SoC01 Je, tatizo ni chanjo ya UVIKO-19 au ni imani potofu?

Stories of Change - 2021 Competition
Jul 15, 2021
15
45
Sakata la chanjo ya UVIKO-19 linazidi kupata sura mpya kila kukicha huku uamuzi wa kuchanjwa ama kutochanjwa ukizidi kuwa na sintofahamu nyingi. Nia ya Makala hii leo sio kushawishi watu kuchanjwa ama la bali kujenga hoja zitakazosaidia kufanya uchaguzi sahihi wa kuchanjwa ama kutochanjwa.

Makala hii haitojikita kabisa kuangalia faida na hasara za kisayansi kuhusu chanjo ya UVIKO-19 bali itasaidia kujenga hoja za namna bora ya kufanya maamuzi juu ya chanjo hii kwa kuzingatia nadharia za sayansi ya jamii.

Kuna msemo wa Kiswahili unasema ‘wasiwasi ndio akili’, msemo huu uko sahihi sana hasa kwa kuzingatia ya kwamba unatukumbusha uwezo wa kuhoji, kujifunza, kudadisi, kutafiti na kujadiliana na wenye uelewa zaidi kuondoa wasiwasi. Kama ilivyo kwa chanjo ya UVIKO-19 watu wengi tumekuwa na wasiwasi mwingi hivyo kuathiri maamuzi yetu ya kuchanjwa ama kutochanjwa.

Swali la kujiuliza kila mmoja, je, wasiwasi wetu dhidi ya chanjo ya UVIKO-19 umetusaidia kuhoji, kujifunza, kudadisi, kutafiti na kujadiliana na wenye uelewa zaidi kuondoa wasiwasi?

Majibu ya swali hili ni mengi na kwa ushahidi uliopo kupitia mijadala ya mtaani na mitandaoni inaonyesha wazi ya kuwa wengi wetu tumeshindwa kupata majibu ya wasiwasi wetu kwa usahihi kwa kuwa tumeshindwa kuhoji na kudadisi kwa kina. Kama nilivyosema hapo awali, wasiwasi ni sehemu muhimu sana ya kufanya maamuzi ila, ili wasiwasi wetu uweze kuondoka ni muhimu sana kujifunza, kuhoji, kudadisi, kutafiti na kujadiliana na mamlaka ama watu wenye uelewa sahihi. Ninachojifunza kutokana na mijadala tunayofanya ni kushindwa kuhoji, kujifunza na kujadiliana na watu ama mamlaka zenye uelewa sahihi badala yake tumeingiwa na hofu na kujenga imani potofu dhidi ya chanjo ya UVIKO-19.

Imani potofu tulizojijengea dhidi ya chanjo ya UVIKO-19 ni kutokana na wogo, kukosa uelewa na kusikiliza propaganda ambazo zinatunyima fursa ya kuhoji, kudadisi na kujifunza. Ni ukweli kwamba wengi wetu watanzania ni wavivu wa kushughulisha bongo zetu kwa kushindwa kujifunza mambo kwa kina badala yake tunawakabidhi watu wachache uwezo wa kufikiri kwa niaba yetu kisha wao ndio huja na majibu ya wasiwasi wetu. Bila hata kuhoji nasi hupokea majibu hayo kama ukweli sahihi na usiopingika.

Ili kuweza kufanya maamuzi sahihi kwa ajili yako binafsi na kwa jamii nzima ni vyema uwe na taarifa sahihi wakati wote bila kushawishika kwa kuogopeshwa na watu wachache wanaohodhi taarifa. Uoga tulionao kwa jambo la kusadikika ni mkubwa sana kuliko jambo dhahiri (UVIKO-19) lililo mbele yetu. Wengi wa wale wanaohodhi taarifa ya chanjo ya UVIKO-19 wametumia mbinu za kuogofya kushawishi watu wasichome chanjo badala ya kuwajengea watu uwezo kuwasaidia kuona faida na hasara ya chanjo husika kisha kuwaacha watu wenyewe wafanye maamuzi. Watu wengi wameishiwa kupotoshwa na kuaminishwa mabaya ya chanjo na mwishowe kuamuliwa kuwa wasichanjwe jambo ambalo linakwenda kinyume na utashi wa mtu husika.

