#COVID19 Je, Watanzania tuchanje mvua au tuote jua? By Dr. Ally Mahadhy (PhD) - UDSM

Pascal Mayalla

Platinum Member
Sep 22, 2008
39,554
2,000
Wanabodi,
Hii ni C&P, kwa msaada wa Classmate wangu ambaye ni dakitari, kanimegea toka group lao la madakitari.

Karibu.

Paskali

TUCHANJE MVUA AU TUOTE JUA?

Imeandikwa na Dr. Ally Mahadhy (PhD) - UDSM.

Ugonjwa wa kirusi cha korona (COVID-19 au UVIKO-19), kwa mara nyengine tena unaku wa ni ugonjwa ulioleta sintofahamu kubwa kwenye jamii. Kwa hapa kwetu Tanzania sintofahamu ilianzia kwenye ujio wake, kuna watu wengi waliamini ni COVID -19 ni ugonjwa wa washua (matajiri), wanaopanda ndege na kusafiri nje ya mipaka ya nchi, walala hoi na wasiosafiri hauwahusu! Sintofahamu ikaibuka tena kwenye upimaji wake, mara mapapai, mbuzi na mafenesi tukaambiwa nayo yamepelekwa maabara yetu ya taifa kupimwa na yakaonekana na UVIKO-19! Hii ikawa habari kubwa sana, habari ilotawala vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi. UVIKO-19 bado hakuishia hapo, sasa imetuletea sintofahamu ya chanjo! Sintofahamu hii ni sintofahamu ya dunia, mkanganyiko ulioikumba jamii. Katika hili la chanjo, kuna wenye mashaka, kuna wanao shangaa, kuna waliohamanika, kuna walozubaa, kuna waliopumbazwa, kuna waliohamaki, na kuna waliofurahi.

Swali ni jee tuchanje au tusichanje?

Kabla sija jibu swali hilo (au kutoa manoni yangu) naomba nitangaze maslahi yangu binafsi kwenye swala husika. Mimi ni mtaalam na mtafiti kwenye nyanja ya bayoteknolojia (Biotechnology) mwenye shahada ya uzamivu (PhD) ya uhandisi wa kibayolojia (Bioengineering). Nimejikita kwenye kufatifi, kutengeneza (development) na kuhariri vitendanishi (diagnostic devices) vya vimelea (pathogens) vya magonjwa na viashiria vya kibayolojia (biomarkers). Mimi ni mwajiriwa wa Chuo Kikuu cha Dar es Saalaam (CKD), Idara ya Molekyuli ya bayolojia na bayoteknolojia (Molecular biology and Biotechnology). LAKINI maoni yangu katika andiko hili hayahusiani kwa namna yoyote na mwajiri wangu (CKD), wala hayahusiani na kampeni ya shirika, kikundi au chama chochote juu ya chanjo ya UVIKO-19.

Katika sintofahamu hii juu ya chanjo ya UVIKO-19, kuna hoja za msingi na rejewa ambazo zimejitokeza. LAKINI kiujumla hoja zote zinagusia USALAMA (safety) wa chanjo, hoja kubwa ni: muda wa chanjo (muda mfupi sana); na madhara ya chanjo (kuna wanaoripotiwa kudhurika). Ila pia kuna hoja nyengine zinaibuka hapa na pale kwa lengo la kukoleza (cementing) msingi wa hoja kuu ya USALAMA WA CHANJO; mfano wapo wanaohoji kwanini iwe bure ikiwa panadoli tu tunauziwa? Kwanini tujaze fomu ya kukubali kuchanjwa (consent form) mbona chanjo nyengine hatujazi fomu? Mbona ulaya wanaandamana kupinga chanjo? Na mfano wa hoja hizo.

