Jenerali Ulimwengu na Barua ndefu ya wazi kwa Jakaya

Shadow

JF-Expert Member
May 19, 2008
2,892
2,000
Rai ya Jenerali


jenerali2.jpg
Barua ndefu ya wazi kwa Jakaya

lC.gif
Jenerali Ulimwengu​
Novemba 17, 2010
rC.jpg


Mpendwa Jakaya,
NAFAHAMU vyema kwamba unaijua vyema nchi uliyoirithi na dola uliyokabidhiwa. Hata hivyo halitakuwa jambo baya iwapo nitayakariri baadhi ya masuala makuu ambayo nadhani wewe na sisi raia zako tutakabiliana nayo katika kipindi cha miaka hii mitano ya uongozi wako.
Naamini kwamba hatuna budi kuwa na mjadala wa kudumu kuhusu masuala ya kitaifa, hata kama tayari tunayajua. Binadamu hachelewi kusahau, na hata asiposahau, hakosi kuyazoea mambo yaliyomzunguka na kuyaona kama ya kawaida na yasiyostahili tafakuri ya kina ya kila siku.
Kwanza umerithi nchi yenye “amani na utulivu”. Hii ni kweli, hasa tukizingatia kwamba tunaishi ndani ya Bara lenye misukosuko mingi na ya kila mara. Tumewashuhudia majirani zetu kadhaa wakikumbwa na milipuko isiyoisha na iliyoambatana na vita, ghasia na umwagaji mkubwa wa damu.
Hayo, Mwenyezi Mungu ametunusuru, na hatuna budi kushukuru kwa hilo, na kutafuta kila njia ya kuiendeleza hali hii tuliyo nayo, na hata kuiboresha.
Lakini pia umerithi nchi yenye kila aina ya neema inayotokana na maliasili ya kila aina—ardhi nzuri yenye rutuba, maji ya kutosha, misitu, madini na kadhalika.
Ni maliasili ambayo nchi nyingi barani Afrika zingefarijika kama zingekuwa nayo, lakini hazina. Ni maliasili maridhawa, ambayo ikifanyiwa kazi inaweza ikawa ni chanzo cha utajiri mkubwa.
Kubwa zaidi ni kwamba umerithi pia raia wema, walio wengi, watu waungwana na wasikivu kwa viongozi wao, alimradi viongozi wawatendee mema. Na hata viongozi wanaposhindwa kuwatendea mema raia zako bado ni wavumilivu, ni wenye kuvuta subira. Silika ya Watanzania si kuhamaki mara moja wanapohisi watawala wao hawawatendei mema.
Ziko nchi, na unazijua, ambazo raia zake hawachelewi kuingia mitaani kwa maandamano ya rabsha mara tu wanapobaini kwamba watawala wao wanafanya mambo siyo. Hapa kwetu ni nadra hilo kutokea.
Kwako wewe binafsi umekabidhiwa nchi iliyojaa raia wanaokupenda sana, kama ninavyoeleza mwanzoni mwa waraka huu. Unayo karama ya kipekee ambayo wanasiasa wengi huitafuta kwa udi na uvumba, hata kwenda Mlingotini kupiga ramli, lakini wasiipate. Wewe unayo hiyo tunu ya kupendwa na watu wako, na hiyo ni amali kubwa kupindukia kwa kiongozi ye yote wa watu.
Lakini pia umerithi nchi ambayo, pamoja na sifa zote hapo juu, raia zake wamebaki kuwa masikini, na umasikini wao unazidi kuongezeka mwaka hadi mwaka. Maisha ya Mtanzania wa kawaida yamezidi kuwa duni na ameelemewa na madhila ya kila aina—umasikini, ujinga, maradhi, na sasa rushwa.
Hii si hali nzuri hata kidogo. Hali inayochanganya utajiri wa asili kama tulio nao, na watu wema na wasikivu kwa viongozi wao, pamoja na umasikini unaozidi kujichimbia na kuwafanya wakate tamaa, si hali ambayo inaashiria amani ya kudumu.
Hali kama hiyo huzaa mikanganyiko, watu wakachanganyikiwa na wasielewe ni nini hasa kinawafanya waendelee kuwa masikini katika neema iliyowazunguka.
