Jeetu Patel: Kutoka kuuza vipuri hadi kuwa bilionea fisadi

MmasaiHalisi

Senior Member
Jan 15, 2009
192
23
Alipata kupigwa ‘PI’ mwaka 1994

MENGI yameandikwa na kusemwa juu ya sakata ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ikiwahusisha watu mbalimbali na upotevu/uporaji wa zaidi ya shilingi bilioni 133 kutoka akaunti ya EPA.
Wanaotajwa zaidi katika sakata hiyo ni aliyekuwa gavana, Dk. Daudi Ballali na mfanyabiashara mwenye asili ya kiasia, Jayantillal Kumar Patel, maarufu kama Jeetu Patel.
Makampuni kadhaa ya kweli na ya bandia, yanatajwa kutumika kufuja fedha hizo. Serikali imeunda Tume ya kuchunguza kashfa hiyo na imetoa wito kwa wananchi wenye taarifa kuhusiana na tuhuma hizo wazitoe kwa tume.
Wakati Serikali ikiendelea na uchunguzi juu ya tuhuma hizi, umma unajiuliza kwa kuwa ni utamaduni wa vyombo vya usalama kukamata watuhumiwa wa makosa ya jinai kwa kile kinachoitwa “kuisaidia Polisi”, kwa nini watuhumiwa hawa hawajakamatwa? Au “kuisaidia Polisi” ni kwa watu wadogo tu? Kama ni hivyo uko wapi utawala wa sheria unaotaka sheria kuchukua mkondo wake sawa kwa watu wote, wakubwa kwa wadogo?
Mbali ya maswali hayo wengi wanataka kujua kwa undani huyu Ballali ni nani, ameingiaje katika tuhuma za sakata hii na huyu Jeetu Patel naye ni nani?
Daudi Ballali, mdogo kwa umbo na mtumishi wa zamani wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), ni Mtanzania aliyerejea nchini mwaka 1995 kama mshauri wa lkulu juu ya sera za IMF na Benki ya Dunia. Baadaye mwaka 1997, aliteuliwa kuwa Gavana wa Benki Kuu kuchukua nafasi ya Dk. Idris Rashid, ambaye sasa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme (Tanesco).
Katika nchi zenye sera za uchumi tegemezi kwa IMF na Benki ya Dunia mashirika hayo yana kauli kwa kiwango cha kutosha tu katika uteuzi wa Gavana wa Benki Kuu na hata Waziri wa Fedha kwa baadhi ya nchi.
Inasemekana Ballali ni mshirika au mmiliki wa makampuni ya biashara hapa nchini, Afrika Kusini, Dubai, Mauritius, Monaco, Switzerland na Washington. Wakati uteuzi wake wa nafasi ya gavana ukitenguliwa hivi karibuni, mshahara wake ulikuwa dola za Marekani 12,000, karibu sawa na shilingi milioni 15 kwa mwezi.
Sakata la ubadhirifu wa fedha za EPA linahusisha malipo kwa njia ya hati bandia kwa makampuni ya kimataifa na makampuni hewa. Makampuni ya kimataifa yanayodaiwa kulipwa yameonyesha kutokujua lolote juu ya malipo hayo, wala hayakutoa ridhaa kwa kampuni zake tanzu hapa nchini kulipwa jumla ya dola milioni 150 zilizoidhinishwa na BOT, (na si milioni 133 zinazotajwa mara kwa mara).
Tutaona baadaye katika makala chimbuko la baadhi ya makampuni haya yanayoelezwa kushiriki katika kashfa hiyo linalozua utata mkubwa juu ya madhumuni ya kuanzishwa kwake. Inaelezwa kwamba ingawa malipo haya ya dola milioni 150 yaliyofanywa kwa fedha za Kitanzania, “walipwaji” walizibadili kuwa fedha za kigeni katika maduka ya kuuza fedha hatua hiyo ikisababisha mzunguko mkubwa wa fedha nchini kiasi kwamba shilingi ya Tanzania iliporomoka kwa zaidi ya asilima 25 katika mwaka mmoja.
Katika hatua ya kushangaza Ballali alishauri Serikali, nayo ikakubali, kutoa dola zaidi kutoka EPA kuziingiza katika soko akifahamu athari za hatua hiyo kwa uchumi na ambayo inaweza kuwa iliwazesha “walipwaji” wa fedha huo za “madafu” kununua dola hizo na kuzitoa nje.
Jeetu Patel ana historia ndefu katika nyanja za biashara nchini. Alianza kama muuzaji wa vipuri vya magari jijini Dar es salaam mwaka 1978 chini ya kampuni ya kifamilia iliyojulikana kama Azania Investments and Management Service Ltd (AIMS). Yeye ni mfanyabiashara mkubwa wa kimataifa anayemiliki makampuni lukuki mengine yakijishughulisha na biashara tata.
AIMS ilivyozidi kupanuka aliingia katika kilimo kwa kuanza na shamba la hekta 1,500 Kimamba, wilayani Kilosa, Morogoro chini ya usimamizi wa kampuni tanzu ya Azania Agriculture akilima miwa, mahindi na tumbaku.
Mwaka 1980 alinunua hekta 22,000 kwa ajiri ya kilimo cha mkonge kutoka Mamlaka ya Mkonge (TSA) huko Mvomero, Kilosa na baadaye viwanda vya kusindika matunda vya Shirika la Usagishaji la Taifa (NMC) huko Korogwe.
Mbali na viwanda hivyo Patel pia alimiliki kampuni ya kutengeneza viatu ya Liberty Shoe Company na pia duka la vifaa vya mawasiliano, Electronic and Telecommunication Ltd., kampuni hizi zilikwisha kuvunjika zote.
Sasa Jeetu Patel ni kiongozi wa kundi la makampuni nchini lijulikanalo kama Noble Azania Group of Companies mengi yakituhumiwa katika sakata la BOT la sasa. Anadaiwa pia kumiliki kampuni London, Dubai, na anadhaminiwa kushikilia pasi za kusafiria nyingi kwa majina mbalimbali.
Jeetu Patel alikimbia Tanzania mwaka 1994 kuepuka kukamatwa kwa makosa ya jinai, alirejea nchini baada ya jalada la shauri lake kupotea. Yeye ni kati ya wamiliki wa benki mpya, Bank M Ltd., iliyoanzishwa hivi karibuni.
Chini ya sheria ya benki ya 2007, leseni ya kufungua na kuendesha benki haiwezi kutolewa kwa mtu mwenye historia au rekodi ya makosa ya jinai, kufilisika, kukosa uaminifu, au hujuma kwa Serikali. Lakini kwa kuangalia rekodi za makampuni haya na baadhi ya wamiliki wake, kuna wingu kubwa la giza kama kweli BoT imeruhusu na kutoa leseni kwa benki inayomilikiwa pia na Jeetu Patel.
Tuhuma nyingine zinazoelezwa kwa Ballali na washiriki wake ni pamoja na ufujaji wa fedha kwa mradi wa ujenzi wa ghorofa pacha za BoT, kampuni ya uchimbaji dhahabu ya Meremeta na kampuni ya ukaguzi mahesabu ya Alex Stewarts. Kwa vipi?
Inadaiwa kuwa ujenzi wa majengo pacha ya BoT utaingiza nchini hasara ya dola milioni 265, kutokana na gharama kuongezwa zaidi ya maradufu. Inaelezwa kwa mfano, kwamba wakati gharama ya ujenzi nchini ni dola 700 kwa mita ya mraba, ujenzi kwa BoT ni dola 8,625 kwa mita mraba ujenzi kama huo kwa miji ya New York na Tokyo hauzidi dola 2,000 pamoja na thamani ya ardhi.
Mradi huo umeghubikwa na tuhuma za rushwa tangu mwanzoni mwa mwaka 1978, chini ya mjenzi, kampuni ya Skanska, ambayo baadaye ilikasimu ujenzi huo kwa kampuni yake tanzu ya Group Five ya Afrika Kusini.
Kwa upande mwingine katika mlolongo wa tuhuma ndani ya BoT, kampuni ya Meremeta Gold ilianzishwa na kujihusisha na uchimbaji dhahabu mkoani Mara. Mwaka 1999 aliyekuwa gavana Daudi Ballali, kwa niaba ya Serikali, aliidhamini kampuni hiyo dhamana ya dola milioni 100.
BOT iliwekeza kwa kiwango kikubwa katika mradi huo kwa pamoja na wabia kutoka Afrika Kusini. Lakini habari zinasema kwamba baadaye wabia hao walichukua fedha zao zote baada ya kuuza hisa. Baadaye Meremeta ilitangaza kuwa mufilisi na hivyo ikabidi BoT ilipe dhamana ya dola milioni 132 za dhamana na riba.
Malipo mengine yalifanywa kwa kampuni ya Time Mining ambayo ilikuwa imeingia Meremeta kama mwedeshaji na ambayo inaelezwa kuwa ya Anna Muganda, mke wa Dk. Ballali.
Ni wakubwa ndani ya BoT na Hazina azina HHwalioajiri kampuni ya Alex Stewarts ya Washington, Marekani kukagua mahesabu ya mauzo ya dhahabu nchi za nje huku ikijulikana kwamba kampuni hiyo ilikuwa haijawahi kukagua kampuni za madini hata mara moja. Kwa bahati nzuri au mbaya, inaelezwa kuwa watumishi wa kigeni wa Alex Stewarts walikuwa ni wale wale waliofanyakazi kwenye kampuni ya Time Mining.
Kampuni hii ya ukaguzi ililipwa ujira wa asilimia 1,9 ya mirahaba ya asilimia 3.9 iliyokuwa ikilipwa Serikali na wawekezaji katika madini. Kwa hiyo Alex Stewarts walilipwa dola millioni 1.5 kwa mwezi dola million 18 kwa mwaka au dola million 72 kwa kipindi cha miaka mitatu cha mkataba kati yake na BOT kwa kazi iliyofanywa na wakaguzi watatu wa kigeni na watatu wa hapa nchini kiasi ambacho wataalamu wengi wanaona ni kubwa mara 30 kwa hadhi ya kampuni hiyo na kazi halisi iliyopaswa kufanywa.
Kama umma wa Kitanzania unaweza kuona na kupigia kelele maovu yaliyo wazi matumaini ya wengi ni kwamba jicho na mdomo wa Serikali unaweza kufanya makubwa zaidi katika kupata ukweli huo na kuchukua hatua zinazostahili ili kukomesha aibu hii kwa taifa. Na kama Tume iliyoteuliwa kuchunguza sakata hiyo itageuka ya fisi kumchunguza fisi, umma utatakiwa kufanya nini?
 
nakubalian na wewe kama bongo ni shamba la bibi,hawa wahindi hawakuanza kutuibia leo tangu enzi za mwalimu kwa sasa is enough
 
Wananchi wazalendo walivamia lile shamba la Kilosa maana lilishakuwa kichaka (forest) linahifadhi nyoka tu. Hilo sakata sijui liliishia wapi maana wananchi wenye nchia yao walitaka lirejeshwe kwa. Kazi ipo!!!!
 
unajua huwa haiingi akilini au ni suala zima la uzalendo limepotea kama kuna vielelezo na historia ya mtu inajulikana kwa nini wasiwajibishwe,?
 
Back
Top Bottom