JICHO LA RA; Kujiachia na kufunguka na Kiswahili! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

JICHO LA RA; Kujiachia na kufunguka na Kiswahili!

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Kiganyi, May 9, 2012.

 1. Kiganyi

  Kiganyi JF-Expert Member

  #1
  May 9, 2012
  Joined: Apr 30, 2012
  Messages: 1,244
  Likes Received: 4
  Trophy Points: 0
  By Zavara Mponjika [​IMG]
  Namna gani watu wangu? Natumia fursa hii kufanya utambulisho mdogo wa jina la kona hii: Jicho La Ra. Pole kwa jamaa zangu wenye athari zinowakwaza kutofautisha herufi “L” na “R”. Ladha ya lugha ni matamshi.  Jina la “Jicho-La-Ra” lilikuwa ni jaribio langu la kuenzi wahenga wetu wa kale. Wanaofuatilia wanaweza kukumbuka nilirekodi santuri miaka ya 2003 (kwa sababu kadhaa haikutoka), na ilikwenda kwa jina hilo.  Nakumbuka moja ya waandaaji, Sani, mwenye asili ya Kinaijeria, alishtuka sana baada ya kuona mantiki ya jalada la santuri ile, alisisitiza kuwa ile nembo ni ya ‘kishetani’. Tuliingia kwenye mjadala mrefu na nikajaribu kufunguka naye, huku nikizingatia kwa kiasi gani mafunzo ya kigeni yalivyotufanya tushindwe kuthamini ama kusahau urithi wetu. Jicho la Ra ambayo ilikuwa na nembo ile ya asili, ilitufanya tufahamiane vyema hasa kuhusu mitazamo yetu ya ulimwengu; hiyo nembo ilikuwa ni utambulisho wa mafunzo ya ndani sana.  Ra au Horus kama alivyoitwa na Wayunani, ni moja ya mizimu ya kale sana na unaweza kusema moja ya nembo ya kiroho ya awali kuliko yoyote kwenye sayari hii. Urithi wetu wa utamaduni na maarifa mengine bado umebakia kule bonde la mto Hapi (unajulikana sasa hivi kama Mto Naili). Kule ndio mahala Wahenga wetu waliweza kufinyanga maarifa yote tuliyonayo leo duniani – imani, hesabu, siasa, teknolojia na mengineyo.  Pitia hii filamu ambayo kama hujaiona ilibidi uione miaka 5 iliyopita. Humo wanamwelezea kidogo Ra. Melezo kamili ya jina hilo yanahitaji makala pekee. Kwa kifupi tu, napenda uelewe lile Jicho linawakilisha ufungukaji katika ulimwengu wa uyabisi na kuona yale unayoyajua kwa mnyumbuliko tofauti kabisa.
  Kufunguka na Kiswahili
  Jamvi hili tayari limeanza kufahamika na watembeao mtandaoni; Wahenga husema, ‘Muambaa ambaa na ufukwe hali uchu.’ Basi wengi waliopitia kwenye jamvi letu hawakuondoka watupu. Nimefanya gumzo la hapa na pale na watu kadhaa waliotoa nasaha zao, na pia sinyamazii wale waliosoma na kutosema lolote. Yote hayo ni namna tofauti za mapokeo.
  Katika pitapita za huku na kule nilipata kumtembelea Profesa John Mtembezi, yeye ni mmoja wa wadau mahiri sana wa Kiswahili duniani. Kwa vile muambaa na ufukwe hali uchu, nilipata mambo kadhaa nitayowamegea nanyi pia.  Kwenye gumzo letu niliweza kujenga naye mawaidha kadhaa kuhusu makala zangu na masuala ya ushairi wa Kiswahili. Majina ya watu mahiri sana kwenye kuenzi Kiswahili yalitajwa kwenye gumzo hilo, kama vile Hamisi Akida, Mzee Kibao, Salim Ali Kibao, Sheikh Mohamed Alli (ambaye ni ndugu wa Mzee Kibao), mwandishi wa kamusi ya zamani ya sheria, na Abdul Bary Diwani. Mtu ambaye alisisitizwa kwenye gumzo hilo alikuwa Mohamed Mwinyi, aliyekuwa mwandishi wa vipindi vya RTD (Radio Tanzania Dar es Salaam).  Ujenzi
