Jenerali Ulimwengu amfananisha Pinda na mbwa wa PAVLOV | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Jenerali Ulimwengu amfananisha Pinda na mbwa wa PAVLOV

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by sikiolakufa, Jun 24, 2011.

 1. s

  sikiolakufa JF-Expert Member

  #1
  Jun 24, 2011
  Joined: Feb 1, 2010
  Messages: 411
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 0
  Kuvimbiwa kwa watawala: Jibu si kuvua gamba


  Jenerali Ulimwengu
  22 Jun 2011
  Toleo na 191

  Wahitaji kula haluli kusafisha tumbo

  SI kazi rahisi kwa yeyote miongoni mwetu kujaribu kueleza, na akaeleweka kuhusu nini kinatendeka hivi sasa katika siasa za nchi yetu, hususan kuhusu nafasi ya chama ambacho kimeliongoza Taifa hili kwa nusu karne sasa.

  Yapo mambo mengi sana, ikiwa ni pamoja na matendo na matamko ambayo yanaashiria kwamba ndani ya chama hicho mchoko umefikia viwango vya kushangaza kwa wale wasiojua umetokea wapi.

  Wapo watu wachache wanaojua, angalau kidogo, mchoko huo umetokea wapi, na nasaba yake ni nini, na wanajua jinsi ulivyoanza na jinsi ulivyoanza kukua ndani ya chama hicho hadi kufikia hali tunayoishuhudia leo, yaani hali ya mchoko wa hoi-bin-taaban.

  Waswahili husema usiangalie ulipoangukia bali chunguza ni wapi ulipojikwaa, kwani anguko lako ni matokeo ya kujikwaa kwako, ambako usipoangalia unaweza ukakusahau ukiangalia tu pale ulipoangukia. Gharama mojawapo inayolipwa na mwangukaji asiyejua ni wapi alipojikwaa ni kuiona ardhi alipoangukia kama ndilo tatizo lake.

  Siwezi kudai kwamba mimi binafsi nina uelewa mkubwa kuliko wa watu wengi kuhusu chanzo cha mchoko tunaouona, lakini ninaweza nikachanga mawazo yangu ambayo yanaweza, kwa kuchakatwa pamoja na ya wenzangu, yakatoa mwanga kidogo katika hili ninalolijadili sasa.

  Naamini kwamba zoezi hili lina umuhimu wake kama tunataka kuepukana na zahma za kutupiana lawama, na hata kuumizana, kwa sababu ama hatutaki, ama hatuwezi kufanya tafakuri ya masafa marefu, na hamasa zetu zisizo na mafunzo zinatutuma kutafuta majibu mepesi mepesi na majibizano yasiyosumbua akili.

  Kwa kuwa mjadala huu hauna budi kuingia katika mijadala mipana inayoendelea kuhusu umuhimu wa kubadili kwa kina namna tunavyoendesha shughuli zetu za kitaifa, masuala kama vile ya Katiba mpya na mipangilio mipya ya kisiasa na kiutawala, bila shaka yataibuka mara kwa mara, na hivyo ndivyo ilivyo katika mjadala wo wote ambao unaangalia masuala kwa mtazamo kamilifu (holistic). Kwa jinsi hii tuanweza tukatambua mti mmoja mmoja na pia tukatambua msitu ambamo ndani yake ndimo inapatikana miti hiyo.

  Uvuaji gamba

  Leo hii ningependa nijiunge na wale wanaojadili suala la chama-tawala kufanya kila kilichopachikwa jina la ‘kuvua gamba'. Nisingependa kuingilia mijadala ya kishabiki na mabezo mengi yaliyotolewa katika vyombo vya habari kuhusu uteuzi wa nahau ya kuvua gamba, ambayo imeelekezwa moja kwa moja upande wa silka ya nyoka. Nitaliacha hilo, kwa sababu naamini halina uzito mkubwa kwani ni utelezi wa ulimi ambao naamini katika miezi ijayo hatutausikia sana.

  Mimi nitakwenda katika dhana yenyewe ya kutaka kujisafisha kwa kuwaondoa katika nafasi za uongozi wanachama watatu,au watano, au 10, au 20, au 40, au hata 100. Nimekuwa nikifuatilia mijadala (nyingi zikiwa ni kelele) kuhusu ‘mapacha' ambao wanatakiwa ‘watoswe' ili ‘kukinusuru chama.'

