Je, Mapungufu haya yamepangwa Makusudi kama Uchochoro wa rushwa?

Karikenye

JF-Expert Member
Apr 11, 2011
564
279
KAMATI ya Nishati na Madini ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imekubali wazo la wadau kuhusu rasimu ya sheria ya gesi kuwa na mapungufu makubwa ikiwemo waziri kupewa madaraka makubwa ya maamuzi.
Pia kamati hiyo imekubali kuwa sheria ya gesi haiwezi kupitishwa bungeni hadi hapo itakapofanyiwa marekebisho ambayo yatawanufaisha Watanzania wote na gesi badala ya wawekezaji au wajanja wachache.
Akizungumza na wajumbe wa kamati hiyo katika ukumbi wa utawala bungeni jana, Mwenyekiti wa Mtandao usio wa Kiserikali wa Oil Natural Gas Environmental Alliance (ONGEA) Denis Mwendwa alisema kama rasimu hiyo itapitishwa bila marekebisho, haitakuwa na manufaa yoyote kwa Watanzania.
Alisema moja ya mapungufu hayo ni namna ambavyo rasimu hiyo imetoa uhuru zaidi kwa Waziri wa Nishati na Madini katika kusaini mikataba mbalimbali bila ya kushauriana na wadau wengine.
Alisema mbali na mamlaka makubwa ya waziri katika kusaini mikataba, pia mgawo wa rasilimali kwa wahusika wa maeneo ambako gesi inapatikana ni mdogo.
“Moja ya mapungufu ya sheria hiyo ya gesi ni pamoja na madaraka makubwa ya waziri ambapo anaweza kusaini mkataba bila hata ya kuhojiwa na mtu yeyote, hivyo tumeona lazima tuzungumze na wahusika ili iweze kuboreshwa,’’ alisema Mwendwa.
Alisema kuwa ONGEA kwa kushirikiana na Mtandao wa Wanahabari wa Kupambana na uharibifu wa Mazingira (EMNet), walitumia wataalamu mbalimbali katika kuyabaini mapungufu hayo na ndio maana wakaona ni vema kuyafikisha kwa wahusika ili yaweze kufanyiwa kazi kabla ya kuanza kutumika kuwa sheria.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini Seleman Zedi, ambaye pia ni mbunge wa Bukene (CCM) alikiri kuyapokea maoni ya taasisi hizo na kueleza kuwa watawashawishi wabunge wengine kuipinga sheria hiyo kama haitafanyiwa marekebisho.
Zedi alisema kwa sasa hakuna mkataba wowote ambao waziri anaweza kuingia kuhusu uchimbaji au utafutaji wa mafuta kwani hata kabla ya kupewa elimu hiyo ya jana, tayari kamati yake ilishabaini mapungufu kadhaa na hivyo wakataka serikali izuie uwekaji mikataba yoyote kwa sasa.

Source: Tanzania Daima 23 July 2012
 
Back
Top Bottom