Matukio Jamii
Member
- Sep 9, 2015
- 12
- 8
Jeshi la Polisi mkoani Morogoro linawashikilia watu 21 wakiwemo wenyeviti wa vijiji vya Mkindo, Dihombo na Kambala wilayani Mvomero, kwa tuhuma za kuwakata mifugo wa mfugaji mmoja wa jamii ya Kimasai, na mmoja kati yao ambaye ni mfugaji akituhumiwa kulisha mifugo kwenye shamba la mkulima na kujeruhi.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu chanzo cha kikundi hicho cha wakulima kuvamia na kukata kata mifugo, kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro Leonard Paulo, amesema awali mnamo Februari 7 mwaka huu, kundi la Ng’ombe zaidi ya 50 likiwa na wachungaji watatu wa jamii ya kimasai, waliingia kwenye shamba la mpunga la hekari moja la Rajab Issa, mkazi wa Dihombo, ambapo mmiliki wake aliwazuia Ng’ombe hao, lakini walijitokeza vijana wanaosadikiwa kuwa morani wa kimasai na kuwachukua ng’ombe hao kwa nguvu, jambo lililofanya mmiliki wa shamba hilo kuripoti tukio hilo polisi.
Kamanda Paul amesema wakati tukio hilo likishughulikiwa na polisi, kikundi cha kijadi cha wakulima maarufu kama mwano kilivamia nyumbani kwa mfugaji wa kimasai, Bi Nuru Keteboi, akiwa nyumbani huku mifugo yake aina ya mbuzi, kondoo na ndama wakiwa malishoni, na kumpokonya simu ya mkononi asiweze kuomba msaada, badala yake wakaipeleka mifugo hiyo porini na kuwakata kata kwa vitu vyenye ncha kali na kusababisha baadhi yake kufa na wengine kujeruhiwa, na polisi wamewatia mbaroni watu 21 wakiwemo 20 waliohusika na tukio hilo, na mfugaji Kashu Moreto ambaye ni mwenyekiti wa kijiji cha Kambala kwa tuhuma za kumjeruhi Ramadhani Juma, huku ikiwasaka wengine zaidi kuhusiana na tukio hilo.
Wenyeviti wengine waliokamatwa ni wa kijiji cha Mkindo Patrick Longomiza na mwenyekiti wa kijiji cha Dihombo, Christian Thomas wakituhumiwa kwenye tukio la kukatwa katwa mifugo.
Amewaonya wananchi kuacha kujichukulia sheria mikononi, hususani vijana akiwaonya kuacha kukubali kutumika kushiriki vurugu au kufanya matukio ya kiuhalifu, huku akibainisha mgogoro wote unachangiwa na tatizo la umiliki wa bonde la mgongola ambalo kesi yake bado inashughulikiwa na mahakama.
Awali kwenye mkutano na waziri wa kilimo, mifugo na uvuvi Mwigulu Nchemba aliyetembelea kijijini hapo, mtuhumiwa kashu ambaye ni mwenyekiti wa kijiji cha Kambala, ambaye wananchi walisema hakamatiki kirahisi, alidai serikali ilishawazuia makundi ya wakulima na wafugaji kutumia vikundi vya kijadi inapotokea mgogoro wowote lakini wanashangazwa wakulima kuendelea kutumia vikundi hivyo.
Kwa hisani ya Radio one