Je kwa nini jeshi la misri halikutumia nguvu kumbakisha mubarak madarakani? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Je kwa nini jeshi la misri halikutumia nguvu kumbakisha mubarak madarakani?

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by dmalale, Feb 17, 2011.

 1. d

  dmalale Member

  #1
  Feb 17, 2011
  Joined: Jun 7, 2009
  Messages: 34
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 13
  Kwanini jeshi la Misri halikutumia nguvu kumbakisha Mubarak madarakani?

  [​IMG]
  Lula wa Ndali-Mwananzela​
  Februari 16, 2011[​IMG]

  “Jenerali Tantawi, ingilieni kati kuwazuia waandamanaji.”
  “Jenerali Tantawi, mnangoja nini?”
  “Jenerali Tantawi, nisikilizeni, mimi ndiye Rais.”
  “Jenerali Tantawi, ninawaamuru kwa madaraka yangu watawanyeni waandamanaji.”
  “Jenerali Tantawi, wanaandamana bila kibali! Wazuieni” “Jenerali Tantawi, wanahatarisha amani, umoja, utulivu.”
  “Jamani Jenerali Tantawi, nisaidieni jamani eh.”
  “Jamani tumetoka mbali pamoja Tantawi please”
  Akawabembeleza akashindwa; akawatisha hadi vitisho vyote vikageuka vichekesho; akavunja baraza la mawaziri, akamleta makamu wa rais kwa mara ya kwanza kwa miaka karibu thelathini, akalazimisha uongozi wa chama chake ujiuzulu akiwamo mwanae mpenzi aliyemuandaa kumrithi.
  Akabembeleza kuwa ameelewa matatizo ya wananchi wake. Vyote havikufua dafu kubadilisha mioyo ya Wamisri ambao walijua hakuna kitu kingine walichokitaka toka kwake; si sura yake, si urafiki wake na Marekani, si maneno yake ya kizalendo - hawakutaka chochote zaidi ya yeye kutoka madarakani; pamoja na chama chake! Walimkataa.
  Tumaini lake kwa miaka yote ya utawala wake ni utii wa jeshi ambalo yeye mwenyewe aliwahi kulitumikia. Kwa miaka yote iliyopita jeshi lake limekuwa pamoja naye kumlinda na kumhakikishia usalama wake na mwendelezo wa utawala wake.
  Aliamini anapendwa na watu wake. Aliamini kuwa watu wake wasingeweza kuishi bila yeye; aliamini kuwa wananchi aliowatumikia kwa miaka zaidi ya 60 wangekumbuka mazuri aliyoyafanya na kumsamehe angalau amalizie ngwe yake hadi Septemba. Wamisri walimkataa.
  Chama chake kiliamini kabisa kuwa chenyewe ndicho pekee chenye uwezo wa kutawala Misri; kilibeza juhudi zozote za mabadiliko; kilizuia makundi ambayo kiliyaona kuwa ni ya kidini ambayo yalikuwa yanakitishia.
  Alitumia karata ya kuwa “hao ni wadini” wapo walioamini wakamkumbatia, wakamuimbia na kumpigia na vigelegele kila alikopita. Kumbe zilikuwa sifa za woga, ilikuwa ni nidhamu ya wanaokandamizwa! Siku alipotaka huruma yao - walimkataa!
  Aliitisha uchaguzi na akashinda, tena kwa kishindo. Alikitambia chama chake kuwa ushindi wao ulikuwa ni ushindi ‘mnono’. Walimshangilia. Mtoto wake wa kiume alijipitisha pitisha akionekana kumtetea baba yake na hata kuonekana kuwa ni mrithi mtarajiwa.
  Naam, mwanae alipewa hata uongozi katika chama, tena katika nafasi za juu. Alipopita mwanae aliheshimiwa, watu wazima walinyenyekea mbele yake na wazee walimbusu mikono yake - kwa sababu tu ni mtoto wa Rais. Walimuonesha heshima; kumbe heshima ya wanaokandamizwa.
  Ndugu zangu, kuanguka kwa Hosni Mubarak hakukuja kwa bahati mbaya. Kukataliwa kwa utawala wake na yeye mwenyewe kutupwa katika shimo lisilosamehe la historia kulitokana na msingi aliouweka yeye mwenyewe. Huwezi kuzuia mioyo ya watu kupata uhuru.
  Hosni Mubarak alitarajia jeshi hatimaye lingekuja kumsaidia. Aliwatendea mazuri majenerali. Jeshi hilo lilipokea misaada ya karibu dola bilioni moja na nusu kila mwaka. Walikuwa ni marafiki na wengine waliwahi kutumika pamoja jeshini na Mubarak.
  Lakini wananchi wa Misri walipoamua kuikataa serikali yao kwa maandamano jeshi halikuingilia kati. Wengine wanauliza kwanini? Kwanini jeshi halikufanya kile kilichofanywa na Jeshi la China mwaka 1989 pale uwanja wa Tianmen jijini Beijing.