Nadhani ni hayati Bob Marley aliyewahi kuimba, “In the abundance of water, the fool is thirsty.” Katikati ya maji, mpumbavu ana kiu. Hiyo ndiyo hali waliyo nayo Watanzania. Katikati ya neema wao wana njaa, ni wagonjwa, ni wajinga. Lakini upumbavu unaoimbwa na Bob Marley si wa raia. Huu ni upumbavu unaotokana na watawala wao kushindwa kuwaongoza kwa kuwaonyesha maji yalipo na namna ya kuyateka. Kwa hiyo, ingawaje kiu ni ya wananchi, upumbavu (au uzembe) ni wa watawala.
Hili linadhihirika zaidi tunaposhuhudia watawala wale wale wanaoshindwa kuwaongoza wananchi wao kwenye maji, wao wamekwisha kunywa, si tu kukata kiu, bali pia kujimwagia, na kuogelea hadi wengine wanazama, na kuachia maji ya ziada yatiririke kwenye mitaro yasikohitajika, na hata kuoshea mbwa wao, huku wakijua fika kwamba wananchi bado wanakabiliwa na kiu kali. Mbele ya binadamu ni matusi, na mbele ya Mungu ni dhambi ya mauti.
Zipo dalili zisizo shaka kwamba kadri mwananchi wa kawaida anavyozidi kutota katika umasikini ndivyo watawala walafi wanavyozidi kujilimbikizia mali bila woga wala haya. Umeyasema mwenyewe majuzi: Mtu alikuwa hana cho chote kabla ya kupata nafasi eti ya uongozi, lakini mara anapoipata tu anakuwa ni mtu mwingine kabisa kutokana na ukwasi ambao hawezi kuueleza kama matokeo ya ujira halali alioupata kutokana na utumishi wake.
Kwa maneno mengine, watawala wa aina hii ni wezi na wala rushwa. Nilipokuwa mbunge katika miaka ya mwanzo ya 1990, nilipeleka hoja ya mbunge binafsi ikitaka viongozi walazimike kutoa taarifa za mali zao pindi waingiapo madarakani na pia walazimike kuzihuisha taarifa zao mwaka hadi mwaka.
Wapo waliotoa taarifa hizo baada ya hoja kupitishwa na Bunge na kutungiwa sheria, na hata baadhi yao kuzitangaza hadharani, lakini baada ya hapo sijui kama wameendelea kufanya hivyo kila mwaka.
Kilicho dhahiri ni kwamba watu wameendelea kujilimbikizia mali haramu, na inaelekea hakuna wa kuwasaili. Kadri watu kama hawa wanavyozidi kujitajirisha ndivyo matapeli wa kila aina wanavyojiingiza katika kinyang’anyiro cha kutafuta nafasi za “uongozi” ili nao wanufaike. Ndiyo maana tunaona watu wanauza nyumba, mashamba, magari, na kila walicho nacho ili wapate fedha za kununua nafasi ya “kuwatumikia wananchi.”
Kwa kuwa wengi wanahusika na mchezo huu mchafu, na hakuna wa kumsema mwenziwe, ndiyo maana hata rushwa katika uchaguzi imebatizwa jina bandia la “takrima”. Katika upotoshaji wa jumla unaofanyika katika magendo ya siasa, sasa hata lugha yetu ya Kiswahili inapotoshwa, tena inapotoshwa na hao hao wanaodai kuwa “viongozi” wetu.
Iwapo tutaendelea hivi tunavyoenenda tusije tukashangaa tukifika mahali Bunge letu, halmashauri zetu, nafasi zote za uongozi hadi Ikulu, zikashikwa na wanunuzi wa kura. Tukifika hapo tutakuwa tumekwisha, na wala mazungumzo kuhusu “amani na utulivu” hayatakuwa na maana tena.
Nashukuru kwamba umelisemea hili nalo, na umeahidi kwamba utashughulikia suala la matumizi haramu ya fedha katika chaguzi zetu. Wapo wananchi wengi walio tayari kukusaidia katika kuiondosha hatari hii kubwa ambayo huko mbele ya safari ina madhara makubwa. Fedha zinahitajika katika uchaguzi, lakini si kwa matumizi tunayoyashuhudia hivi sasa.
