Jeshi la Polisi: Tanzania ipo salama dhidi ya vitendo vya ugaidi

beth

JF-Expert Member
Aug 19, 2012
3,877
6,326
1578555134726.png

Jeshi la Polisi nchini limewahakikishia raia wa kigeni wakiwemo watalii, kuwa nchi ipo salama dhidi ya vitendo vya kigaidi; na linaendelea kuimarisha ulinzi katika maeneo yote ya nchi.

Kauli hiyo imetolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, David Misime. Alisema hayo wakati akizungumzia hali ya usalama nchini, kwa kipindi hiki ambacho kumeibuka sintofahamu kati ya taifa la Marekani dhidi ya nchi za Iran na Iraq.

Pia, kuwepo kwa taharuki kuhusu usalama wa raia wa Marekani na washirika wake duniani kote, hasa baada ya kutokea shambulio la kigaidi mjini Lamu, Kenya na kusababisha askari watatu na magaidi wanne kuuwawa.

Mtafaruku huo umesababishwa na hatua ya Jeshi la Marekani, kumuua aliyekuwa Kiongozi wa Jeshi la Ulinzi wa Iran Nje ya nchi, Jenerali Qasem Soleiman wakati akiwa nchini Iraki katika ziara ya kikazi.

Kutokana na hatua hiyo, vikundi mbalimbali vya kigaidi wakati wa maziko ya Jenerali Soleiman juzi, vilisisitizia msimamo wa kulipiza kisasi kwa Marekani.

Tayari kikundi cha kigaidi cha Al Shabaab cha Somalia, chenyewe kimeshambulia karibu na Kambi ya Kijeshi ya Simba iliyopo Lamu Kenya, kambi inayotumiwa na nchi za Kenya na Marekani.

Pia jana nchini Iraq kambi mbili za Marekani, zililipuliwa kwa makombora 13 kutoka Iran na inadaiwa watu 80 wamekufa. Washirika hao wa Marekani wa karibu ni nchi za Israel, Uingereza, Ufaransa, Canada, Italia na nyinginezo za Ulaya.
Raia wa nchi hizo wamekuwa wakitembelea mataifa mbalimbali duniani na Bara Afrika, ikiwemo Tanzania, kwa shughuli za utalii au miradi ya maendeleo.

Misime aliwataka wageni hao, kutambua kuwa wapo salama, na aliwataka waendelee na shughuli za kila siku za maendeleo zilizowaleta. Aliwataka watalii kuendelea kutalii na wengine kuendelea kuja nchini kama kawaida.

Alisema “Jeshi la Polisi lipo timamu na litaendelea kuimarisha ulinzi wa wananchi wake na wasiokuwa raia pia, watalii waendelee kuwa na amani na jeshi litakabiliana na kila anayetaka kuhatarisha usalama”.

Kauli hiyo ya Misime imekuja siku chache, baada ya Ubalozi wa Marekani nchini kutoa taarifa ya kuwataka raia wake, kuongeza umakini katika kuhakikisha ulinzi wa usalama wao kutokana na vitisho hivyo, vilivyotolewa na magaidi. Ubalozi huo uliwataka raia wake, kutembelea tovuti ya ubalozi huo kila wakati, ili kupata taarifa za mara kwa mara kuhusu hali ya usalama.

Kamanda wa Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alibainisha kuwa askari wake, wapo kila kona ya mkoa huo, hasa kwenye maeneo ambayo yanatembelewa kwa wingi na mara kwa mara na raia wa nje, hasa wa kutoka Bara la Ulaya.

Chanzo: Habari Leo
 
Nchi ipo salama kabisa,ila kuna wachawi wa Afrika huubiri uongo wa kiwango cha flying over katika mataifa yao dhidi ya Tanzania.
 
Kama Jiwe mwenyewe anahisi hayuko salama mpaka anaagiza helicopter za kumlinda nani yuko salama
 
Back
Top Bottom