  Kuna maoni kadhaa yalijitokeza na nimeona leo ujenzi wangu utafakuri maudhui niliyokutana nayo kwenye mijadala hapa na pale, na kiujumla nimeona nifunguke na Kiswahili. Ama si’ ndio wana? Haya ndio maoni yangu kuhusiana na mjadala niliokumbana nao kuhusu matumizi yangu ya neno ‘mtu chengu’ au ‘mchenguaji’.
  Nilikumbana na mdahalo mkali ambao kwa bahati mbaya ulinipita. Nilivutiwa sana na ule mjadala, ningefurahi ningeuwahi na kujumuika siku ile ile ulivyokuwa ukiendelea. Ningepewa fursa ningeweka ule mjadala kwenye huu waraka.  Nimefurahishwa na mjadala huo ulivyokuwa na uchambuzi uliofanyika; nilitaka tu nikupe, mtu wangu msomaji, mchanganuo wangu hasa kuhusu neno mchenguaji. Hilo neno ni neno la kawaida sana na wala sio la kutunga. Mtu yeyote ambaye ameishi Temeke, zama za Dhahabu za Hip Hop (1990-1995) na kurudi nyuma anaweza akakueleza. Kuna maneno mengi mno ambayo yalikuwa hayavuki Machinjioni (makutano ya barabara za Mandela na Chang’ombe, Dar es Salaam) wala Tazara (barabara za Nyerere na Mandela, Dar es Salaam) kwa sababu ya mila na desturi za TMK. Zamani kule ilikuwa kama sayari (nyingine), na unafahamu kwa kanuni za kijografia sayari zikiwa na viumbe mara nyingi huwa na namna yao inayojitosheleza kuishi.  Lahaja ya kitaa TMK
  Hivyo ndivyo TMK ilivyokuwa hususan kwenye matumizi ya lugha ya Kiswahili. Kwa hiyo, hilo neno sio la kubuni leo bali lilikuwa na matumizi toka miaka ya 80, lakini halikuhusishwa na michano hadi miaka ya 90.  Tena kwenye gumzo langu na Samia X hivi karibuni alinikumbusha alivyonisikia mimi nikitumia neno “machata” kwenye wimbo wangu unaoitwa ‘Vilinge’ uliorekodiwa kwenye studio ya Radar Records kule Darby Uingereza mwaka 2003. Machata ni moja ya hayo maneno ya kale toka zama za ubaharia miaka ya 70.
  [​IMG]
  Yale machata ya ukutani Uswahilini jina lake ni hilo hilo kabla hatujajua mambo ya Hip Hop (miaka ya 1985 kurudi nyuma). Pia, nilikumbana na maoni yanayohusu maneno ‘maonesho’ na ‘maonyesho’: kwenye hilo nasema kwamba, tukumbuke kuwa lugha ni kitu hai; na huwa na matumizi na taswira tofauti sehemu mbalimbali. Kwenye Kiswahili hayo maneno yote ni sahihi. Na ule mfano pia uliotolewa kuwa lile neno ‘Mtu Chengu’, ambalo nilikuwa naliwasilisha, lingeweza kuingia kwenye msamiati, ni sahihi kabisa na si kama kuna jambo litakuwa limekiukwa hapo.  Lugha hai
  Narejea kidogo gumzo langu na Profesa Mtembezi. Tuliweza kudodosa namna maneno na lugha zinavyojenga misamiati (mipya). Moja ya mambo ambayo ningependa tuelewe ni kuwa lugha ya Kiswahili ni lugha yenye kujitosheleza, kinyume na inavyosaidikiwa. Mtindo wa kutohoa ni uvivu tu; ingeweza kufanywa kwa namna bora zaidi ya kukuza lugha hasa tukizingatia kuna lugha nyingi sana za Afrika tunazoweza kuchukua maneno.  Hapo jambo la kufahamu na kuzingatia ni kuwa hakuna mamlaka yenye kumiliki lugha na ndio maana kikoloni (Kiingereza) kinatumia muundo huo huo. ‘Broadcast’ (masuala ya utangazaji) ni neno lililokuwa likitumiwa kwenye kilimo, na maana yake ni upandaji wa kutupa mbegu mbali. Kwa mtindo huo huo, neno kama ‘podcast’ linahusiana na upandaji wa maua. Hii lugha kule Ulaya ilikuwa ni ya wakulima (ya kishamba), kwa nyakati zile ilikuwa inadharauliwa sana. Nyakati hizo Kiyunani ndio ilikuwa lugha ya maana, na baadae kufuatia Kilatini kilipokuwa kimeshika hatamu. Hadi karne ya 13 bado hii lugha ilikuwa inaonekana kama lafidhi ya kikulima.  