Jeshi la Polisi Tanzania Lifanyiwa Marekebisho Makubwa sana Yakimfumo

Mwanahabari Huru

JF-Expert Member
Mar 9, 2015
14,243
34,903
Na Malisa Godlisten

Historia ya Jeshi la Polisi duniani ilianzia nchini China zaidi ya miaka 2000 iliyopita. Himaya mbili za Chu na Jin (Chu and Jin kingdoms) ndizo zilizoasisi mfumo unaotumika duniani leo wa kuwa na watu maalumu wakusimamia na kufanya uchunguzi wa mambo mbalimbali ya kihalifu (Law enforcement and handling investigations). Watu hao waliitwa Polisi.

Baadae nchi nyingine zikaiga kutoka Uchina na hatimaye duniani kote Polisi ikawa taasisi rasmi inayotambulika.

Kabla ya kuja kwa wakoloni Jamii za kiafrika hazikuwa na mfumo rasmi wa Jeshi la Polisi. Zilikua na askari wake wa Ulinzi waliohusika na kulinda mipaka pamoja na kusimamia sheria.

Mfumo rasmi wa kipolisi uliletwa na wakoloni. Ujio wa wakoloni ulitofautisha Askari wa Kulinda mipaka (wanajeshi), Askari kusimamia utekelezaji wa Sheria (Polisi) na askari wa kusimamia wafungwa (Magereza).

Taasisi ya Polisi ilipoanzishwa na wakoloni huku Afrika ilianzishwa kama Jeshi (force) lengo likiwa ni kulinda maslahi ya wakoloni dhidi ya watu weusi. Na hapa ndipo Polisi ilipopewa hadhi ya Jeshi ili waweze kutumia silaha katika kutekeleza na kusimania sheria.

Polisi wakawa wanapiga raia, wanatoa amri, wanatii maagizo ya wakoloni, wanatumikisha raia, na mambo mengine yenye maslahi kwa wakoloni.

Ajabu ni kuwa askari waliotumika ni weusi lakini waliwapiga na kuwanyanyasa weusi wenzao kwa maslahi ya wakoloni (weupe).

Baada ya Uhuru Tanzania ilirithi sheria nyingi za kikoloni ikiwemo Sheria ya uanzishaji wa Jeshi la Polisi ya mwaka 1939 [THE POLICE FORCE AND AUXILIARY SERVICES ACT OF 1939) PRINCIPAL LEGISLATION].

Sheria hii ndiyo inatumika hadi sasa japo imekua ikifanyiwa marekebisho ya mara kwa mara. Kwahiyo Sheria iliyoanzizha Jeshi la Polisi Tanzania ni sheria ya kikoloni, iliyoanzishwa na wakoloni kwa maslahi ya wakoloni.

Leo sheria hii inatumika katika Tanzania huru. Je inakidhi haja? Maslahi ya mkoloni ni tofauti na maslahi ya Tanzania huru. Kazi za Polisi wakati wa ukoloni zinapaswa ziwe tofauti na kazi za Polisi katika Tanzania huru.

Lakini sivyo ilivyo. Utendaji kazi wa Polisi wakati wa ukoloni na utendaji kazi wa Polisi kwenye Tanzania huru unaonekana kufanana kwa kiasi kikubwa licha ya kwamba wakoloni wameshaondoka miaka mingi iliyopita lakini bado Polisi wako vilevile.

Wanapiga, wanaua, wanajeruhi kwa maagizo ya watawala kama ilivyokuwa kipindi cha ukoloni. Jeshi la Polisi katika Tanzania huru limeshutumiwa kuua raia wasio na hatia, kujeruhi na kufanya vitendo vya kikatili kwa raia.

Mwaka 1999 Jeshi la Polosi mkoani Mbeya lilituhumiwa kumuua kijana Michael Skupya aliyekua mwanafunzi wa kidato cha tatu shule ya sekondari ya ufundi Iyunga. Polisi wanadaiwa kumpiga Michael kwa kudaiwa kuwa muasisi wa mgomo wa wanafunzi shuleni hapo ambapo walimjeruhi sehemu za kichwani hali iliyosabanisha damu kuvilia kwenye ubongo na kufariki.

