selemala
JF-Expert Member
- Feb 14, 2007
- 367
- 245
A. UTANGULIZI
Napenda kuweka wazi kwamba nimeanzisha mjadala huu, ili kuondoa mkanganyiko na mkwamo ninao uona wazi wazi katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano Wa Tanzania. Kwa mara nyingine katiba yetu imejaribiwa (imekuwa tested), hivyo ni busara kuwepo kwa mjadala wa kuondoa shaka na hoja gonganishi katika katiba yetu kwa ustawi bora na imara wa Taifa letu Pendwa.
B. HISTORIA KIDOGO
Jamhuri ya Muungano Wa Tanzania iliundwa Tar.26 April 1964, ikiwa ni muungano wa maTaifa huru ya Jamhuri ya Tanganyika (1962) na Jamhuri ya watu wa Zanzibar (1964). Jamhuri hizi mbili ziliingia mkataba wa pamoja 1964 na kuanzisha dola la Jamhuri Ya Muungano Wa Tanzania.
Kwa mujibu wa Katiba ya J.M.T ya mwaka 1977, ibara ya 4(3) imeorodhesha mambo 22 ya muungano baina ya pande mbili zilizo-ungana.
Kwa upande wa Tanzania bara (Tanganyika) mambo yasiyo ya muungano yanasimamiwa na serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, na Kwa upande wa Zanzibar, mambo yasiyo ya muungano yanasimamiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Kwa Lugha rahisi, Muungano wetu ni wa serikali Mbili, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Serikali ya Jamhuri ya Tanganyika ilifutwa na haipo.
C. MAMBO YA MUUNGANO
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977), ibara ya 4, ibara ndogo ya 3, imetoa mwongozo kuhusu mambo ya muungano. Na, yameorodheshwa katika nyongeza ya kwanza ya katiba yetu.
Yafuatayo ni mambo 22 ya muungano kwa mujibu wa Katiba yetu.
1. Katiba ya Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
2. Mambo ya Nchi za Nje.
3. Ulinzi na Usalama.
4. Polisi.
5. Mamlaka juu ya mambo yanayohusika na hali ya hatari.
6. Uraia.
7. Uhamiaji.
8. Mikopo na baiashara ya Nchi za Nje.
9. Utumishi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
10.Kodi ya Mapato inayolipwa na watu binafsi na mashirika, ushuru wa forodha na ushuru wa bidhaa zinazotengenezwa nchini Tanzania unaosimamiwa na Idara ya Forodha.
11.Bandari, mambo yanayohusika na usafiri wa anga, posta na simu.
12.Mambo yote yanayohusika na sarafu na fedha kwa ajili ya malipo yote halali (pamoja na noti); mabenki (pamoja mabenki ya kuweka akiba) na shughuli zote za mabenki; fedha za kigeni na usimamizi juu ya mambo yanayohusika na fedha za kigeni.
13.Leseni ya viwanda na takwimu.
14.Elimu ya juu.
15.Maliasili ya mafuta, pamoja na mafuta yasiyochujwa ya motokaa na mafuata ya aina ya petroli na aina nyinginezo za mafuta au bidhaa, na gesi asilia.
16.Baraza la Taifa la Mitihani la Tanzania na mambo yote yanayohusika na kazi za Baraza hilo.
17.Usafiri na usafirishaji wa anga.
18.Utafiti.
19.Utafiti wa hali ya hewa.
20.Takwimu.
21.Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano.
22.Uandikishaji wa Vyama vya siasa na Mambo mengine yanayohusiana navyo.
Angalau kwa mujibu wa katiba yetu, haya yaliyo orodheshwa ndiyo mambo ya muungano.
D. HOJA MEZANI (HOJA KINZANI)
Kwa kuwa Rais aliyeko madarakani ni asili ya Zanzibar, hivyo ni mZanzibari, na anaongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na yeye ni zao la muungano wetu. Na, kwa kuwa Katiba yetu imebainisha dhahiri mambo ya muungano, Je? Ni sahihi kwa Rais wa sasa kuongoza Tanzania Bara (Tanganyika) hata kwa mambo yasiyo ya muungano?
1.Kama ni sahihi, anaongozaje mambo yasiyo ya muungano ilhali yeye ni mZanzibari na ni zao la muungano na ana uishi muungano pamoja na mambo ya muungano, tukumbuke kwamba , tumeungana lakini hatujaungana katika mambo yoye, tumechagua mambo ya kuungana.
2.Kama sio sahihi nini kifanyike?
E. HITIMISHO
Kuna watu mtaacha kujibu hoja na kuleta vioja, kuna watu mtauliza kwa nini hoja hii inaletwa sasa. Majibu yake ni kwamba, Jana(26.04.2021) ilikua siku ya kukumbuka Muungano wetu, hivyo ni busara kuujadili kipindi hiki, na jana kuna kongamano lilifunguliwa ,kuendeshwa na makamu wa Rais Dkt.P.Mpango. Lakini, kwa maya nyingine tumepata Rais Mzanzibar kwa mujibu wa Katiba, hivyo nimeona ni vyema tujadili jambo hili ili kutoa/kuondoa hoja hizi kinzani.
Kwa maoni yangu, Kuna haja ya kuangalia maslahi ya Tanzania bara(Tanganyika) katika muungano wetu. Sioni maana ya Mzanzibari kuwaongoza waTanganyika katika mambo yasiyo ya muungano, unless tukubali kuungana kwa kila jambo. Pia, kuna haja ya kuwalinda waTanganyika kama ambavyo katiba inawalinda waZanzibari, Mathalani;
-Mtanganyika hawezi kumiliki ardhi Zanzibar kwa hoja mufilisi kwamba Zanzibar ni ndogo, lakini kwenye mgawanyo wa pesa za Maadhimisho ya Muungano watataka equal share.
-Wakati anahutubia Bunge, Rais Samia alitoa ahadi ya kununua Meli za uvuvi nne, huku mbili zikielekezwa Zanzibar na mbili Bara. Kwanza hii sio haki, kwani Uvuvi, na Usafirishaji wa majini siyo mambo ya muungano, sioni matiki kwa nini Rais wa Muungano aanze kuhangaika na mambo yasiyo ya muungano kwa Zanzibar kwa kutumia pesa za Watanganyika.
Niko Tayari kurekebishwa na kusahihishwa katika mjadala huu, ili tujenge Muungano utakao kidhi matakwa ya pande zote za Muungano.
Hakutakiwa,. hata hivyo katiba ya Warioba ingerekebisha hii kitu .