Je, ni halali polisi kuwakamata watuhumiwa wikiendi? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Je, ni halali polisi kuwakamata watuhumiwa wikiendi?

Discussion in 'Jukwaa la Sheria (The Law Forum)' started by sulphadoxine, Jan 20, 2012.

 1. sulphadoxine

  sulphadoxine JF-Expert Member

  #1
  Jan 20, 2012
  Joined: Nov 1, 2010
  Messages: 2,264
  Likes Received: 9
  Trophy Points: 135
  HAKI ya mtu kuwa huru ni haki ya kikatiba na kisheria ambayo haipaswi kuingiliwa na mamlaka yoyote ila kwa mujibu wa maelekezo ya sheria ambayo, hata hivyo, sheria hiyo nayo haipaswi kupingana na Katiba.

  Ikitokea mtu amenyang’anywa haki hiyo bila sababu yoyote ya kisheria kwa namna yoyote ile kama vile kuwekwa mahabusu au rumande au kufungwa jela, anaweza akitoka baada ya kubainika haikuwa halali (hasa anapokata rufaa dhidi ya kifungo), anaweza kufungua mashtaka ya “kufungwa bila halali” na kudai fidia.

  Kielelezo kizuri ni uamuzi wa moja ya kesi za mpigania haki za binadamu maarufu nchini, Mchungaji Christopher Mtikila, ambaye aliwahi kudai haki ya fidia kwa kukamatwa na polisi wikiendi na kuwekwa katika mahabusu ya polisi kwa muda wa zaidi ya saa 24 bila kufikishwa mahakamani.

  Katika kesi hiyo ya MCHUNGAJI CHRISTOPHER MTIKILA dhidi ya MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI [2004] TLR 172, polisi walimkamata mlalamikaji siku ya Ijumaa mchana na kumwachia huru siku ya Jumatatu baada ya kubaini hakuwa na kosa alilotuhumiwa la kuwa na nyaraka za uchochezi.

  Polisi walimkamata Mtikila siku ya wikiendi na wakamweka mahabusu bila ya kumfikisha mahakamani baada ya kumhoji kwa tuhuma zilizomkabili. Mtikila aliamua kuishtaki Serikali kwa kesi ya madai akidai fidia ya kunyimwa uhuru wake bila halali.

  Eti wakati wa kusikilizwa kesi hiyo ya rufaa Wakili wa Serikali aliiambia Mahakama kwamba kumkamata Mtikila siku ya wikiendi bila kumfikisha mahakamani kulikuwa ni halali kwani isingewezekana kumfikisha mahakamani siku ambazo si za kazi yaani Jumamosi na Jumapili.

  Mahakama ya Rufaa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilikataa utetezi huo na kusema kuwa polisi walikuwa na njia mbadala ya kumrudishia uhuru wake kwa kumpa dhamana ya polisi kuliko kumweka mahabusu zaidi ya saa 24.

  Kifungu cha 32 cha SHERIA YA MWENENDO WA MAKOSA YA JINAI, SURA YA 20 [R. E. 2002] maarufu “CPA” ndicho kinakataza kumweka mtu rumande zaidi ya saa 24 bila kumfikisha mahakamani. Hivyo kutokana na ukiukaji huo wa sheria Mahakama iliiagiza Serikali imfidie Mchungaji Mtikila kwa kumweka mahabusu zaidi ya muda unaoruhusiwa kisheria.

  Kutokana na hukumu hiyo ya Mahakama ya Rufaa ni msimamo wa kisheria kwamba polisi hawapaswi kumkamata na kumweka mahabusu mtuhumiwa wa kosa lolote la jinai wakati wa wikiendi. Polisi inapaswa kumpa dhamana mtuhumiwa kama kosa analotuhumiwa kutenda ni la dhamana.

  Hivyo tabia iliyokithiri ya polisi kuwakamata watu na kuwaweka mahabusu siku za wikiendi ili “kuwakomoa” wakae siku mbili au tatu ndani ni uvunjaji wa sheria ambapo Serikali pamoja na Jeshi la Polisi wanaweza kushtakiwa kwa kesi ya madai na kudaiwa fidia.

