Je, Unatambua Wajibu Wako Mtandaoni Kama Raia wa Kidigitali?

The Sheriff

JF-Expert Member
Oct 10, 2019
617
1,794
WAJIBU WA RAIA WA KIDIGITALI MTANDAONI 1.jpg


Wajibu wa Raia wa Kidigitali inamaanisha uhusiano mzuri ulipo kati ya watu na mwingiliano wao mtandaoni. Hii ina maana kuwa nadhifu mtandaoni, kufanya matendo yanayofaa, na utayari wa kuwajibika kwa matendo binafsi mtandaoni.

Wajibu huu unamaanisha maadili ambayo mtu anapaswa kuonesha anapowasiliana na mwingine kupitia mitandao ya kijamii, barua pepe, ujumbe wa papo hapo, n.k. Ni wajibu wa kila mmoja kuwasiliana mtandaoni na watumiaji wengine kwa njia ya adabu na heshima.

Wajibu wa Raia wa Kidigitali ni suala muhimu na linalopaswa kila mmoja wetu kujifunza. Elimu endelevu kuhusu somo hili inaweza kukuza tabia chanya mtandaoni.

Hapa chini ni baadhi ya wajibu wa kila Raia wa Mtandaoni:

Huruma na utu mtandaoni: Hii ni nyenzo muhimu katika kupambana na unyanyasaji wa mtandaoni kwani hutukumbusha kwamba kuna mtu halisi upande mwingine wa skrini. Katika kizazi kilichojaa unyanyasaji wa mtandaoni, jumbe za chuki na maoni yanayoegemea upande mmoja, ni muhimu kukumbuka kuwa tuna jukumu la kurudisha ubinadamu kwenye teknolojia.

Ili kutengeneza kizazi cha watumiaji wa mtandao wanaofahamu wajibu wao, sote tunapaswa kuzuia unyanyasaji wa mtandaoni kwa kuwasaidia wengine katika umri mdogo kuachana na tabia zisizokubalika.

Utengenezaji wa maudhui yenye maadili: Hili ni jukumu la mtayarishaji wa maudhui ya mtandaoni kutotengeneza maudhui hatari, yenye chuki, ya kuudhi, yenye kusababisha usumbufu au athari za kiafya kwa watumiaji wengine. Urahisi wa kupakia maudhui kwenye mitandao ya kijamii kama vile Tik Tok, Instagram, Snapchat, na YouTube inamaanisha kila mtu anaweza kuwa mtayarishaji wa maudhui ilimradi tu awe na kifaa (simu au kompyuta) na intaneti.

Hata hivyo, kila mmoja anapaswa kufahamu kwamba picha na video wanazochapisha mtandaoni zinaweza kuwa na matokeo mabaya. Michezo hatari kama vile “Milk Crate Challenge” imeundwa na watengeneza maudhui yasiyo ya maadili ambayo yamesababisha madhara kama vile kuwaacha watu na ulemavu au hata kusababisha vifo.

Matumizi sahihi ya maudhui yenye hakimiliki na kutambua vyanzo: Hili ni miongoni mwa matatizo mengi ambayo yanawakabili watengeneza maudhui wengi siku hizi. Hata hivyo, tunapaswa kupambana nalo kama watumiaji wa mtandao. Teknolojia imerahisisha kwa kubofya "copy" na "paste" lakini si sahihi kufanya hivyo kwenye kazi ya mtu mwingine. Ni muhimu pia kuelewa umuhimu wa kutaja vyanzo sahihi vya maudhui fulani unayotumia. Si sahihi kutumia kazi za wengine bila kuwatambua; huo unakuwa ni wizi.

Kuripoti matendo yasiyofaa: Usalama ni jambo muhimu sana. Kwa mfano, ungeona shughuli zisizofaa zikifanywa kwa jirani yako ungepuuza? Ikiwa ungeshuhudia unyanyasaji dhidi ya mtoto ungekaa kimya na kutoegemea upande wowote? Sehemu ya Uraia wa Kidigitali unaowajibika ni kukabiliana na wakosaji wa kidigitali kwa njia ambayo inaweza kumaliza makosa hayo. Hii haijumuishi ubadilishanaji wa jumbe kali au matusi; inahitaji tu kuripoti wahalifu kwa wasimamizi wa tovuti au, ikibidi, kwa mamlaka zinazofaa za kisheria.

Kutosambaza habari za uongo: Sasa hivi ni rahisi kwa habari za uongo kuenea kwa haraka, hasa katika kizazi cha leo ambapo tovuti na mitandao ya kijamii inakuwa; unaweza kushiriki machapisho kwa kubofya mara moja tu. Habari za uongo zinaweza kusababisha watu kufanya maamuzi mabaya au zinaweza kuwapa hofu. Kwa hivyo kabla ya kuishiriki, hakikisha umeisoma kwanza na unaangalia ukweli kutoka kwa vyanzo vya kuaminika.

Kila mmoja ana wajibu wa kufahamu wajibu wake awapo mtandaoni. Watu wazima wana kiasi kikubwa cha wajibu wa kidigitali – yaani kama kielelezo cha tabia njema kwa vizazi vijavyo. Wazazi, waelimishaji, na makampuni ya teknolojia wanapaswa kutekeleza jukumu lao kutengeneza uwanja salama kwa watoto na vijana kukuza uhusiano mzuri na teknolojia, ambao utawaruhusu kustawi kidigitali.
 
Back
Top Bottom