Jeshi la Polisi sasa linaipeleka nchi pabaya | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Jeshi la Polisi sasa linaipeleka nchi pabaya

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Don Alaba, Jan 6, 2011.

 1. Don Alaba

  Don Alaba Senior Member

  #1
  Jan 6, 2011
  Joined: Nov 3, 2010
  Messages: 158
  Likes Received: 2
  Trophy Points: 35
  Jeshi la Polisi sasa linaipeleka nchi pabaya Send to a friend Wednesday, 05 January 2011 20:37 0diggsdigg

  [​IMG]Kwa mara nyingine katika kipindi cha wiki moja, polisi wamefanya vitendo vya kinyama na kihuni, zamu hii wamewashambulia na kuwajeruhi kwa silaha za kivita wafuasi wa Chadema waliokuwa wanaandamana kwa amani kuelekea katika Viwanja vya Unga Limited, mjini Arusha kwa ajili ya mkutano wa hadhara ambao viongozi wa juu wa chama hicho walikuwa wahutubie.

  Maandamano hayo, ambayo yalikuwa yahitimishwe na mkutano mkubwa wa hadhara, ajenda yake kuu ilikuwa ni kupinga hatua ya serikali kuvunja sheria kwa makusudi na kukipa ushindi CCM kinyume cha sheria katika uchaguzi wa umeya uliofanyika hivi karibuni. Chadema pia ilikuwa itumie mkutano huo kutoa msimamo wake kuhusu madai yake ya katiba mpya yaliyoanzishwa na chama hicho kabla na baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu uliofanyika miezi miwili iliyopita.

  Itakumbukwa kwamba Alhamisi iliyopita, polisi waliwashambulia kwa mabomu ya machozi, risasi za moto, virungu na maji ya kuwasha wafuasi wa Cuf waliokuwa wanaandamana kwa amani kuwasilisha rasimu ya katiba mpya kwa Waziri wa Sheria na Katiba, Celina Kombani. Wakati wakifanyiwa unyama huo wa kutisha na polisi, waandamanaji hao wa Cuf waliendelea kuwa watulivu pasipo kujibu mapigo.

  Katika vurugu zilizoanzishwa na polisi jana mjini Arusha kwa kujeruhi vibaya baadhi ya waandamanaji na kuwasweka rumande baadhi ya wabunge, akiwamo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe wananchi katika Jiji la Arusha walipata hofu kubwa, huku wakikimbia hovyo bila kujua la kufanya kutokana na polisi kuonekana kudhamiria kuwakomoa waandamanaji.

  Polisi hao walitumia nguvu kubwa kupita kiasi na hawakutilia maanani ukweli kwamba licha ya waandamanaji hao kutokuwa na silaha yoyote, pia walikuwa katika hali ya utulivu mkubwa. Kinyume na kauli ya Inspekta Jenerali wa Polisi, Said Mwema aliyedai juzi kuwa jeshi lake lilikuwa na taarifa za intelijensia zilizodai kwamba iwapo maandamano ya Chadema yangeruhusiwa waandamanaji wangefanya vurugu, badala yake ni polisi ambao walianzisha vurugu kwa kumwaga damu ya watu wasiokuwa na hatia.

  Ni jambo la kushangaza kwamba ingawa awali maandamano hayo yalikuwa yameruhusiwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Thobias Andengenye ambaye alisema alitoa kibali hicho baada ya Chadema kufuata taratibu zote zilizotakiwa, kitendo cha IGP Mwema kujitokeza ghafla na kupiga marufuku maandamano hayo katika dakika za lala salama kinatia shaka na kuibua hisia kwamba pengine alifanya hivyo kwa amri na shinikizo la chama tawala. Vinginevyo, haiingii akilini kuona mkuu wa jeshi hilo kitaifa akiingilia taratibu zilizo ndani ya mamlaka ya kamanda wa polisi wa mkoa bila sababu za msingi.

  Tumekuwa tukilikumbusha jeshi la polisi mara kwa mara kupitia safu hii kwamba jeshi hilo halina mamlaka kisheria kutoa ruhusa kwa vyama vya siasa kufanya kazi za siasa kwa njia zozote zile, zikiwamo maandamano au mikutano ya hadhara. Sheria ya Vyama vya Siasa ya Mwaka 1992 inaeleza bayana kwamba vyama hivyo vikitaka kufanya shughuli hizo vinalijulisha tu rasmi jeshi hilo ndani ya saa 48 ili liweze kuwapa ulinzi. Tulisema kuwa kitendo cha jeshi hilo kujipachika mamlaka ya kutoa vibali kwa vyama hivyo ni kuvunja sheria.

  Tunarudia kusema leo kwamba ukatili wa kutisha unaofanywa na polisi dhidi ya wananchi wanaotimiza haki zao za kidemokrasia kwa amani utaipeleka nchi yetu pabaya. Polisi waache ubaguzi katika kuhudumia vyama vya siasa, kwani kama sheria hiyo ya vyama vya siasa inavyosema, vyama vyote viko sawa mbele ya sheria.

  Tunawashauri wahanga wote wa vitendo viovu na ukatili wa polisi unaoendelea kwa kasi nchini kwamba sasa waanze kufikiria hatua za kisheria za kukomesha vitendo hivyo, hata ikibidi kulishtaki jeshi hilo katika Mahakama ya Kimataifa iliyoko The Hague, nchini Uholanzi.
   
Loading...