  Inaelekea mantiki iliyotumika ni kwamba hawa watu wamekipa chama-tawala jina baya machoni mwa Watanzania kwa sababu wao ndio wanaosemwa sana kwamba wanahusika na ufisadi, na kwa hiyo ikiwezekana ‘kuwatosa' chama kitakuwa kimejitakasa mbele ya wananchi, nao wananchi wataanza kutuamini tena na kuturuhusu tuwaongoze.

  Utaalamu wangu mdogo wa masuala ya kisiasa haunipi taswira ya chama ambacho kwa kuwaondoa watu watatu au wanne, au hata 100, kinakuwa kimejisafisha kwa kufanya hilo tu. Sijasikia chama hicho kikijadili au kupendekeza mapitio ya misingi ya kifalsafa na kiitikadi ndani ya chama hicho; mijadala ya programu za kisiasa; marejeo ya sera za chama kuhusu utekelezaji wa programu hizo za kisiasa; wala miundo yake itakuwa ipi ili kubeba programu hizo na kuhakikisha utekelezaji wake unafanyika inavyopasa; wala maandalizi ya makada wenye uangavu wa msimamo unaowawezesha kutekeleza programu hizo.

  Ninachosikia, na ambacho kinachosha kama walivyochoka wanaokiendeleza, ni ‘kuvua gamba', ni kupambana hadi ‘tone la mwisho la damu' na mambo mengine ambayo, kusema kweli, mimi nayaona ni ya kipuuzi. Hao ‘mapacha' wana nguvu gani ndani ya chama ambayo wamejilimbikizia kwa kuipora bila wanachama na mifumo ya chama hicho kujua?

  Ni lini hasa walipoanza kuwa na nguvu hii, na wenzao ndani ya chama walikuwa wanafanya nini wakati wote huo, na leo ndiyo wanatanabahi wakati ‘mapacha' wamekwisha kukiteka chama kizima kiasi kwamba nusura ya chama ni kwa hao ‘mapacha' kuondoka?

  Hebu tujiulize, hicho ni chama cha siasa kinachoongoza serikali au ni chama cha wacheza dhumna? Hata wacheza dhumna, pale Saigon mathalan, huwezi kuchezea chama chao kwa muda wa wiki mbili, ukafanya mambo yanayowaudhi wanachama wengime, halafu ukawa salama na wakakuachia uendelee kuendesha shughuli za chama chao.

  Seuze kwa chama kinachoongoza serikali. Wote wanaozungumzwa hivi leo wamewahi kuwa na nyadhifa kubwa katika chama-tawala, na wengine katika serikali. Hao wanaotaka tuamini kwamba hawa ni watu hatari kiasi hicho hawana budi waseme pia ni kwa nini wananchi wa Tanzania waendelee kukiamini chama hicho ambacho kinafanya kazi kama kimelala usingizi hadi kizinduke miaka kadhaa baada ya mambo kuwa yamekwenda hovyo.

  Msimamo wangu

  Nieleze msimamo wangu kuhusu hao ‘mapacha' maarufu. Kwanza sidhani miongoni mwao yupo hata mmoja ambaye anazo sifa za kuwa kiongozi mkuu wa Tanzania, kama tunaitakia mema nchi hii.

  Niseme ukweli wangu: Naamini hadi sasa, na hili nitaliamini hadi kufa, kwamba, kwa jinsi nchi ilvyovurugika, tunahitaji Julius Nyerere mpya, ambaye nitamweleza baadaye, ambaye ataongoza mapambano ya ukombozi mpya wa nchi hii na wananchi wake.

  Katika hao wanaotajwa hakuna mtu wa aina hiyo, na kwangu mimi ye yote mwenye njozi za aina hiyo angefanya vyema kutia tamati na afanye mambo mengine.

  Lakini si lazima waondoke katika chama-tawala kwa ajili eti ya kukisafisha. Kwa kuwa kwa njia hiyo hakisafishiki. Muasisi wa chama hicho, Mwalimu Nyerere alikwisha kukiona chama chake kwamba kimechafuka mno kiasi kwamba sababu moja iliyomsukuma kufanya kampeni ya kurejesha mfumo wa vyama vingi (aliokuwa ameukomesha mwenyewe) ilikuwa ni kupata vyama vya kukizindua chama-tawala kutoka usingizi wa pono kiliokuwa kimelala.

