ni mdudu hatari sana wa mahindi ya kuhifadhiwa kote barani Afrika. Osama hula ndani ya nafaka na kuacha shimo na ganda tupu. Ghala safi ya kuhifadhia ni muhimu ili kuweza kuzuia uharibifu wa osama. Kukoboa nafaka kutoka kwa gunzi kabla ya kuhifadhi na kuvuna kwa wakati kunaweza kupunguza uharibifu.

5. Funza wa vitumba (Helicoverpa armigera)
Funza wa vitumba ni mdudu msumbufu wa mimea mingi muhimu ya chakula, mafuta na fedha duniani kote, ikiwa ni pamoja na nafaka mfano Mahindi ikiwa ni mojawapo, mikunde, matunda na mboga. Ushambulizi mkali wa viwavi wa nondo huyu kunaweza kusababisha hasara kwa mavuno yote.

Kudhibiti kwa njia ya kemikali kunapaswa kufanywa kwa makini na wakati mwafaka kwa kuwa viwavi hutoboa na kuingia ndani ya nafaka au matunda ya mmea, hivyo kuweza kulindwa. Usugu kwa dawa, kama vile za pyrethroid, kumeripotiwa katika nchi nyingi.
Bakteria aina ya Bacillus thuringiensis (Bt) na madawa ya mwarobaini hutoa udhibiti wa ufanisi dhidi ya viwavi na wakati huo huo kupunguza uharibifu wa maadui wa kiasili.

Udhibiti muhimu wa kitamaduni ni pamoja na kuondoa na kuharibu mabaki ya mimea baada ya kuvuna, kulima udongo ili uwatoe nje pupae na kupanda kwa wakati mmoja.

MAGONJWA

1. Doa jani la kijivu la mahindi (Cercospora zeae-maydis & Cercospora zeina)
Doa jani la kijivu la mahindi umeibuka kama ugonjwa ulioweka kikwazo kwa mazao ya mahindi nchini Marekani na kusini mwa Afrika katika miaka 25 iliyopita. Ingawa ulidhaniwa kuwa aina moja ya kuvu, Cercospora zeae-maydis, ukaguzi wa chembechembe umeonyesha kuwa kuvu lingine, C. zeina, hupatikana kwa wingi mashariki mwa Marekani na kusini mwa Afrika. Mbegu za kuvu, zinazoishi katika mabaki ya mazao ya awali, hurushwa na matone ya mvua kwenye majani ya chini ya mmea na kusababisha madoa
marefu yanayoungana kwenye mimea isiyohimili na kusababisha baka. Mashina hudhoofika na kuanguka wakati wa mikurupuko ya magonjwa.

Ugonjwa unaweza kusimamiwa kwa kuharibu mabaki ya mimea baada ya kuvuna, kilimo cha mzunguko, kwa kutumia aina zinazovumilia ugonjwa zaidi, na, matumizi ya dawa za kuua kuvu ikiwa zitaleta faida kiuchumi.

2. Muozo wa mahindi na mycotoxin (Fusarium and Aspergillus species)
Kuna aina nyingi za kuvu zinazotokea kwenye mahindi na kuzalisha sumu za kikemikali ambazo huchafua chakula na lishe. Zinajulikana kwa pamoja kama mycotoxins, na sumu hizi zina madhara makubwa kwa afya ya binadamu na wanyama.

Aspergillus inasemekana kuwa mzalishaji muhimu zaidi wa mycotoxin katika Afrika, ingawa kuvu nyingine kama vile Fusarium pia inahusika. Makundi yote mawili ya kuvu hukua kwenye sehemu za mimea zilizokufa na zinazooza na kusababisha kuoza kwa
mahindi katika shamba. Huzalisha unga mwingi wenye mbegu za kuvu juu ya mahindi, kabla na baada ya kuvuna, lakini pia inaweza kuwa bila kuzalisha koga lolote. Muozo wa mahindi unaosababishwa na kuvu zinazozalisha mycotoxin hutokea kwa wingi zaidi wakati mahindi yana matatizo na yanakua vibaya.

Udhibiti bora zaidi wa kuvu hizi huchanganya kuvuna kwa wakati muafaka na kukausha mahindi kabla ya kuyahifadhi. Aflasafe™, njia mpya ya kibiolojia ya kudhibiti Aspergillus, inatumika katika mashamba kabla ya mahindi kutoa maua na imeonyesha matumaini
makubwa katika kupunguza uchafuzi wa mahindi kabla ya kuvuna na baadaye mkusanyiko wa mycotoxins katika bidhaa zilizohifadhiwa.