Ingawa kuna wataalam mbali mbali wamejitokeza kujibu hoja hizi kupitia njia tofauti, ila nikiri kwamba bado majibu au elimu hii haijawafikia walo wengi. Hii inafanya uwepo wa ulazima kwa wenye ufahamu juu ya chanjo hii kwa nafasi zao kutoa elimu kadri wawezavyo. Kwa ulazima huo huo namimi naomba nitoe maoni yangu kama ifuatavyo. Nitaaanza kwa kujibu hoja kuu mbili zilizojitokeza nazo ni: muda mfupi wa chanjo, na madhara ripotiwa! Pengine pia ntagusia na zile hoja kando kando.

Kwanini chanjo hizi zimechukuwa muda mfupi sana?

Kuna uzoefu kwamba kutengeneza chanjo au dawa mpya (vaccine or drug development) kuna hitajika miaka 10 hadi 15 hadi iweze kutumika kwa usalama na uhakika. Hii ni kutokana na hatua inazopitia, kuanzia ugunduzi na kutengeneza ndani ya maabara (discovery, development and pre-clinical trial), na wakati wa majaribio (clinical trials) ambayo hatua hii na yenyewe ina hatua hadi tano (phases 0 – IV), kwa pamoja kikawaida mpaka kukamilisha mchakato huu ni mika 10 hadi 15!

Jee kwanini chanjo ya UVIKO-19 imekuja “fasta” hivi? Ni salama kweli?

Kwanza nianze kwa kuweka wazi kwamba hakuna sehemu yoyote inayoitaka/lazimisha ili chanjo au dawa iweze kutumika lazima iwe imechukua miaka 10 hadi 15 kufanyiwa utafiti. Hii miaka 10 hadi 15, ni kutokana na uzoefu sio sheria wala kanuni! Uzoefu huu ni umepatikana kutokana na teknolojia na mazingira ya wakati husika (kipindi hicho). Hivyo basi kama mazingira na teknolojia yataruhusu kupatikana chanjo au dawa hata ndani ya wiki na mamlaka husika zikajiridhisha juu ya usalama na ufanisi wa chanjo au dawa husika, basi itatumika! Muda sio kigezo, kigezo ni uthibitisho wa kisayansi kwamba chanjo ni salama na ina ufanisi!

Kiulimwengu na kitaalamu kuna sababu (factors) nyingi zinazofanya ugonjwa upatiwe chanjo au dawa ya haraka, hapa ntazitaja chache na muhimu:
1. Ukubwa wa tatizo (disease incidence, severity and prevalence)
2. Uelewa juu ya (sayansi ya juu ya) kimelea husika cha maradhi hayo
3. Uwepo wateknolojia inayo saidia (support) utengenezaji wa chanjo husika
4. Maslahi katika uwekezaji (return on investment) kwenye chanjo husika

Nikianza na sababu ya kwanza ni wazi kwamba UVIKO-19 ni janga la dunia, limegusa nchi zote, tajiri sana, tajiri, maskini na hata maskini sana. Sio kama yalivyo maradhi kama malaria, ukimwi (HIV-AIDS), au kipindupindu ambayo yanajuliakana kama maradhi ya nchi maskini (Poverty Related Diseases). Hivyo ukubwa wa UVIKO -19, ambao umeathiri uchumi wa nchi tajiri na kuangamiza ule wa nchi maskini, umefanya wataalamu wa ulimwengia kuingia kazini kutafuta suluhisho. Uwekezaji huu mkubwa na wapamoja wa utaalam (intellectual investment) na kifedha, bila shaka umechangia kwa kiasi kikubwa katika upatakinaji wa haraka wa chanjo. Maana ugonjwa huu unagusa maslahi ya wakubwa (nchi tajiri) moja kwa moja!