Matendo yote yanayopanua mpasuko uliomo ndani ya jamii, hasa mpasuko baina ya watawala wakwasi wa kupindukia na wananchi masikini hohe hahe, katikati ya kila aina ya utajiri wa asili, hayavumiliki katika jamii yo yote ile. Inakuwa mbaya zaidi inapotokea kwamba watawala walioshiba wanaanza kuwabeza wananchi masikini wanapowahoji wakubwa juu ya matendo hayo.
Waswahili husema, “Njaa mwana malegeza, shibe mwana malevya” . Baadhi ya hao wanaotoa kauli za kebehi zinazotokana na ulevi wa shibe ni wale wale ambao si muda mrefu uliopita walikuwa wakienda miayo ya mlegeo wa njaa. Na iwapo siku moja watapoteza nafasi zao za sasa, si kazi wakarejea miayo yao ya asili.
Hivi, Mheshimiwa Rais, kuna kosa gani kwa wananchi kuhoji ununuzi wa ndege ya kifahari kwa ajili ya matumizi ya Rais wakati usafiri mwafaka unaweza kupatikana kwa gharama nafuu zaidi?
Kuna mantiki gani katika kuwaambia wananchi kwamba ndege hiyo ikichomoka Dar es Salaam, hiyoo.. hadi Tokyo, hadi New York bila kulazimika kutua? Tokyo na New York imegeuka mikoa ya Tanzania, au tunamchagua Rais ili akatuwakilishe huko?
Ni kweli Rais analazimika kufanya kazi za kimataifa, lakini hizi ni za safu ya pili; safu ya kwanza ni ile ya kazi za nyumbani, ambazo zinahitaji ndege au usafiri mwingine wo wote wa kumfikisha kiongozi wetu Tabora, Songea, Kigoma, Sumbawanga na Bukoba. Mtazamo unaomfanya Rais wetu aonekane kama Waziri wa Mambo ya Nje ni mtazamo potofu unaotokana na upangiliaji tenge wa vipaumbele.
Isitoshe, hata kama kweli upo ulazima wa kununua ndege kama hiyo (nasi kweli hatutaki Rais wetu apande punda kama Bwana Yesu) kuna haja gani ya kuwakebehi wale wanaouliza, wakati sote tunajua jinsi maneno matamu yalivyomtoa nyoka pangoni? Kama si ulevi wa shibe ni nini?
Suala jingine lililoibua kebehi ni lile la “uuzaji” wa nyumba za watumishi wa Serikali. Inawezekana nina matatizo, lakini nakiri kwamba kila nilivyojaribu kulitafakari sijapata mantiki yake. Labda mantiki yake ingenielea iwapo wahusika wangetumia lugha inayoeleweka. Jibu lililotolewa, kwamba wote wanaouliza maswali kuhusu nyumba hizo wanalia wivu, si jibu bali ni mzaha mbaya.
Je, ni kweli kwamba uamuzi wa kuuza nyumba hizo ulizingatia mahitaji ya Serikali kuhusu watumishi wake waliopo na wajao? Waliouziwa ni wale waliostahili kuuziwa? Hakuna walioingizwa katika orodha ya kuuziwa wakati hawastahili? Bei ya kuuza ilizingatia bei ya soko, au ilipangwa na hao hao waliouziwa?
Hivi sasa Serikali imekuwa inahaha kukamilisha nyumba kwa ajili ya watumishi wake wapya. Ni nini hasa mantiki ya Serikali kuuza nyumba zake na kisha kuhangaika, kwa njia za zima moto, kujenga nyumba mpya? Je, hao watakaoingia katika hizo nyumba mpya nao watauziwa? Kama jibu ni ndiyo, je, Serikali sasa inaingia katika biashara ya kujenga na kuuza nyumba?
Haya ni maswali yanayoulizwa na watu wengi, na sidhani kwamba jibu lake ni kwamba watu wote wanalia wivu. Binafsi nadhani haya ni maji yaliyokwisha kumwagika, na ambayo hayazoleki. Utaratibu wa kupiga rivasi shughuli nzima unaweza kuwa mgumu sana. Muhimu ni kutambua kwamba jambo lililotendeka si sahihi, na kuweka azma ya kutolirudia huko tuendako.