  Kwa wanaotaka kukumbushwa maandamano ya kudai mabadiliko ya kisiasa nchini China yalizimwa kwa nguvu na jeshi la nchi hiyo bila kujali gharama ya maisha ya wananchi wake. Jeshi la China linadaiwa kuua zaidi ya watu 400 kuamkia Juni 4, 1989! Ndio ulikuwa usalama wa watawala wa China. Kwanini jeshi la Misri halikufanya hivyo?
  Kuna majibu mengi yanayoweza kutolewa kwa nini jeshi halikuingilia kati. Naomba mniruhusu nipendekeze jibu moja ambalo kidogo lina sauti ya kifalsafa. Jeshi la Misri lilielewa kitu ambacho nina shaka hapa kwetu hatujakielewa na hatuko tayari kuelewa.
  Kwamba mamlaka ya kutawala yanatoka kwa wananchi. Watu wengi wanafikiri kuwa mamlaka ya kutawala yanatoka kwenye Katiba na hivyo kwao Katiba ndiyo kila kitu. Watatuambia “tuheshimu Katiba” na ya kuwa “Katiba imesema” n.k na ni kweli katika mazingira ya kawaida Katiba inatakiwa iwe ndiyo mwamuzi wa mwisho. Wananchi wa Misri walikuwa na Katiba ambayo iliwatumikia kwa miaka kadha wa kadha.
  Lakini Katiba haiko juu ya wananchi. Katiba iko kwa ajili ya wananchi na inawekwa chini ya matakwa ya wananchi - si viongozi. Ndiyo maana nilimshangaa sana mzee Pius Msekwa aliposema kwa fahari kwenye ITV kuwa Katiba inabadilishwa inapotokea kile alichokiita “change of sovereignty” na “merger of sovereignty”.
  Alisahau kwamba Katiba inaweza kubadilishwa endapo watu wenye “sovereignty” wanaamua hivyo. Katika ufalme - ni wafalme na katika jamhuri ni wananchi. Ndiyo maana Mfalme wa Jordan na Mfalme wa Saudia wanaweza wakaamua kufanya kitu kwa matakwa yao bila kuhojiwa na mtu yeyote kwani wao ndio “hakimiya” - sovereigns.
  Jeshi la Misri ni miongoni mwa majeshi makubwa kabisa duniani na ambalo watendaji wake wengi wamejifunza nadharia za kijeshi za Magharibi ambazo zinayaweka majeshi chini ya watawala wa kiraia.
  Nadharia hizi za kijeshi zinaamini kuwa majeshi yana majukumu ya kulinda uwepo wa nchi, uhuru wa nchi na hakimiya ya nchi yenyewe. Jukumu lao ni tofauti kabisa na la polisi na vyombo vingine vya dola. Jeshi ndilo mlinzi wa mwisho wa uwepo wa nchi au taifa na ndilo mtetezi wa mwisho wa uwepo wa watu kama taifa.
  Jeshi linaposhindwa kuilinda nchi au kuwalinda watu wake kuendelea kuwepo kama taifa basi nchi hiyo inaangukia chini ya watawala wengine. Hivi ndivyo ilivyokuwa kwenye uvamizi wa Sadam Hussen Kuwait kwani majeshi ya Kuwait hayakuwa na uwezo wa kuzuia jeshi la Sadam.
  Hili lilikuwa kweli vile vile pale Idi Amin alipovamia Kagera na kuanza kujitapa kuwa kama tungemjibu basi jeshi lake lingeweza kutupiga hadi Dar es Salaam. Kama Idi Amin angeshinda vita ile na kuanza kushika maeneo ya Kagera, Mwanza, Shinyanga hadi majeshi yake yakanyage Dar es Salaam basi leo hii Tanzania ingekuwa ni ya tofauti sana. Lakini jeshi letu liliweza si tu kumuondoa nduli katika ardhi yetu lakini kuhakikisha kuwa hawezi kuwa tishio tena.
  Hili ni muhimu kuelewa. Wamisri walikuwa hawatishiwi uwepo wao kama taifa au huru wao kama nchi. Kilichokuwa kinatokea ndani ya Misri ni kuwa wananchi wa Misri hawakukubaliana na watawala wao na waliamua kuwapinga wazi na wakatumia haki yao ya mwisho ya kuwaondoa watawala hao.
  Haki hiyo haiondolewi na katiba wala haiondolewi na jeshi. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kuandika na kusema “wananchi wanapopoteza imani na serikali yao” na ya kuwa njia zote za kuwashawishi watawala wao wabadilike na kuwa inavyotarajiwa na kupaswa na wananchi hao; basi “wananchi wana haki kuchukuka silaha na kuiondoa serikali ile ya kipuuzi”. Silaha zinaweza kuwa bunduki au mawe! Wamisri hawakuwa na bunduki isipokuwa sauti zao!
  Ndiyo sababu basi jeshi lilitamka mwanzo kabisa wa mgogoro ule kuwa “halitoingilia kati”. Baadhi ya watu hawakuelewa kwa nini jeshi halikuingilia kati. Kwani, halikuingilia kati maandamano yalipoanza, na wala halikuingilia kati pale mashabiki wa Mubarak walipoingia kwa nguvu na kuanzisha mapigano dhidi ya wapigania demokrasia. Jeshi liliacha wananchi waamue wenyewe na yule atakayeshinda ndiye atatiiwa na jeshi hilo.
