Jeshi lidumishe heshima yake kwa wananchi

Pdidy

JF-Expert Member
Nov 22, 2007
50,720
21,779
Habari zaidi!
Jeshi lidumishe heshima yake kwa wananchi
Mhariri
Daily News; Tuesday,September 02, 2008 @00:01



Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), jana liliadhimisha miaka 44 tangu lilipoundwa rasmi kutoka jeshi lililokuwa na mizizi ya kikoloni baada ya uasi wa mwaka 1964.

Tunawapongeza makamanda na askari wote kwa maadhimisho hayo ambayo yaliambatana na tukio la Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Comoro la kukabidhi nishani kwa askari wa JWTZ walioshiriki katika Kikosi cha Umoja wa Afrika (AU), kilichokwenda visiwani humo mwanzoni mwa mwaka huu kumng’oa kiongozi wa waasi wa Anjouan, Kanali Mohamed Bacar.

Kama alivyosema Rais Jakaya Kikwete bungeni takribani wiki mbili zilizopita, sifa ambayo JWTZ ilipata Comoro haikutokana tu na kuongoza vizuri Kikosi cha AU, bali pia kitendo chake cha kuweza kukikomboa kisiwa hicho kwa weledi wa hali ya juu wa kijeshi uliowezesha kutomwagika kwa damu.

Wakati tukipokea nishani kutoka Comoro, huu ni wakati mwafaka wa kurejea namna ambavyo JWTZ ilivyolinda na kutuletea heshima kutokana na namna ilivyodhihirisha umahiri wake katika miaka ya nyuma, ikiwamo kulifyeka Jeshi la Nduli Idd Amin wa Uganda lililokuwa limevamia ardhi yetu mwaka 1978.

Kwa kaulimbiu ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ya ‘Uwezo tunao, sababu tunayo na nia tunayo’ Jeshi letu lilishirikiana vizuri na Waganda wenye uchungu na nchi yao na kuweza kumng’oa madarakani Amin.

Lakini pia askari wetu wanakumbukwa kwa jinsi walivyoshiriki katika operesheni nyingine kadhaa ikiwamo kutoa mafunzo ya kivita kwa wapigania Uhuru wa nchi za Kusini mwa Afrika, kuwasaidia wenzao wa Msumbiji kukabiliana na waasi na kutoa mafunzo kwa wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Katika siku za karibuni askari wa JWTZ wamepata pia uzoefu wa kushiriki katika Majeshi ya Kulinda Amani ya Umoja wa Mataifa katika nchi kama Liberia, Lebanon na sasa jimboni Darfur, Sudan. La muhimu ni jinsi askari wetu wanavyowasaidia Watanzania wenzao wakati wa maafa kama mafuriko, moto na mengineyo.

Hayo yote yamewafanya Watanzania walio wengi wawe na mtazamo wa heshima kwa Jeshi wakiamini kwamba linalotokana na Watanzania wenyewe kwa manufaa ya Watanzania wote. Matarajio yetu ni kwamba Jeshi letu litaendelea kutekeleza majukumu yake kwa uaminifu, utii, uhodari, ushupavu na heshima kwa wananchi.
 
Back
Top Bottom