Amani na utulivu
Labda sasa nieleze mtazamo wangu kuhusu maneno yanayotumika mara kwa mara na wakuu wetu, “amani na utulivu”. Kwanza niseme kwamba nalisikia neno “utulivu” kama linaloashiria hali ya kubweteka, kuganda na kukaa mahali pamoja, bila harakati wala shughuli.
Linaashiria jamii isiyohangaika, isiyochakarika kutafuta maisha bora kuliko hayo yaliyopo.
Hata misemo yetu inayotumia neno hilo inatoa mwanga kama huo. Tunasema, “Tulia kama unanyolewa”, au “Ametulia kama maji ndani ya mtungi”. Kama hiyo ndiyo mifano ya utulivu, sina hakika kwamba ni jambo jema kwa nchi yetu kunyolewa, au kwa nchi kubweteka ndani ya mtungi hadi anapokuja mtekaji kuiteka na kunywa.
Inawezekana kilichotakiwa kusemwa ni “utangamano”, kwa maana ya hali ya maelewano na mshikamano ndani ya jamii, hali ya kutokuwa na fujo, vurugu na ghasia, hata kama watu wanahangaika, wanachakarika huku na huko wakitafuta maisha. Watu waliotulia hawahangaiki, na kutokuhangaika katika hali kama yetu ni kutafuta mauti yanayotokana na njaa.
Kwa hiyo, ningekuwa na uwezo ningeshauri kwamba kaulimbiu hiyo ibadilishwe na badala yake iwe “amani na utangamano”, au “amani na mshikamano”. Lakini ubavu huo sina, na nashuku kwamba tutaendelea kuyasikia maneno hayo hayo, “amani na utulivu” hadi hapo itakapokuwa dhahiri kwa kila mtu kwamba hayana maana tena.
Lakini, kwa vyo vyote vile tutakavyoyaelewa maneno hayo, hayawezi kuwa ndiyo sera yetu au mkakati wetu wa kujiletea maendeleo. “Amani na utulivu”, “amani na utangamano” au “amani na mshikamano” ni hali inayozalishwa kutokana na sera na mipango mizuri iliyowanufaisha wananchi na kuwapa matumaini makubwa zaidi katika mustakabali wao kiasi kwamba wanaridhika na maisha yao. Ni matokeo, si chanzo.
Mwaka 1987 tulikuwa sote Kizota katika Mkutano Mkuu wa CCM, na tulimsikia Mwenyekiti, Mwalimu Julius Nyerere akisema maneno haya haya. Alitukumbusha msemo wa Kiswahili, “Usione vinaelea, vimeundwa”.
Alisema kwamba amani tunayojivunia ni matunda ya sera nzuri na mipango madhubuti iliyowasaidia wananchi na kuwapa matumaini, na kisha akaongeza kwa kuuliza, kama amani huzuka hivi hivi tu, kwa nini, basi, isizuke kila mahali?
Ni dhahiri, kwa hiyo, kwamba ili kuvuna amani hatuna budi kuwekeza katika kuwatendea mema, kuwaendeleza wananchi wetu, na kuepukana na matendo yanayowakerehesha wananchi. Katika miaka ya karibuni tumeshuhudia kupanuka kwa ufa baina ya masikini na matajiri katika nchi yetu. Wakati ukwasi mkubwa unajidhihirisha miongoni mwa kikundi kidogo sana cha Watanzania wanaoishi katika pepo ya dunia, mamilioni ya wananchi wenzao wanaishi katika jehannam hapa hapa.
Ni kweli kwamba kila nchi, hata zile zilizoendelea sana, ina matajiri na masikini. Lakini haikubaliki kwamba katika nchi yenye utajiri kama iliyo nao nchi yetu, bado kuna wananchi wengi wanaoishi chini ya kile kinachoitwa msitari wa umasikini.
Kisichokubalika zaidi ni kwamba hali hiyo inazidi kujichimbia kila uchao. Ni lazima tufanye kila linalowezekana kusitisha hali hii kabla haijakomaa na kutugawa kabisa.