Kwenye gumzo langu na mkufunzi wa athropolojia Mohamed Yunus Rafik, nilipojadili uzamani wa Kiswahili na Kiingereza, alinidokeza kuhusu ngano za Mfalme Athur — moja ya wafalme wa taifa hilo, kasisi wa ukoloni Uingereza aliyesadikiwa kuishi zama za karne ya 12 (haina uhakika aliishi kipindi gani hasa). Mfalme Arthur alikuwa akiona haya kuongea Kiingereza kama ambavyo viongozi wetu leo wakienda kwenye mikutano ya kimataifa, hususan viongozi wa nchi.  Katika kipindi cha awali Kiingereza hakikuwa na hata hadhi kubwa ya lugha. Kwa vile ilikuwa ni lahaja mpya ya lugha ya Kijerumani, ikaanza kukopa maneno toka lugha zilizoendelea za wakati huo ili ithaminike. Kwa wakati huu lugha zilikuwa ni Kiyunani, Kilatini, na labda ki -Norman (leo Kifaransa).  Ulimbukeni nadhani ni pale ambapo ukoloni umetufanya tusijue kuwa kipindi ambapo kikoloni hiki kinaitwa “lafidhi ya washamba” (peasant dialect), Kiswahili kilikuwa ni lugha kamili, na napenda kukudokeza juu ya mashairi ya Fumo Liongo — mshairi anayesadikiwa kuishi karne ya 9 hadi 12, Pwani ya Mwambao wa Kushi. Baadhi ya tafiti za chuo kikuu cha Cambrige zinamshabihisha na shujaa wao wa kufikirika, Robinhood.  Iwapo mashairi yalikuwa yanaendelea zama hizi, inachoashiria ni kuwa jamii husika ilikuwa na utamaduni ulioimarika sana kifasihi na kimaendelo kwa ujumla. Nitakosa heshima nisipomtaja na kumuenzi Malenga maarufu sana wa mwambao wa Pwani ya Mashariki ya Ukushi, Bi’ Mwana Kupona binti Mshamu. Hapo sijagusia kabisa yale mashairi ya kale yaliyokutwa karne ya nne Kabla ya Kristo kwenye maktaba ya Alekzandria huko Kemeti (leo Misri).
  Na kukumaliza kabisa, kama ulidhani Kiswahili ni lugha changa, kafanyie kazi taarifa hizi rasmi. Kwa kukukandamizia zaidi, zingatia hili:
  “On the Swahili Coast, Indian Ocean trade began as early as 400 BC between Greece and Azania, as the area was commonly known. Around the 4th century AD, coastal towns and trading settlements attracted Bantu-speaking peoples from the African hinterland.“
  [​IMG]
  Hicho kifungu hapo juu kinasema mibangaizo na mishe na watu wa mbele, Wabongo tumeanza kitambo, tangia nyundo ka’ 400 Kabla ya Kristo. Upo hapo mwana!? Kwa hiyo, viongozi wetu wanaposema kiswahili bado kichanga, tuwapige chini maana wanazingua. Kama toka kitambo bado wanaona ni kichanga basi huo uchanga majita ama kubemendwa? Mtu anayeongea hivyo msameheni, ni athari ya sumu ya ukoloni.  Kwa mujibu wa mtaalamu wa lugha na mshairi mahiri, Bwana Sudi Mwakamadhi (Sudi ni mwana wa Malenga wetu Kibao), Kiswahili ni lugha ya kitambo sana na kimepitia majina mengine kabla ya kuitwa Kiswahili, baada ya mawasiliano na Waarabu — kwa mfano Kingozi, ambacho kiliongelewa toka Uhabeshi hadi Pwani ya Kilwa. Tutaingia zaidi somo hilo tukipata fursa.  Hivyo vidokezo vyote sio katika kujinadhifisha na usomi. Iwapo wasomi wa kitaa wanavutiwa na kutafiti zaidi, kama vipi wanaweza lianzisha hapo!  Mchenguaji (Mtu Chengu)
  Mtu chengu ni kama ufafanuzi tu wa mchenguaji, na nadhani shughuli zangu na isimu yangu kwenye fani kwa muda mrefu vimenijaalia hekima ya kuweza kutofautisha unazi na ukweli kila ninapolazimika kupambanua. Kwa utangulizi huo nawatoeni shaka kuhusu matumizi ya neno hilo.  Juzi nlikutana na jamaa mmoja Mchina, tukaongea naye sana. Nilikuwa na maswali kadhaa kama kawaida ya udadisi wangu. Moja ya maswali ilikuwa kuhakiki habari ya kwamba: Je, ni kweli ule Ufalme wa Shang (Shang Dynasty) ya Uchina ni kweli ni ya watu wa Ukushi?