Polisi pia wametuhumiwa kushiri mauaji ya wafanyabiashara wasio na hatia kutoka mkoani Morogoro mwaka 2006.

Tume ya Jaji Kipenka iliyoundwa kuchunguza mauaji hayo ilitoa ripoti kuwa vijana wale hawakua majambazi kama ilivyodaiwa awali na Jeshi la Polisi. Taarifa hiyo iliongeza pia kuwa lengo la Polisi kuua vijana hao watatu wa familia moja ni ili kuwapora fedha walizokuwa nazo (zaidi ya shilingi milioni 200) na madini aina mbalimbali.

Ilidaiwa kuwa Askari wa Jeshi la Polisi waliwafunga vijana hao vitambaa vyeusi usoni na kuwapiga risasi za kisogo, na kuwapora pesa na mali walizokua nazo kisha wakaeleza vyombo vya habari kuwa wameua majambazi waliojaribu kurushiana nao risasi.

Huu ulikua ukatili wa kiwango kikubwa sana. Kuua watu wasio na hatia kisha kuwapakazia ujambazi ni jambo linalotia hasira sana. Katika mazingira haya tunawezaje kulitofautisha Jeshi la Polisi la sasa na lile la kikoloni?

Matukio haya ya kikatili ya Jeshi la Polisi bado yanaendelea hata sasa. Baadhi ya wanasiasa waliowahi kukumbana na kipigo kutoka Jeshi la Polisi ni pamoja na Profesa Ibrahim Lipumba, Dr.Wilbroad Slaa na Mbunge wa Kilombero Mhe.Peter Lijualikali. Jumamosi ya tarehe 5 halmashauri ya Kilombero na Mhe.Lijualikali alifika katika mkutano huo na kuanza kupigwa mara baada tu ya kushuka.

Nikajiuliza hivi Polisi hawana njia nyingine ya kumkamata mtuhumiwa zaidi ya kumpiga? Hivi wangemwambia Lijualikali waongozane hadi kituo cha Polisi angekataa?

Sheria inataka Polisi kutumia nguvu ya kiasi (reasonable force) na itumike pale inapobidi (where neccessary). Lakini siku hizi ni tofauti.

Polisi anatumia nguvu pale anapojisikia sio pale inapobidi. Na anatumia nguvu kubwa kupita kiasi. Huu ni ubane ambao hata Polisi wa kikoloni hawakuwahi kufanya.

NINI KIFANYIKE?
Jeshi la Polisi linahitaji marekebisho makubwa ya kimfumo kwa sasa ili liendane na wakati. Bado linafanya kazi kwa kasumba ya kikoloni.

Kwanza Sheria inayounda Jeshi la Polisi ifutwe maana ni ya kikoloni na ilitungwa na wakoloni kwa maslahi ya wakoloni. Sheria hiyo ikifutwa na jeshi la polisi nalo linakuwa limefutika "automatically"

Baada ya Jeshi la Polisi kufutika inatungwa Sheria nyingine itakayounda chombo kingine kitakachofanya kazi za Polisi, au polisi wanarudishwa lakini katika mfumo mwingine tofauti na huu wa kijeshi.

POLISI NI HUDUMA SI JESHI.
Kimsingi Polisi inapaswa kuwa huduma sawa na huduma nyingine za kijamii kama maji, elimu, hospitali na usafirishaji. Raia anapaswa kujihisi salama zaidi akiwa Polisi, lakini hali ilivyo kwa sasa ni tofauti. Raia anajihisi kupoteza usalama zaidi akiwa mikononi mwa polisi.

Ndio maana leo mtu akiambiwa anatafutwa na Polisi anapoteza amani hata kama anajijua hajafanya kosa. Hii ni kwa sababu kwa hali ilivyo sasa, Polisi wanaaminika kuwa wanaweza kukubambikizia kosa lolote.

Lakini hali haipaswi kuwa hivi. Polisi wanapaswa kuwa sehemu ya wanyonge kukimbilia sio sehemu ya kukimbiwa na wanyonge.