  Kuhusu dhamana ya polisi tumewahi kujadili katika safu hii tukisema kwamba huwa inatolewa kwa mujibu wa kifungu cha 32 (1) cha CPA pamoja na kifungu cha 31 cha SHERIA YA JESHI LA POLISI NA HUDUMA YA WASAIDIZI, SURA YA 322 [R. E. 2002] ambapo anayehusika kuitoa au mwenye mamlaka hayo ni Ofisa Mfawidhi wa Kituo cha Polisi.

  Polisi inatakiwa na sheria kueleza haki hiyo ya mtuhumiwa anapokamatwa ambapo kifungu cha 64 (5) cha SURA YA 322 kinasema: “Kila ofisa wa polisi anayemkamata mtu amfahamishe mtu huyo haki ya kupewa dhamana chini ya kifungu hiki.”

  Tunachokisoma katika sheria zote mbili yaani CPA na SURA YA 322 ni kwamba mtu yeyote anapokamatwa na kufikishwa kituo cha polisi lazima kwanza aelezwe haki ya kupewa haki ya dhamana kwa kosa analotuhumiwa kulitenda na hasa kama si kosa kubwa.

  Hivyo sheria haijasema kwamba kila mtuhumiwa akifikishwa katika kituo cha polisi lazima kwanza awekwe mahabusu kabla ya kupewa dhamana ya polisi tena baada ya ndugu zake kumuona mkuu wa kituo na pengine kutakiwa kutoa hongo. Kinachotakiwa ni polisi kumhoji mtuhumiwa na baadae kumwachia huru au afikishwe mahakamani baada ya saa 24.
  Kuhusu dhamana ya polisi kabla ya kupelekwa mahakamani, kuna sheria mbili zinazolipa Jeshi la Polisi uwezo wa kumpa dhamana mtuhumiwa wa makosa ya jinai, hasa yale yasiyo mazito sana, kabla ya kufikishwa mahakamani baada ya kuhojiwa na kuandika maelezo. Sheria hizo ni CPA na ile ya Jeshi la Polisi yaani SURA YA 322 ambayo inatoa uwezo huo katika vifungu cha 32 (1) na 31.

  Vifungu hivyo vinasema: “ Iwapo mtu yeyoye ametiwa mbaroni bila hati ya kukamata kwa kosa ambalo adhabu yake sio ya kifo, ofisa mfawidhi wa kituo cha polisi ambacho ameletwa, anaweza, kwa kesi yoyote, na inapaswa kama inaonekana kuwa haiwezekani kumpeleka mahakamani ndani ya muda wa saa ishirini na nne, tangu alipokamatwa, achunguze kesi hiyo na isipoonekana kuwa ya kosa kubwa, amwachie mtuhumiwa kwa kutoa dhamana au bila mdhamini, kwa muda maalumu wa kumwezesha ahudhurie mahakamani kwa wakati…,”

  Aidha, vifungu vya 64, 66, 67 na 68 vinaeleza na kufafanua kwa kina utaratibu wa kutoa dhamana ya polisi, vigezo vya kuzingatia wakati wa kufikiria kutoa dhamana hiyo, masharti ya dhamana, sababu ya kukataa kutoa dhamana, kufuta dhamana na matokeo ya kukiuka dhamana hiyo.

  Kifungu cha 64 cha Sheria ya Jeshi la Polisi kwa mfano kinasema kwamba mtu aliyeletwa polisi chini ya ulinzi wa ofisa wa polisi kwa tuhuma yenye sababu ya maana kuwa ametenda kosa, atapaswa aachiwe haraka katika mazingira ya aina tatu.

  Kwanza, iwapo ofisa polisi aliyemkamata anaamini kuwa mtu huyo hakutenda kosa au hana sababu za maana za kuendelea kumweka chini ya ulinzi. Pili, iwapo ofisa wa polisi anaamini kwamba mtu aliyemkamata si mtu mwenyewe.

  Tatu, baada ya saa ishirini na nne tangu akamatwe, hakuna shtaka lililofunguliwa dhidi ya mtu aliyekamatwa isipokuwa ofisa wa polisi muhusika anaamini kuwa polisi linalotuhumiwa kutendeka ni kubwa sana.

