SoC01 Je, Watanzania wataajirika nje ya mipaka kama wakifundishwa kwa Kiswahili tu?

Stories of Change - 2021 Competition

Filosofia ya Rorya

JF-Expert Member
Sep 20, 2021
3,215
3,587
Nyanja: Haki za Binadamu


OIP.0tcudqXBph0nC6dfL94kEAHaEK

Taswira kwa hisani ya:
Mabadiliko ya sera ya elimu ya Feb 2015 yanalenga matumizi ya lugha ya taifa Kiswahili kuwa ndiyo lugha ya kufundishia kwy taasisi zote za elimu. Hii ni sahihi kabisa na nia ni njema sana na wanafunzi walifurahia sana mabadiliko haya. Lakini pia, wanafunzi hawakustahili kufurahia mabadiliko haya na kuyashangilia bila kuyapembua kiyakinifu kwanza, maana yana gharama kubwa kwao kwa namna mbalimbali na kwa vizazi vyao pia. Wapo wanaoyashangilia kuwa sasa wataepukana na ugumu wa lugha ya Kiingereza! Kwa hakika huku ni kupotoka na kuota ndoto za adhuhuri kabisa, ukweli ni kuwa Kiswahili kitakachotumika siyo Kiswahili rahisi kama wanavyotarajia bali ni kile kigumu kama kilivyo Kiingereza.

Mfano mdogo tu ni kuwa hivi sasa kuna misamiati ya Kiswahili inayozuka [maana Kiswahili bado kinakuwa kutokana na mabadiliko ya kasi ya mfumo wa maisha ya dunia] ambayo ni migumu kuielewa na inaacha hatari ya kupotosha maana na mantiki ya ujumbe unaotolewa kupitia kwazo. Angalia misamiati kama hii hapa chini na ujiulize kama leo ikitungwa kwy mtihani wa Kiswahili ni wanafunzi wangapi wanaelewa maana zake: mtambuka, maduhuli, voti, kuhawilisha, ombwe, nguli, bangokitita, udakuzi, durusu, durufu, urari, kuchakata, ithibati, dahili, nakisi, mustakabali, muamala, ukokotoaji, taathira, jaramba, utakatishaji [siyo maana yake ile tuliyozoea ya usafi], kuna mwingine leo ukimwambia shida yako ipeleke kwa Kabidhi Wasihi Mkuu bila shaka atakuuliza kuwa akifika stendi ya mkoa apande basi la kwenda mkoa gani? Yaani hajui maana ya Kabidhi Wasihi Mkuu!

Zaidi ni pale ambapo hata semi za Kiswahili kama nahau zinapojikita sehemu moja tu ya kijiografia na kueleweka huko lakini zisieleweke sehemu nyingine ya kijiografia ambapo mazingira yanatofautiana kwa mbali, mfano achilia mwanafunzi tu, tuchukulie hata waangalizi wa elimu wenyewe kama Afisa Elimu wa kule Katavi ambaye hakupata kusoma shule mazingira ya pwani umuulize akufafanulie maana ya Mgaagaa na upwa hali wali mkavu, naamini atapata sifuri, lakini siyo kosa lake maana hajazaliwa, hajafanya kazi wala hajasomea pwani ambako kuna bahari. Mimi mwenyewe nimekuja kuelewa tafsiri ya nahau hii baada ya kufika Dsm mwaka 1989 na baada ya kulazimisha sana kupelekwa kuzuru ufukweni ambapo nilikuta maji ya bahari yamekupwa na kuacha nafasi ambapo watu walikuwa wakigaagaa [wakirandaranda] na pakacha wakiokoteza vidagaa, kauzu, kaa nk vilivyoachwa na maji yaliyokupwa, ndipo nikagundua kuwa wanaokoteza kwa ajili ya mboga, nikaunganisha na nahau hiyo kufuatia ukweli kwamba Dsm wali ni chakula kikuu, hivyo anayegaagaa na upwa akirudi nyumbani atakuwa japo na kauzu wa kuandaa mchuzi wa kulia wali, hivyo hatakula wali mkavu.

Kutokana na kuwa Kiswahili bado kinakuwa, kuna hatari ya wanafunzi kuingiza misamiati ya kihuni ya kuchafua ubora wa lugha siyo kwa makusudi bali kwa kutokujuwa tu; misamiati ambayo ama haipo kwy kamusi ya Kiswahili fasaha na wala haijafanyiwa tafiti na taasisi za Kiswahili, hali hii inaweza kuhujumu matokeo ya mitihani ya taifa.