Pia ieleweke kwamba kirusi cha KORONA (corona virus) si kigeni kihivyo, kama ambavyo hivi karibuni wataalamu mbali mbali wamekuwa wakieleza. Dunia ilishawahi kupigwa na kirusi cha korona kabla ya huyu wa 2019! China, Taiwan na Canada ni baadhi ya nchi zilizokumbwa na kirusi cha Korona aina ya SARS 2002- 2004; na baadae akaja dada yake SARS ajulikanae kama MERS kule Saudi Arabia 2012! Hivyo kuanzaia 2002 hadi 2019 yaani takribani miaka 17 tangu ajulikane SARS hadi alipokuja kaka yake, SARS-COV-2 (anaesababisha UVIKO-19), wataalamu (wanasayansi) walishakuwa na uelewa wa kutosha juu ya kirusi huyu wa KORONA! Ujio wa SARS-COV-2 haukuwakuta wanasayansi kwenye mshangao, bali kwao ilikuwa ni ku-upgrade tu uelewa wao. Ndo maana katika kipindi cha muda mfupi sana, tayari kulishapatikana vitendanishi vya haraka (rapid tests) za kila aina, na vile vya kijenetiki (mfano PCR based tests), vya kila aina (ingawa cha ajabu kwa hili hatukuhoji vyereje vipimo (tests) vipatikane haraka?)! Kutengeneza chanjo kunategemea kwa kiasi kikubwa jinsi unavyokijua kimelea kinachosababisha ugonjwa – uwelewa wake ki-immunolojia na ki-jenetikia unarahisisha upatikanaje wa chanjo salama na fanisi! Hivyo basi uwepo wa uelewa wa KORONA aina ya SARS na kumefanya kuwepo na njia za kumuelewa SARS-COV-2 kwa haraka kumesaidia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa chanjo ndani ya muda mfupi,chini ya makadirio ya ki-uzoefu.

Nikielezea sababu ya tatu ya UWEPO wa TEKNOLOJIA SAIDIZI; ni muhimu kuelewa kwamba ulimwengu wa teknolojia unaenda kasi sana, sio tu kwenye teknolojia ya mawasiliano na habari bali hata huku kwenye teknolojia ya uhandisi wa kibayolojia (bioengineering)! Wakati ule chanjo ilikuwa ikichukua miaka 15 hadi kukamilika, bado ‘nanotechnology’ na matumizi ya seli shina (stem cells) kwenye kutengeneza chanjo na dawa ilikuwa ni elimu ya nadharia! Ahsante kwa teknolojia hizi, hivi sasa si hadithi tena, ni matumizi halisi. Matumizi ya ‘nanoparticles’ kwenye chanjo yanasaidia ufanisi na usalama wake katika utendaji kazi, hivyo kufupisha muda unatumika katika kujaribu njia mbali mbali za majaribio katika kuifanya chanjo iwe na ufanisi. Vile vile muda unafupishwa sana katika hatua ya kuelewa USALAMA wa chanjo na ufanisi. Awali ilikuwa chanjo ikisha jaribiwa usalama wake kwa wanyama wasio binaadamu (mbao haihakikishi sana usalama kwa binaadamu) chanjo hiyo ilikuwa lazima ijaribiwe kwa idadi ndogo ya binaadamu ili kuelewa usalama wake, kabla ya kwenda kwa idadi kubwa na kubwa zaidi! Hivi sasa, kwa uwepo wa matumizi ya seli shina (stem cell technology) za binaadamu, inawezesha kuelewa USALAMA wa chanjo kwa binaadamu halisi bila kuwepo binaadamu mwenyewe (wote)! Seli shina hizi za binaadamu hutoa taswira halisi ya jinsi chanjo itakavyokuwa inafanya kazi na athari zake ndani ya mwili wa binaadamu. Hivyo pia teknolojia hii imesaidia sana kufipisha muda wakutengeneza chanjo ya UVIKO-19, chini ya muda wa uzoefu! Pia teknolojia za uzalishaji wa chanjo (vaccine manufacturing platforms) zilikuwepo kwa muda mrefu (zimekuwa zikitumika kuazalisha chanjo za magonjwa mbali mbali ya virusi kama mafua ya ndege n.k), hivyo uwekezaji katika uzalishaji wa chanjo ya UVIKO-19 viwandani haukuwa mkubwa wala kuhitaji muda mrefu. Hii imesaidia uzalishaji (mass production) wa haraka.

