Je, Unajua kuwa kutikisa makalio kwa lengo la kumtega mtu ni unyanyasaji wa kingono? Jifunze hapa juu ya unyanyasaji wa kingono

sajo

JF-Expert Member
Nov 8, 2010
3,021
5,253
UNYANYASAJI WA KINGONO NA RUSHWA YA NGONO

Kumekuwa na tabia isiyopendeza katika jamii hususani mahali pa kazi ambapo baadhi ya waajiri au mameneja wa waajiri wamekuwa na tabia ya kuwanyanyasa kingono na kuwaomba rushwa ya ngono wafanyakazi walio chini yao au watu wasio wafanyakazi wanaoomba ajira katika ofisi zao.

Watu wengine wamekuwa wakiwaomba ngono watu wanaoomba huduma fulani katika ofisi zao kwa masharti kuwa wasipotoa ngono basi hawatapewa huduma hiyo au watapewa lakini kwa kuchelewa sana.

Lakini wengine wamekuwa wakiwabughudhi wafanyakazi wenzao kwa kuwafanyia matendo yasiyokubalika kwa lengo la kushawishi ngono nk. Basi leo tunajifunza kuhusu vitu hivi viwili na namna ya kuvifanyia kazi au kuvichukulia hatua.

Naitwa Lusajo W. Mwakasege, Mwanasheria, namba yangu ya simu ni 0713-368153 (inapatikana WhatsApp öffnen<+255713368153> na telegram) na barua pepe yangu ni mwakasege@gmail.com. Tuanze somo letu:​

A: Nini maana ya Unyanyasaji wa Kingono
Ni aina yoyote ya uoneshaji au ufanyikaji wa tabia ya kimapenzi isiyokubalika na mtu inayofanywa kwa mtu mwingine kwa lengo la kudhalilisha, kufedhehesha au kumdhoofisha mtu.

Je, Ni matendo yapi yakifanyika yanaweza kuwa ya kinyanyasaji ngono?
  • Kushika au kugusa mwili wa mtu mingine pasipo ridhaa yake,​
  • Kutoa maoni (comments) zenye tafsiri za kingono​
  • Kuomba ngono au vitu vya kingono (kimapenzi)​
  • kutoa viashirio vya kingono kwa mtu mwingine (mf. kukonyeza, kulamba lips nk)​
  • kufanya miondoko ya kingono / kimapenzi (kutikisa makalio, kuvaa nguo za kubana ili kuonesha maungo nk)​
  • kutoa vichekesho vya kingono kumuelekea mtu,​
  • Kumuuliza mtu kuhusu maisha yake ya kimapenzi/kingono​
  • maongezi kwenye simu yanayoweza kukufanya ujisikie vibaya (mfano kubana au kulegeza sauti nk)​
  • kujiachia kihasara kwa mavazi au kuonesha maungo ya mwili kwa mtu,​
  • kumwangalia au kumtazama mtu kwa muda mrefu isivyo kawaida,​
  • Kutoa maneno yenye kutaja viungo vya mwili kwa lengo la kudhalilisha;​
  • kutumia nguvu kufanya jambo la kimapenzi ambalo sio ubakaji;​
  • Kumfanyia mwanamke usiye na mahusiano nae ya kimapenzi jambo lolote au kumtamkia neno lenye kuashiria ngono au kiungo chochote cha mwili, au kutoa sauti ya neno la kudhalilisha ili tu mtu fulani alisikie, au kuingilia faragha ya mwanamke (kumchungulia chooni, bafuni nk)​
  • Kufanya shambulio la kingono (sexual assault)​

B: Je, Nini tofauti ya shambulio la kingono (sex assault) na unyanyasaji wa kingono (sexual harassment)?
👉Shambulio la kingono
ni pale mtu anapolazimishwa kufanya shughuli au jambo la kingono kama kubusiana, kugusana kwa kutomasana, kunyonyana ndimi au viungo vya mwili, kufanya ngono nk
WAKATI
👉Unyanyasaji wa kingono inahusisha mambo mengi mpaka yale yasiyokuwa moja kwa moja, mfano kutoa vichekesho vya kingono, maoni ya kingono nk.


C: Je, kwa Tanzania, unyanyasaji wa kingono ni kosa kisheria?
NDIYO
, kwa mujibu wa kifungu cha 138D cha Kanuni ya adhabu, ni kosa kwa mtu yoyote kumfanyia unyanyasaji / udhalilishaji wa kingono mtu mwingine.

