Je Wewe Ni Mjasiriamali Au Mfanyabiashara Mdogo? Soma Hapa Kujua.

Makirita Amani

JF-Expert Member
Jun 6, 2012
1,877
3,307
Tokea kuanza kutumika sana kwa neno ujasiriamali na mafunzo mengi ya ujasiriamali kutolewa, kila mtu anayefanya biashara ya aina yoyote anajiita mjasiriamali. Hata mtu mwenye biashara yake ambayo ameendesha kwa miaka mitano na bado iko vilevile anajiita mjasiriamali. Kumekuwa hakuna tofauti kubwa kati ya mjasiriamali na mfanyabiashara(hasa mfanyabiashara mdogo).
Japokuwa hakuna ubaya kuwa mjasiriamali au kuwa mfanyabishara mdogo ni vyema kuzijua tofauti na kujijua uko wapi kwa sababu hii ina matokeo makubwa katika mafanikio. Ni muhimu sana kujua upo katika kundi gani ili pia kujua ni jinsi gani unafikia mafanikio.
Zifuatazo ni baadhi ya tofauti kati ya mjasiriamali na mfanyabiashara mdogo.
1. Msukumo wa kufanyanya biashara.
Japokuwa mjasiriamali na mfanyabiashara wote wanaweza kuwa wanafanya biashara ila wana misukumo tofauti. Mfanya biashara anasukumwa na kutengeneza faida kutokana na biashara anayofanya wakati mjasiriamali anasukumwa na kuleta mabadiliko au kutatua tatizo kubwa ambalo linawasumbua watu. Wote wanaishia kuwa na biashara zinazotengeneza faida.
2. Malengo makubwa ya mbeleni.
Wafanyabiashara wadogo hawana malengo makubwa ambayo wanayaishi kila siku. Ndio maana unakuta wengi wako na biashara moja ambayo haibadiliki kwa miaka mingi. Wajasiriamali wanakuwa na malengo makubwa sana na biashara zao na baada ya muda fulani biashara zao zinakuwa kubwa sana.
3. Kujitegemea kwa biashara.
Wafanyabiashara wadogo ndio kila kitu kwenye biashara zao. Hufurahia kusimamia au kuendesha biashara zao wenyewe na kujua ziko salama chini ya mikono yao au familia zao. Wajasiriamali hujipanga biashara zao kuweza kuendeshwa bila ya wao kuwepo moja kwa moja. Wajasiriamali hufurahia biashara inapojiendesha wenyewe na wao kuwa wasimamizi tu.
4. Kupenda hali hatarishi(Risk)
Wafanya biashara wanaogopa sana kufanya maamuzi ambayo ni hatarishi na yanaweza kuepelekea kupata hasara kubwa, wako makini sana kwenye faida na hasara na kujaribu kwa kila hali kuepuka hasara. Wajasiriamali wanapenda kufanya maamuzi hatarishi ambayo yanaweza kuwapelekea kufanikiwa au kushindwa, wanajua maamuzi ya aina hii ndio yanayowezesha biashara kukua kwa kiwango kikubwa sana.
5. Ubunifu na kuiga.
Wafanyabiashara wadogo wana ubunifu kidogo sana na wakati mwingine hakuna kabisa. Wanafanya biashara ambayo watu wengine wanafanya na imeshaonesha kuleta faida. Wajasiriamali hupenda kufanya mambo mapya ambayo huenda hata hayajafanyika ili kutoa suluhisho la matatizo ya watu. Hata pale wanapofanya kitu ambacho tayari kinafanywa hupenda kuweka ubunifu mkubwa ili kuwa tofauti na bora zaidi ya wengine wanaofanya wanachofanya.
Kwa tofauti hizo wewe upo kundi gani? Mjasiriamali au mfanyabiashara mdogo? Usione haya kujikuta wewe ni mfanyabiashara mdogo wakati ulifikiri ni mjasiriamali. Hakuna ambao ni bora zaidi ya wengine, tunawahitaji wote katika maisha yetu ya kila siku na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Ni vizuri kujua kundi ulilopo ili kuweza kuweka malengo yanayoendana na kundi lako. Kama nia yako ni kuwa mjasiriamali basi ufikiri na kutenda kijasiriamali zaidi.
Nakutakia mafanikio kwenye jambo lolote unalofanya kwenye maisha yako.
Kumbuka TUKO PAMOJA.
 
Back
Top Bottom