Uzalishaji wa chanjo ni uwekezaji, tena uwekezaji mkubwa sana, wa kifedha na ki-utaalamu! Tuelewe kwamba BAYOTEKNOLOJIA ni BIASHARA pia (Entrepreneurship in Biotechnology). Hakuna anaekeza ambako hakuna faida! Tukubali tukatae, UVIKO-19 ni hasara na majanga kwa wengine, LAKINI pia ni FURSA pia kwa wengine (ikiwemo Biotech industry). Kuwekeza mabilioni ya dola kwenye kutafiti na kutengeneza chanjo ya magonjwa ya nchi maskini kama malaria, kipindupindu na HIV- AIDS ambayo wateja wake ni hao nchi masikini, ni kujitaftia hasara! Kwa hiyo usishangae chanjo ya maradhi hayo kufika hiyo miaka 15, maana pamoja na sababu nyengine za kitaalamu, lakini pia SIO 'of their interest’ kihivyo! ILA hii chanjo ya UVIKO-19 ‘market share’ yake ni kubwa sana, uwekezaji wake unalipa, wanunuaji ni nchi tajiri na masikini. Hivyo usilinganishe uhitaji wa chanjo hii na ile ya kipindu pindu wala HIV-AIDS katika uwekezaji! Wawekezaji na watafiti wamewekeza kadri wawezavyo katika kupata chanjo UVIKO-19 kwa muda mfupi, muda mfupi chini ya kadirio la ki-uzoefu.

Mbona kuna wanaoripotiwa kupata madhara?

Kwanza ni kuhakikishie kwamba hakuna chochote hapa chini ya jua ambacho hakina madhara, sumbuse chanjo!!!! Chanjo hizi za UVIKO-19 kabla ya kuruhusiwa kutumika zina hakikiwa usalama wake na mamlaka husika za ki-taifa na kimataifa, likiwemo shirika la afya duniani (WHO) ambalo kazi yake kubwa ni kusimamia na kulinda afya ya binadaamu. Hivyo basi chanjo hizi hadi zimetufikia sisi kwa matumizi ni kwamba zimeshathibitiswa USALAMA wake na wataalam! Ama swala la uzio (allergy) au madhara yasiyotarajiwa (side effects) ni swala la kipekee na tatizi (complex) sana, huwezi kutoa maamuzi ya kukataa chanjo kwa sababu tu kuna watu wachache walipata uzio (allergy) au madhara baada ya kuchanjwa! Jee wajua kwamba kuna zaidi ya watu 68 katika kila watu 100 hapa duniani wanadhurika (people with lactose intolerance) wakinywa maziwa fresh ambayo hajaondolewa sukari aina ya lactose; jee ulishawahi kuwaza kususia maziwa? Jee wajua kwamba si kila atakae kula karanga yu-salama? Anagalu kila mtu 1 katika kila watu 100 akila karanga anadhurika (uzio). Kwani pia si wapo wanadhuriwa (side effects) na paracetamol (Panadol), dawa mseto (ALU) za malaria, azithromycin (na antibiotics nyengine), lakini wewe na sisi wengine wengi tu zinatuponesha na tusalama! Hivyo hata kama chanjo hii ingejaribiwa kwa miaka 100 kwa zaidi ya nusu ya watu duniani, bado wangetokea ambao chanjo hii ingewadhru …kila mtu ana uzio (allergy) ya kitu flani (hata vitu flani) ni vile tu hujakutana nacho bado! Mpaka sasa dawa na chanjo zote zinatengenezwa kwa mtindo wa 'free size' , yaani saizi moja inawafaa wote (one size fits all)! Ila kwa sababu ya uwepo wa baadhi ya watu kuitika tofauti katika matibabu au chanjo hiyo hiyo moja, wataalamu sasa wameanza juhudi za kuipeleka fani ya utabibu kwenye 'personalized medicine', yaani baadae tutakuwa tunapata tiba (dawa na chanjo) kulingana na jenetiki za kila mmoja wetu! Ila kwa sasa ni mwendo huu wa 'one size fits all'! Hata hivyo walioripotiwa kudhurika kwa chanjo ya UVIKO-19 ni wachache mno ya wale walochanjwa ambao wapo salama na chanjo imewasaaidia kupambana na UVIKO-19. Mfano, nchini Marekani pekee inaripotiwa kwamba mpaka kufika April 2021, zaidi ya watu milioni 8 walikuwa wameshapatiwa chanjo ya Johnson & Johnson’s Janssen (J & J/Janssen), katika hao ni watu 15 tu ndo waliripotiwa kupata tatizo la kuganda damu (kwa mujibu wa Centers for Disease Control and Prevention, CDC), ambayo idadi hiyo ni chini ya 0.0002 % (yaani watu 2 katika kila watu milioni moja (1,000,000)) ya waliochanjwa. Ijulikane pia watu hao walioriporiwa kupata madhara wengi wao tayari walikuwa na maradhi mengine na ni wazee! Kwa data hizi ni dhahiri hii chanjo ni SALAMA kuliko kutokuchanjwa!