3. Ugonjwa wa maize lethal necrosis (Multiple virus infections)
Maize lethal necrosis disease (MLND) ni ugonjwa mpya wa virusi barani Afrika. Umesababisha wasiwasi mkubwa kwa sababu mimea hufa na hakuna nafaka au ni nafaka kidogo tu zinazozaliwa.

Chanzo cha ugonjwa
Wataalamu katika tafiti zao wanasema kuwa, ugonjwa huu husababishwa na virusi vya aina mbili vinavyoathiri mmea wa mahindi kwa pamoja ambavyo ni Maize Chlorotic Mottle Virus (MCMV) na Sugarcane Mosaic Virus (SCMV). Virusi hivi husambazwa na wadudu wa aina mbili, ambao ni Thrips pamoja na Aphids, japo kuna wadudu wengine wanaweza kubeba na kusambaza ugonjwa huo kama vile beetles and leafhoppers pamoja na matumizi ya mbegu zilizoathirika.

Dalili za mahindi yalioathirika
  • Majani machanga ya juu hugeuka na kuwa na rangi ya njano na hatimaye kukauka kuanzia pembezoni mwa jani kuelekea katikati na hatimaye mmea kufa.
  • Mmea huweza kutoa machipukizi mengi sana.
  • Mbelewele hukosa chamvua hivyo mmea kutozaa.
  • Mahindi yakishambuliwa wakati yanajaza mbegu, gunzi husinyaa na kuweka mbegu chache au kutojaza kabisa.
  • Mahindi yaliyoathirika hushambuliwa na magonjwa nyemelezi hasa ukungu.
Kwa mimea iliyoanza kusinyaa, huonyesha dalili za kukomaa kabla ya wakati, huku hindi likiwa katika hali ya kuchoma maganda na kuonesha utayari wa kuvunwa.

Aidha, ugonjwa huo unaposhambulia katika hindi lililokomaa, basi huingia moja kwa moja katika kiini cha punje. Mahindi yaliyoathiriwa na ugonjwa huu huota fangas ambayo wataalamu wanasema ina sumu kali ijulikanayo kama Aflatoxin. Sumu hiyo, husababisha madhara kwa binadamu na wanyama.

Utafiti uliofanywa na wataalamu mbalimbali wakiwepo wataalamu kutoka Taasisi ya utafiti wa Kilimo ya Seliani (SARI) wamebaini kuwa, sumu hiyo (Aflatoxin) inayotokana na fangasi, husababisha ugonjwa wa saratani ya ini kwa binadamu na wanyama. Utafiti huo
pia unaeleza kuwa, ugonjwa huo unaweza usionekane kwa haraka na huweza hata kuchukua muda wa mwaka ndipo kujitokeza.
Hivyo basi, ni lazima mataifa yote kuwa makini na kuchukulia jambo hili kwa uzito zaidi.

Mbinu za kuepuka ugonjwa huu
  • Panda mbegu bora zilizothibitishwa na Taasisi ya Uthibiti wa Ubora wa Mbegu (TOSCI) nchini.
  • Usipande mbegu zilizovunwa msimu uliopita kutoka katika shamba lililoshambuliwa na ugonjwa.
  • Safisha shamba kwa kuondoa magugu na masalia yote ya mazao na kuyachoma/kuyafukia kuepuka maficho ya wadudu na virusi vya ugonjwa. Kagua shamba mara kwa mara na kama utaona dalili zilizotajwa hapo juu, toa taarifa kwa mtaalamu wa kilimo aliye karibu nawe.
Namna ya kudhibiti
  • Ng’oa mapema mahindi yote yaliyoathirika, na kuyateketeza haraka.
  • Usipande mahindi katika shamba lililoathirika angalau kwa msimu mmoja. Panda mazao mengine kama vile viazi mviringo, mihogo kama utakavyoshauriwa na mtaalamu wa kilimo.
  • Katika maeneo yenye ugonjwa, dhibiti wadudu wasambazao ugonjwa huo kwa kunyunyizia kiuatilifu kulingana na maelekezo ya mtaalamu.
  • Zingatia kilimo cha mzunguko wa mazao na toa taarifa mapema kwa afisa ugani wa kilimo endapo utaona dalili za ugonjwa. Ugonjwa wa MLND bado unafanyiwa utafiti kwa undani zaidi na dawa bado haijapatikana.
Hivyo wakulima wote wanatakiwa pindi wanapoona kuna dalili zozote zimeanza kujitokeza katika mashamba yao, hawana budi kung’oa mimea yote bila kujali kama mengine hayajaambukizwa kasha waziteketeze kwa moto. Hii ni kutokana na sababu kuwa hata mimea ambayo bado haijaonesha dalili za kuambukizwa, hana budi kuonesha dalili mapema kwani maambukizi husambaa kwa kasi sana na kwa muda mfupi.

