Je, Watamnyamazisha huyu kwa kumpa Uwaziri?

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,007
Tunaisubiri kwa hamu Ripoti ya BoT - Anne Kilango

2008-02-11 10:16:54
Na Joseph Mwendapole

Mbunge wa Same Mashariki (CCM), Bi. Anne Kilango, amesema Wabunge wanaisubiri kwa hamu kubwa Ripoti ya Tume ya Kuchunguza ufisadi ndani ya Benki Kuu (BoT), ili waichambue kama ile ya Kampuni hewa ya Richmond.

Kadhalika, amesema wataendelea kuwaumbua viongozi wanaojihusisha na ulaji rushwa na ufisadi serikalini bila woga na bila kujali kuwa wanatoka CCM.

Aliyasema hayo juzi wakati akihojiwa na Televisheni ya Taifa (TVT).

Alisema zama za kulindana zimekwisha na kinachotakiwa hivi sasa ni kuangalia maslahi ya Taifa.

Alisema kuna viongozi wabinafsi ambao wamekuwa wakitumia madaraka wanayopewa kujilimbikizia mali na kwamba hawatawavumilia.

``Ufisadi ndani ya BoT umetukera sana Wabunge kuliko mnavyofikiria na nawahakikishia tutaungana katika masuala kama hayo kwa maslahi ya Watanzania,`` alisema Bi. Kilango ambaye ameibukia kuwa Mbunge machachari na mtetezi wa maslahi ya Taifa bungeni.

Alisema kuna wakati Wabunge walikuwa wakinyamazishwa wanapojadili mambo ya rushwa na ufisadi hasa yanapowagusa viongozi lakini hivi sasa wataendelea kuyaweka wazi bungeni.

Alisema kuna wakati aliuliza swali kuhusu kampuni ya Richmond na akaitwa na kuelezwa kuwa hatakiwi kuzungumzia suala hilo Bungeni na badala yake alipeleke kwenye chama hali ambayo ilimshangaza.

Alisema kuwa huo ni utaratibu mbovu wa kuwalinda viongozi wala rushwa ambao wanakichafua chama na serikali kwa kisingizio kuwa wanafanya hivyo kuilinda CCM.

``Tulipoonywa tukawaambia viongozi hapana tutaendelea kuikosoa serikali kwa maslahi ya wananchi kwa kuwa tukiacha kufanya hivyo watu wachache wataendelea kukichafua chama na serikali,`` alisema na kuongeza kuwa wabunge wamechoka kufanywa mihuri (rubber stamp).

Aliongeza kuwa kuna watu wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya rushwa na kujificha kwenye mwavuli wa chama na serikali.

``Tumebaini kuwa mambo mengi yanayoharibika si kwa sababu ya serikali wala chama bali ni watu binafsi na tutaendelea kuwasema bila woga ili wasiendelee kutuchafua,`` alisema.

SOURCE: Nipashe
 
Back
Top Bottom