Kwanini ni iwe salama kuliko kutokuchanjwa?

Jambo moja la msingi ni kwamba (karibia) sote tunakubali kwamba UVIKO-19 ipo! Ipo na ukiipata inatesa kimwili na kiakili (saikolojia), inasumbua, inafilisi, hata kuuwa! Wale walowahi kuumwa, wakawekewa mitungi ya gesi, kisha wakapona wanalo lakuhadithia, ni balaa usiombe upitishwe huko. Wale walopoteza wapendwa wao kwa UVIKO-19 wanalo lakusimulia, ni hudhuni usiombe ikukute…! Ni kweli kuchwanjwa hakuku hakikishii kwa asilimia 100 kwamba hutaumwa UVIKO-19, ila Kuchanjwa kuna kuhakikishia kwa asilimia kubwa kwamba hutoumwa UVIKO-19 hasa wa hizi aina zilizopo sasa. Nikama vile usivyouliza kwanini nivae helment (kofia ngumu) wakati wapo wanaopata ajali na helment zao kichwani kisha wanavunjika vichwa, au usivyouliza wakati unafunga mkanda wa gari wakati wapo wanaopata ajali wakiwa na mikanda wamefunga na wanarushwa kupitia kioo cha mbele ya gari, au unapobeba mwevuli mvua ikinyesha na bado wapo wanaorowana kwa upepea wa mvua, au kuvaa mpira wakati tendo la ndoa, na bado wapo wanaopata maradhi ya zinaa na mipira ikiwa imevaliwa….huulizi kwa sababu zote hizo kinga, hakuna kinga ya 100 %, ila pia huwezi kuacha kinga kwa kuwa tu wapo walodhurika japo walikuwa na kinga. TWENDE TUKAPATE KINGA, tujiongezee uhakika wa kutokuumwa na UVIKO-19, tusipopata kinga tunajiweka kwenye hatari kubwa ya kupata UVIKO-19! Avukae bara bara akiwa amejifunika macho kwa kitambaa na yule avukae kwa tahadhari zote huku macho yake yakiwa wazi (hayajafukiwa) panauwezakano wote wakavuka salama, ILA najua kamwe hutajaribu kuziba macho kwa kitambaa kisha uvuke bara bara, maana una nafasi chache ya kuvuka salama! Basi usijaribu kuacha kuchanja kwa maana hutakuwa na tofauti na avukae barabara huku kafunika macho yako.