  Badala ya chama-tawala kuuelewa msimamo wa Kambarage na kufanya marekebisho ndani yake kwa kunoa falsafa yake na kutakasa itikadi yake, kikazidi kujichimbia katika kila aina ya uovu na kukaribisha kila aina ya wanachama wasio na nasaba yo yote na chama hicho.

  Chama cha makabwela (Baba kabwela UNO- kumbuka) kikageuka, kikawa ni chama cha wenye ‘vijisenti.' Naye Mwalimu aliwauliza warithi wake katika utawala: Tumefanya mambo mengi mabaya, lakini pia tumefanya machache mazuri. Mbona inaelekea nyiye mnang'ang'ania mabaya yetu na mazuri yetu hamyataki?

  Hali hii haikutokea ghafla, na wala haikusababishwa na hao mapacha maarufu. Pia si kweli kwamba hakukuwa na watu wa kutahadharisha kuhusu hatari ya chama kutekwa na siasa zisizokuwa zake. Wale waliokuwa ndani ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kati ya miaka 1992 na 1997 watakumbuka kwamba baadhi yetu tulisema, tukazomewa na wajumbe wachovu waliokuwa na haraka ya kuwahi kula nyama-choma mnadani Dodoma. Wenye kumbukumbu na wakumbuke.

  Nayaandika haya leo, na (Insha Allah) nitayaandika mengine mengi katika kipindi hiki, kwa sababu miaka inakwenda, tunazidi kuwa watu wazima, wengi miongoni mwetu wanaondoka, nasi tu njiani pasi na shaka. Nayaandika haya, ili angalau wale ambao bado wangali hai, waseme kama huu ni uongo.

  Baadhi yetu tulifadhaika kuona chama kilichoanzishwa chini ya siasa ya utu na udugu wa binadamu wote kikigeuka kuwa chama cha manyang'au wasiojali watu bali wanajali vitu, chama kilichosimamia misingi ya haki kwa wote kikigeuka chombo cha utetezi wa wenye nguvu dhidi ya wanyonge.

  Chama kilichonasibika Afrika na dunia nzima kuwa ngao ya kutetea nchi na mali zake kikibadilika na kuwa chama-na-serikali-dalali cha kuuza nchi na rasilimali zake kila kinapopata fursa ya kufanya hivyo.

  Sasa, na aseme mtu kwamba haya yote wamefanya mapacha wetu maarufu, na wakiondoka ndani ya chama hicho, chama kitarejea misingi yake ya kale, nami nitajiunga na maandamano ya kuwang'oa hao mapacha maarufu.Wenyewe wanajua lakini wanajifanya hamnazo.

  Ni kweli baadhi ya mambo yaliyofanywa na mapacha maarufu ni ya hovyo, na mengi hayahitaji mjadala, lakini je, ni wao peke yao? Tukiisha ‘kuwatosa' (Waswahili kwa kupenda kutosana!) ndiyo tutakuwa tumemaliza kazi?

  Hao ‘watosaji' na wanaovua magamba bila mpangilio wanajua kwamba kwa muda mrefu chama chao na serikali yao vimetekeleza sera za ugawaji (‘uuzaji' wanasema wasiojua Kiswahili) mali za Taifa kwa bure, bure! Mifano ni mingi: madini yetu na Benki ya Taifa, na sasa ardhi kwa ajili ya kilimo cha petroli. Nyerere alipopiga kelele kuhusu kuigawa benki yetu kwa Makaburu alipuuzwana kudharauliwa ungedhani aliyesema Jenerali miye.Kisa, wakubwa wa Washington wamesema, na watawala wetu wakiambiwa na wakuu hao ‘Ruka!' wanachouliza watawala wetu ni ‘Hadi wapi?'

  Yamesemwa mengi, nami sina haja ya kuyarejea yote, kwani wakati mwingine yanatia kinyaa... rada, ndege, ma-green na ma-meremeta, nyumba za serikali walizogawiwa maofisa waliochaguana katika wizi wa mchana ambao haujawahi kutokea, hata Nigeria.

  Mwenyekiti wa chama-tawala wakati huo aliamua kwenda mbali zaidi kwa kujizawadia mgodi mzima wa serikali, kama mjasiriamali-mamboleo. Chama chake, kimya! Najiuliza hilo gamba wanalosema wanajivua ni gamba lipi, mbona yako mengi? Na wakitaka kutafuta mapacha wa ‘kuwatosa' si itawabidi wapange mafungu kadhaa ya mapacha, halafu waanze kuwatosa kwa zamu, kila fungu na msimu wake wa ‘kutoswa?' Na hawatawamaliza, jinsi walivyo wengi na walivyokikamata chama chao.

  Ubanaji posho za vikao

  Sasa hebu tuangalie namna ya kujivua gamba hili jingine. Kama alivyotabiri Kambarage, kumbuka, chama kikuu cha upinzani kimeamua kuitikisa misingi mibovu ya matumizi ya fedha za umma kwa kuasisi wazo la kubana posho za vikao ambazo kinadhani si halali hata kama zinalipwa kwa utaratibu uliowekwa kisheria (kumbuka kila kinachofanyika kisherria si lazima kiwe halali; ndiyo tofauti kati ya legal au lawful na legitimate).

  Jinsi alivyolileta Kabwe Zitto suala hili lilizua malumbano kana kwamba ni tatizo kati yake na Ofisi ya Spika, lakini baadaye ikaonekana kwamba ni sera ya CHADEMA ambayo inaambatana na mahesabu ya bajeti ambamo wanapendekeza kuokoa shilingi bilioni 900 kwa kufuta posho zisizokuwa na maelezo isipokuwa mazoea ya kula bila kufikiri, zoezi ambalo wanapendekeza liguse ngazi zote za serikali.

  Mjadala haujafanyika kuhusu hili, lakini kinachosikika ni kelele zaidi, kwani inaelekea chama-tawala hakijaamua kifanye nini kuhusu hili, na hapa napo kimechelewa, kinafuata yale yanayosemwa na wengine, kama kinadhani yanawavutia wananchi, badala ya kuongoza. Na kama kawaida yao, inaelekea hawajakubaliana miongoni mwao: msemaji wa chama anasema lake, kiongozi wa serikali anasema lake.

  Lakini ni msemaji wa serikali aliyenivutia. Waziri Mkuu Mizengo Pinda anasema kwamba hizi ni posho za kawaida tu, na wala mtu asije akataka kuwaambia wananchi kwamba wabunge wanawaibia. Sawa, wabunge hawaibi kwa sababu kisheria posho hizi zimepangwa. Hata hivyo, nadhani wanachosema CHADEMA, kama nimeelewa vyema, si kwamba wabunge wanaiba, la hasha, bali kwamba hizi posho hazina uhalali kwa sababu tayari wabunge wanalipwa mishahara na posho stahili na maridhawa, na kwamba fedha zinazoweza kuokolewa kwa kufuta hizi kodi zingekuwa na manufaa kwa wananchi.

  Hapa tena niseme kwamba nashindwa kuelewa ugumu wa kulielewa hili unatoka wapi. Kama mbunge analipwa mshahara wa mwezi, kisha analipwa masurufu ya kuwa kazini nje ya kituo chake, posho ya kikao, ambacho ndiyo kazi yake ni ya nini? Ni nini cha zaidi anachofanya kuliko kuhudhuria kikao cha Bunge ambacho ndicho kimempeleka Dodoma na ambacho kwacho amelipwa per diem?

  Maneno mengine hayapendezi, na si jambo jema kumsuta waziri mkuu, hasa kwa sababu Pinda ninamheshimu sana. Lakini haipendezi kusema eti hata hao wabunge wa Upinzani "wanazimezeamezea mate fedha hizo, lakini wafanyeje?" Nini maana yake? Kwamba wangekuwa huru kusema wangesema wapewe hizo fedha lakini labda wamebanwa na uongozi wao? Nini hasa maana yake, kwamba mtu wa kawaida atazimezeamezea mate tu hizo posho hata kama hazina sababu, na kwa hiyo ni halali zilipwe, kwa sababu ya kumezewamezewa mate?

  Hapa hakuna msaada wa kujisafisha kitakaopata chama-tawala kupitia njia ya kujivua gamba. Shughuli inayomezewamezewa mate hapa haina uhusiano na gamba la mnyama ye yote, bali inahusu tumbo. Mate ya mbwa wa Pavlov huanza kumdondoka anapopata ishara kwamba mlo wake unakaribia, na mlo wake ukicheleweshwa inabidi ameze mate. Sijui kama hivyo ndivyo wanavyofanya wabunge wa Upinzani.

  Lakini wale wanaoendelea kutaka kula hicho chakula ambacho wenzao wanakimezea mate ajue kwamba wananchi sasa wamejua kwamba wawakilishi wao wanalipwa masurufu wasiyostahili, hata kama wanalipwa kisheria.

  ‘Mavyakula' kama haya hayaathiri afya ya ngozi, bali huathiri tumbo. Kulakula hovyo ni dalili ya ulafi, na ulafi ni mojawapo ya dhambi za mauti, hasa kwa Wakristo. Miongoni mwa mambo mengi wanayolalamikia wananchi wetu, moja kubwa ni ulafi wa watawala wao katika mazingira ya hali mbaya mno za maisha ya watu wa kawaida.

  Chama cha upinzani kitakuwa si chama cha upinzani kama kitashindwa kuliona hilo na kuwapiga nalo watawala na kupata kuungwa mkono na wananchi.

  Tamko jingine la kushangaza ni lile la Mustafa Mkulo anayesema kwamba wanaokataa posho wanatafuta umaarufu wa kisiasa. Sasa je, ni mwanasiasa gani asiyetafuta umaarufu wa kisiasa? Suala ni kujua umaarufu huo anautafuta kwa mbinu gani, mbinu za kuwaangamiza watu wake au za kuwasaidia?

  Kiafya, ulafi husababisha mtu kuvimbiwa, na kuvimbiwa dawa yake si kuvua gamba bali ni kula haluli (laxative) inayosafisha tumbo chafu na kutoa uchafu wote nje. Katika makala ijayo nitaijadili hiyo haluli wanayohitaji watawala wetu.
   
 2. J

  Jasho la Damu JF-Expert Member

  #2
  Jun 24, 2011
  Joined: Mar 10, 2011
  Messages: 958
  Likes Received: 12
  Trophy Points: 0
  Big up Ulimwengu.
   
 3. samirnasri

  samirnasri JF-Expert Member

  #3
  Jun 24, 2011
  Joined: Nov 8, 2010
  Messages: 1,377
  Likes Received: 8
  Trophy Points: 135
  kazi ipo mwaka huu.
   
 4. delabuta

  delabuta Senior Member

  #4
  Jun 24, 2011
  Joined: May 23, 2011
  Messages: 179
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Asante kwa taarifa nzuri inayoeleweka kwa watu wote, kwa kuuona upungufu wa gamba na sera za mapacha watatu.
   
 5. PakaJimmy

  PakaJimmy JF-Expert Member

  #5
  Jun 24, 2011
  Joined: Apr 29, 2009
  Messages: 16,236
  Likes Received: 309
  Trophy Points: 180
  Kwa mada hii, Jenerali ametumia kichwa, na rejea zisizo shaka. Kama PM anasoma makala hizi alipashwa kuchukua maamuzi magumu mara baada ya kufika kwenye nukta ya mwisho wa makala hii. Tuamini ama tusiamini, kazi ya upinzani ni kubwa na ya maana mno. Nimepata hasira sitaendelea kuandika zaidi ya hapa...wenye vifua jadilini.
   
 6. Horseshoe Arch

  Horseshoe Arch JF-Expert Member

  #6
  Jun 24, 2011
  Joined: Aug 10, 2009
  Messages: 11,230
  Likes Received: 4,951
  Trophy Points: 280
  Well said Jenerali...
   
 7. Lunyungu

  Lunyungu JF-Expert Member

  #7
  Jun 24, 2011
  Joined: Aug 7, 2006
  Messages: 8,836
  Likes Received: 75
  Trophy Points: 145
  Duh saga la uraia kesha lisahau ? Wataanza kumwambia si raia tena maana CCM hawana maana .
   
 8. Nyunyu

  Nyunyu JF-Expert Member

  #8
  Jun 24, 2011
  Joined: Mar 9, 2009
  Messages: 4,370
  Likes Received: 130
  Trophy Points: 160
  Really inspiring reading. Big up JU
   
 9. Dingswayo

  Dingswayo JF-Expert Member

  #9
  Jun 24, 2011
  Joined: May 26, 2009
  Messages: 4,011
  Likes Received: 86
  Trophy Points: 145
  Ameongea kila kitu. Asante sana kwa kuweka mambo hayo yote bayana.
   
 10. Tuyuku

  Tuyuku JF-Expert Member

  #10
  Jun 24, 2011
  Joined: Jan 6, 2011
  Messages: 3,149
  Likes Received: 1,407
  Trophy Points: 280
  ahsante sana Jenerali Ulimwengu...ama kwa hakika umenigusa sana kwa makali hii ya kifalsafa.
   
 11. j

  jnuswe JF-Expert Member

  #11
  Jun 24, 2011
  Joined: Nov 2, 2010
  Messages: 1,271
  Likes Received: 4
  Trophy Points: 135
  Kwa makala hii ,Ulimwengu ni Mzalendo wa kweli
   
 12. Dingswayo

  Dingswayo JF-Expert Member

  #12
  Jun 24, 2011
  Joined: May 26, 2009
  Messages: 4,011
  Likes Received: 86
  Trophy Points: 145
  Hivi hii ameiweka katika gazeti lipi?
   
 13. s

  sikiolakufa JF-Expert Member

  #13
  Jun 24, 2011
  Joined: Feb 1, 2010
  Messages: 411
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 0
 14. Mwendabure

  Mwendabure JF-Expert Member

  #14
  Jun 24, 2011
  Joined: Mar 10, 2011
  Messages: 2,056
  Likes Received: 298
  Trophy Points: 180
  Jenerali Ulimwengu wewe ni shujaa wangu daima!!!
   
 15. T

  Tanganyika Member

  #15
  Jun 24, 2011
  Joined: Nov 4, 2010
  Messages: 67
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Bwana Pinda asitudanganye yeye ni mtoto wa mkulima.......hivyo anatetea wanyonge.......hata kidogo! Watumisi wa serikali na Wabunge ambao wanaona mshahara hautoshi waachie hizo nafasi kwani kuna wengine wengi wako tayari kuzifanya bila ya kulipwa hizo posho!!
   
 16. M

  Mwanaweja JF-Expert Member

  #16
  Jun 24, 2011
  Joined: Feb 8, 2011
  Messages: 3,576
  Likes Received: 10
  Trophy Points: 135
  ulimwengu uko juu hata wafanyeje kifooooooooooo hicho kina bisha hodi. na wakuokoa chama hayupo maana wote vichwa vinaaangalia chini. endelelea kutuhabarisha na Mungu akupe maarifa na busara zaidi. Thanks.
   
 17. Majoja

  Majoja JF-Expert Member

  #17
  Jun 24, 2011
  Joined: Jun 10, 2011
  Messages: 610
  Likes Received: 11
  Trophy Points: 0
  Nina wasi wasi kama anaikumbuka njia ya kuelekea Rwanda/Burundi
   
 18. 0717436862

  0717436862 Member

  #18
  Jun 24, 2011
  Joined: Jun 23, 2011
  Messages: 13
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Asante ulimwengu natamani kama ningekuwa na Mzee pinda hapa 2some wote hi makala alf nimwulize amejifunza nn?
   
 19. kweleakwelea

  kweleakwelea JF-Expert Member

  #19
  Jun 24, 2011
  Joined: Nov 29, 2010
  Messages: 2,422
  Likes Received: 437
  Trophy Points: 180
  hongera ulimwengu! you are really insipiring the young generation while warning the elder one!
   
 20. B

  Bobuk JF-Expert Member

  #20
  Jun 24, 2011
  Joined: Oct 8, 2010
  Messages: 5,876
  Likes Received: 481
  Trophy Points: 180
  Hakuna njia ambayo ninaweza kutumia kumfikishia haya makala mhe. PM Pinda.
  Maana kwa jinsi alivyochoka kimwili na kiakili sidhani kama hata anao mda wa
  kusoma Raia mwema zaidi ya Uhuru na Habari leo.

  His email address please? au FB yake?
   
Loading...