  Matokeo yake, vijana wa Uwanja wa Tahrir, ule uwanja wa ukombozi, uwanja uliotakaswa kwa damu ya Wamisri Wakristu na Waislamu; ule uwanja ambao daima utakumbukwa kuwa ni mahali wananchi wa Misri walisimama na kuweka mguu chini na kuambia utawala wa kifisadi imetosha!
  Ndugu zangu, waliposokumwa hawakurudi nyuma, walipotishwa hawakufumba macho, walipoangushwa hawakulala chini kwa kujificha na walipouawa hawakunyamaza.
  Jeshi la nchi hiyo liliwaacha wananchi wawe waamuzi wa mwisho. Matokeo yake ndani ya siku 18 za kukosa usingizi, za kulia sana, za kukaa mbali na familia zao wananchi wa Misri waliweza kumlazimisha Hosni Mubarak kuachia ngazi.
  Na hapa ndipo Nyerere wetu anaonekana ni shujaa kati ya wenye kiu ya madaraka. Hata wale wanaosema Nyerere alikuwa dikteta ni lazima waone haya leo hii kwani madikteta hawaachii madaraka kwa furaha na kwenda kulima! Jeshi la Misri lilikaa pembeni ili wananchi wa Misri watumie haki yao ya mwisho ya kubadilisha utawala wao.
  Matokeo yake baada ya Mubarak kuondoka Jeshi likasimamisha Katiba - kwa sababu wananchi wametumia haki yao kuuondoa utawala walioingiza kikatiba, na wakavunja Bunge - kwa sababu hiyo hiyo moja wananchi wamewakataa watawala wao.
  Ndugu zangu, natumaini nasi tumejifunza somo hili la demokrasia. Maana watu wanafikiria demokrasia ni uchaguzi tu! Kwamba tukishakuchagua basi tusubiri miaka mitano kubadilisha serikali.
  Jamani Wamisri walikuwa na uchaguzi miaka mitano iliyopita na walitarajia kuwa na uchaguzi Septemba mwaka huu. Lakini wananchi walisema hawawezi kusubiri miezi tisa. Serikali haiwezi kuwa mbaya hadi miaka mitano ipite.
  Sawa, kuna mambo ambayo serikali inavumiliwa kwa sababu inaonekana kweli inajitahidi, lakini kama kujitahidi huko matokeo yake ni miaka 30 ya vitisho, kuburuzana na kuwapuuza wananchi mwisho wananchi wanafikia kikomo.
  Tumejifunza nini? - kwamba tuache mchakato wa kisiasa uanze hadi mwisho wake ili taasisi kma jeshi liwe tayari kumpigia saluti yule mshindi.
  Kama kuna kitu kilitukera wengi mwaka jana ni jinsi jeshi lilipoingilia kati mchakato wa kisiasa kwa matamshi yale ya kutisha wananchi kiasi kwamba maana ya “uchaguzi huru” haikuwapo tena.
  Kwangu Luteni Jenerali Shimbo hakupaswa kutoa matamshi yale ambayo yalionekana wazi kujenga mazingira ya vitisho na ninaombea mbingu na nchi hawatofanya hivyo tena.
  Ni matumaini yangu jeshi letu litaacha Polisi wafanye kazi zao na liwe kama Jeshi la Wamisri ambalo lilisema wazi kabisa kuwa halitanyanyua silaha zake dhidi ya wananchi wake.
  Yawezekan bado hatujafika hapo. Yawezekana labda baada ya miaka 50 Watanzania wanaweza kufika walipofika wa Misri baada ya miaka thelathini. Na tusiombee kufika huko, na tujitahidi pamoja kama taifa kutofika huko. Tusije kulazimika kuandika Katiba mpya katika mazingira ya machafuko.
  Ninaamini, kati ya mambo ambayo yataamua tunakotaka kwenda ni kuhakikisha kuwa tuna Katiba mpya ifikapo uchaguzi wa 2015. Hili halina mjadala. Watanzania wanataka Katiba Mpya na wanaitaka kabla ya uchaguzi mkuu ujao.
  Vyombo vya dola vikae pembeni, tukiandamana wakae pembeni, tukibishana na kumwagiana maji ya kuwasha na Polisi, Jeshi likae pembeni. Haki ya kutawala inatoka kwa wananchi, na milele inabakia kwa wananchi. Hili ni somo la kukumbukwa.
  [​IMG]


   
 2. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #2
  Feb 17, 2011
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,362
  Likes Received: 6,393
  Trophy Points: 280
  Ni swali la kifilosofia
   
 3. G

  Gad ONEYA JF-Expert Member

  #3
  Feb 17, 2011
  Joined: Oct 26, 2010
  Messages: 2,641
  Likes Received: 4
  Trophy Points: 135
  They thought of masses claims at heart, and saw a point in them!
   
Loading...