  Akaniambia ndiyo na akanipa ushahidi. Na la pili; nikataka kujua kama neno China linasemwaje kikwao na maana yake. China kikwao ni ”Chung-hwa” (nikabakia kushangaa, kumbe jamaa kwao kunaitwa ‘chungwa’!). Swali la tatu; nilitaka kujua neno mchenguaji linasemwaje kwa Kichina. Ameniambia neno mchenguaji kwao ni “Zhu chi”.
  Shauku yangu ilipelekewa na huu mjadala wetu; yeye alitokea siku ile ile ambayo tulikuwa na mjadala kwa barua pepe. Nina hakika nikiuliza kwa watu wa lugha nyingine, kwa mfano labda Kijapani, Kihindi na Kihispania, nitapata majibu yasiyoshabihiana.  Somo kwenye zoezi hilo ni kuwa tamaduni huwa zina hulka ya kuakisi jamii na mazingira yao. Ilikuwa dhahiri alichokuwa anakifanya mtetezi wa Kiswahili kwenye ule mjadala si kuwa analazimisha tafsiri, bali ni kwamba alikuwa anaenzi utamaduni kulingana na mazingira yake. Hoja iliyotumiwa kule ni ya mara kwa mara kwenye mijadala ya matumizi na maendeleo ya lugha ya Kiswahili. Kuna watu wanaamini hadi leo kuwa Kiswahili hakifai kufundishia, mimi binafsi naona hiyo dhana ni sawa na kuishi zile zama za nadharia ya kuwa dunia ni bapa. Nadharia hiyo ilitokea Ulaya, zama ambazo maeneo mengine ya dunia tayari walikuwa wanafahamu mizunguko ya mfumo jua na elimu za hali ya juu za kinajimu.  Kuchukua jukumu
  Wakati nasema ‘machata’ kwenye wimbo yangu 2003, wala sikuwaza kama naongea neno tofauti; ni sababu tu kuwa ndio neno tunalotumia kuwasilisha ile taswira. Sidhani kama kuna ulazima wa kuwapelekea BAKITA ama kutaka idhini kwao. Ila wanachofanya wanaharakati wa Kiswahili wa zama hizi labda ni namna yao ya kurasimisha, ambayo nadhani inafaa kuheshimiwa.  Kuna wageni wengi tu wanakuja na kufanya mambo mengi kuhusu utamaduni wetu na hakuna vitu tunavyovifanya sisi wenyewe kuhifadhi na kuenzi. Sasa, hii kwangu nadhani ni hatua nzuri na wengine waje waanze kuandika kamusi, na wala wasiogope mamlaka maana lugha ni mali na urithi wa jami iitumiayo.
  Kiingereza kinatumika kwa namna tofauti sehemu mbalimbali duniani, ukienda Sierra Lionne, Ghana, Naijeria na ukienda Jamaika utaona namna wanavyokitumia. Wale hawabuni maneno kama ‘dunza’, yaani pesa, bali mazingira yao kama Waafrika wakitumia maneno ya kigeni kuwasilisha fikra za Kiafrika.  Kuwasilisha fikra
  Matumizi ya maneno ya lugha ya kikoloni kuelezea mawazo ya Kiafrika si jambo geni. Hilo jambo liko hivyo maeneo mengi sana. Nilidokezwa na watu kadhaa toka Jamaika, hususan Baba T, kwamba hata wazazi Jamaika walikuwa wakiwachapa watoto wao wanapoongea Kipatwa. Hiyo ndio nguvu ya udhalimu wa ukoloni.
  Marekani hali kadhalika kuna lahaja iitwayo Ebonic, ambayo ni matumizi ya maneno ya Kiingereza kuwasilisha fikra ya Mwafrika. Nayo ina utata mwingi katika ya jamii ile. Kuna wazazi wa jamii zilizo na unafuu (kiuchumi) zinazokemea sana uongeaji wa namna ile.
  Mijadala yetu mara nyingi inapoteza dira na kuruhusu jazba kubwa kuliko kuangaliwa kwa mada na maudhui ya ndani yake. Kwa mfano, kuna dhana kwamba kwa vile Hip Hop imeanzia Bronx hivyo inabidi iangaliwe kama kule wao ndio wamiliki. Sikubaliani na dhana hii ambayo inaashiria kwamba kama utamaduni basi ubakie hivyo hivyo milele, kuna maudhui mengi yanabadilika kukidhi jamii inayokutana nayo.  Harakati za Hip Hop Afrika