D: Je, Nini adhabu ya unyanyasaji wa kingono?
Endapo itathibitika mahakamani kuwa mtu amefanya kosa hilo la unyanyasaji wa kingono, basi anaweza kupewa kifungo kisichozidi miaka 5 jela au kulipa faini isiyozidi Tshs. 200,000/= (shilingi laki mbili) au vyote viwili kwa pamoja, faini na kifungo na pia anaweza kuamriwa kumlipa fidia mtu aliyeathirika na matendo yake ya unyanyasaji.

Fidia itakuwa kwa kiwango kitakachoamriwa na mahakama.

ZINGATIA
🔹Sio lazima mtu kulipwa fidia kwa unyanyasaji wa ngono aliofanyiwa, ni mahakama yenyewe ikiona inafaa inaweza kutoa amri ya mshtakiwa aliyekutwa na hatia kulipa fidia,

🔹Mwathirika wa unyanyasaji wa ngono hawezi kutaja kiwango cha fidia – bali mahakama yenyewe ndiyo itaamua kiwango hicho cha fidia.


E: Nini Maana ya Rushwa ya Ngono?
Rushwa ya ngono ni pale ambapo mtu yeyote mwenye mamlaka na ambaye katika kutekeleza mamlaka yake, akaomba ngono au akatoa masharti ya kingono au feva yoyote ile kwa mtu mwingine kama sharti la kutoa ajira, kupandishwa cheo, kutoa haki, kufanya upendeleo au kumjali mtu.

Adhabu ya rushwa ya Ngono
Endapo kosa hilo likithibitishwa mahakamani atahukumiwa kulipa faini isiyopungua shilingi milioni 5 au kifungo kisichopungua miaka 3 JELA au vyote viwili kwa pamoja.


Je, Rushwa ya Ngono na unyanyasaji wa kingono ni jambo sawa?
HAPANA
, hivi ni vitu viwili tofauti ingawa dhima zake ni kama zinafanana.

▪️Rushwa ya ngono ni lazima ifanywe na mtu mwenye mamlaka dhidi ya mtu asiye na mamlaka kwa lengo la kumpa asiye na mamlaka upendeleo au wa lengo la kuwa ni sharti kwa jambo fulani kufanywa kwa mtu asiye na madaraka,​
WAKATI

▪️Unyanyasaji wa kingono unaweza kufanywa na mtu yoyote bila kujali kama ana madaraka au la. Mfanyakazi wa chini anaweza kumfanyia bosi wake unyanyasaji wa kingono.

Vilevile, Rushwa ya ngono inatengeneza kosa la jinai chini ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 Marejeo ya 2022 wakati unyanyasaji wa kingono unatengeneza kosa la jinai kupitia Kanuni ya Adhabu sura ya 16 Marejeo ya 2022;

Adhabu zake pia zinatofautiana kama nilivyoeleza.


F: Nini cha kufanya unapofanyiwa unyanyasaji wa kingono?
Kila mmoja anastahili kuthaminiwa kwa utu wake akiwa mahali popote ikiwa ni pamoja na mahali pa kazi. Unyanyasaji wa kingono unatweza utu wa mtu na kumdhalilisha. Ikitokewa umefanyiwa unyanyasaji wa kingono fanya yafuatayo:

▪️ Zungumza na mnyanyasaji
Mkataze kuendelea kufanya matendo yasiyokufurahisha. Mwambie aache ama sivyo utamripoti katika mamlaka za kazi na za kisheria,

▪️Zungumza na watu wengine;
Unaweza kuwasilisha malalamiko kwenye idara ya rasilimali watu ambao wataweza kumwita mtendaji wa kosa na kufanya vikao pamoja nawe na kumwonya mtu huyo kutoendelea na tabia zake mbaya, AU wanaweza kuchukua hatua za kinidhamu kulingana na kanuni za shirika husika,

▪️Rekodi na Kutunza ushahidi
Unaweza kuandika katika kidaftari chako cha kumbukumbu kila jambo ulilofanywa na jina la mhusika. Unaweka kumbukumbu za tarehe na muda jambo lilipofanyika.

Kama kuna ushahidi wa sauti, video nk basi pia uhifadhiwe;

▪️Fanya malalamiko rasmi
Ikiwa unaona hakuna hatua zinazochukuliwa juu ya malalamiko yako au unaona mtendaji wa unyanyasaji hajirekebishi licha ya kumwonya, basi unaweza kuwasilisha malalamiko rasmi juu ya unyanyasaji uliofanyiwa.


G: Malalamiko Rasmi yanawasilishwa wapi?

👉 Malalamiko ya Unyanyasaji wa Kingono

Kwa kuwa ni kosa linaloangukia katika makosa ya Jinai, malalamiko haya yanatakiwa kuwasilishwa katika kituo chochote cha Polisi kilicho karibu. Huko kuna dawati la jinsi nk

Polisi watachukua maelezo yako mlalamikaji na watamwita na kumhoji mlalamikiwa na kisha watafungua jalada la kesi na kumfikisha mtuhumiwa mahakamani.