Kama ambavyo umeme ukikatika mtu hupiga simu Tanesco muda wowote kudai huduma hiyo, ndivyo hivyo inapaswa kuwa kwa jeshi la Polisi. Kwamba raia akijihisi kutokuwa salama ana uwezo wa kuwaeleza Polisi muda wowote na akapewa msaada. Kimsingi Polisi inapaswa kuwa huduma sio jeshi.

Nimetembelea Zambia mara kadhaa, nilipofika Makao makuu ya polisi niliona bango kubwa limeandikwa “Zamba Police Service, Headquaters.” Yani Makao Makuu ya Huduma ya Polisi Zambia.

Nilipouliza kwa wenyeji wakasema Polisi ni huduma kama zilivyo huduma nyingine za kijamii kama maji, afya au elimu.

Siku moja usiku mwenzetu mmoja alitoka Hotelini tulikoshukia akaelekea klabu ya usiku. Wakati wa kurudi akasahau jina njia ya hotelini. Akakamatwa na polisi waliokuwa doria. Akajitetea kuwa yeye ni Mtanzania. Akaagizwa kutoa pasi ya kusafiria lakini hakuwa nayo, kwa sababu aliicha hotelini.

Akataja jina la hoteli. Polisi wakaja nae hotelini akawapatia pasi yake ya kusafiri. Wakamwachia. Kufikia hapo hapakuwa na shaka kuwa Polisi Zambia ni huduma.

Nikajaribu kuvuta taswira ingekuwa Tanzania. Unakamatwa wewe ni raia wa kigeni na huna pasi ya kusafiria. Labda utapelekwa kituoni baada ya kipigo kikali na hakutakuwa na muda wa kusikiliza porojo za kusahau pasi hotelini.

Polisi wa Tanzania hawasikilizi. Wangekuwa wanasikiliza wasingemuua Mwandishi Daudi Mwangosi maana walioshuhudia tukio hilo wanasema Mwangosi alipokuwa wakipigwa na Polisi aliomba wasimuue lakini hawakumsikiliza.

Polisi wetu wanachojua ni kulazimisha utii wa sheria bila shuruti. Lakini hata unapotii sheria bila shuruti bado hujiweki kwenye nafasi salama bali nafasi ya hatari zaidi.

Mwaka 1996 aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Usalama wa taifa Jenerali Imrani Kombe aliuawa na Jeshi la Polisi licha ya kutii sheria bila shuruti pale alipotakiwa kusimamisha gari na kushuka. Kwa mujibu wa mke wa marehemu ambaye alikuwa shahidi namba moja wa kesi hiyo iliyokuwa ikisikilizwa Mahakama Kuu kanda ya Kilimanjaro Jenerali Kombe alisimamisha gari, akashuka chini na kupiga magoti kisha akanyoosha mikono juu lakini bado Polisi walimpiga risasi na kumuua.

Kwa mfumo ulivyo sasa ukiambiwa tii sheria bila shuruti sio kwamba unajihakikishia usalama. Ukitii unajiweka kwenye hatari na usipotii unajiweka kwenye hatari pia.

Ripoti ya Jumuiya ya Madola juu ya Uwajibikaji wa Jeshi la Polisi Tanzania ya mwaka 2006 (Police Accountability in Tanzania, 2006) inapendekeza jeshi la Polisi kufanyiwa marekebisho. Marekebisho hayo yanaweza kuwa ya kimfumo au ya kiutendaji.

Ni aibu kwamba nchi za kikoloni zilizotuletea Mfumo wa Polisi kutumika kama Jeshi zimeshaacha mfumo huo na sasa zinatumia Polisi kama huduma.

Nchini Uingereza, Uswisi na Norway Polisi haruhusiwi kushika silaha yoyote labda kuwe na tukio maalumu. Yani Polisi wakiwa katika shughuli zao za kawaida au doria hawaruhusiwi kutembea na silaha unless wanapokua kwenye shuguli maalumu kama kulinda maandamano, kupambana na majambazi ndipo wanakuwa na silaha.

Lakini hapa kwetu ni tofauti. Polisi anatembea na silaha muda wote hata kama hana shughuli inayomtaka kufanya hivyo. Tunahitaji kubadili mfumo wetu la Polisi kuwa huduma badala ya Jeshi.

Malisa GJ.!
 
Back
Top Bottom