  Kama Kool Herc angeamua kupiga tu zile Dub za Studio One alizopiga mzee wake bila kuchanganya Soul na Jazz ya Marekani, basi labda tusingekuwa na Hip Hop. Hivyo tufanyacho hapa Bongo, ni kuwa tumeshukuru Hip Hop kufika Afrika, tumeipokea na kuijenga kwa namna yetu na tunasonga bila kuharibu misingi.
  [​IMG]
  Kuna vuguvugu kubwa la kisiasa Afrika. Tuanzie na Sugu kuingia mjengoni. Wengine naona mnachukulia hili ‘poa tu’. Yaani, sio kesi wala nini? Lakini ukweli ni kwamba yeye ndio mchenguaji wa kwanza duniani kuingia mjengoni. Hiyo ilikuwa Dar, Bongo. Natumai mmeshasikia kilichotokea kule Dakar Senegal miezi ya awali ya mwaka huu.

  Niendelee ama nisiendelee!?  Je, bado tuko pamoja? Vipi wana, mnajua wapiga machata wa Nairobi weshakinukisha? Wana machatta Nairobi sasa hivi wanawatia tumbo joto wanasi-hasa (wanasiasa).
  [​IMG]
  Haya, natumai wasanii wa machatta wa Bongo wana habari ya kinachotokea kwa jirani zetu, kama bado wajulisheni. Tulianzishe Bongo pia.
  Baada ya yote hayo, nashauri tupitie tena hii mijadala yetu mara kwa mara kwa jicho lililo la haki ili tuone kwa namna ipi tunaiendesha. Sitaki kutoa hukumu yoyote bali natoa rai: Tungeweza kuendesha mijadala hii kwa namna bora zaidi ya ile inayotumika hivi sasa. Kwa kuangalia mstari baada ya mwingine inadhihirisha kwa kiasi gani kila mtu amehusika kuufikisha mahala ufikiapo.  Kusonga mbele kwa mbele
  Sishangazwi na hizi changamoto bali ni mambo ya kawaida yanayojirudia, mahala ambako jambo linafanyika ili kutoa fursa adimu changamoto kadhaa hutokea. Nakumbuka dhahiri mashambulizi yaliyojitokeza enzi za WAPI (Jukwaa endelevu la wazi Afrika), badala ya watu kusherehekea kuwepo fursa ya wao kuonesha vipaji vyao na kukutana na wasanii wenzao na wadau mbali mbali wa fani. Hii inanikumbusha ule usemi wa Kiswahili kwamba, hata umwage mpunga kiasi gani kuku bado watapekuwa tu kwa udadisi wa kwamba ‘hapa hivi, je huko chini kukoje’.
  Watu waliotarajiwa kuwa wa karibu kabisa wakawa wanatengeneza majungu na uzushi kuhusu vitu kama “hela”; yaani kuna fungu linatolewa na haliwafikii wasanii. Waliokaa Uingereza watanisaidia, mmekaa na wakoloni muda mrefu sana zaidi yangu na mnawajua Waingereza na hulka zao kuhusu fedha. Mtu mwenye akili timamu anaelewa kabisa kuwa mkoloni hawezi kuwa na tamasha la aina ya WAPI, ambalo ni la wazi na bure, halafu awe anatoa fedha kuwapa wale watu aliowaandalia hilo jukwaa.  Nia sio kutoka kwenye maudhui, bali kwa upande wa wanachokifanya waandishi wa TZhiphop na hizi makala za Jicho La Ra, ni kwamba tutarajie kutakuwepo ukosoaji tu. Tungetarajia kuungwa mkono na kubadilishana mawazo ya kujenga zaidi, ila kwa sababu mbalimbali mambo hayatokwenda kwa mujibu wa matarajio yetu.  Ingevutia iwapo ukosoaji ungeshabihiana na uungaji mkono na hilo kwenye mijadala yetu huwa halipewi nafasi yoyote. Tusonge mbele kwa vile inaonekana kwamba kuna kiu kubwa ya haya madini tunayoshusha. Nakaribisha mjadala zaidi kwa anayetaka, ningependa wa kujenga kuliko mzunguko usioleta matokeo ya manufaa. Hivyo, kwa vile Kiswahili chetu, ka’ namna gani vipi tujiachie nacho tu mwanzo mwisho.  Pamoja


  Zavara Mponjika


  @Rhymson

  Art coordinator, emcee, beat maker, Afrikologist, filmmaker, videographer, animator, visiting scholar at Yale University, Hip Hop activist.


   
Loading...