4. Ugonjwa wa matupa kwenye mahindi (SMUT).
Ugonjwa huu hushambulia sehemu za uzazi za mahindi. Mashambulizi hufanywa na aina mbili za vimelea jamii ya uyoga (ukungu) vijulikanavyo kwa majina ya kitaalamu kama Sphacelotheca reliana na Ustilago maydis. Vimelea hivyo husababisha magonjwa ya aina mbili ambayo dalili zake zinafanana.

Mimea iliyoshambuliwa na ugonjwa huu ama haizai kabisa ama inazaa kiasi kidogo ukilinganisha na jinsi ambavyo ingeweza kuzaa kama isingekuwa imeshambuliwa. Kwa hiyo mashambulizi ya magonjwa haya husababisha hasara ya mavuno. Inakadiriwa kwamba hasara ya mavuno inawezakuwa kidogo tu ama asilimia kumi (10%) au hata zaidi ya kiwango hicho, lakini kupoteza ni kupoteza hata kama ni kiwango kidogo. Ugonjwa wa “matupa” unaosababishwa na kimelea kijulikanacho kama Ustilago maydis hufahamika kama “Common Smut” kwa kiingereza.

Dalili zake huwa kuota kwa uvimbe katika sehemu za mmea zinazokua kama vile punje za mahindi, mbelewele na hata kwenye majani. Uvimbe huo ukikauka na kupasuka hutoa vumbi jeusi kama masizi ambayo ndiyo viini vya/mbegu ya huo ugonjwa. Dalili ya msingi ya ugonjwa huu kwenye mhindi ni kwamba inawezekana kuwa na baadhi ya punje zilizoshambuliwa na zingine ambazo hazina dalili katika gunzi moja.

Ugonjwa wa “smut” unaosababishwa na kimelea kijulikanacho kwa jina Sphacelotheca reliana hufahamika kama “Head smut” kwa kiingereza. Kama ilivyo kwa ugonjwa wa “smut” ya kawaida, dalili za ugonjwa huu hujitokeza mara nyingi katika hindi lenyewe na mbelewele na mara chache katika shina la mhindi. Tofauti na ugonjwa wa “smut” ya kawaida, katika ugonjwa huu badala ya mhindi kuathiriwa baadhi ya punje, hindi zima hujaa vumbi jeusi ndani ambapo kwa nje ni kama mfuko mweupe ambao kabla ya kukauka hufana na uyoga. Vumbi hilo jeusi ndilo viini vya kimelea. Vivyo hivyo kwenye mbelewele.

Wakati mwingine mmea ulioshambuliwa na ugonjwa huu hudumaa na hushindwa kuzaa. Dalili nyingine ya ugonjwa huu ni mhindi kuotesha vijani vidogo badala ya mbelewele.

UDHIBITI WA MAGONJWA YA”SMUT”
  • Tumia mbegu bora ingawa mpaka sasa haipo mbegu maalumu yenye kustahimili ugonjwa huu. Kwa kutumia mbegu bora, mkulima utajihakikishia mavuno bora.
  • Daima hakikisha unalima kilimo cha kisasa kikijumuisha urutubishaji wa udongo. Epuka kuijeruhi mimea uwapo shambani. Mimea iliyo na majeraha hushambuliwa kwa urahisi na ugonjwa huu. Pia dhibiti wadudu waharibifu ambao pamoja na madhara mengine wanayosababisha pia huijeruhi mimea na kwa hivyo kurahisisha maambukizo ya ugonjwa huu wa “smut”.
  • Kila inapowezekana tumia kilimo cha kubadilisha mazao. Katika kubadilisha mazao ni vema kutumia mzunguko wa mazao yasiyoshambuliwa na ugonjwa wa “smut” kama vile ngano, shayiri, njegere, viazi na maharagwe.
Unapolima hakikisha masalia mabua yamefukiwa chini sana.
Ahsanteni
Imetayarishwa na:
Marcodenis E. Misungwi
Agriculture Extensionist
0768004323
mmarcodenis@gmail.com
Tembelea www.kilimoforum.wordpress.com
 
Shukrani mkuu, nimeweka kambi hapa nitarudi kusoma vizuri maana nina mpango wa kulima mahindi mwaka huu, hivo naimani nitajivunza mambo mengi ya muhimu hapa
 
Shukrani mkuu, nimeweka kambi hapa nitarudi kusoma vizuri maana nina mpango wa kulima mahindi mwaka huu, hivo naimani nitajivunza mambo mengi ya muhimu hapa
Bila Shaka Mkuu karibu sana ujifunze
 
Nisaidie dawa ya kuua mchwa kwenye mahindi na dawa ya kuua panya shambani, mchwa wanasumbua sana Mkuu,.
 
Back
Top Bottom