Aidha hatuna budi kuhakikisha kwamba rasilimali kubwa tulizo nazo zinatumika kwa manufaa ya wananchi na Taifa lao, na si kwa manufaa ya tabaka dogo tu la watawala na makampuni ya nchi za kigeni. Nakushukuru sana kwa tamko lako la majuzi kuhusu umuhimu wa kuipitia mikataba yote inayohusiana na utumiaji wa rasilimali zetu, hasa madini.
Hili limekuwa ni eneo la mgogoro mkubwa kati ya Serikali iliyopita na wazalendo waliothubutu kuuliza ni nini hasa inachopata Tanzania kutokana na uchimbaji wa madini yetu. Kila suala hili lilipoibuka majibu kutoka kwa wakubwa yamekuwa ya kiburi na kejeli.
Wasaili wameambiwa kwamba ni vipofu, viziwi na wenye “uvivu wa kufikiri”. Sasa, angalau, tumepata nafuu kutokana na tamko lako hilo, kwani sitaraji kwamba na wewe utaambiwa una “uvivu wa kufikiri”.
Kumrejea tena Mwalimu Nyerere, haya madini hayaozi, kwa hiyo hatuna sababu ya kuwa na haraka kubwa kuyachimba kana kwamba tukichelewa tutayapoteza. Kama hatuna utaalamu wa kuweza kujadili na kubishana bei hadi tupate mradi wetu, basi tuyaache hadi hapo watoto wetu watakapokuwa na uwezo huo.
Lakini mimi siamini kwamba hatuna uwezo huo, bali ni kwamba wawakilishi wetu katika mijadala ya biashara hawawakilishi maslahi yetu, bali, nashuku, wanatanguliza maslahi yao binafsi. Shaka yangu inatokana na ukali wanaouonyesha kila wanapoulizwa kuhusu usiri wa mikataba waliyotia saini.
Inawezekana kwamba mikataba hiyo haina walakini, na kama hivyo ndivyo kuna sababu gani ya kuifanya siri? Mali inayohusika si mali ya maofisa wa Serikali; ni yetu sote. Na wala si ya kizazi hiki; kizazi kilichopo leo kina dhamana ya kuitunza mali hiyo kwa ajili ya vizazi vijavyo, na kuitumia pale tu inapobidi kutumika kwa maslahi ya Taifa la leo na la kesho na keshokutwa. Haiyumkiniki kwamba wajukuu wetu watakuta mashimo makubwa ardhini mahali yalipokuwa madini, huku hatuna cha kuwaonyesha kama fidia ya uharibifu wa ardhi yao.

Tuna sababu za kuwa waangalifu kuhusu madini na rasilimali nyingine, kwa sababu ushahidi tulio nao hadi sasa unadhihirisha kwamba amali kama hizi hazijazisaidia nchi zilizobahatika kuwa nazo barani Afrika. Tukiangalia wenzetu wenye hazina kubwa za madini kama dhahabu, almasi, mafuta na kadhalika, tunaona jinsi utajiri huo ulivyogeuka kuwa laana, laana ambayo duniani inaitwa the “Dutch Disease”, au ugonjwa wa Kidachi kufuatia matatizo yaliyoikumba Uholanzi baada ya kugundua mafuta katika Bahari ya Kaskazini (North Sea). Nchi kama Kongo (zote mbili), Angola, Nigeria, Sierra Leone, Equatorial Guinea na kadhalika, ni nchi zenye utajiri mkubwa wa machimbo ya kila aina, lakini utajiri huo haujaonekana kuwasaidia raia wa nchi hizo. Kinyume chake, walichovuna ni vita, vurugu, maombolezo makubwa na mitafaruku ya kitaifa.
Wapo wataalamu wanaodhani kwamba katika hali fulani fulani ni heri kutokuwa na utajiri huo kwa sababu inaelekea Waafrika hatujaweza kujenga utaratibu wa kuwa na utajiri na kisha tukajua namna gani ya kuutumia kwa manufaa yetu wenyewe.
Tunapozungumzia amani hatuna budi kukumbushana kwamba nchi zote zinataka amani, lakini zinashindwa kuipata, au kuidumisha, kwa sababu ya siasa mbovu na mipangilio tenge ya kisiasa na kiuchumi, hasa mipangilio inayowanyima walio wengi nafasi ya kushiriki katika mgawanyo wa mali za taifa.
