Jeshi la Polisi Njombe limepiga marufuku wananchi kuandamana kupinga mauaji

The Watchman

JF-Expert Member
Nov 7, 2023
1,161
2,017
Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe limepiga marufuku wananchi kuandamana baada ya uwepo wa taarifa ya kuhamasisha maandamano inayotajwa kutolewa na Mwenezi wa Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA) taifa, Sigrada Mligo wakati wa mazishi ya Atugafile Mtulo (90) aliyepoteza maisha baada ya kupigwa na watu wasiojulikana.

Akitoa taarifa ya kifo cha bibi huyo mkazi wa kijiji cha Igima Halmashauri ya Wilaya ya Wanging'ombe, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe Mahamoud Banga amesema kifo cha Atugafile kilitokea Machi 2, 2025 nyumbani kwake wakati akiendelea kuuguzwa na watoto wake baada ya kutoka Hospitali ya Wilaya ya Wanging'ombe alikokuwa akipatiwa matibabu ya majeraha yaliyotokana na kupigwa na watu nyumbani kwake.

"Bibi Atugafile alifikishwa kituo cha Polisi Igwachanya tarehe 15 Februari na baadaye katika Hospitali ya Wilaya ya Wanging'ombe ambako alipatiwa matibabu aliyokuwa nayo usoni huku akiwa hawezi kuzungumza jambo lolote.

Tangu tarehe 20 mwezi huo aliendelea kupata matibabu akiwa nyumbani akiuguzwa na wanawe hadi ilipofika tarehe mbili Machi alipopoteza maisha", amesema Banga.

Amesema Machi 3 wakati wa mazishi yake kulitokea sintofahamu baada ya wanasiasa kuingilia kati na kulitaka jeshi la Polisi kutoa taarifa mpaka ifikapo Machi 17 la sivyo wataandamana.

"Niwaombe wananchi tuyapuuze maagizo hayo ya wanasiasa ambao wanasema wataandamana lakini vile vile tuutahadharishe umma, maandamano ya aina yoyote yapo kwa mujibu wa sheria na kukiuka kwa kufanya maandamano hayo tutawachukulia sheria wote watakaoandamana, jeshi la polisi tunaendelea na uchunguzi na wale wote waliohusika na tukio hili watakapobainika watakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria", amesema Banga.

Wakati wa mazishi ya Bibi Atugafile, Mwenezi wa BAWACHA Taifa Sigrada Mligo katika hotuba yake alinukuliwa akiwataka wananchi wa Igima bila kujali itikadi za vyama vyao kuungana na kwenda Kituo cha Polisi Wanging'ombe kujua hatima ya vifo vinavyotokana na mauaji hususani kwenye maeneo yao.

"Tarehe 17 bila kujali itikadi zetu tutaenda Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Wanging'ombe kuuliza hatima ya misiba hii kuwa upelelezi umefikia wapi, hakuna wa kuwapiga mabomu wala kuwazuia, ni haki yako ya kikatiba na majibu yao ndio yatakayofanya tuandamane au tusiandamane", alisema Sigrada.

Chanzo: Jambo TV
 
Back
Top Bottom