Kwanini tupewe bure?

Kwani dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI unauziwa? Si vinatolewa bure! Au unadhani ni rahisi kuliko Panadol? Kwani chanjo ya TB na polio na nyengine nyingi unalipia? Hivyo basi chanjo ya UVIKO-19 kutolewa kwake bure hakupunguzi usalama wala ufanisi wake…TWENDE TUKACHANJWE!

Kwanini tujaze fomu ya kukubali kuchanjwa, serkali inajitoa lawama?

Ridhaa (consent) ya mgonjwa ni sehemu muhimu katika maadili ya kitabibu (respect for autonomy), mara zote unapohudumiwa hospitalini au kwenye kituo cha afya umekuwa ukiulizwa ridhaa yako. Riadhaa hii inaweza kuwa ya maandishi au maneno, kwa mfano Daktari (mganga) kabla hajakuwekea ‘stethoscope’ kupima kifua chako, huwa anakuomba wewe mwenyewe ufungue vishikizo vya shati lako na baada ya kukueleza anataka kukufanyia nini, inabaki hiari yako kukubali au kukataa! Kamwe hawezi kukuvamia na kuanza kukufungua vishikizo bila ridhaa yako, anahitaji ridhaa ya mdomo! Vile vile unapofanyiwa upasuaji unajaza fomu ya ridhaa! Chanjo hii pia inakuhitaji ridhaa yako. Kuombwa ridhaa haimaanishi unataka kudhuriwa…TWENDE TUKACHANJWE!

Mbona hadi Ulaya na Marekani wanaipinga?

Hivi unajua kwamba mpaka leo kuna wanaopinga kwamba UKIMWI (HIV) hakuna ni fix tu? Jee wajua kwamba mpaka hii leo kuna kundi kubwa tu la watu duniani na mpaka wana chama chao wanaamini sayari yetu hii (DUNIA) ni TAMBARARE (flat), wewe unaamini ni duara ni mzushi tu? Jee wajuwa kwamba kuna watu wanaamini UVIKO-19 haipo ni njama za Mabeberu tu? Kila kinachoanzishwa duniani kiwe kizuri au kibaya kina wanaokiunga mkono na wanaokipinga! Hata chanjo nyengine ambazo hivi sasa tunaziona zina manufaa makubwa kama ile ya ndui (smallpox) na polio wakati wa ujio wake zilipingwa pia! Hivyo katika ulimwengu huu wa UHURU wa kidemokrasia na uhuru wa teknolojia ya habari kuwepo wanaopinga chanjo ya UVIKO-19 si jambo la ajabu wala lakutia shaka, muhimu ni HOJA zao za kupinga! Jee hoja zao ni zipi? Binafsi nimefuatilia mahojiano ya baadhi yao kwenye vyombo mbali mbali vya habari, hoja zao nyengine nizakufikirika zaidi (fiction) mfano wanaogopa kuwa mazombi (immortal) kama wakichomwa chanjo (hahahahah)! Wengine hoja zao ni kupambania tu uhuru wao wakujiamulia wanavyotaka kuishi, hawataki kuingiliwa juu ya maisha yao (serkali zao zisiwapangie juu ya chanjo), wengine hawaamini kwamba UVIKO-19 ni hatari hivyo, wanaamini vyombo vya habari vinaongeza chumvi, hivyo hawana imani tu na chanjo! Wengine wasi wasi wao ni USALAMA wa chanjo, ukitoa hoja hii ambayo nimeshaitolea ufafanuzi hapo juu, hizo hoja nyengine ni ama hazihusiani na usalama au ufanisi wa chanjo yenyewe bali ni hoja ya zoezi la (utaratibu wa) utowaji chanjo kwenye nchi husika au ni imani (utashi) wa anaepinga chanjo…kwa mfano kama kama unaamini utakuwa zombie wakati kuna zaidi ya watu milioni 8 wameshachanjwa na hakuna hata mtu aliegeuka kuwa nusu zombi mpaka sasa, wewe tunakusaidiaje sasa! TWENDE TUKACHANJWE!