Ikumbukwe kuwa wakati wa utawala wa Nyerere kulikuwa na kozi ya Kiswahili kigumu ambacho ili mtumishi wa umma aweze kustahili kupanda daraja; ambalo liliambatana na maslahi bora, hakuwa na budi kwenda kujifunza kozi ya Kiswahili kigumu kwanza na kufuzu na kutunukiwa cheti kwy vyuo vya utumishi wa umma kama Magogoni na Tabora, jambo ambalo leo halipo kabisa na kusababisha kuwa na viongozi ambao ni wachafuzi wa Kiswahili kwy majukwaa ya hotuba.

Japo Kiswahili ni bidhaa ambayo tunaweza kuiuza katika soko la kimataifa kama bidhaa zingine zinazozalishwa Tz, ukifanya uchunguzi makini kwa kurejea hotuba zote za safu ya urais wa nchi yetu utabaini kuwa ufasaha na ubora wa Kiswahili kwy hotuba za viongozi wa taifa hili uliishia kwa rais Mkapa kuanzia kwa rais Nyerere akifuatiwa na rais Mwinyi basi, huku safu ya urais kwa upande wa Tz visiwani ubora na ufasaha huo kwy hotuba za viongozi wakuu wa dola umeendelea kuenziwa tangu zama za rais Abeid Karume hata sasa.

Ugumu wa Kiswahili pia utaletwa na maingiliano ya lugha mbalimbali za kibantu katika lafudhi [accents], fonimu [phonemes], misamiati [vocabularies], istilahi [terminologies] hali ambayo hata sasa tayari tunaishuhudia kwa kuwa na viswahili vya kikanda mfano kuna Kiswahili cha Kikongo, cha Kipemba, cha Ki-tanga cha Shaaban Robert, cha Kiunguja cha akina Thabit Kombo na Adam Shafi, cha Mwambao, cha Kiarami, cha Kikenya-Mombasa, cha bara, cha Kingazija nk.

Pia kama mabadiliko ya sera ya elimu katika lugha ya kufundishia yatatekelezwa, basi kuna hatari ya wahitimu kutoajirika kabisa nje ya eneo fulani la Kiswahili cha kikabila au cha kikanda ambako mhitimu atakuwa ameandaliwa kwa kuzingatia lafudhi, fonimu, misamiati, istilahi za eneo husika, tofauti na Kiingereza ambacho kwa sehemu yake kubwa hakina mabadiliko ya kutisha ya istilahi na misamiati isipokuwa tu utofauti kidogo wa lafudhi na fonimu ambazo hata hivyo bado hazijaleta ugumu wa mawasiliano, mathalani Kiingereza cha US hakipishani sana na kile cha UK, Ireland, Canada, Zim, Nigeria, A/Kusini nk.

Ninachambua hili nikitambua kwa dhati kabisa umuhimu wa kuenzi Kiswahili kama bidhaa na tunu ya taifa letu tukizingatia kuwa mataifa kama Ufaransa, UK, US, Urusi, Uchina, Japani, nchi za Kiarabu nk yamepata maendeleo kwa kutumia lugha zao za taifa, lakini kwa Tz tulikengeuka na madhara ya ukoloni wa lugha tukapunguza uwekezaji wa kukiendeleza Kiswahili chetu [kazi ambayo Nyerere aliifanya kwa dhamira kubwa kabisa lakini waliomfuata wakaelemewa na athari za ukoloni wa lugha]; tukakumbatia lugha za kikoloni kama Kiingereza, Kifaransa, Kiarabu, Kireno, Kiispanola na sasa kuna uwezekano mkubwa kuwa maingiliano haya ya kasi kubwa ya kutisha sana baina ya Uchina na nchi za dunia hakika yataendeleza ukoloni ule ule wa lugha za kigeni kwa kutulazimisha kujifunza Kichina kama ambavyo tunafanya kwy Kifaransa, Kiarabu nk. Hali hii itasababisha Kiswahili ambacho bado ni maskini wa misamiati ya kufundishia taaluma mbalimbali kuazima misamiati toka lugha za kigeni [loanwords] na kuvuruga asilani mfumo wa isimu katika voweli na consonanti kwa kuzusha diphthongs, monophthongs na triphthongs. Wangapi wanajuwa: Tafsida, Tashbiha, Sitiari, Mubaalagha, Mdokezo, Takriri, Tashtiti, Onomatopea/tanakali sauti