Maamuzi ya wasiwasi wako yatokane na jitihada zako wewe mwenyewe kujua kuhusu chanjo ya UVIKO-19 faida na hasara zake nafasi yako kwenye jamii na utayari wako kuchanjwa ama kutochanjwa. Endapo mtu atafanya maamuzi kwa niaba yako kujibu wasiwasi wako wewe binafsi hautokuwa umejitendea haki kwani kama binadamu nafsi na utashi ni mali yako wewe hivyo ni vyema sana ukatumia busara na hekima zako kusikiliza hitaji la moyo wako baada ya kupata majibu ya maswali na wasisi wasi wako uliokuwa nao. Hii inatukumbusha pia kujifunza kutoka kwa watu wenye taarifa na ujuzi sahihi badala ya kujifunza kwa kila mtu kisa anamamlaka ama ana hadhira ya watu.

Tukumbuke kuwa sehemu kubwa ya kumwezesha mtu kufanya mamuzi sahihi ya kufanya jambo ni msukumo wa ndani, uhalisia wa mazingira, upatikanaji wa taarifa sahihi na tathimini ya mtu husika. Haya yote yakitumika kwa usahihi yatakupa taarifa sahihi ya kufanya uamuzi na tukumbuke maamuzi yako yanaweza kubadilika kila mara kutokana na namna unavyojifunza kila siku kuhusu jambo husika. Woga, hofu na imani potofu ni sumu kwenye kufanya maamuzi bila kuwa na taarifa sahihi ya jambo unalotaka kulifanyia uamuzi. Uamuzi mara nyingi ni mali ya mtu binafsi na sio mali ya jamii nzima hivyo usifanye maamuzi yako binafsi kwa kutegemea kichocheo cha ushawishi isio na tija kwani madhara ya uamuzi wako wewe ndio utakuwa mtu wa kwanza kujuta ama kufurahi.

Kwa kuwa binadamu anajengwa na nadharia kubwa ya mahusiano ya jamii (socialization) ni vyema tukaitumia nadharia hii kwa faida yetu sote kwani hakuna jamii kama hakuna watu hai na wenye afya njema. Na hapa maamuzi ya kupata ama kutopata chanjo ya UVIKO-19 ndio yataamua uhai wa jamii yetu kwa ujumla. Jamii yetu inapaswa kujifunza kutofautisha woga, imani potofu na ukweli, mara nyingi ukweli hudhihirishwa kwa tafiti na uthibitisho endapo haya yatakosekana basi mengine yote yatakosa uhalali.

Ni vyema tukajifunza mambo kwa uhalisia wake badala ya kuwa mashabiki tusiokuwa na uhakika na kile tunachokishabikia. Chanjo ya UVIKO-19 ni jambo lisilohitaji ushabiki wa kinadharia kwani jambo hili la kisayansi linahitaji majibu ya kisayansi na sio propaganda. Maamuzi utakayofanya ya kuchanjwa ama la yatokane na uthibitisho wenye hakika na sio majibu yenye kuleta hofu, woga na taaruki kwenye jamii yetu.

Kwa kuhitimisha, tujifunze kuhoji kila jambo kwa kina bila kujali aliyekupa taarifa mpaka utakaporidhika ya kuwa unataarifa za kutosha kisha ufanye uamuzi sahihi kwa faida yako binafsi na jamii nzima.
 
kinachokufanya kuamini kua hizo taarifa unazoziita sahihi kua ni sahihi ni nini hasa ?

kifupi ni kuangalia wapi kuna usalama maana tumepewa akili ya kuchanganua mambo.

ila mimi hata angekuja Yesu akasema Chanjo ni salama siwezi kuchanja
 
Mada yako imekosa wachangiaji...ww dalali wa chanjo...bado hushituki tu kujua watanzania hawatiki ujinga huo?
 
Back
Top Bottom