TWENDENI TUKACHANJWE, KINGA NI BORA UVIKO-19 HAINA TIBA!

“It is better to be roughly right in due time, bearing in mind the consequences of being very wrong, than to be precisely right too late”
 

zacha

JF-Expert Member
Feb 28, 2009
1,125
2,000
Mkuu,

Ni bora kukaa kimya kuliko kuja na masredi marefu ya kuhamasisha chanjo....

Mnatumia nguvu kubwa sana kushawishi raia wakachome hizo chanjo....

Nini kimejificha nyuma ya hizi movement zenu....

Watanganyika siyo wajinga kama zamani mjue...


Chanjo ni hiari sioni haja ya kulazimishana.....


Mkome....!

Shukrani!!
 

Nafaka

JF-Expert Member
Feb 17, 2015
6,146
2,000
Watanzania wakishaamua kitu hata uwaonyeshe ukweli basi hawawezi kubadili mtazamo wao.
Ila nimeshangaa watu wamejazana kuchanja, nashukuru hata mzee wangu na mama yangu wamechanja.
 

macho_mdiliko

JF-Expert Member
Mar 10, 2008
14,864
2,000
Hawa sasa ndiyo wataalam waliotakiwa wapewe nafasi kuelezea haya mambo kwa wananchi. Siyo wanaachia yule mama kichaa anayetembea na furushi la ''makopo'' ya juisi za tangawizina malimao. Wale ni ma-clown tu na walishaharibu hivyo hawawezi kuaminika tena. Asante Pascal Mayalla kwa ku-share hata madini adimu.
 

macho_mdiliko

JF-Expert Member
Mar 10, 2008
14,864
2,000
Watanzania wakishaamua kitu hata uwaonyeshe ukweli basi hawawezi kubadili mtazamo wao.
Ila nimeshangaa watu wamejazana kuchanja, nashukuru hata mzee wangu na mama yangu wamechanja.
Mkuu hii chanjo watachanja wengi, hasa wenye miaka 35 kwenda juu. Hawa wanaochanja sasa hivi wakimaliza kama mwezi basi wengine wataona kumbe woga wao ni wa bure tu.
 

GwaB

JF-Expert Member
Mar 19, 2014
2,103
2,000
Hawa ndio wasomi wetu wanaonangwa na Msukuma Bungeni. Huyu PHD holder ama ni Kigwangala mwingine au anashiriki kuhamsisha chanjo kama wanasiasa wengine.

Hivi kweli mtaalamu wa Biotechnologie anaandika kusifia kazi ya watalaamu wengine wa level yake kuhusu usalama wa chanjo yenye utata ambao kwa kweli upo badala ya kuingia kazini kutafuta chanjo ya COVID-19 hapa hapa Tanzania kama Uganda walivyoanza kuonyesha njia na nyuma yake Rwanda ?

Nilitarajia anakuja kutoa elimu ya hiyo chanjo inayonadiwa imetengenezwa kwa material gani na inafanyaje kazi tofauti na chanjo zilizotangulia na madhara yake ni yapi... Yeye anaishia tu kusema ni salama tukachanje? Hivi alichoandika hapa na tathimini na tahadhali aliyetoa Mchungaji Gwajima kuhusu chanjo hii Kuna tofauti yoyote?. Huyo msomi ameiangusha taasisi iliyomuajiri. ... Angekaa kimya tu.
 

4IR

JF-Expert Member
Apr 21, 2014
995
1,000
PhD zingine bora zikalime tu, mimi nikajua kaingia walau maabara kujiridhisha juu ya usalama wa chanjo zilizoletwa nchini, kumbe porojo zake tu.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom