Jeshi la Polisi lamshikilia mmoja kwa kujifanya Daktari na kutibu wananchi

beth

JF-Expert Member
Aug 19, 2012
3,877
6,326
1578640411395.png

Mkazi wa Panyakoo mkoani Mara, Ismail Onyango (42), anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji kwa tuhuma za kujifanya daktari na kutoa tiba kwa wananchi bila kuwa na taaluma hiyo.

Onyango anadaiwa kuelekeza tiba zake wanawake ambao aliokuwa akiwatoa mimba nyumbani kwa mtu katika Kata ya Ngarambe, Rufiji mkoani Pwani.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Rufiji, Juma Njwayo, akizungumzia tukio hilo, alisema jana kuwa alipewa taarifa na raia wema juu ya kuwapo kwa daktari feki.

"Tulipata taarifa kutoka kwa raia wema, yupo mtu anadai ni daktari, amefikia Kijiji cha Ngarambe, Kata ya Ngarambe na kutoa huduma za tiba, lakini cha kushangaza zaidi anatibu wanawake tu. Baada ya taarifa hizo, tuliagiza ofisi ya Kata Ngarambe ifuatilie na kutoa taarifa," alidai.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Rufiji alidai walibaini uwapo wa jambo hilo na kupiga simu kwa Mganga Mkuu wa Wilaya ambaye alitoa wataalamu wake, wakiwamo wa maabara, Hamis Bungala na Said Muba na Ofisa Afya wa Wilaya, Ali Rashid, ambao walishirikiana na Mganga wa Zahanati ya Kijiji cha Ngarambe kufuatilia na kufanikiwa kumpata akiwa nyumba ya mtu ambaye bado anatafutwa.

Alidai kuwa Onyango alikutwa na vifaa mbalimbali vya hospitali, ikiwamo mikasi, mabomba ya sindano, kipimo cha ugonjwa wa kisukari, hadubini na pamba na kwamba alipohojiwa, hakuwa na cheti chochote cha taaluma ya daktari, uuguzi wala utabibu.

"Alihojiwa aonyeshe vyeti vyake vya taaluma hakuwa navyo na uchunguzi umebaini alikuwa akitoa pia huduma za utoaji mimba na wateja wake wengi aliwalenga wanawake," alidai.

Njwayo alidai Jeshi la Polisi linaendelea kuchunguza watu aliokuwa akishirikiana nao kufanya biashara hiyo baada ya kubaini kuna watu nyuma yake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rufiji, Onesmo Lyanga, akizungumza na Nipashe, alithibitisha kukamatwa kwa mtu huyo, ingawa alidai suala hilo bado halijamfikia ofisini.

"Nipo nje ya ofisi, pengine linazunguka zunguka, likinifikia, nitalizungumzia. Kwa sasa sijalipata," alidai.
 
Back
Top Bottom