Nilipata bahati nilipokuwa kijana kutembea bara zima la Afrika na kujionea mwenyewe nchi zilizokuwa na amani kama sisi hivi leo. Sierra Leone ilikuwa ni nchi ya amani, nchi ya raia wastaarabu, wapole, wakarimu hadi wanachosha. Lakini kutokana na siasa chafu, uongozi mbovu na kukithiri kwa rushwa miongoni mwa watawala, mambo waliyofanyiana wananchi wa Sierra Leone hayaelezeki.
Nasi tunatakiwa kujifunza kutokana na wenzetu waliokumbwa na matatizo huko nyuma. Tusiwachokoze wananchi mpaka wakafikia hatua ya kusema, “Sasa basi; liwalo na liwe”.
Tunajifunza vile vile kutoka Sierra Leone kwamba watu wapole na wavumilivu mara wanapopoteza upole huo na uvumilivu hugeuka kuwa wanyama, na kwamba kuwarudisha katika utu inakuwa kazi ngumu sana.
Hii ni kwa sababu wanakuwa wamelimbikiza manung’uniko mioyoni kwa muda mrefu, na unapokuja kutokea mlipuko wa kwanza wanakuwa hawajui kwa uhakika chanzo chake ni nini, kwa sababu mambo ni mengi na ya muda mrefu. Ni hatari kuruhusu manung’uniko yakarundikana kwa miaka mingi, huku tukijidanganya kwamba hiyo ndiyo “amani na utulivu”.
Wakati mwingine ni bora kuwa na watu wanaolipuka kila wanapohisi wameonewa, kwa sababu ikitokea hivyo suala husika linaweza kushughulikiwa mara moja kwa sababu linaeleweka na linaweza likadhibitiwa, na wananchi hawapati nafasi ya kulimbikiza visasi mioyoni mwao.
Ndiyo maana naamini kwamba itakuwa vigumu kwa nchi kama Zambia kuwa na vita ya wenyewe kwa wenyewe kwa sababu kila mara linapotokea jambo la kuwakera Wazambia, maelfu huingia mtaani na kufanya fujo hadi linaporekebishwa.
Kama nilivyosema awali, raia zako ni watu wema, wapenda amani. Lakini lazima watendewe haki. Hivi sasa manung’uniko yapo mengi, kuhusu rushwa na ufisadi, kuhusu ufukara unaoongezeka, kuhusu mikataba ya uongo na kweli, kuhusu matumizi mabaya ya fedha katika uchaguzi, na kadhalika. Haya yote yanakusubiri wewe na timu nzima ya uongozi.
Ndugu Rais, huwa napenda kutoa mfano wa afya ya mtu binafsi. Mtu mwenye busara ni yule anayeamka asubuhi akijisikia mzima wa afya, lakini bado akaenda kwa daktari wake kufanyiwa uchunguzi ili ajue ni hatari gani zinazomnyemelea katika siku za usoni. Anafanya hivyo kwa sababu anajisikia vizuri na anapenda hali hiyo iendelee, lakini anajua kwamba zinaweza kuwapo ishara mwilini mwake kwamba huko mbele ya safari anaweza kukumbwa na matatizo ambayo leo hayajui. Daktari atajua.
Iwapo atasubiri mpaka augue, yu hoi kitandani, anaweza akashindwa hata kwenda kwa daktari kwa sababu ya kukosa nguvu. Katika mazingira hayo anaweza akajikuta anapata ushauri wa “kiganga” kutoka kwa ye yote atakayemwona, hata mtumishi wake wa nyumbani.
Kwa taifa pia ni hivyo hivyo. Daktari wetu ni sisi wenyewe. Inatubidi tujichunguze ili tuone kama kuna kitu mwilini mwetu ambacho hapo baadaye kinaweza kikatuondolea afya hii ambayo leo tunaifurahia. Tukijichunguza kwa makini tutagundua dalili nyingi zinazoashiria saratani huko tuendako.
Itaendelea.Barua ndefu ya wazi kwa Jakaya
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom