Jela miaka 240 kwa ufisadi

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,005
Haya huyu atanyeshewa mvua kwa miaka 240, tusubiri tuone hao waliokwapua mabilioni ya BoT watapata kibano cha miaka mingapi.

Jela miaka 240 kwa ufisadi

na Alpius Mchucha, Songea
Tanzania Daima~Sauti ya watu

MHASIBU wa Shule ya Sekondari ya Mbinga, mkoani Ruvuma, Omari Millanzi (56), amehukumiwa kifungo cha miaka 240 jela, baada ya kupatikana na hatia ya makosa 60 ya kughushi nyaraka za serikali na kuiba sh milioni 24.1.

Kati ya makosa hayo 60 aliyotiwa nayo hatiani, 30 yalikuwa yakihusu mashitaka ya kughushi nyaraka kwa nia ya kutenda kosa na makosa mengine 30 yalihusu wizi wa fedha hizo, zaidi ya sh milioni 24.1.

Akitoa hukumu hiyo iliyosomwa kwa zaidi ya saa moja na nusu, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Ruvuma, Baptist Mhelela, alisema ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo, umeonyesha pasipo shaka kuwa, mshitakiwa alitenda makosa hayo kwa makusudi, kwa nia ya kuiba fedha ambazo zililetwa na mwajiri wake kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa serikali.

Hakimu Mhelela alisema kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo, mahakama inakubaliana na upande wa mashitaka na kuamua kumtia hatiani mshitakiwa kwa makosa yote 60.

Akifafanua zaidi juu ya adhabu hiyo, Hakimu Mhelela alisema mahakama inatoa hukumu hiyo kwa mshitakiwa kwa makosa 30 ya kughushi nyaraka za serikali na atatumikia kifungo cha miaka mitatu kwa kila kosa, hivyo kufanya idadi ya miaka atakayotumikia jela, kufikia 90.

Kwa upande wa makosa ya wizi huku akiwa mtumishi wa serikali, hakimu huyo alisema mahakama inamhukumu kwenda jela miaka mitano kwa kila kosa, hivyo kufanya jumla ya miaka atakayotumikia kwa makosa hayo, kufikia 150.

“Kwa hali hiyo, mshitakiwa huyo, anatumikia kifungo cha miaka 90 kwa makosa 30 ya kughushi nyaraka kwa nia ya kutenda kosa la wizi na miaka 150 kwa ajili ya makosa 30 ya wizi wa sh milioni 24.1,” alisema Hakimu Mhelela.

“Kutokana na makosa haya, mshitakiwa atapata adhabu hiyo ambayo itamfanya ajue kwamba alifanya kosa kubwa la wizi,” alisisitiza hakimu huyo.

Alisema adhabu zote zitakwenda pamoja, hivyo mshitakiwa Millanzi atatumikia kifungo cha miaka mitano jela na kwamba mara amalizapo kifungo chake, anatakiwa kulipa fedha alizomuibia mwajiri wake ambazo ni sh milioni 24.1.

Fedha hizo zilikuwa zimeletwa kwenye ofisi yake kutoka Hazina kwa ajili ya watumishi wa serikali waliostaafu na waliokufa.

Kabla ya kusoma hukumu hiyo, Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Inspekta George Omary, aliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa mshitakiwa, kwani makosa ya wizi na kughushi fedha za umma, yamekithiri ili liwe fundisho kwake na kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.

Kabla ya kutoa hukumu hiyo, mahakama ilitoa nafasi kwa mshitakiwa kujitetea, kwa nini asipewe adhabu kali ili iwe fundisho kwake na kwa wengine.

Katika utetezi wake, Millanzi aliiomba mahakama imuonee huruma kwa sababu kesi hiyo imechukua muda mrefu na kwamba umri wake ni mkubwa na ana mke na watoto wanaomtegemea.

Awali Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Inspekta George Omary, alidai mahakamani hapo kuwa, Omary Millanzi (56), mhasibu wa Shule ya Sekondari ya kutwa ya Mbinga, anashitakiwa kwa makosa ya wizi na kughushi nyaraka kwa nia ya kutenda kosa la wizi.

Ilidaiwa kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo kati ya Januari na Julai mwaka 1998, akiwa mtumishi wa serikali, ambapo alighushi nyaraka mbalimbali za serikali na kuiba kiasi hicho cha fedha, mali ya mwajiri wake.

Inspekta George, alibainisha zaidi mahakamani hapo kuwa mshitakiwa, Millanzi, alitenda kosa hilo, huku akijua anatenda kosa la kuiba mishahara ya watumishi iliyokuwa ikiletwa kutoka Hazina kwa ajili ya kuwalipa wastaafu na wengine waliokwisha kufariki dunia.
 
Back
Top Bottom