  Kifungu kidogo cha pili cha kifungu hicho cha 64 cha Sheria ya Jeshi la Polisi kinasema ikiwa shtaka limeshafunguliwa rasmi dhidi ya mtu yeyote aliye chini ya ulinzi wa polisi, ofisa wa polisi mfawidhi wa kituo anaweza, baada ya mtu huyo kuleta nyaraka za udhamini akiwa au bila mdhamini, za kuhudhuria mbele ya mahakama, akitakiwa mtu huyo aachiwe.

  Naye mtu aliyekamatwa akiwa chini ya umri wa miaka kumi na tano, kifungu kidogo cha cha tatu cha kifungu cha 64 cha Sheria ya Jeshi la Polisi kinasema, mrtu huyo anaweza kuachiwa baada ya mzazi, mlezi, jamaa au mtu yeyote anayeaminika kuingia mkataba wa udhamini kuhakikisha anahudhuria anapohitajika.

  Sheria ya Jeshi la Polisi inazungumzia pia kutokuwepo kwa ada yoyote ya udhamini wa polisi katika kifungu cha 64 (4). Kwamba mtu aliyekamatwa hapaswi kulipa ada yoyote ya kupewa mdhamana wa polisi. Hii ni muhimu kwa sababu wananchi wengi wanadhani dhamana ya polisi inahusiana na ulipaji fedha. Polisi wasio waaminifu au walarushwa wamekuwa wakijinufaisha kwa wananchi kukosa uelewa huo!

  Polisi wanapaswa kumfahamisha mtu yeyote aliyekamatwa juu ya haki hiyo ya dhamana. Kifungu cha 64 (5) ndicho kinachosema kwamba ofisa wa polisi aliyemkamata mtu yeyote anapaswa kumfahamisha mtu huyo haki ya kupewa dhamana ya polisi.

  Kifungu hicho kinasema: “Kila ofisa wa polisi anayemkamata mtu anayemtuhumu kutenda kosa atapaswa amfahamishe mtu huyo haki yake ya kupewa dhamana chini ya kifungu hiki.”

  Hivyo kwa kifupi na katika lugha rahisi tunapaswa kujibu swali la uhalali wa dhamana ya polisi kwa kusema kwamba mtu yeyote anapokamatwa na kupelekwa katika kituo cha polisi, kwanza anapaswa aelezwe kuwa ana haki ya kupewa dhamana ya polisi kwa kosa analotuhumiwa kutenda iwapo si kosa kubwa sana.

  Pili, ofisa wa polisi anapaswa kufahamu kwamba sheria haijasema kuwa kila mtuhumiwa akipelekwa kituo cha polisi lazima awekwe mahabusu kabla ya kupewa dhamana ya polisi. Hiyo siyo sahihi ingawa ndivyo mara nyingi maofisa polisi wanafanya hivyo!

  Rumande ya polisi sio sehemu ya kumpa adhabu mtuhumiwa bali ni kwa ajili ya usalama wake hasa iwapo amefanya kosa kubwa linalotishia hata usalama wake mwenyewe na ili apatikana kirahisi kila akihitajika kutoa maelezo.

  Suala lingine muhimu ni kwamba mtuhumiwa yeyote wa kosa la jinai, anapaswa apelekwe mahakamani mapema iwezekanavyo, ambapo muda usizidi saa 24 tangu alipokamatwa au kutiwa mbaroni.

  Ofisa wa Polisi Mfawidhi wa Kituo cha Polisi ndiye mtekelezaji mkuu wa sheria inayohususu dhamana ya polisi na anapaswa kuitekeleza bila upendeleo, woga au kwa kupewa fedha au zawadi yoyote. Huu ni wajibu halali wa kisheria kama ambavyo nimewasilisha leo katika mada hii.
   
 2. m

  moshingi JF-Expert Member

  #2
  Jan 20, 2012
  Joined: Nov 15, 2011
  Messages: 278
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  No general rule without exceptions
  Ingawa thread ndefu sana, inachosha kusoma, lakini ingekuwa bora kama ungeweka exceptions\
  mfano k/f 148 cha Sura ya 20 ya sheria, ukikisoma na viambatanisho vyake vyote utaona malengo ya watunzi wa sheria.
  Kazi ya mahakama ni kutafsiri malengo ya watunzi wa sheria(Bunge) na siyo vinginevyo.
  Mwisho, napenda kufahamu; kumbe ipo TLR ya mwaka 2004?! Kama ipo kweli itakuwa ni mpya tuwekee humu nasi tuiosome.
   
Loading...