Wakati Nyerere anang’atuka uongozi, alitoa wosia wa mambo makuu manne yaliyomsaidia kudumu kwy uongozi nayo ni: Kiswahili [kilimsaidia kuunganisha watu wa lugha mbalimbali za makabila tofauti], jeshi, ukweli na itikadi ya ujamaa na kujitegemea ambayo alisema ujamaa umekufa lakini kujitegemea kunaendelea. Aidha kuna tabia inaota mizizi taratibu kwy jamii yetu kuwa baadhi ya wataalamu wetu wamejijengea tabia ya kujinasib na tafiti wanazofanya kujipatia tuzo za heshima tu [titles] na siyo kutafsiri matokeo ya tafiti hizo katika uhalisia wake ili kutoa majibu sahihi kwa matatizo ya jamii, hali hii inaweza kulipeleka taifa kusiko kama Ugiriki ambayo inaaminika kuwa ndiyo chanzo cha ustaarabu duniani na ni ya kwanza kuzalisha wanafalsafa waliobobea na kwa idadi kubwa ambapo kuna falsafa zilizotungwa na wasomi ambao wengine wao elimu zao hazikuwahi kuzidi kiwango cha shule ya msingi au upili lakini falsafa zao zimedumu kwa nguvu na umri mkubwa hata leo na zimetumika kuzalishia maprofesa wanaoheshimika duniani, lakini leo Ugiriki ina hali ngumu kuliko taifa lolote duniani ukiachilia yale yenye vita. Katika kila fani ya masomo chini ya jua ikiwemo theolojia lazima utakutana na misamiati na misemo ya Kigiriki. Shime tusije tukaua Kiswahili kama Kiyunani kilivyokufa.

Ni dhahiri kabisa kuwa hatujajiandaa vya kutosha kutekeleza mabadiliko haya ya ghafla sana, mfano tu ni kuwa, tumetanuaje bajeti za wizara ya elimu ili kuandaa rasilimaliwatu yaani walimu wa Kiswahili, upatikanaji wa vitabu vya kiada na ziada [ilhali nchi yetu haina waandishi wengi maana soko la uandishi wa vitabu halilipi kama sanaa ya muziki na maigizo inavyolipa; kutokana na kuwa Watz hawana utamaduni wa kujisomea vitabu, ambapo nafikiri kuna haja ya kuruzuku waandishi wachache waliopo na kuwavutia wengine ili waandike], taasisi ya ukuzaji mitaala, taasisi za Kiswahili kwa ajili ya kutanua na kuendeleza tafiti za Kiswahili ndani na nje ya mipaka ambako hivi sasa Kiswahili kinafundishwa takriban vyuo 100 duniani vinavyopatikana katika mabara yote.

Ni afadhali tungeanza na mradi wa majaribio kwanza kwa baadhi ya shule na vyuo kwa muda fulani ili kuona faida na hasara za mabadiliko haya kabla hatujaanza kuyasambaza nchi nzima, ni afadhali madhara ya utekelezaji wa mabadiliko haya yawaangamize wachache ambao wangeweza kuwekwa kwy mradi wa majaribio kuliko yakiangamiza taifa zima kama yakitekelezwa nchi nzima kwa wakati mmoja.

Tukumbuke lugha ni chombo cha mawasiliano ambacho asili yake ni Mungu pekee ndiye ajuaye kama tunavyosoma mashuleni kuwa lugha ni sauti za nasibu zilizozuka tu bila kupangiliwa wala kutarajiwa lakini ambazo hizo zinaleta maana au uelewa, hakuna anayempeleka mtoto wa umri wa mwaka mmoja na nusu kusomea lugha inayotumika kwy familia yake ili aweze kuwasiliana bali huwa anaiga, anasikiliza na zaidi lugha humuijia kama nasibu. Nachelea kuamini kuwa wote wanaohusika na kuasisi mabadiliko haya ya sera ya elimu kwy lugha ya kufundishia wanakusudia kufanya ujenzi wa mama yetu Tz uingie matatani kama ujenzi wa mnara wa Babeli ambao ulisambaratika kufuatia Mungu kusambaratisha lugha ya taifa la Babeli kama njia ya kuzuia mnara usiendelee kujengwa kumfikia yeye maana hiyo siyo njia aliyoagiza ya watu kumuendea isipokuwa kwa njia ya Yesu pekee, yumkini mnara ungefanikiwa kujengwa hadi Mbinguni wenye dhambi nao wangeukwea na kuingia Mbinguni kirahisi.

Je, mabadiliko haya ya sera ya elimu ya Feb 2015 kama yalivyotangazwa na serikali yetu ni homa ya uchaguzi? Mungu ondoa boriti kwy macho ya serikali ya awamu ya 6 ili ione hili kama ambavyo uliondoa kibanzi kwy macho ya serikali ya awamu ya 4 ikaona mapungufu ya mabadiliko ya mitaala ya elimu yaliyoasisiwa na serikali ya awamu ya 3.

Naomba kura yako.
 
Back
Top Bottom