👉 Malalamiko ya Rushwa ya Ngono
Ikiwa mtu uliombwa rushwa ya ngono wakati wa kuomba ajira, au kwa masharti ya kupewa haki fulani nk, basi malalamiko yako utayawasilisha katika mamlaka ya kuzuia na kupambana na Rushwa yaani TAKUKURU.

TAKUKURU watakuchukua maelezo, watamwita au kumkamata mtuhumiwa na kumhoji kisha watafungua jalada la uchunguzi na baadae kufungua kesi mahakamani dhidi ya mtuhumiwa.

Kama upo mbali na ofisi za TAKUKURU TZ unaweza wasilisha malalamiko kwa kupiga simu ya bure namba 113 au ripoti kituo cha polisi kilichopo karibu nawe watakusaidia;


H: Je ni muda gani mtu anatakiwa kuwasilisha malalamiko ya unyanyasaji / udhalilishaji wa kingono?
Ni ndani ya siku 60 tu kutoka mtu alipoambiwa neno au kufanyiwa tendo lililomdhalilisha. Ukichelewa kutoa malalamiko ndani ya siku 60 basi jambo lako linakuwa limekufa lenyewe, Itachukuliwa kama halikuwahi kutendeka.


Je, unaweza kuacha kazi ikiwa unaona hujaridhishwa na hatua zilizochukuliwa juu ya lalamiko lako na ukastahili kupata haki za kisheria?
NDIYO
, ikiwa hukuridhika na hatua zilizochukuliwa na mwajiri wako au ikiwa mwajiri wako ndiye aliyekuwa anakunyanyasa na ukaona mazingira ya kazi yanakuwa magumu sana, unaweza kuacha kazi na ukadai stahiki zako za kazi kutoka kwa mwajiri wako kwa barua au kwa kuwasilisha mgogoro katika tume ya usuluhishi na uamuzi (CMA).

Stahiki utazoomba ni kama malipo kutokana na kuvunjwa kwa mkataba wako wa ajira, malipo ya likizo ya kazi, fidia kutoka na uvunjwaji wa mkataba wa ajira nk


I: Je, unaweza kudai fidia kutokana na unyanyasaji wa ngono?
NDIYO
, Ingawa jambo la unyanyasaji wa kingono ni la kijinai – kama mahakama haikutoa amari ya kulipwa fidia katika hukumu, bado mtu unaweza kudai fidia kwa njia ya madai.

Kama utadai fidia kwa njia ya kesi ya madai, utatakiwa kuthibitisha madhara uliyoyapata kutokana na unyanyasaji huo.

▪️Ni jambo gumu kidogo na lenye mtego (technical) na hivyo kuhitaji umakini sana kabla na wakati wa kulifungua tofauti na likifunguliwa kwa jinai. Nakushauri uonane na wanasheria wakusaidie katika uandaajai wa madai yako.


Natumai Nimeeleweka. Ahsante.
 
UNYANYASAJI WA KINGONO NA RUSHWA YA NGONO

Kumekuwa na tabia isiyopendeza katika jamii hususani mahali pa kazi ambapo baadhi ya waajiri au mameneja wa waajiri wamekuwa na tabia ya kuwanyanyasa kingono na kuwaomba rushwa ya ngono wafanyakazi walio chini yao au watu wasio wafanyakazi wanaoomba ajira katika ofisi zao.

Watu wengine wamekuwa wakiwaomba ngono watu wanaoomba huduma fulani katika ofisi zao kwa masharti kuwa te.
Bila video ni uongo
 
Duuh acheni uuambaji wa Mungu udhihirike jamani..unajua kuna ile kufosi unaona kabisa ila kitu kama na natural mnataka watu watembee kama wamebanwa na haja kwa kujibana lol nyie wanaume ndo msiangalie 😆 😆 😆 😆
Basi vaeni baibui zile.....mnasababisha tunajikwaa sana 😅😅
 
Asa hivi nikiona tu mdada anatingisha naenda kumstaki, na sitaki afungwe nilipwe tu hiyo laki mbili nikawale wengine uwanja wa fisi au buza asante sana wakili nitakuwa nakupa buku 7 kila mkeka ukitiki ameen
 
Duuh acheni uuambaji wa Mungu udhihirike jamani..unajua kuna ile kufosi unaona kabisa ila kitu kama na natural mnataka watu watembee kama wamebanwa na haja kwa kujibana lol nyie wanaume ndo msiangalie 😆 😆 😆 😆
Tembea ya kubanwa na haja😄😁
 
Back
Top Bottom